HUDUMA TRENI YA TAZARA KUREJEA LEOHuduma katika Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara), zinatarajiwa kurejea leo baada ya Serikali kupatia ufumbuzi matatizo yaliyosababisha mgomo wa wafanyakazi kuanzia Jumatatu iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka, alisema Serikali imekuwa ikifanya mikutano na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu) na uongozi wa Tazara na kukubali  kuendelea kutoa huduma huku Serikali ikifanyia kazi matakwa yao.
Dk Mwinjaka alisema Serikali ya Tanzania  imekubali kutoa mshahara wa Aprili na Februari, huku Serikali ya Zambia ikishughulikia mshahara wa Machi na Mei.
“Tumefikia hatua kubwa jana (Jumamosi) baada ya mkutano na Chama cha Wafanyakazi na Menejimenti ya Tazara  kuafiki huduma zirejee huku madai yao yakiendelea kufanyiwa kazi,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imeshindwa kusubiri hadi mwisho wa mwezi bila kupatia suluhu madai ya wafanyakazi hao, kwani haitokua na sura nzuri kwa umma huku wasafiri wakipata taabu.
 “Mshahara wa mwezi Machi na Mei utashughulikiwa na serikali ya Zambia,” alisema.
Alisema katika mkutano utakaofanyika mwisho wa mwezi huu, Serikali ya Tanzania itapata fursa ya kujua ni kwa nini mshahara wa Machi haujawafikia wafanyakazi wa Tazara.
Mgomo wa wafanyakazi wa Tazara ulianza wiki iliyopita kwa kudai kulipwa mishahara yao ya Februari pia Machi, April  i2014, ambapo walisisitiza kuendelea kugoma hadi walipwe.

No comments: