KIMEI WA CRDB ATINGA FAINALI TUZO ZA BENKI AFRIKA

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amefanikiwa kuingia katika hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo ya Mtendaji Bora katika Sekta ya Benki barani Afrika.
Mshindi wa tuzo hiyo anatarajiwa kupatikana Mei 21 mwaka huu wakati wa Mkutano Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika (ADB),  utakaofanyika Kigali, Rwanda.
Kwa mujibu wa Omar Ben Yedder wa jarida la African Banker, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za Benki barani Afrika, mbali ya Dk Kimei, wengine ni Bisi Onasanya, Mkurugenzi Mtendaji wa First Bank of Nigeria, Bola Adesola wa Benki ya Standard Chartered, Afrika Kusini na Joao Figueiredo wa benki ya Unico ya Msumbiji.
Wengine ni Pedro Pinto Coelho, Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard ya Angola, Segun Agbaje wa benki ya Guaranty Trust ya Nigeria na Vivienne Yeda, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB), Uganda.
Mbali ya tuzo ya Mtendaji Bora wa sekta ya benki, tuzo nyingine zitakuwa kwa ajili ya benki bora barani Afrika. Katika kundi hili, zimo Attijariwafa Bank na BMCE za Morocco, Nedbank na Standard Bank za Afrika Kusini na GTBank ya Nigeria.
Kutakuwa pia na tuzo ya benki bora, inayorudisha faida kwa jamii, benki bora ya kitegauchumi, benki inayoongoza kwa ubunifu na nyingine.

No comments: