CCM YAGOMA KUWABEMBELEZA WAJUMBE WA UKAWAChama Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza kwamba hakina mpango wa kushawishi viongozi wa Serikali au viongozi wa kitaifa,  wawalazimishe au wawabembeleze wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika juzi.
Nnauye alisema badala yake, CCM kupitia Sekretarieti yake itaendelea kushughulika na wajumbe hao mitaani, kutokana na upotoshaji ambao wamekuwa wakiueneza.
“Watu wenyewe hata kwenye kiganja cha mkono hawajai,” alisema Nape akielezea Mkakati wa CCM kukabiliana na upotoshaji wa Ukawa.
Alisema kama ni theluthi mbili, itapatikana hata bila wao kurudi bungeni na kuwataka waendelee kukaa hukohuko.
Nape alisema Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya CCM kwa kazi inayoifanya ya kujibu uongo unaoenezwa na baadhi ya wajumbe hao wa Ukawa, kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya.
“Tayari tumefanya mkutano Unguja na Pemba iliyokuwa na mafanikio kwa hiyo hatuna sababu ya kuwa na hofu,” alisema.
Mbali na uamuzi huo, Nape pia alisema Kamati Kuu imesikitishwa na baadhi ya watu au vikundi ambavyo kwa makusudi, wamekuwa wakieneza uongo au kupotosha kuhusu mchakato  wa Katiba.
Alisema kwa mujibu wa tathimini iliyofanywa na Kamati Kuu, pamoja na upungufu uliojitokeza, imeridhishwa na jinsi mchakato huo unavyoendelea.
“Kamati Kuu imewapongeza Wazalendo ambao waliendelea kubaki ndani ya Bunge kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuandika Katiba,” alisema.
Alisema Kamati Kuu pia imesikitishwa na baadhi ya wajumbe ambao kwa maneno na vitendo vyao wameonesha hawana nia ya kutunga Katiba, hasa wajumbe wa Ukawa waliokimbia chombo cha kisheria cha kutengeneza Katiba mpya, badala yake wamekimbilia kwa wananchi.
Nape alisema Kamati Kuu inawakumbusha kwamba muda wa kupeleka Rasimu ya Katiba kwa wananchi bado haujafika na sasa si wakati wake.

No comments: