KIKWETE KUZINDUA MPANGO WA BILIONI 100 WA UBORA WA ELIMUSerikali inatarajia kuzindua mpango wa Sh bilioni mia moja unaolenga kufanya ubora wa elimu kuwa uhai wa madarasa hapa nchini.
Mpango huo utazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete Mei, 10 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Mratibu wa Taifa wa Equip Tanzania,  James Ogondiek wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema lengo kuu la uwekezaji huo ni kuboresha mchakato wa kufundisha na matokeo ya kujifunza kwa watoto nchini Tanzania.
Alisema mpango wa kuinua ubora wa elimu Tanzania- Equip Tanzania  ni mpango wa miaka minne unaoongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ukiwa na lengo la kuboresha utoaji wa elimu kwa kuhakikisha watoto wanapata alama bora katika mitihani yao.
Aidha kuwawezesha wanafunzi kushiriki kikamilifu kutimiza azma ya kukua na kuchangia kupata maendeleo ya haraka nchini Tanzania.
Alisema mpango huo unafadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Misaada la Uingereza (DFID-UKAID) na unafanya kazi katika wilaya 48, shule 3,700 na utawafikia watoto milioni 2.1.
Alisema malengo mengine ni kuimarisha uongozi na  usimamizi wa shule kuwa na mwongozo wa kitaifa wa vigezo vya shule bora na kuwaendeleza kitaalamu.
Pia walimu wakuu na walimu wakuu wasaidizi zaidi ya 7,200 na waratibu elimu kata 755, kuimarisha usimamizi wa elimu katika ngazi za Wilaya na Mikoa ili kusaidia menejimenti za wilaya na mikoa katika wilaya 48 na mikoa saba kuboresha tija na ufanisi wa shule na mifumo inayowasaidia katika utoaji wa
elimu.
Alisema Equip Tanzania inafanya kazi katika mikoa saba ya Tanzania bara ambapo mwaka 2014 shirika hilo ilianza kazi katika mikoa mitano ya Dodoma, Tabora, Kigoma,Shinyanga na Simiyu na mwaka 2015 watafikia mikoa ya Lindi na Mara.

No comments: