BUNGE FUPI LA BAJETI LEO, KILA WIZARA KUJADILIWA SIKU MOJA TU



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo linaanza kikao chake cha Bajeti, ambapo muda wa kuchangia na kuwasilisha bajeti za wizara mbalimbali, umepunguzwa.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, alisema muda wa kuchangia Bajeti hiyo, umepunguzwa kutoka dakika 10 hadi saba na muda wa uwasilishaji wa bajeti za wizara mbalimbali, pia umepunguzwa.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo, sasa kila wizara itapewa siku moja ya kuwasilisha bajeti yake na kujadiliwa. “Tumepima muda tukaona unatosha,“ alisema.
Kwa mujibu wa Joel, Bunge litaanza kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu leo jioni kuanzia saa kumi baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu na kikao cha kupeana ratiba.
Joel alisema  Bunge hilo pia limeongeza siku za kufanya kazi na litakaa mpaka siku za Jumamosi, lengo likiwa ni kuokoa muda uliopotea.
“Vikao vitaanza saa tatu asubuhi hadi saa nane mchana na kutakuwa na mapumziko, ambapo vitaanza tena saa 10 hadi saa mbili usiku na kwa siku za Ijumaa, vikao vitaanza saa tatu hadi saa saba na Jumamosi vitaanza saa tatu mpaka saa saba,” alisema.
Alisema wabunge wawili wapya, Ridhiwani Kikwete wa Jimbo la Chalinze Mkoa wa Pwani na Godfrey Mgimwa wa Jimbo la Kalenga  Mkoa wa Iringa wataapishwa leo, kabla ya kuanza kwa mkutano wa kawaida. 
Huko Kalenga, Mgimwa aliwashinda wagombea wenzake, Grace Tendega wa Chadema na Richard Minja wa Chausta, kwa kupata kura  22,943 dhidi ya kura 5,800 za Chadema huku Chausta ikiambulia 143.
Ridhiwani  alishinda uchaguzi wa Jimbo la Chalinze kwa kupata kura 20,812, akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa Chadema, Mathayo Torongey aliyepata kura 2,628, mgombea wa CUF, Fabian Skauti aliyepata kura 473 na mgombea wa AFP, Munir Husein aliyeambulia kura 78.
Uchaguzi mdogo wa Kalenga ulifanyika hivi karibuni baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Dk William Mgimwa na Uchaguzi wa Chalinze, ulifanyika  baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Said Bwanamdogo.

No comments: