KDU KASKAZINI YAMNING'INIZA MKURUGENZI WA MIRERANIKikosi dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini kimemtia hatiani Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mji mdogo wa Mirerani, Nelson Noman Msangi (54) kwa kosa la kukutwa na meno matatu ya tembo na kipande cha pembe ya faru chenye uzito wa gramu 80 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 10.
Mbali ya Msangi ambaye ni Ofisa wa Serikali mwingine aliyekamatwa naye ni pamoja na mfanyabiashara  maarufu wa jijini Dar es Salaam, Shabani Salumu Mpara (42).
Meno hayo ya tembo yalikuwa na thamani ya dola za kimarekani 5,720 sawa na fedha za kitanzania Sh 9,323,600 na kipande cha pembe ya faru chenye gramu 80 kilikuwa na thamani ya dola za kimarekani  600 sawa na Sh za kitanzania 978,000  jumla nyara zote zilikuwa na thamani ya Sh 10,301,600.
Wakisomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa KDU, Michael Msokwa ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao wameshitakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kukutwa na nyara za serikali na kuhujumu uchumi.
Msokwa aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha mbele ya Hakimu Devota Msofe kuwa watuhumiwa walikutwa na nyara za Serikali mnamo Aprili 4 mwaka huu katika Kijiji cha Kibilashi Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kinyume na sheria.
Akizungumza nje ya Mahakama Msokwa alisema kuwa nyara hizo za washitakiwa zilikamatwa na gari aina ya Toyota Opa lenye namba za usajili T249BUA baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

No comments: