HIZI NDIZO SABABU ZA KIFO CHA BALOZI WA MALAWIMaofisa wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wenzao wa Serikali ya Malawi, wameendelea na maandalizi msiba wa ghafla wa Balozi wa Malawi nchini, Flossie Chiyaonga.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alisema misa ya kumuaga Balozi Flossie itafanyika leo katika ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Balozi Flossie alifariki Ijumaa iliyopita akiwa njiani wakati akipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu, baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake.
 Kwa mujibu wa Haule, Jumatatu iliyopita usiku, Balozi Flossie alijisikia vibaya na kupelekwa Aga Khan  ambako alipatiwa matibabu na kuwekwa mapumziko kati ya saa sita usiku saa 12 asubuhi, ambapo alipatiwa dawa za kutumia nyumbani na kuruhusiwa.
Hata hivyo, Haule alisema Ijumaa iliyopita, hali ilibadilika mchana na kurejeshwa hospitalini, lakini alipofikishwa Aga Khan, madaktari walimfanyia vipimo  na kubaini ameshafariki.
Haule alisema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi jana, ambapo madaktari walibaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kuvimba na kupasuka kwa mshipa mkubwa wa moyo, uliosababisha damu kujaa na kwenye mfuko wa moyo na kushindwa kufanya kazi.
Balozi Flossie alizaliwa Juni 16 mwaka 1960  Blantyre nchini Malawi na alitumikia Serikali ya Malawi katika nyadhifa mbalimbali.
Kati ya mwaka 2006 hadi 2010, alikuwa Naibu Balozi wa Malawi nchini Uingereza, ambapo baadae alikuwa Kaimu Balozi hadi alipoteuliwa kuwa Balozi wa Malawi nchini.
Haule alisema wakati wa uhai wake, Balozi Flossie alifanya kazi zake kwa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi na kushirikiana vizuri na mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao Tanzania.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Leo utapelekwa ukumbi wa Mwalimu Nyerere kwa misa na kuaga kabla ya kusafirishwa kesho kwenda nyumbani kwao, Blantyre, Malawi  kwa ajili ya maziko, yatakayofanyika Jumatano wiki hii.

No comments: