KESI YAMKALIA VIBAYA MKURUGENZI WA ZAMANI WA ILALAHakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Devotha Kisoka, amesitisha nia yake ya kutoa uamuzi wa ombi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, anayeomba afutiwe kesi ya mauaji ya watu 27 inayomkabili na wenzake 11 kwa kuwa jalada la kesi hiyo halipo.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Kisoka alisema hawezi kutoa uamuzi wa ombi hilo kwa kuwa jalada la kesi hiyo lipo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na hajui sababu ya jalada hilo kuitwa huko.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 27 mwaka huu itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika na washitakiwa wataendelea kusota rumande.
Katika ombi lake alilowasilisha kupitia kwa mawakili wake John Mhozya na Ndurumah Majembe, Fuime aliiomba Mahakama kuangalia kwa makini hati ya mashitaka kwa kuwa madai ni batili na hati iliyopo mahakamani haikidhi matakwa ya sheria.
Alidai kuwa kwa mujibu wa sheria, hati ya mashitaka  inatakiwa kuwa na viashiria vya kosa  ambalo mshitakiwa anashitakiwa nalo lakini hati iliyopo mahakamani haina viashiria vinavyoonesha  kosa la mauaji.
Mbali na Fume washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Laza Radha, Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed (59), vigogo wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Charles Ogare(48), Mhandisi wa Majengo Godluck Sylivester (35) na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa Majengo, Willibrod Mugyabuso (42).
Wengine ni Mhandisi Mohamed Abdulkarim (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoshaodaga Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo (60), Mkadiriaji Ujenzi, Vedasto Ruhale (59), Msanifu Majengo, Michael.
Inadaiwa kuwa Machi 29 mwaka jana, katika mtaa wa India Gandhi Ilala, Dar es Salaam kwa makusudi washitakiwa waliwaua watu 27.

No comments: