HATIMAYE KAMPUNI YA SIMON GROUP YAUFYATA KWA WABUNGEKampuni ya Simon Group inayoendesha Shirika la Usafiri Dar es Salaam  (UDA), imewaomba radhi wabunge wa Dar es Salaam akiwemo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA)  kutokana na habari zilizoandikwa kwamba Mwenyekiti wake, Robert Kisena aliwatuhumu wabunge hao kuhongwa ili kuihujumu UDA.
Akizungumza na vyombo vya habari jana, mwenyekiti huyo Robert Kisena amesema kuwa haikuwa lengo la Simon Group katika mkutano wake na waandishi wa habari ulioitishwa  Mei 18, mwaka huu kuwakashifu wabunge wala mtu yeyote.
Alisema ajenda kubwa katika mkutano huo ilikuwa uhalali wa umiliki wa hisa za Shirika la UDA, kutokana na mjadala uliokuwa umeibuka bungeni juu ya uuzwaji wa hisa za shirika hilo.
Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, serikali ilitamka kupitia kwa Naibu Waziri wa Fedha, kwamba mwaka 2010 ilitoa maagizo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya UDA kusitisha mpango wa kuiuzia Simon Group hisa zozote kwa kuwa utaratibu wa kumpata mwekezaji huyo ulikuwa umekiuka taratibu na misingi ya sheria.
 Serikali ilitamka bungeni kuwa kampuni ya Simon Group haimiliki hisa za UDA bali zinamilikiwa na wabia wawili ambao ni serikali yenyewe kupitia Msajili wa Hazina (asilimia 49) na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (asilimia 51).
Kisena alisema kwa kuzingatia kauli ya serikali, uongozi wa Simon Group uliona haja ya kuueleza umma upate kufahamu taarifa za upande wa pili, kwa sababu kampuni hiyo haikuwa na fursa ya kujitetea bungeni.
Alisema baada ya mkutano huo na waandishi wa habari, kumetokea mkanganyiko katika jamii juu ya masuala kadhaa ambayo baadhi ya vyombo vya habari havikuripoti kwa usahihi taarifa husika.
“Miongoni mwa kasoro zilizojitokeza ni baadhi ya vyombo vya habari vilitoa tuhuma kwa baadhi ya wabunge binafsi, kwa kuwataja majina kwamba walitajwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
“Kwa ujumla baadhi ya maudhui katika baadhi ya habari si tu kwamba yamesababisha mkanganyiko kwa umma, lakini pia kusababisha usumbufu mkubwa kwa Mbunge wa  Ubungo, John Mnyika na baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla wao.
“Natumia nafasi hii kumwomba radhi Mbunge wa Ubungo, Mheshimiwa Mnyika, wananchi wake wa Ubungo na Watanzania kwa ujumla kwa maneno hayo ambayo kama tulivyoeleza yameleta usumbufu kwake binafsi na wananchi hao,” alisema.
Akizungumza, Kisena alisema amechukua hatua hiyo ya kuwaomba radhi wabunge wa Dar es Salaam, hususan Mnyika ili kujenga uhusiano mzuri baina ya kampuni hiyo na wadau mbalimbali kwa lengo la kuiwezesha Simon Group kupata ushirikiano na wadau wote wa maendeleo katika mipango yake ya uwekezaji mkubwa ndani ya UDA.
“Kwa kweli tumeona tuwaangukie wabunge na watu wengine wote walioguswa na habari hizi ili kujenga uhusiano mwema na wabunge, hususan Mheshimiwa Mnyika, wananchi wa Ubungo, wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania wote hasa kwa kuzingatia kwamba kampuni yetu ni ya Watanzania na hivyo inahitaji kuungwa mkono na Watanzania wote ili iweze kutekeleza mipango yake,” alisema.

No comments: