LESENI ZA BIASHARA ZAINGIZA MABILIONI KINONDONI

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekusanya Sh bilioni 2.4, sawa na asilimia 93 ya bajeti ya manispaa hiyo, kupitia leseni za biashara
Mapato hayo yalikusanywa kupitia huduma iliyoanzishwa na manispaa hiyo ya kulipia kodi kwa njia ya simu za mkononi na MaxMalipo. Fedha hizo zilikusanywa mwezi Machi.
Ofisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kipindi cha miezi mitatu tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo, kimewasaidia kupata mapato haraka na kwamba wamekusanya Sh milioni 339 katika kodi ya majengo, tofauti na mwaka jana ambapo walikusanya Sh milioni 126.
"Ushuru wa masoko umeongezeka kwa asilimia 20 ya lengo la kila mwezi, hivyo ni mafanikio makubwa tuliyoyapata kwa kipindi kifupi sana," alisema Mhowera.
Aliongeza kuwa katika ada ya kuchangia huduma za afya, imeongezeka kutoka Sh milioni 45 hadi Sh milioni 69. Awali, ongezeko la mapato lilizidi bajeti ya mwaka iliyotakiwa kukusanywa, kwani bajeti za huduma za jiji zimezidi kwa asilimia 18.
“Napenda kuwahakikishia wananchi wa Kinondoni kuwa manispaa itazidi kuboresha huduma zake ili kufikia malengo yaliyokusuidiwa," alisema.
Mhowera alisema huduma hiyo mpya, inatolewa kupitia mfumo wa E-payment System, ambayo itamwezesha mwananchi kulipa kodi yake muda wowote.

No comments: