DEREVA WA DALADALA ADAIWA KUUA MPIGADEBE AKIJIHAMI

Jeshi la Polisi katika Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya linamsaka dereva wa basi dogo la abiria `daladala’ linalofanya kazi kati ya mji mdogo wa Sirari, Tarime na Mugumu wilayani Serengeti akihutumiwa kumuua mpigadebe wa stendi ya Sirari, Chacha Suguta (28).
Dereva huyo, Mokemo Mwita anatuhumiwa kumpiga Suguta kwa bomba kichwani na kumsababishia umauti.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Tarime/Rorya, Justus Kamugisha, tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika eneo la stendi, baada ya kutokea ugomvi baina ya Suguta na Makemo, wakigombea abiria.
Alisema katika ugomvi huo, Suguta ambaye alikuwa mpigadebe maarufu katika stendi ya Sirari, alimshikia kisu dereva wakati wakigombea abiria waendao Mugumu.
Kutokana na hali hiyo, inaelezwa Makemo aliingia ndani ya gari lake na kufunga milango na madirisha, kisha akatokea mlango mwingine na kukimbia akiliacha gari lake, lakini alifuatwa na Suguta huku akiendelea kushikilia kisu.
“Katika kujihami, Makemo aliokota bomba katika eneo la waziba pancha na kumpiga nalo kichwani Suguta ambaye alipasuka kichwa na kuanguka chini. Baadaye alijikongoja hadi polisi kuomba apewe PF3 ili akimbizwe hospitali ya wilaya Tarime, lakini alifariki wakati anapatiwa matibabu,” alisema Kamanda Kamugisha.

No comments: