DC AHIMIZA MAPAMBANO MAPANA DHIDI YA FISTULAMkuu wa Wilaya ya Pwani, Halima Kiemba, ametoa mwito kwa kila Mtanzania  kujitolea kuwa balozi wa Fistula, ili kuunganisha nguvu katika kupambana na tatizo hilo na kufikia malengo ya kulitokomeza ifikapo 2015. 
Mkuu huyo wa Wilaya alitoa mwito huo juzi, wakati akizindua mafunzo maalum kwa mabalozi 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Fistula Duniani, inayoadhimishwa kila Mei 23.
 “Niwapongeze, Vodacom Foundation kwa kushirikiana na CCBRT pamoja na UNFPA na kuwezesha mafunzo haya ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika katika Wilaya ya Pwani. Tatizo hili limekuwa kikwazo kwa wanawake wengi ndani ya jamii yetu na bado limeendelea kuwepo katika baadhi ya maeneo kutokana na imani zetu,” alisema Kiemba.
 Alisema kunahitajika nguvu katika kupambana na ugonjwa huo na kusisitiza Mtanzania ajitolee kuwa balozi kwa kutoa taarifa katika vituo vya afya, hasa pale anapo gundua eneo alilopo kuna mgonjwa na kuwahimiza wagonjwa wenyewe wajitokeze ili wapate matibabu.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea mabalozi hao uwezo wa kutoa elimu watakaporudi katika jamii zao na kusambaza ujumbe kwamba ‘Fistula Inatibika’ kuelekea kilele cha maadhimisho hayo. 
Juhudi hizo zinaratibiwa duniani kote ambapo watu wameungana katika kutoa elimu siku hiyo  na hapa nchini, sherehe hizo zitafanyika katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
 Naye Mkuu wa Vodacom Foundation, Yesaya Mwakifulefule, alisema wamejipanga kuwafikia akinamama waliopo vijijini ambao wanaamini ugonjwa huu hautibiki kwa kuwaleta mjini  kupata matibabu.
Aidha Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemans amesema kuwa mabalozi wao 500 wamefanya kazi kubwa na inayostahili pongeza kwa kuweza kuwatambua wanawake wenye tatizo la fistula lakini mafunzo haya yanawataka mabalozi wetu 100 wamepiga hatua zaidi kwa kwenda kutoa semina kwenye sehemu zao ambazo zitazinduliwa tarehe 23 nchi nzima.

No comments: