KISHAPU YAOMBA TAMISEMI IIREJESHEE MILIONI 86.8/-

Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, imeiomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI), kuirejeshea  mara moja halmashauri hiyo Sh milioni  86.8  zilizotumwa  kutoka Hazina  kupitia Benki Kuu (BoT)  baada ya kubainika  fedha  hizo  za  mfuko wa barabara hazikuingizwa katika akaunti zake.
Fedha hizo zinatajwa kuwa sehemu ya milioni 210 zilizoingizwa  benki katika bajeti  ya mwaka wa fedha wa 2011/12, lakini hazikuonekana na  ndipo baraza la madiwani lilipounda tume ya madiwani ili kufuatilia fedha hizo kuanzia Agosti 19, mwaka jana.
Waliounda tume hiyo ni Samson  Gelewa, Ferdinand  Mpogomi,  David  Matungwa, Albert Kapongo, Mohammed Shaaban na wataalamu  wengine wawili katika masuala ya fedha.
Ripoti ya tume hiyo iliyowasilishwa hivi karibuni na Katibu wake,  Mpogomi  ambaye  pia  ni diwani wa Kata ya Sekebugoro ilibaini kutokea kwa mapungufu hayo katika fedha za Mfuko wa Barabara. Taarifa  ya  Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), imetajwa kuthibitisha mapungufu hayo.
“Hata hivyo kwa mwaka 2011/12 wilaya ya Kishapu  katika bajeti yake  ya barabara,  ilikuwa ni Sh milioni 412 na kulingana na  bajeti hiyo  vielelezo  vilionesha  fedha  hiyo ilipokewa wilaya ya Kishapu na katika  utafiti  huo ilithibitika  kuwa Shilingi milioni  123.3  ziliingizwa katika mfuko wa barabara wa halmashauri na kiasi cha Shilingi milioni 86.8 hazikuonekana zilipo…tukajiuliza zimekwenda wapi?” alisema Mpogomi.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Wilson Nkhambaku  aliwataka madiwani wanapounda kamati, washirikiane na ofisi yake.
Alisema mara nyingi tume wanazoziunda,  amekuwa akizisikia  bila kufahamu lengo lake. Hata hivyo, alisema anaipongeza tume  hiyo kwa kufanya kazi nzuri.

No comments: