BENKI 19 ZATOA MIKOPO YA NYUMBA KWA MIAKA 15

Serikali imesema jumla ya benki 19 zinatoa mikopo ya nyumba kwa miaka 15 hadi 20, tofauti na benki 10 zilizokuwa zikitoa mikopo ya nyumba kwa kipindi kisichozidi miaka 15.
Aidha, imesema Mfuko wa Mikopo Midogomidogo ya Nyumba umeanza kwa mtaji wa Dola za Marekani milioni tatu (zaidi ya Sh bilioni nne).
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema hayo juzi usiku bungeni wakati akiwasilisha bajeti yake ya mwaka 2014/15.
Profesa Tibaijuka alisema mkataba wa mkopo wa Tanzania Housing Finance ulirejewa upya ili kuipata Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company.
Alisema kampuni hiyo iliwezeshwa kutoa mikopo ya nyumba au mitaji kwa benki za biashara ili nazo zitoe huduma ya mikopo ya nyumba kwa wananchi hata kama benki hizo hazijaanza kutoa mikopo kwa wananchi wanaonunua nyumba.
“Hadi Aprili, 2014, jumla ya benki 19 zinatoa mikopo ya nyumba kwa miaka 15 hadi 20, tofauti na benki 10 zilizokuwa zikitoa mikopo ya nyumba kwa kipindi kisichozidi miaka 15,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema katika mwaka wa fedha 2014/15, wizara yake itatoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa mikopo ya nyumba, ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wa mkopaji na mkopeshaji kwa mujibu wa sheria.

No comments: