KITENDAWILI CHA USAFIRI TRENI YA TAZARA BADO KUTEGULIWAAbiria wa treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), ambayo inatakiwa kuondoka leo kwenda Zambia, wako njia panda kutokana na wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea na mgomo wakidai mishahara yao.
Wakati mgomo huo ukiendelea, leo treni ya abiria kwa mujibu wa ratiba ya shirika hilo inatarajiwa kusafiri, hali inayotia wasiwasi kuwa huenda abiria watakwama stesheni, kwasababu hawajarudishiwa fedha zao kama walivyorudishiwa abiria wa treni iliyotarajiwa kuondoka Jumanne ya Mei 13 mwaka huu. 
Wafanyakazi wa Tazara jana waliendelea kukusanyika katika viwanja vya Tazara, wakisubiri uamuzi wa Menejimenti ya shirika hilo kuhusu malipo yao, ndipo waendelee na kazi hata hivyo hakujitokeza kiongozi yeyote katika Menejimenti kuzungumza nao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (Trawu) Kanda, Yusuph Mandari aliwataka wafanyakazi wenzake kuwa na uvumilivu katika kipindi hicho wakati wakisubiri kikao kitakachofanyika leo cha Bodi ya Wakurugenzi wa Tazara kutafutia ufumbuzi tatizo lao kama walivyoahidiwa na Mkurugenzi Mkuu wao Phiri.

No comments: