BALOZI WA MALAWI KUZIKWA LEO JIJINI BLANTYRE



Balozi wa Malawi nchini Tanzania aliyefariki ghafla Ijumaa iliyopita jijini Dar es Salaam, Flossie Gomile-Chidyaonga, anatazamiwa kuzikwa leo katika jiji alilozaliwa la Blantyre, Malawi. 
Mwili wa Balozi huyo uliyosafirishwa na Serikali ya Tanzania, uliwasili jana saa 5:45 mchana (kwa sasa za Tanzania) katika kiwanja cha ndege cha Chileka, Blantyre na kupokelewa na Rais wa Malawi, Dk Joyce Banda aliyelazimika kukatisha kampeni za kugombea urais ili kushiriki katika tukio hilo la majonzi. 
Kulikuwa na mamia ya ndugu na marafiki waliofika katika uwanja huo wa kimataifa ili kumpokea mpendwa wao. Malawi inafanya uchaguzi mkuu Mei 20 ambapo Rais Banda anakabiliwa na upinzani wa wagombea urais wengine 11.
Akiongea katika hafla fupi ya kupokea mwili wa Balozi huyo, Rais Banda alimshukuru Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kwa kuchukua jukumu la kusafirisha mwili wa Chidyaonga hadi nyumbani na kuonesha ushirikiano mkubwa.
“Rais Kikwete alinipigia simu baada ya kupata habari za msiba. Tena hakuwa nchini mwake lakini akaonja ni vyema anijulishe. Nilimwambia basi tutafanya utaratibu wa kuleta mwili wa balozi nyumbani, lakini akasema hilo litakuwa jukumu lake,” alisema na kumshukuru kwa niaba ya wana Malawi.
Alisema Balozi Chidyaonga ndiye aliyemshawishi kuhudhuria katika sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar akimwambia ilikuwa ni muhimu ashiriki sherehe hizo akiwa kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Naye Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema katika hafla hiyo kwamba Watanzania wanaungana na wenzao wa Malawi kuombeleza msiba huo wa gahfla wa Balozi Chidyaonga ambaye alimuita kuwa ni ‘Malkia wa Amani’.
“Alikuwa Malkia wa Amani na mchapakazi. Baada ya Mkutano wa SADC, Balozi Chidyaonga aliendeleza mijadala mingi ya amani bila kuchoka,” alisema Waziri Membe na kuahidi kwamba ujumbe wa Rais Kikwete kwa Wamalawi utasomwa leo wakati wa mazishi.
Naye kiongozi wa familia ya balozi huyo, Andrew Machinjire, aliishukuru Tanzania kwa kuchukua jukumu la kutoa ndege ya serikali ili kusafirisha mwili wa balozi huyo.
“Kwa kweli Tanzania imeonesha kwamba siyo tu ni jirani mwema, bali ndugu wa karibu na mwenye upendo,” alisema.  

No comments: