FENELLA AHIMIZA 'KUWATEMA' WANAOKATAA MUUNGANOWaziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara  amewataka wananchi kusimama imara kutetea Katiba mpya na kuwaacha  watu wanaopandikiza mbegu ya kukataa Muungano.
Alisema hayo jana Dar es Salaam, alipozungumza na wananchi  kwenye maadhimisho ya Siku ya Uanuwai wa Utamaduni Duniani,  ambapo maonesho yanayoambatana na siku hiyo, yalianza kufanyika kuanzia jana hadi Jumapili ijayo.
Alisema Muungano ni moja ya utamaduni wa Tanzania ambao unatakiwa kuenziwa kama ilivyo kwa tamaduni nyingine za Watanzania.
Dk Mukangara alisema Taifa lipo katika mchakato wa kupata Katiba mpya na  uanuwai wa utamaduni unakumbusha kuwa mjadala na mabadilishano ya mawazo vinapaswa kuzingatia usawa na kuheshimiana.
Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu ya ‘Tudumishe amani, tuuenzi Muungano wetu’, ambapo Dk Mkangara alitaka kauli mbiu hiyo itumike kulinda na kuhamasisha watu kuenzi Muungano kwani ni tunu imara katika ulinzi na usalama wa Taifa letu.
Aidha, alitoa mwito kwa watanzania kuendeleza uanuwai wa utamaduni kwa kushiriki katika shughuli za maadhimisho hizo.
“Wajasiriamali wa bidhaa za sanaa wanatakiwa kuzalisha na kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuinu akipato chao, vivyo hivyo kwa wasanii wanatakiwa kukuza vipaji vyao na kuitangaza sanaa ya Mtanzania,’’ alisema Mukangara.

Alisema endapo watanzania wataeneza lugha ya adhimu ya Kiswahili kitaifa na kimataifa, itasaidia kuwa na mila na desturi zinazozingatia maadili mema na kuleta maendeleo.

No comments: