'KILIMANJARO CHALLENGE' KUSAIDIA VITA DHIDI YA UKIMWI

Wananchi wametakiwa kuongeza kasi ya kupunguza ongezeko jipya la ugonjwa wa Ukimwi, kwani bado ni tishio.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Amina Mrisho wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa kampeni ya 'Kilimanjaro Challenge'.
Kampeni hiyo inayoratibiwa na Mgodi wa Geita, itachangia fedha zitakazotumika katika kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU.
Mrisho alisema ugonjwa huo, bado ni tishio nchini, ambapo hadi sasa kuna ongezeko la maambukizi kwa wastani wa watu 86,000 kila mwaka.
Alisema watu 1.6 wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini, huku watoto milioni 1.3 wamepoteza wazazi  wao kutokana na ugonjwa huo.
"TACAIDS kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita na wadau mbalimbali kupitia Kilimanjaro Challenge tutasaidia kuhamasisha waathirika waliokata tamaa,” alisema Amina.
Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuielimisha jamii, kuhusiana na ugonjwa wa Ukimwi, maambukizi na jinsi ya kujikinga na  ugonjwa huo.
Aidha, kampeni hiyo inalenga kukusanya fedha taslimu kusaidia waathirika wa VVU kupitia taasisi zisizo za kiserikali.
Wadau mbalimbali wameombwa kujitokeza kuchangia mfuko wa Kilimanjaro Challenge, ambao utatumika kusaidia kupambana na maambukizi ya VVU nchini kupitia tovuti yake ya www.geitakilichallange.com.
Makamu wa Rais wa Mgodi huo, Simon Shayo alisema kampeni hiyo itakayoanza hivi karibuni, itahusisha upandaji wa Mlima Kilimanjaro kupitia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo wamelenga kukusanya Sh bilioni 1.5.

No comments: