HALMASHAURI ZAASWA KUTENGA BAJETI ZA VYOO, MAJI SHULENI

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebainisha kuwa halmashauri nyingi za wilaya, miji, manispaa na majiji, hazitengi bajeti ya miundombinu ya ujenzi wa vyoo na mifumo mbalimbali ya maji shuleni.
Kukosekana kwa miundombinu hiyo muhimu, kumesababisha shule nyingi za msingi kuwa na mazingira magumu ya kusomea na utoro kwa wanafunzi shuleni kuongezeka.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Elimu katika wizara hiyo, Profesa Eustella Balalusesa, juzi  mjini hapa kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira  yenye lengo la kuinua kiwango cha afya huo katika kaya na shule za msingi.
Mkutano huo uliwashirikisha maofisa elimu wa mikoa, maofisa afya wa mikoa  na maofisa elimu wa shule za msingi wa halmashauri za wilaya nchini.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo, hali hiyo inarudisha nyuma jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kufikia lengo namba saba la Maendeleo ya Milenia.
Alisema, lengo hilo linalohusu kuhakikisha taasisi zote zikiwemo za elimu kuwa na huduma bora za maji safi na salama  na huduma ya usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuwa na vyoo bora kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015.
“Shule zetu nyingi hazikidhi viwango vinavyokubakika vya matundu ya vyoo, mifumo ya maji safi na salama, na vifaa stahiki vya huduma za maji, afya na usafi wa mazingira  kutokana na kukosa rasilimali, ujuzi au taasisi za kiutendaji zinazojitosheleza, hivyo ni vigumu kufikia malengo husika kwa muda mfupi,” alisema Kamishina huyo.
Mwongozo huo umeibuliwa ili kufikia malengo ya kitaifa kwa awamu, ikimaanisha kwamba matatizo yanayohitaji utatuzi wa haraka yashughulikiwe kwanza.
Alisema kwa kuzingatia jambo hilo, wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi imeingiza kipengele cha kuboresha miundombinu katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
“Wizara inashirikiana na jamii katika kuchangia ujenzi wa vyoo na uvunaji wa maji kwenye shule kwa kupitia kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamishina huyo wa Elimu, hadi sasa jumla ya vyoo bora 110 vimejengwa na vingine kuboreshwa katika shule za msingi na hivyo  kuvuka lengo lililowekwa  lililokuwa kuboresha shule 88 kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Mratibu wa Huduma za Maji Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Theresia Kuiwite, alisema utafiti uliofanyika katika Halmashauri 16 za Tanzania Bara  mwaka 2012 ulibaini kuwa hali ya vyoo na maji kwenye shule za Msingi ni mbaya .
Alisema ni asilimia 11 ndiyo iliyokuwa  na miundombinu ya vyoo vinavyokidhi viwango vya msingi vilivyowekwa na wizara, wakati  asilimia 32 ya shule ndiyo ilikuwa na mifumo ya maji katika sehemu za shule na asilimia 96 ya shule zilikuwa hazina vifaa vya kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu.
Kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi mwaka 2012 na  Rais Jakaya Kikwete, ambapo mikoa 12 na halmashauri 42 zilikuwa kwenye utekelezaji kwa awamu ya kwanza.

No comments: