KITALE AZUNGUMZIA JINA LAKE JIPYA LA MKUDE SIMBA



Pengine si mgeni wa kichekesho cha Mkude Simba kilichoanza kuzagaa pole pole katika jiji la Dar es Salaam  na hatimaye karibu nchi nzima.
Ni kichekesho ambacho kilianza kupitia mitandao ya kijamii,  taratibu  kikapokewa na madereva pikipiki na  sasa kwenye kituo cha redio mpya inayokwenda kwa jina la 'E' Fm.
Lakini unaweza usijue  sauti inayotumika katika kichekesho hiki ni cha msanii maarufu ambaye anatambulika zaidi katika tasnia ya filamu kwa mtindo wa kuigiza utumiaji wa dawa za kulevya 'teja'  Kitale ambaye jina lake halisi ni Musa Kitale.
Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya,  Kitale anasimulia sababu za kuanzisha kichekesho hicho ambacho sasa kinatishia kulipoteza jina lake la Kitale.
Anasema Mkude Simba ni kichekesho kinachotumia lafudhi ya Kiluguru ambaye anaonesha ushamba wa hali ya juu na maswali ya kukosa majibu ya msingi.
Kitale anasema yeye ni Mluguru na  kwa muda mrefu alikuwa na wazo na kulitangaza kabila lake kupitia sanaa, lakini hakuwa na njia ya kutumia.
Anasema kipindi hicho alitaka kutumia "Bwana mjomba... Mjomba Mkude" ambayo hutumiwa na Waluguru na wazo lingine lilikuwa kutumia mtindo wa Uteja.
Aliamua kuchagua Uteja akafikiria kutumia  kichekesho hicho  ambacho kitakuwa cha peke yake, kitakacholeta  mabadiliko katika  tasnia ya sanaa.
"Niliweza kupata umaarufu mkubwa na watu wengi wakanijua kupitia tasnia ya filamu, kwa kuigiza kama mtumiaji wa madawa ya kulevya, mkorofi na mtu wa vurugu," anasema.
Lakini tofauti na vile ambavyo alidhani  mwanzo wakati anatumia mtindo huo, kwani yalianza kuibuka matatizo mengi kutokana na  mtindo huo.
"Nilitumia mtindo huo kwa muda mrefu na ndipo imani hiyo ikakaaa kichwani mwa watu, nikaanza kuingia kwenye matatizo mengine," anasema.
Anasema matatizo madogo madogo ni mengi, lakini miongoni mwa matatizo makubwa ni kufuatiliwa na polisi wakidhani anahusika na biashara ya dawa ya kulevya.
Anasimulia zaidi kwamba akiwa kwenye matembezi yake ya kawaida, alimtembelea rafiki yake Mwananyamala ambapo alipoingia ndani dakika chache walivamiwa na polisi waliokuja na gari nakuanza kupitisha msako wa nguvu mle ndani wakidhani Kitale alikuwa na madawa ya kulevya.
"Hapo ndipo nilipojua kwamba baadhi ya jamii inanichukulia tofauti sana, kufikia hadi kuvamiwa na polisi na kukaguliwa," anasema Kitale kwa mshangao.
Anasema matatizo mengine kuna baadhi ya watu hawana imani naye kabisa kwa kudhani ni mwizi, ingawa anajaribu kuwaelewesha kwamba anaigiza  na ni sehemu ya kazi.
Katika tukio lingine anasema aliwahi kuwekwa polisi  katika ugomvi wa mtaani kisa  alikuwepo  kuamualia ugomvi huo.Anasema ugomvi huo ulikuwa mtaani kwao Mwananyamala ambapo vijana wa kihuni walikuwa wakigombana na kupelekea kuvunja kioo cha gari lililoegeshwa ofisi za CCM.
Anasema baada ya ugomvi kuisha kila mtu alitawanyika, lakini polisi walipokuja na kuchunguza aliyevunja kioo cha gari watu wakamtaja kutokana na kujulikana kama raisi wa Mateja Mwananyamala.
"Nikiwa nyumbani nilifuatwa na kukamatwa na kupelekwa polisi, ndipo nikawapa maelezo ya kutosha na kuachiwa huru," anasema.
Anasema lakini yote hayo yalitokea kutokana na Mwananyamala kujulikana zaidi kama raisi wa mateja, ndio maana kila tatizo linaangukia kwake hata kama alikuwa akipita njia.
Anasema matatizo hayo na mengine mengi, ndiyo yaliyomfanya afikirie kutambulisha mtindo mpya wa Mkude Simba.
Mtindo wa Mkude Simba anasema anaamini anaweza kupunguza kasi ya Kitale teja na hata jamii kumuelewa kwa mtindo tofauti.
"Kweli hivi sasa jamii inanijua zaidi kwa jina la Mkude Simba na jina la Kitale limepungua nguvu," anasema.
Anasema alitumia mtindo huo, ili kujaribu kuleta tumaini kwa jamii na kumuona ni mtu anayeigiza,  na kwamba maisha ya uteja sio halisi.
Kwa sasa anasema kila sehemu anayopita humuita Mkude Simba sio Kitale kama zamani, tena wanatamani  kuwa karibu naye kumsikiliza tofauti na zamani aliogopeka zaidi.
Kitale anasema kwa sasa anatarajia kutumia mitindo yote miwili, akiwa kama Mkude Simba na Kitale.
"Mkude Simba nitakuwa tofauti na Kitale, na kazi zao zitakuwa tofauti kabisa kama inavyojulikana sasa," anaelezea.
Pia ana malengo ya kutengeneza filamu za Mkude Simba, ambazo zitakuwa na vichekesho vya Mkude Simba.
Lakini anasema ipo siku ataigiza filamu ya pamoja kati ya Mkude Simba na Kitale, jambo ambalo anaamini ataleta mshangao kwa watu wengi.
Kitale anasema kwa sasa hajaanza kupata faida ya vichekesho hivyo, ingawa vimeenea karibu kila mahali.
Lakini ana imani kwamba ipo siku vitamletea fedha kupitia miito ya simu, filamu, matangazo ya redioni kwa kuwa watu wameshaanza kuvikubali.
Zaidi ya sanaa ya kuigiza sauti na filamu, Kitale anasema muziki pia ni sehemu ya kazi yake.
"Tayari nilishafanya kazi nyingi, nikitumia mtindo wa Mchiriku na bado nafanya kazi mpya zinakuja," anasema.
Miongoni mwa kazi ambazo alishazifanya ni Hili Toto aliyomshirikisha Sharomilionea,  Hili Dude na wimbo unaokuja sasa ni Mapenzi yanauma.
"Mtindo ninaotumia ni mchiriku kwa kuwa ndio unaozitambulisha nyimbo zetu nje ya nchi," anasema.
Kitale anasema yeye ni mzaliwa na Morogoro, Matombo na kwamba alianza kupata elimu yake Morogoro mjini kabla ya kuimalizia Dar es Salaam. Sanaa alianza katika kundi la Kaole.
Makala hii kwa mara ya kwanza imechapishwa kwenye gazeti la HabariLEO Jumamosi.

No comments: