BENKI YA POSTA YASAIDIA SHULE MAGOLEBenki ya Posta Tanzania (TPB) Tawi la Morogoro, imetoa msaada wa madawati 32 yenye thamani ya Sh milioni tano kwa Shule ya Msingi Magole iliyopo wilayani  Kilosa baada ya madawati mengi kuharibiwa na mafuriko.
Meneja wa Benki ya TPB Tawi la Morogoro, Fumbuka Ng'onge, alikabidhi msaada huo juzi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Magole.
Meneja huyo alisema uongozi wa benki hiyo, umeguswa baada ya kupata taarifa ya  maafa yaliyowakuta wakazi wa Tarafa ya Magole, yaliyotokana na mafuriko hayo ya mvua  ambayo pia yaliharibu miundombinu, yakiwemo majengo ya Shule ya Msingi  Magole.
"Uongozi na wafanyakazi wa Benki ya Posta unatoa pole kwenu  wananchi wa Magole na uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kilosa ...katika kufanya hivyo tumeona tutoe msaada kwa upande wa shule ya msingi kwa madawati 32 yenye thamani ya Shilingi milioni tano na leo tunayakabidhi,"  alisema Meneja huyo.
Alisema licha ya kutoa huduma za kibenki,  Benki ya Posta  imeendelea kuwa karibu na wananchi  siku zote kwa kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwemo sekta ya elimu.
Kwa upande wake, baada ya kupokea msaada huo, Tarimo aliishukuru Benki ya Posta Tanzania na kusema msaada huo ni mkubwa na umepunguza uhaba wa  madawati katika shule hiyo.
Awali, Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Kilosa, Chidelinga Julius, aliwasihi walimu wa shule hiyo kuwa wavumilivu na kufundisha kwa bidii baada ya kupatiwa majengo ya Shule ya Sekondari Magole, kwa vile jambo hilo ni la mpito.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Colletha Mahululu aliishukuru Benki ya Posta kwa msaada wa madawati hayo.
Alisema bado idadi kubwa ya wanafunzi, wanaketi sakafuni na kubanana wanafunzi watatu hadi wanne kwenye dawati.

No comments: