EXIM BANK YAKABIDHI MAABARA YA KOMPYUTA SHULE YA MSINGI KILAKALABenki ya Exim Tanzania imekabidhi maabara ya kompyuta kwa Shule ya Msingi Kilakala iliyopo wilayani Temeke, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya shughuli zake za kijamii katika kukuza uwezo wa maendeleo miongoni mwa vijana nchini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo jana shuleni hapo, Meneja wa Benki ya Exim Tawi la Temeke, Joyce Sinamtwa, alisema msaada huo wa maabara ya kompyuta, unadhihirisha jitihada za benki hiyo katika kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kwa kuwekeza katika rasilimaliwatu bora ya baadaye.
"Mbali na maktaba iliyowekwa mwaka jana, maabara hii ya kompyuta pia itasaidia kuwaletea maendeleo watoto hawa na kuonesha dhamira yetu ya kuwekeza katika viongozi wa baadaye wa Taifa hili. 
“Baadhi ya wanafunzi hawa wana uwezo mkubwa wa kufikiri, lakini wanakosa fursa ya kupata vifaa kama hivi vya kielimu. Benki ya Exim imeamua kuwajengea uwezo zaidi katika kuwafungulia njia wanafunzi hawa ili kukabiliana na changamoto za kimaendeleo hapo baadaye.” Alisema Sinamtwa.
Meneja huyo alisema uongozi wa benki yake unaamini kwamba kwa kuweka maabara hiyo ya kompyuta katika shule hiyo, wanafunzi wengi wataweza kutumia fursa hiyo kuendeleza ujuzi wao na hivyo kuwa wabunifu katika maisha yao ya kielimu na ya kila siku.
Alifafanua kuwa tangu benki hiyo iichukue shule hiyo na kuwa mlezi wake Agosti 2012, shule imekuwa ikipiga hatua zaidi kutokana na misaada mbali mbali iliyotolewa na benki hiyo, ambayo ni pamoja na ukarabati wa miundombinu, kutoa madawati, vitabu na vifaa vingine vya kitaaluma.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kilakala, Abdul Kuratasa alisema, "Ni dhana nzuri ya kuwajengea mazingira mazuri watoto kuwa wataalamu katika sekta ya sayansi na teknolojia na kuendana na mabadiliko ya dunia. Sasa nao pia wana nafasi ya kushindana vilivyo na wanafunzi kutoka shule binafsi. Tunawashukuru Benki ya Exim kwa uwekezaji huu kwa watoto."

No comments: