HOMA YA DENGUE SASA YATAPAKAA KILA KONA



Wakati watu 400 wakithibitika kuwa na ugonjwa wa  homa ya dengue, huku wengine watatu wakifariki dunia, Serikali imetoa taarifa kuhusu dalili za ugonjwa huo na namna inavyokabiliana nao.
Mbali na kutoa taarifa hizo, Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania popote walipo, wakipata dalili hizo, wasinywe dawa hovyo, badala yake waende kupima hospitali na kufuata ushauri wa kitaalamu.
“Naomba watu wakiona dalili za homa waende hospitali kupima maana hivi sasa kuna ugonjwa huu wa dengu…msinywe dawa tu bila kupima  maana  sasa unasambaa hivyo muende hospitali,” alisema Rais Kikwete.
Pia Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Wizara ya Fedha, kuhakikisha kunakuwa na dawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha kudhibiti ugonjwa huo, kwa kuwa ni wa dharura.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema dalili za ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu na dalii hizo huanza kujitokeza kuanzia siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue.
“Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na dalili za malaria, hivyo basi tunawaomba wananchi wakipata homa kuhakikisha wanapima kama wana malaria au la, ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Pallangyo.
Aliongeza kuwa kuna aina tatu tofauti za ugonjwa huo katika namna unavyojitokeza, iwapo mtu aking’atwa na mbu mwenye virusi hivu.
Aina ya kwanza ndio homa ya dengue yenyewe, ambayo huambatana na dalili kuu tatu za homa kali ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo au uchovu. Kwa Tanzania mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wamejitokeza wakiwa na dalili hizo.
Aina ya pili ni dengue ya damu, ambayo huambatana na dalili za magonjwa kutokwa na damu kwenye fizi au puani na kutokwa na damu chini ya ngozi. Iwapo mgonjwa huyo ataumia sehemu yoyote, ni rahisi kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.
Aina ya tatu ni dengue ya kupoteza fahamu, ambayo huambatana na mgonjwa kupoteza damu nyingi ambayo husababisha mgonjwa kupoteza fahamu.
Mpaka sasa dalili hizo zimeonekana kwa mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa 400 waliokwishwa thibitika kuwa na ugonjwa hapa nchini.
Pallangyo alisema kwa wiki iliyoisha Mei 9, idadi ya wagonjwa waliogundulika mkoani Dar es Salaam ilikuwa  60; katika Wilaya ya Kinondoni watu 42; Temeke  14 na Ilala wanne. Mpaka sasa wagonjwa waliopo wodini 13 na wengine wameruhusiwa kwenda nyumbani.
Alifafanua kwamba mlipuko wa ugonjwa huu si mpya hapa nchini, kwani uligundulika kawa mara ya kwanza Juni 2010 mkoani Dar es Salaam ambapo idadi ya watu 40 walithibitika kuwa na ugonjwa huo. Pia kati ya Mei hadi Julai 2013 wagonjwa 172 walithibitika kuugua ugonjwa huu.
Alisema ugonjwa huu unasababishwa na mbu aina ya Aedes na kirusi cha dengue kinaambukiza kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kwa kuunmwa na mbu huyo.
Mbu huyo anaishi katika mazingira ya makazi ya binadamu na huuma wakati wa mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli, hususani asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Aliwashauri wananchi kutokuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo, kwani hauambukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kwa kugusa maji yanayotoka kwa mgonjwa.
Akizungumzia kinga, Pallangyo alisema kinga pekee iliyopo ni   kuangamiza mazalia ya mbu ikiwemo kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyuzia viatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo.
Katika kuua mazalia hayo, ametaka wananchi kuondoa vitu vyote vinavyoweka mazalio ya mbu kama vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yalipotupwa hovyo.
Pia alitaka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu vifyekwe na kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko imara na kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
Alisema mpaka sasa ugonjwa huu hauna chanjo wala dawa maalumu kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa huo, na njia kubwa ya kupambana na ugonjwa huo ni kumzuia binadamu asiumwe na mbu.
Wakati huo huo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi  Muhimbili (Muhas) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kinatarajia kufanya utafiti kuhusu ugonjwa wa dengue ili kupata matokeo yatakayowezesha
kukabiliana nao.            
Utafiti huo utakaoanza hivi karibuni, utafanyika kupitia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya, alisema  hayo jana  na kufafanua kwamba kuanzia Aprili 3 mwaka huu hadi Mei 9, wanafunzi 56 walikuwa na dalili za ugonjwa huo na baada ya kufanyiwa vipimo 17 walithibitika kuugua na kupewa matibabu na kupona.
Kutokana na dalili za awali kuonesha wameathirika, chuo kimeamua kupeleka sampuli za wale wengine NIMR kwenye vipimo madhubuti ili kupimwa na kupatiwa majibu sahihi.
“Baada ya kuna wanafunzi wetu wameathirika, tuliamua kuchukua tahadhari kwa kushughulikia maeneo yote yanayoonesha kuna mazalio ya mbu, lakini bao tunahitaji ushirikiano na manispaa kudhibiti maeneo kama katika bonde la Jangwani,” alisema.
Akizungumzia utafiti watakaofanya, alisema pia watashirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili na manispaa  za jiji ili kuangalia tatizo na kujipanga kukabiliana nalo.

Alisema muda wa kutoa matokeo ya utafiti huo itategemea aina ya utafiti watakaofanya kama kutumia wagonjwa kuchukua sampuli au kuangalia maeneo yanayozaliana mbu na baadhi ya viashiria lakini alihaidi kutoka mapema.
Wakati Serikali ilishaanza kufanyia kazi ugonjwa huo, Bunge jana lilitaka taarifa rasmi juu ya ugonjwa huo ulioibuka hivi karibuni na kusababisha vifo kikiwemo cha  Mganga wa Hospitali ya Temeke, mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alitoa agizo hilo jana bungeni kutokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile (CCM) akitaka wabunge na wananchi waelezwe rasmi juu ya ugonjwa huo kupitia bungeni.

No comments: