Mabalozi 100 wa Taasisi ya CCBRT wanatarajiwa kuendesha mafunzo ya wazi sehemu
mbalimbali nchini, yenye lengo la kuzijengea jamii uelewa kuhusu ugonjwa wa
fistula nawanawake wenye matatizo hayo, wametakiwa kujitokeza kupata matibabu.
Wiki iliyopita mabalozi 100 kutoka
mikoa 25 Tanzania walihudhuria mafunzo ya namna bora ya kuendesha semina hizo
za kijamii kwa mafanikio na kuwezeshwa vifaa vya kazi. Mabalozi hao wanasambaza
ujumbe wa 'Fistula inatibika'.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa
Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemans alisema, "maelfu ya wanawake sehemu
mbalimbali hapa nchini, wanaishi maisha ya aibu na kutengwa, kutokana na
kusumbuliwa na fistula bila kufahamu kwamba CCBRT na wabia wake wanatoa
matibabu bure, ikiwa ni pamoja na kubeba gharama zote za usafiri wa wagonjwa
kufika Dar es Salaam, malazi na chakula".
Mtandao wa mabalozi wa CCBRT, hutumika
kuwabaini na kuwasafirisha wanawake wenye tatizo la fistula kwa ajili ya
matibabu.
Balozi wa fistula anapombainisha na
kumthibitisha mgonjwa, hufanya mawasiliano na CCBRT kupitia namba maalum,
ambayo ni bure kwa wateja wote wa Vodacom.
Baada ya hapo, CCBRT hufanya utaratibu
wa kutuma fedha za nauli kusafiri kuelekea CCBRT Dar es Salaam au kwenye moja
ya hospitali inazofanya kazi nazo za Kigoma, Arusha na Moshi.
Kwa kila mgonjwa mmoja anayefikishwa
hospitali, balozi wa CCBRT hupata Sh 10,000 kama motisha kwa kusaidia kumaliza
tatizo la fistula Tanzania.
Kwa sasa mtandao wa mabalozi wa
fistula, unafikia mabalozi 500 wanaofanya kazi
kwa utaratibu wa kujitolea na
wameshafikisha hospitali wagonjwa wapatao 2,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene
Meza alisema "Kutumika kwa teknolojia ya Vodacom kumesaidia kupunguza
vikwazo kwa wanawake wanaotafuta matibabu na ni moja kati ya ubunifu mkubwa
kwenye sekta ya afya kuwahi kushuhudiwa hapa Tanzania".
Siku ya kimataifa ya kutokomeza fistula
huadhimishwa Mei 23 kila mwaka, kutambua umuhimu wa juhudi za kumaliza tatizo
hilo na pia kuonesha nia ya dhati ya Umoja wa Mataifa kwa juhudi zote
zinazofanywa za kutibu na kukinga fistula duniani.
No comments:
Post a Comment