KESI YA SHEHE PONDA YAKWAMA TENA

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Morogoro kwa mara nyingine jana, imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya Katibu wa Taasisi na Jumuiya ya Waislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa, kutokana na jadala  la kesi hiyo, ambalo liko Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutorejeshwa mahakamani hapo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mkoa, Mary Moyo alilazimika kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 14, mwaka huu.
Jana Shehe Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 3 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa Polisi. Wafuasi wake waliokuwepo mahakamani hapo, walizuiwa nje ya uzio wa mahakama hiyo.
Hakimu Moyo anayesikiliza kesi hiyo, alitumia dakika tatu kufikia uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo. Aliufahamisha upande wa Wakili wa Serikali na utetezi  kuwa hakuwa na jalada halisi la kesi hiyo.
Jalada hilo limepelekwa Mahakama Kuu kwa ajili  ya kusikilizwa ombi la Shehe Ponda la kutaka uamuzi wa mahakama hiyo, kupitiwa upya na Mahakama ya juu.

No comments: