DC AZUNGUMZIA 'DHAHABU' INAYOFOKA KWA BABU WA LOLIONDOMkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Lali amesema haijathibitishwa kama madini, yanayodaiwa kugundulika Kijiji cha Mgongo huko Samunge kuwa ni dhahabu au la.
Amesisitiza kuwa idadi ya watu wanaofika  wilayani hapo kusaka dhahabu ni ndogo, ikilinganishwa na iliyojitokeza enzi za `Kikombe cha Babu wa Loliondo', Mchungaji Ambilikile Mwaisapile. 
Mkuu wa Wilaya alilazimika kutoa ufafanuzi huo jijini hapa jana,  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, waliotaka kujua je, ni kweli madini hayo yanapatikana juu juu, kama inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Alisema ni kweli madini yamegundulika, lakini haijathibitishwa kama madini hayo ni dhahabu kweli au ni madini ya aina nyingine.
Alisema muda wowote kuanzia sasa, wataalamu wa madini Kanda ya Kaskazini watatoa taarifa juu ya aina ya madini waliyoyagundua. Alisema timu ya wataalamu imeshafika eneo hilo, kuchunguza na kutoa elimu ya uchimbaji wa madini hayo.
Alisema, awali wakati taarifa hizo zilipotoka kuwa madini yanapatikana `nje nje' karibu na mto Mgongo, alifika eneo hilo  akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama  ili kujua kama ni kweli au la.
Lakini, waligundua kuwa madini hayo, si kweli yapo juu juu kama inavyodaiwa, bali waliwakuta wachimbaji wadogo wanaoshi maeneo hayo, wakiwa wanachimba madini hayo pembezoni mwa mto.
Alisema idadi ya watu si kubwa kama inavyodaiwa, bali watu waliopo ni 400 hadi 600  huku asilimia 80  ya watu hao ni wakazi wa Kijiji cha Mgongo, asilimia 10 wanatoka ndani ya Kata ya Samunge, asilimia 5 wanaotoka nje ya wilaya ya Ngorongoro na asilimia 5 wanaotoka ndani ya Wilaya ya Ngorongoro.
Alisema wamejipanga kuhakikisha kuwa huduma muhimu za ulinzi na usalama, zinakuwepo ikiwemo huduma za maji na vyoo.
Alisitiza kuwa ni kweli madini hayo, yapo, lakini bado hayajathibitishwa rasmi kama ni dhahabu au la.
Alitoa rai kwa watu wanaopenda kutoa taarifa, hata kama ni za kweli, wawasiliane na mamlaka husika ili kutoa taarifa za uhakika, badala ya kutoa taarifa wanazozijua wao.

No comments: