JUMUIYA AFRIKA MASHARIKI KUKABILI UGAIDI KWA NGUVU ZOTE

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais  Uhuru Kenyatta wa Kenya, amesema nchi wanachama katika jumuiya hiyo, zitatumia  rasilimali zao kukabiliana  na  ugaidi na uhalifu unaozikabili. 
Alisema hayo jana alipokuwa kwenye mkutano wa 12 wa marais  wa nchi wanachama wa EAC, ulifanyika jijini Arusha.
Alisema masuala ya uhalifu na ugaidi kwa sasa katika nchi hizo  ni tishio, hivyo vyema waungane pamoja kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumzia kuhusu Sudan Kusini  ambayo iliomba kujiunga na
Jumuiya hiyo, alisema wameamua kusogeza mbele mazungumzo yake, kutokana na maombi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Kenyatta,  pia nchi ya Somali nayo mazungumzo yake bado mpaka hali ya usalama iwe nzuri na Jumuiya  itahakikisha hali ya usalama inakuwa nzuri.
Katika hatua nyingine, Kenyatta alipongeza majaji watatu walioapishwa jana kuongoza Mahakama ya Afrika Mashariki  (EACJ) kwa miaka mitatu.
Majaji hao ni Edward Rutakangwa (Tanzania) , Aaron Ringera (Kenya) na Fakihi Jundu (Tanzania), ambao baada ya kuapishwa wataanza kazi rasmi katika mahakama hiyo Juni mwaka huu.
Mbali na majaji hao, pia Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Enos Bukuku naye aliongezewa muda wa miaka mitatu wa kufanya kazi, huku Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki akishika Emmanuel Ugirashebuja na Makamu wake, Liboire Nkurunziza.
Msajili wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Profesa John Luhangisa, alisema pia katika mkutano huo, wamefungua tovuti mpya , itakayotumiwa na wateja wa mahakama hiyo katika kufungua kesi zao.
“Tovuti hii mpya  itaepusha upotevu wa mafaili ambao ulikuwa ukileta usumbufu kwa wateja au Mahakama kuchelewa kuanza muda wake, maana kila mteja atakuwa akifuatilia hali ya Mahakama ya kesi yake kwenye tovuti na kufahamu kila anachotaka,” alisema.
Alifafanua kwamba tovuti hiyo, itachukua muda kuanza kutumika na wateja mpaka kanuni zitakaporekebishwa ili ianze kutumika.
Marais Jakaya Kikwete, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda, walihudhuria mkutano huo, wakati Rwanda na Burundi zilituma wawakilishi.

No comments: