Chama cha Madaktari wa Dawa
ya Usingizi Tanzania, kimeiomba serikali kuweka chombo maalumu
kitakachofuatilia watoa huduma wenye weledi wa dawa hizo wakati wa upasuaji.
Imeelezwa kuwa, kwa Tanzania wapo madaktari 20
na kati yao 17 wapo Dar es
Salaam, wawili wapo Hospitali ya Rufaa
ya Bugando, Mwanza na mwingine katika
Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi, Kilimanjaro.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam na
Rais wa chama hicho, Mpoki Ulisubisya katika mkutano wa kwanza wa
kimataifa wa Madaktari wa dawa za usingizi uliohusisha nchi ya Uswisi,
Marekani, Afrika Kusini na Kenya.
Alisema Tanzania wapo madaktari wengi
lakini wanaotoa huduma ya dawa za usingizi wakati wa upasuaji ni wachache,
hivyo wanahitaji madaktari wa kutosha kutoa huduma hiyo.
Alisema wameamua kufanya mkutano huo
baada ya utafiti wa kisayansi uliofanywa na madaktari hao ili kujadili
changamoto zinazowakabili.
‘’ Wapo wasaidizi wasioelewa matumizi ya
dawa hizo kwa wagonjwa wakati wanafanya upasuaji hivyo wakati mwingine inaleta
madhara kwa mgonjwa kwa kumsababishia matatizo mbalimbali,’’ alisema
Ulisubisya.
Alitaja hospitali zilizopo Dar es Salaam
ambazo zina madaktari wa kutoa huduma hiyo kuwa ni Lugalo, Aga Khan, Hospitali
ya Taifa Muhimbili, Kitengo cha Mifupa
(Moi).
Alisema serikali iwasaidie madaktari
kupata wataalamu watakaotoa mafunzo katika hospitali zote nchini, kuleta ari
kwa madaktari kujifunza kutoa huduma hiyo.
Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Margareth Mhando alisema serikali itafadhili mafunzo ya elimu ya juu
kwa madaktari wa dawa hizo. Alisema
wanatarajia kuongeza wataalamu wa aina hiyo katika hospitali zote ili kuepusha
madhara yanayojitokeza wakati wa upasuaji.
No comments:
Post a Comment