BOSI WA UNDP DUNIANI ATAKA UKAWA WARUDI BUNGENI



Kiongozi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Helen Clark, ameshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kurejea kujadili katika bunge hilo.
Akijibu swali la waandishi wa habari jana, Clark ambaye ndiye kiongozi wa Shirika hilo duniani, aliwataka Ukawa kutumia fursa ya Bunge Maalumu la Katiba kuipa nchi Katiba bora, badala ya kuyumbisha mchakato kwa kususia vikao vyake.
Alisema Katiba bora inawezekana kwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu, kinyume cha hapo ni kudhoofisha nia njema ya Serikali ya kupatikana kwa Katiba mpya, akijibu maswali ya waandishi wa habari aliokutana nao jana Dar es Salaam ili kutoa tathimini ya ziara yake ya siku nne nchini.
Clark ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand, katika mkutano huo na waandishi wa habari wa kutoa tathimini ya ziara yake ya siku nne nchini, aliisifu Tanzania kuwa ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kupigiwa mfano, huku akiitakia kila la kheri katika mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kususia vikao vyake, Clark alionekana kushangazwa, lakini akatumia fursa hiyo kushauri kundi hilo lililojitenga, kuunganisha nguvu ili kuipa nchi Katiba bora.
Alisema Bunge Maalumu la Katiba ni mahali pekee ambako wazalendo wa kweli wanaweza kujenga hoja nzito kwa lengo la kuhakikisha inapatikana Katiba bora.
“Kwa maoni yangu kama ninayoyasikia ya kuwepo kwa kundi lililotoka nje ya Bunge la Katiba ni kweli, nawashauri wabadilishe msimamo; kazi ya kutunga Katiba inapaswa kuwa na wigo mpana, si wa makundi.
Kauli ya Clark, kiongozi anayeshika nafasi ya tatu kicheo katika Umoja wa Matifa baada ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, imekuja wakati kundi la Ukawa likiwa limetangaza kuendelea kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba hata litakaporejea tena Agosti 5, mwaka huu kwa awamu ya pili ya mchakato wa Katiba mpya baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kuongeza siku 60 zaidi.
Awali, wajumbe hao walikutana kwa siku 70, lakini mchakato wake ulisuasua kutokana na mivutano ya mara kwa mara, hasa kutoka kundi la Ukawa linaloundwa na baadhi ya viongozi wa Kambi ya Upinzani na wafuasi wachache, kutoka katika kundi maalumu la watu 201 walioteuliwa na Rais kwa ajili ya Bunge hilo. 
Aidha, Clark alitumia nafasi hiyo kuelezea kufurahishwa kwake na jinsi Tanzania inavyoendesha uchaguzi katika nafasi mbalimbali za uwakilishi kwa ufanisi, hata baada ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi.
“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika hili. Katika uchaguzi uliofanyika mara nne ndani ya mfumo wa vyama vingi, hakujatokea tatizo la viongozi kushindwa kuheshimu ukomo wa madaraka unaotajwa katika Katiba. Nawapongeza sana viongozi wa Tanzania kwa kusimamia hili,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema kama kweli Clark, ana nia ya kutoa ushauri kwao, asingetoaushauri kwa waandishi wa habari ambao ni mtu wa tatu, kwa kuwa kwanza hana hakika kama ni ushauri sahihi au umechakachuliwa.
Pili alisema angetarajia Clark kama kweli anataka kutafuta suluhu, asikilize malalamiko ya anaotaka kuwasuluhisha, ndio atoe ushauri badala ya kutoa ushauri kama alivyofanya. 
Katika ziara yake, Clark pia alikutana pia na Rais Kikwete na kumpongeza kwa juhudi anazofanya katika kupiga vita ujangili.
"Tunashirikiana kwa karibu na Rais Kikwete katika suala hili la ujangili, lengo ni kuona hatimaye tunafanikiwa katikla vita hii,” alisema Clark ambaye akiwa nchini alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Mkuu huyo wa UNDP ameendelea kuzitaka serikali duniani kote, kuongeza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na biashara haramu ya bidhaa za wanyamapori, kama meno ya tembo.
Alisema uhalifu unaotokana na biashara ya meno ya tembo, una madhara makubwa kwa watu wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi zinazoendelea kwa kuliibia Taifa utajiri wake, kuharibu maliasili kwa ajili ya kizazi kijacho, kuchochea uhalifu, rushwa na kudhoofisha usalama wa jamii na Taifa.
"Vitendo hivi vya uhalifu vinawaweka wanawake, watoto na wengine katika hali ya umasikini na maisha magumu na yaliyo na hatari," alisema.
Clark alisema sheria zenye nguvu na zinazotekelezeka zinahitajika, ili kupunguza mahitaji ya bidhaa haramu za wanyamapori na jamii kufanya shughuli za kujiimarisha na kujipatia kipato Tanzania na nchi zingine zenye tembo na wanyamapori.
Alisema shirika lake limejizatiti kusaidia juhudi za kupambana na biashara ya wanyamapori kwa kusaidia utawala bora, utekelezaji wa Sheria, kupunguza umasikini na kulinda mazingira kwa kushirikiana na serikali na washirika wengine.
Kiongozi huyo wa UNDP ameelezea kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na kuwaandaa wanawake, vijana na walemavu kwa fursa zaidi za uongozi, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho.
“Tanzania ipo mstari wa mbele katika ahadi ya kuboresha ushiriki katika siasa kwa makundi yaliyotengwa kutokana na dhamira ya vyama vya siasa kufanya hivyo katika uteuzi wa wagombea kuelekea uchaguzi wa mwaka ujao (2015),” alisema na kuelezea alivyofurahishwa kukutana na wabunge wanawake mjini Dodoma, wakiongozwa na Spika Anne Makinda.
Alisema kutokana na dhamira ya kutaka kuona uchaguzi wa mwaka kesho nchini unafanikiwa, UNDP imetenga dola za Marekani milioni 22 (sh bilioni 35.8) kwa ajili ya kuunga mkono utoaji elimu kwenye uchaguzi mkuu ujao. 
Alisema fedha hizo zitatolewa chini ya Mradi wa Uchaguzi unaoendeshwa na shirika lake. Alisema shirika lake limepokea maombi kutoka vyama vya siasa kuomba kuungwa mkono hususani kwenye suala la elimu, kujenga uwezo na uhamasishaji katika shughuli za uchaguzi mkuu ujao. 
Alisema fedha hizo zitajikita katika kuelimisha na kuhamasisha wanawake na vijana kujihusisha kwenye mchakato wa uchaguzi huo hususani kugombea nafasi za uongozi. 
Kiongozi huyo wa UNDP, alipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikia katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya millennia; hasa malengo namba moja, sita na saba. 
Alisema pia Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika juhudi za kutokomeza umasikini, kuimarisha afya kwa watoto na kuwezesha watoto kuendelea na masomo hadi sekondari. 

No comments: