BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI

HOTUBA YA WAZIRI WA UCHUKUZI, MHE. DKT. HARRISON G. MWAKYEMBE (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015

1.0       UTANGULIZI


1.     Mheshimiwa Spika, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuchambua bajeti ya Wizara ya Uchukuzi na kuweka mezani taarifa ya Kamati mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba sasa Bunge lako likubali kupokea, kujadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2014/2015.
2.   Mheshimiwa Spika, naomba hotuba nzima ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2014/2015 iingizwe yote kwenye kumbukumbu rasmi za bunge na uniruhusu niwasilishe muhtasari tu unaobeba maudhui ya hotuba nzima. Vitabu vya Hotuba yangu na andiko maalum la ukanda wa kati (The Central Corridor: A Wider Concept Note) vimesambazwa kwa waheshimiwa Wabunge.  

3.        Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia zawadi ya uhai na kutuwezesha kukutana tena kujadili utendaji wa Sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa kwa mwaka 2013/2014 na mipango ya Sekta hizo kwa mwaka 2014/2015 kwa maendeleo ya Taifa letu.

4.   Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha hoja ya Wizara yangu, naomba niungane na Wabunge wenzangu kuwalilia Wabunge wenzetu waliotutangulia mbele za haki. Ninaomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao peponi. Aidha, nawapongeza Wabunge wapya waliojiunga nasi kwenye Mkutano huu wa Bunge. 



5.                          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii vilevile kuwapa pole wananchi wa jimbo la uchaguzi la Kyela kwa mafuriko makubwa yaliyoikumba Wilaya ya Kyela na kuwashukuru kwa kunipa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo ya Jimbo na Taifa kwa ujumla. Naomba tuendelee kushirikiana katika kipindi hiki kigumu ili kurudisha hali ya miundombinu yetu ya kiuchumi na kijamii iliyoharibiwa na mafuriko hayo.

6.            Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa naomba kumpongeza Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msukumo alioutoa katika kuanzisha na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Programu ya Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN) ambayo imechochea mabadiliko makubwa katika kuufungua Ukanda wa Kati wa Uchukuzi kwa kutekeleza miradi ya reli, bandari na barabara. Waheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nao nawapongeza kwa uchapakazi na uongozi wao thabiti wa mfano uliotutia nguvu na matumaini katika kufikia malengo ya BRN.



7.   Naomba nimalizie Mheshimiwa Spika, kukupongeza wewe na uongozi mzima wa Bunge kwa kazi nzuri mnayoifanya. Vilevile naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Mjini na Makamu wake Mhe. Prof. Juma Athuman Kapuya, Mbunge wa Urambo Magharibi kwa kuendelea kunipa ushirikiano mimi na viongozi wenzangu wa Wizara katika kuiongoza Wizara ya Uchukuzi. Ushirikiano na ushauri wao umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha utendaji wa sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa.  Binafsi nina imani kubwa na Kamati na naichukulia kama think tank ya Wizara. Ninaihakikishia Kamati hii kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa lengo la kuendeleza Sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa. 



8.   Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi ya utangulizi, napenda kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu taarifa ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa kwa mwaka 2013/2014 na mipango ya mwaka 2014/2015.

2.0 HALI YA UTENDAJI NA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA WIZARA KWA MWAKA 2013/2014 NA MALENGO YA MWAKA 2014/2015




9.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara iliidhinishiwa bajeti ya Shilingi bilioni 529.41. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 420.52 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shilingi bilioni 108.88 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Fedha za maendeleo zinajumuisha Shilingi bilioni 252.68 fedha za ndani na Shilingi bilioni 167.84 fedha za nje. Hadi kufikia Aprili, 2014 Wizara ilikuwa imepokea fedha za maendeleo Shilingi bilioni 201.21. Kati ya fedha zilizopokelewa, Shilingi bilioni 180.13 ni fedha za ndani sawa na asilimia 71.29 na Shilingi bilioni 21.08 ni fedha za nje sawa na asilimia 12.56. Kwa kuzingatia mwenendo huo wa upatikanaji wa fedha ni dhahiri kuwa sehemu kubwa ya utekelezaji wa Bajeti umefanywa kwa fedha za ndani.

 








2.1       UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW – BRN)




10.                 Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa katika mwaka 2013/2014 Wizara yangu iliteuliwa kuwa moja kati ya Wizara sita kuanza kutekeleza Programu ya BRN. Katika kipindi hicho, Wizara imepata mafanikio na kufanya maandalizi yote muhimu katika kufikia malengo ya BRN. Wizara itaendelea kutekeleza miradi ya reli na bandari na kufikia malengo ya BRN katika mwaka 2014/2015.



2.1.1  BANDARI

11.                 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bandari katika mwaka 2013/2014, Mamlaka imekamilisha majadiliano na Benki ya Dunia wakishirikiana na TradeMark East Africa (TMEA) na Idara ya Serikali ya Uingereza ya Maendeleo ya Kimataifa  (DFID) ili kupata fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi wa kupanua na kuchimba lango la kuingilia na kutokea meli katika bandari ya Dar es Salaam. Nilibainisha kuwa Mradi huu utatekelezwa sambamba na uboreshaji wa gati namba 1-7. Kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2014 na kukamilika mwezi Agosti, 2016. Aidha, kazi za uchimbaji na upanuzi wa lango la bandari ya Dar es Salaam zinatarajiwa kuanza mwezi Agosti, 2015 na kukamilika mwezi Agosti, 2016.



12.                 Mheshimiwa Spika, miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kwa lengo la kuboresha utendaji wa Bandari ya Dar es salaam ni pamoja na: ujenzi wa jengo lenye ghorofa 35 (one stop center building) la kuwaweka pamoja wadau muhimu wanaotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam, ambalo hadi Mei, 2014 lilikuwa tayari na ghorofa 26 zilizojengwa na kazi inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2015; kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kuwaunganisha pamoja watoa huduma kwa njia ya mtandao (Electronic Single Window System) mwezi Aprili, 2014 na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2014; kuanza kuweka (installation) mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao (Electronic Payment System) ifikapo mwezi Juni, 2014 na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2014.



13.                 Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupunguza msongamano bandarini, Mamlaka imepata maeneo kwa ajili ya kutumiwa katika shughuli za kibandari ikiwa ni pamoja na vituo vya kupokelea na kuhifadhia mizigo kwa muda kwa nchi jirani za DR Congo, Burundi, Rwanda, Uganda na Zambia. Maeneo hayo ni pamoja na eneo lenye ukubwa ekari 132 linalomilikiwa na Jitegemee Trading Co. Ltd lililopo katika bonde la mto Msimbazi na eneo lenye ukubwa wa ekari 39 lililopo Kiwalani linalomilikiwa na TAZARA. Mamlaka vilevile kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, inaanzisha mradi wa maegesho ya magari makubwa ya mizigo eneo la Kurasini linalomilikiwa na Manispaa ya Temeke lenye ukubwa wa ekari 7.5. Aidha, Mamlaka ya Bandari ipo katika hatua za mwisho kupata eneo la Katosho na Kibirizi mkoani Kigoma. Vilevile, taratibu za kupata maeneo mengine zinaendelea.



14.                 Mheshimiwa Spika, utendaji wa Mamlaka ya Bandari umeendelea kuwa bora kama inavyooneshwa katika viashiria mbalimbali vya utendaji. Muda wa meli kukaa bandarini (Ship Turnround Time) umepungua kutoka wastani wa siku 6.3 mwaka 2012 hadi wastani wa siku 4.8 mwaka 2013; muda wa Makasha kukaa bandarini (Dwell time) umepungua kutoka wastani wa siku 9.6 mwaka 2012 hadi wastani wa siku 9.3 mwaka 2013. Uwezo wa bandari wa kupakua magari (Roll On Roll Off capacity) kwa kila shifti moja ya saa 8 uliongezeka na kufikia magari 671 Desemba, 2013 ikilinganishwa na magari 400 Desemba, 2012. Mwezi Februari, 2014 ulisainiwa mkataba wa wadau wote wa Bandari kuanza utaratibu wa utoaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam kwa saa 24 kwa siku zote na Mamlaka ya Bandari tayari inatekeleza utaratibu huo. Benki mbili, NMB na CRDB, tayari zimehamishia huduma za kibenki ndani ya bandari na ni matarajio ya Wizara kuona benki zingine zikifanya hivyo.



15.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015 Mamlaka ya Bandari itaendelea na utekelezaji wa miradi iliyoainishwa katika Programu ya BRN. Miradi hiyo ni: uboreshaji wa Gati Na. 1-7, uongezaji wa kina na upanuzi wa lango la Bandari ya Dar es salaam, ujenzi wa kituo cha kuhudumia mizigo Kisarawe, mradi wa kuwaunganisha wadau pamoja kwa njia ya elektroniki, kuweka mfumo wa ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka (scanning), kuboresha barabara na reli za kuingia na kutoka bandarini, kuongeza nafasi ya kuhudumia mizigo kwa kuhamisha maghala yaliyopo Bandarini na kukamilisha ujenzi wa jengo la bandari (one stop center).



2.1.2. RELI



16.                 Mheshimiwa Spika, kwa upande wa miundombinu ya reli, ujenzi wa madaraja matatu umekamilika. Ujenzi wa daraja lililopo kati ya stesheni za Bahi na Kintinku ulikamilika Novemba, 2013 na ujenzi wa madaraja mawili yaliyopo km 303 na km 293 kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe ulikamilika kwa kiwango cha kuweza kupitika kuanzia Machi, 2014. Kukamilika kwa madaraja haya kumeongeza uhakika na usalama wa huduma ya usafiri wa reli ya Kati ambao kwa nyakati tofauti ulikuwa ukikwamishwa kutokana na ubovu na uchakavu wa madaraja hayo.



17.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia kugharamia mradi wa kuinua uwezo wa madaraja yaliyo chini ya tani 15 kwa ekseli ili kufikia tani 25 kwa ekseli kati ya Dar es Salaam na Isaka. Mshauri mwelekezi atakayefanya kazi ya uthamini na usanifu wa madaraja yote yaliyo katika reli ya kati ili yawe na uwezo wa kubeba mzigo wenye uzito wa tani 25 kwa ekseli amepatikana. Aidha, katika mwaka 2014/2015 ujenzi madaraja 16 kati ya madaraja 25 yaliyo katika hali mbaya kati ya stesheni za Dar es Salaam na Tabora utaanza. 

18.     Mheshimiwa Spika, mradi wa kutandika reli za ratili 80 kwa yadi kati ya stesheni za Kitaraka na Malongwe urefu wa km 89 umekamilika na matengenezo ya eneo la reli kati ya Kilosa na Gulwe lililoathiriwa vibaya na mafuriko, nayo yamekamilika. Kukamilika kwa ujenzi wa njia ya reli kati ya stesheni za Malongwe na Kitaraka nilikoelezea hivi punde, kunafanya reli zilizotandikwa zenye uzito wa ratili 80 kwa yadi kati ya Dar es Salaam na Tabora kufikia jumla ya km 527. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na utandikaji wa reli za uzito wa ratili 80 kwa yadi kati ya stesheni za Igalula na Tabora (km 37) na maeneo mbalimbali kati ya stesheni ya Dar es Salaam na Munisagara (Km 283). Faida ya kuwa na reli nzito ni pamoja na kupunguza ajali za treni, kuongeza mwendokasi na uwezo wa treni kubeba mizigo.



19.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu tatizo la kujaa mchanga kwenye makaravati yaliyopo kati ya stesheni za Gulwe na Godegode kila mara mvua inaponyesha, Serikali imechukua hatua zifuatazo ili kudhibiti hali hiyo:

·               Ujenzi wa daraja na miundombinu mingine ya kuepusha kujaa kwa mchanga karibu na karavati lililopo Km 349/450c. Rasimu ya mkataba wa Mshauri Mwelekezi atakayefanya usanifu wa kina wa mradi huo ndani ya mwaka ujao wa fedha, imewasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushauri;

·               Kufanya usanifu na ujenzi wa mabwawa mawili makubwa ya kupunguza kasi ya maji maarufu kama “punguza”. Bwawa la kwanza litajengwa sehemu ya Kimagai karibu na stesheni ya Godegode na bwawa la pili litajengwa karibu na stesheni ya Msagali kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015: na

·               Shirika la Maendeleo la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Serikali kupitia mradi wa Tanzania Intermodal Rail Project (TIRP) litatuma timu ya wataalam mwezi Julai mwaka huu kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la uharibifu wa mara kwa mara wa miundombinu ya reli kutokana na mvua kati ya stesheni za Kilosa na Gulwe.



20.                 Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014, Wizara ilipanga kuanza maandalizi ya kuunda Mfumo wa Kusimamia na Kufuatilia Mizigo na Vyombo vya Uchukuzi (Cargo Tracking & Management System). Napenda kutoa taarifa kuwa, awamu ya kwanza ya usambazaji wa mfumo huu itaanza mwaka 2014/2015. Kukamilika kwa mfumo huu kutarahisisha ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu za kiutendaji kuhusu wingi wa shehena, usalama wake, mwendo wa vyombo vya uchukuzi wa shehena (pamoja na treni) na usalama wake.



21.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu uboreshaji wa huduma za reli, Serikali imefanya maandalizi yafuatayo:

·      Ununuzi wa vichwa vipya vya treni 13. Mkataba wa manunuzi ulisainiwa Aprili, 2013 na malipo yote yamefanyika. Vichwa hivyo vinatarajiwa kuanza kuwasili nchini Desemba, 2014;

·      Ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria. Mkataba ulisainiwa Machi, 2013 na malipo yote yamefanyika. Mabehewa hayo yanatarajiwa kuanza kuwasili nchini mwishoni mwa Septemba, 2014;

·      Ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo. Mkataba ulisainiwa Machi, 2013 na malipo ya awali yalikamilika Februari, 2014. Malipo ya mwisho yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Juni, 2014 na mabehewa hayo 274 yataanza kuwasili nchini Septemba, 2014;

·      Ununuzi wa mabehewa 34 ya breki ulisainiwa Machi, 2013 na malipo yote yamekamilishwa. Mabehewa hayo yanatarajiwa kuanza kuwasili nchini mwezi Julai, 2014;

·      Ununuzi wa mabehewa 25 ya kubebea kokoto. Malipo yote yamekamilika na mabehewa hayo yanatarajiwa kuanza kuwasili nchini Julai, 2014;

·      Kujenga upya vichwa vinane vya treni. Kazi ilianza Machi, 2013 kwenye karakana yetu ya Morogoro na hadi kufikia Aprili, 2014 vichwa vitatu vilikuwa vimekamilika. Vichwa vitano vilivyobaki vinatarajiwa kukamilika kufikia Septemba, 2014.



22.                 Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza miradi ya reli chini ya BRN, kwa mwaka 2013/2014 Wizara iliidhinishiwa bajeti ya maendeleo ya Shilingi bilioni 165.68. Hadi kufikia Aprili 2014, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi bilioni 145.08 sawa na asilimia 88 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi. Napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali kwa kuweka kipaumbele katika utoaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya BRN.



23.                 Mheshimiwa Spika, Katika mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015, Serikali imetenga shilingi bilioni 126.9 chini ya Mpango wa BRN kwa ajili ya kuunda upya vichwa vya treni vingine nane; kununua mabehewa mengine mapya ya mizigo 204; kununua vichwa vingine vya treni vipya 11 na kuendelea na matengenezo ya njia ya reli ya kati yenye mtandao wa urefu wa km 2,707.

 


2.2       HUDUMA ZA UCHUKUZI KWA NJIA YA NCHI KAVU


2.2.1       Usafiri na Uchukuzi kwa Njia ya Barabara




24.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Sekta ya usafiri na uchukuzi kwa njia ya barabara imeendelea kuimarika na kutoa mchango wake katika kutekeleza shughuli za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo. SUMATRA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imeendelea kuchukua hatua kukabiliana na matukio ya ajali barabarani. Hatua hizo ni pamoja na kununua vifaa kwa ajili ya kupima ulevi na mwendo kasi na kuvikabidhi kwa Jeshi la Polisi. Hatua nyingine ni kusimamisha leseni za mabasi yaliyohusika katika matukio ya ajali ambapo katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Machi, 2014, jumla ya leseni 34 za usafirishaji wa abiria zilisimamishwa na wamiliki wa mabasi walitakiwa kuwasilisha kwa maandishi mpango utakaotumika katika kudhibiti ajali za barabarani. Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo ili kupima matokeo na mafanikio yake. 



2.2.2       Huduma za Usafiri na Uchukuzi Mikoani na Vijijini




25.                 Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia SUMATRA imeendelea kuruhusu aina mbalimbali za usafiri kama vile pikipiki za magurudumu mawili na matatu, magari aina ya Noah n.k. Hatua hizo zinaenda sambamba na ukaguzi wa kushtukiza wa vyombo vyote vya usafiri, kutoa nauli elekezi, na kutoa elimu, mafunzo na ushauri kwa watumiaji na watoaji wa huduma za usafiri wa barabara. Aidha, Wizara imeendelea kushirikiana na wasafirishaji wa abiria na mizigo kupitia vyama vyao ili kuboresha huduma za uchukuzi wa barabara. 

2.2.4       Huduma za Usafiri wa Reli Jijini Dar es Salaam




26.                 Mheshimiwa Spika, huduma za usafiri wa reli katika Jiji la Dar es Salaam kati ya stesheni za Dar es Salaam hadi Ubungo Maziwa na Mwakanga hadi Kurasini zimeendelea kukua na kupendwa na wananchi. Kampuni ya Reli (TRL) ilisafirisha abiria 1,343,763 katika mwaka 2013 ikilinganishwa na abiria 230,009 waliosafirishwa katika mwaka 2012. Aidha, kwa upande wa TAZARA, abiria 1,460,506 walisafirishwa katika mwaka 2013 ikilinganishwa na abiria 148,524 waliosafirishwa katika mwaka 2012. Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma hii ikiwemo mpango wa kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye usafiri wa treni Jijini.  Mikakati hiyo inalenga kuongeza eneo la ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa usafiri jijini kutoka umbali wa kilometa 20 za sasa hadi kilometa 50 ili kujumuisha wilaya za Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Bagamoyo. Kuhusu uwekezaji katika usafiri wa treni Jijini Dar es Salaam kwa utaratibu wa PPP, kampuni kadhaa za ndani na nje ya nchi zimeonyesha ari ya dhati. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na TRL na RAHCO inaangalia uwezekano wa kuanzisha kampuni tanzu ya kutoa huduma za usafiri wa reli mijini ambayo itatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki.  Katika mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa njia mpya za reli Jijini Dar es Salaam zikiwemo zile za kwenda maeneo ya Pugu, Mbagala/Chamazi, Luguruni/Kibaha na Bunju/Kerege.



2.3       Usafiri na Uchukuzi kwa Njia ya Reli




27.                 Mheshimiwa Spika, licha ya sekta ya reli kukabiliwa na changamoto mbalimbali, miundombinu na huduma za reli zimeendelea kuboreshwa ili ziendelee kuchangia katika pato la Taifa na kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi kwa kupitia njia ya reli. Mwelekeo uliopo katika sekta ya uchukuzi ni kuhakikisha kuwa mizigo mizito na mingi inayosafirishwa umbali mrefu inatumia usafiri wa reli.

28.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, mshauri mwelekezi (Kampuni ya COWI kutoka Denmark) alianza kazi ya usanifu wa uboreshaji wa njia ya reli ya Tanga – Arusha (km 438) Septemba, 2013 na anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Julai, 2014. Mshauri mwelekezi (Kampuni ya H.P. Gauff kutoka Ujerumani) alianza kazi ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli mpya ya Arusha – Musoma (km 660) Septemba, 2013. Kazi hii inatarajiwa kukamilika Septemba, 2014. Aidha, katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 7.55 kwa ajili ya kukamilisha kazi ya kufanya usanifu wa ujenzi wa reli ya Tanga – Arusha; kukamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa reli mpya kati ya Arusha – Musoma pamoja na matawi ya kwenda Engaruka na Minjingu; kukarabati njia ya reli ya Tanga hadi Arusha na kufanya usanifu wa kina wa kuinua kiwango cha reli itakayounganisha reli ya kati na ile ya kaskazini (yaani Tanga-Arusha), kutokea stesheni ya Ruvu Junction hadi Mruazi kuwa katika kiwango cha kimataifa na kuunganisha reli ya Mruazi na Bandari ya Mbegani, Bagamoyo.



29.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu ulipaji fidia kwa wakazi wa eneo la Mwambani-Tanga ili kupisha ujenzi wa sehemu ya kupanga mabehewa na kugeuzia (marshalling yard), jumla ya wakazi 607 kati ya 619 wamekwisha lipwa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 4.7. Aidha, hadi Aprili, 2014 hundi 187 kati ya 188 za fidia ya makaburi zilikuwa zimelipwa.  Hundi 13 zenye thamani ya shilingi milioni 231.4 bado hazijachukuliwa kutokana na zuio la mahakama au wahusika kutojitokeza.



30.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, kazi ya ukarabati wa tuta la reli linalokatiza mto Ugala pamoja na daraja lake ilifanywa na Kampuni ya R & A Works Ltd na kukamilika Oktoba, 2013. Aidha, kazi ya kuondoa reli nyepesi na zilizochakaa zenye uzito wa ratili 45 kwa yadi na kuweka reli zenye uzito wa ratili 56.12 kwa yadi kwa umbali uliobaki wa km 4.59 kati ya 9 zilizobainishwa kuhitaji ukarabati wa haraka kati ya sehemu ya Lumbe - Mto Ugala - Katumba ilikamilika Februari, 2014. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuendelea na matengenezo ya njia ya reli kati ya Kaliua - Mpanda, kufanya usanifu wa kina wa uboreshaji wa njia ya reli kati ya Kaliua – Mpanda kuwa kiwango cha kimataifa na kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli mpya ya kutoka Mpanda hadi Karema.



31.                 Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikiana na Serikali za Rwanda na Burundi katika uendelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya Dar es salaam – Isaka – Keza - Kigali (Km 1,464) na Keza – Musongati (km 197) kwa kiwango cha kimataifa. Mshauri mwelekezi, Kampuni ya CANARAIL kutoka Canada alikamilisha kazi ya kufanya upembuzi wa kina Februari, 2014. Serikali inaendelea na juhudi zake za kupata wawekezaji/fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya hiyo. Aidha, Machi, 2014 Serikali za Tanzania na Burundi zilitiliana saini ya Makubaliano ya Awali (MoU) ili kuendeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kutoka Uvinza hadi Musongati.  



32.                 Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu wa kina wa kuinua kiwango cha reli ya Isaka - Mwanza ilianza Septemba, 2013 na inatarajiwa kukamilika Julai, 2014. Aidha, Halmashauri ya Jiji la Mwanza imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 148 sehemu ya Buhongwa kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya kupanga mabehewa na kugeuzia treni (marshalling yard). Mshauri mwelekezi anayefanya tathmini ya ulipaji fidia anaendelea na kazi. Vilevile, katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina wa kuinua kiwango cha njia ya reli kati ya Tabora – Kigoma na kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli za kutoka Uvinza hadi Musongati.



33.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa reli ya Mtwara – Songea – MbambaBay na michepuko ya kwenda Mchuchuma na Liganga, Mtaalam mwelekezi wa kufanya kazi hii ameshapatikana. Mkataba wa kutekeleza kazi hii utasainiwa wakati wowote kabla ya mwisho wa Juni, 2014 na kazi hiyo ya usanifu itakamilika baada ya miezi 12.



34.                 Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kituo cha kupakua na kupakia makasha (ICD) cha Mwanza ulikamilika Desemba, 2013. Kituo hicho kimepata mwendeshaji Kampuni ya Transpark Ltd. Kukamilika kwa kituo hiki pamoja na kile cha Shinyanga kutasaidia kufikia malengo ya Programu ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ya kuongeza mzigo unaosafirishwa katika njia ya reli ya kati na pia kupunguza muda wa mzunguko wa mabehewa.



35.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, TAZARA ilianza kutekeleza Itifaki ya 15 kwa kuagiza vichwa vya treni vipya 4; vichwa vya sogeza vipya 4; mabehewa ya abiria mapya 18; mashine za okoa 2, mitambo na vifaa vya usalama. Vifaa hivyo vinatarajiwa kuanza kuwasili nchini Desemba, 2014.



36.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 nilitoa taarifa kuhusu Serikali za Tanzania na Zambia kuendelea kurekebisha Sheria ya TAZARA Na. 23 ya mwaka 1975 kama ilivyohuishwa na Sheria Na. 4 ya mwaka 1995 Sura ya 143. Napenda kutoa taarifa kuwa marekebisho ya Sheria hiyo yalifanyika na Rasimu kuwasilishwa katika kila nchi mwanahisa ili kuboresha na kutoa maoni. Aidha, rasimu hii ya Sheria itawasilishwa kwenye Bodi ya TAZARA Juni, 2014 na kuwasilishwa katika Baraza la Mawaziri la TAZARA litakalokutana Julai, 2014 kwa ajili ya kupata idhini ya kuendelea na mchakato wa kutunga sheria.



  2.4 Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini



37.                  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, udhibiti wa huduma za usafiri wa nchi kavu na majini umeendelea kusimamiwa na kutekelezwa na SUMATRA kwa kusogeza huduma zake karibu na wananchi. Hadi Machi, 2014, SUMATRA ilikuwa imefungua ofisi zake katika mikoa hiyo na hivyo kufanya Mamlaka kuwa na ofisi katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara.

 


2.6       Udhibiti wa Huduma za Usafiri kwa Njia ya Barabara




38.                 Mheshimiwa Spika, kupitia Hotuba ya mwaka 2013/2014 nilitoa maagizo kwa SUMATRA kuhakikisha kuwa inaandaa utaratibu stahiki utakaowezesha kutoa leseni kwa magari aina ya Noah kwa kuzingatia usalama wa abiria na mali zao. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, SUMATRA iliandaa utaratibu huo na sasa magari aina ya Noah yamesajiliwa na kutoa huduma za abiria katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.



39.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, SUMATRA ilizifuatilia Halmashauri saba ambazo zilikuwa hazijasaini mkataba wa Uwakala wa kusimamia utekelezaji wa kanuni za usafiri wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu katika maeneo ya halmashauri zao. SUMATRA sasa imekwishaingia makubaliano na Halmashauri 135. Baada ya kusaini makubaliano na Halmashauri hizo, kwa sasa SUMATRA inaendelea kusaini makubaliano na Halmashauri nyingine mpya 29. Utekelezaji wa makubaliano hayo utapunguza ajali na uhalifu unaohusisha matumizi ya pikipiki hizo.

2.7       Udhibiti wa Usalama wa Vyombo vya Usafiri Majini




40.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kupitia SUMATRA iliendelea kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini, abiria na mizigo yao. SUMATRA na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) wameendelea kushirikiana katika kufanya ukaguzi na uhakiki wa ubora wa vyombo vya usafiri majini na kubadilishana taarifa kuhusu usalama wa vyombo vya usafiri majini bandarini na uhifadhi wa mazingira. Aidha, Kituo cha kuratibu taarifa za Utafutaji na Uokoaji, ulinzi na usalama Majini (MRCC) kilichopo Dar es Salaam kiliendelea kupokea na kuratibu taarifa za utafutaji na uokoaji. Kwa upande wa Tanzania Bara kituo hicho kiliripoti ajali 13 ambazo watu 125 waliokolewa na wengine 24 kupoteza maisha.





3.0       USAFIRI NA UCHUKUZI MAJINI




3.1       Huduma za Uchukuzi Katika Maziwa






41.                 Mheshimiwa Spika, wakati nawasilisha bajeti ya mwaka 2013/2014, niliahidi kuanza ujenzi wa meli mpya tatu katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa na ukarabati wa meli za MV. Victoria, MV. Umoja na MV. Serengeti. Pamoja na kwamba mradi huu mkubwa tayari una Mshauri Mwelekezi (Kampuni ya OSK Shiptech ya Denmark), umechelewa kuanza kutokana na gharama zake kupanda kwa asilimia 163 ya gharama zilizokadiriwa awali. Serikali inajadiliana na Serikali ya Denmark inayofadhili mradi huo kuhusu ongezeko hilo la gharama. Aidha, kutokana na mahitaji makubwa ya uchukuzi katika ziwa Tanganyika, mradi huo sasa utajenga meli mpya nne, moja katika Ziwa Victoria, mbili Ziwa Tanganyika na moja Ziwa Nyasa pamoja na kukarabati meli tatu.



3.3       Huduma za Bandari




42.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, niliahidi kuhudumia shehena ya tani milioni 13.84 ikijumuisha makasha 430,600 yatakayohudumiwa katika kitengo cha TICTS. Napenda kutoa taarifa kuwa katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014, Mamlaka ilihudumia shehena ya tani milioni 13.7 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya lengo la mwaka. Matarajio ni kwamba kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2014 tutakuwa tumefikia lengo la tani milioni 13.84. Katika kipindi hicho kitengo cha makasha (TICTS) kilihudumia makasha 348,811 ambapo ni sawa na asilimia 76 ya lengo la mwaka.



43.                 Mheshimiwa Spika, shehena iliyohudumiwa kwenda na kutoka nchi jirani za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Uganda katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014 ilikuwa ni tani milioni 3.654, ikilinganishwa na tani milioni 3.182, (sawa na ongezeko la asilimia 12.9) zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2012/2013. Ongezeko la shehena hii limetokana na jitihada zinazofanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuvutia wateja toka nchi jirani kuendelea kutumia bandari zetu. Aidha, uboreshaji wa huduma, uimarishaji wa usalama wa mizigo ya wateja na utoaji huduma za bandari kwa saa 24 kila siku umesaidia kurudisha imani kwa wateja kutoka nchi hizo.



44.                 Mheshimiwa Spika, katika  hotuba ya mwaka 2013/2014 tuliahidi utekelezaji wa miradi ya bandari kama ifuatavyo: 

     i.         Ujenzi wa gati la bandari ya Mafia ambao ulikamilika Septemba, 2013 na gati hilo kufunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba, 2013. Vilevile, katika mwaka 2014/2015 Mamlaka imetenga kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuweka kivuko cha kupanda na kushuka kwenye vyombo vidogo vidogo kwa kutumia gati lililopo na kuimarisha usalama wa abiria kwa kuziba uwazi uliopo pembezoni mwa gati. Aidha, katika mwaka 2014/2015 TPA itakarabati na kuboresha gati la Nyamisati (Mkuranga) ili kuhudumia wasafiri wanaokwenda Mafia;

   ii.         Ujenzi wa gati la bandari ya Kipili katika Ziwa Tanganyika, umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na unatarajiwa kuisha Julai, 2014. Kazi za ujenzi wa magati ya Karema, Lagosa na Sibwesa (Kalya) katika Ziwa Tanganyika zimetelekezwa na Mkandarasi M/S Modspan. Aidha, kazi za ujenzi wa magati ya Kagunga katika Ziwa Tanganyika na Kiwira katika Ziwa Nyasa zilizokuwa zinatekelezwa na Mkandarasi Canopies International hazijakamilika na Mkandarasi amekimbia eneo la kazi. Serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari kuchukua hatua zifuatazo mapema iwezekanavyo:

·           Iwanyang’anye Makandarasi hao kazi hizo na kuzitangaza upya na washindi waanze ujenzi mwezi Agosti, 2014 na kukamilisha kazi mwezi Julai, 2015 chini ya usimamzi wa karibu wa Mamlaka. Kazi hizo zimetangazwa upya tarehe 17 Aprili, 2014;

·           Iwashtaki Makandarasi hao kwa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ili kuzifutia usajili Kampuni hizo. Kazi hiyo imefanyika;

·           Mamlaka iitishe dhamana walizoweka Makandarasi hao (Advance guarantee and Performance Bonds) ili kufidia sehemu ya gharama. Wakati kazi hii inafanyika, imebainika kuwa Mkandarasi M/S Canopies International aliwasilisha Mamlaka ya Bandari nyaraka za kughushi za dhamana ya malipo ya awali na hivyo kupata kazi hiyo. Mamlaka imeagizwa imfungulie Mkandarasi huyo kesi ya jinai haraka iwezekanavyo na ichunguze misingi ambayo watendaji wake walizipokea dhamana hiyo ya Benki;

Vilevile, katika mwaka 2014/2015 Mamlaka imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa gati katika bandari ya Ndumbi katika Ziwa Nyasa ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na makaa ya mawe kutoka eneo la Ngaka.

 iii.         Ujenzi wa bandari ya Mbegani Bagamoyo. Mnamo Desemba, 2013 Serikali ilisaini makubaliano ya kutekeleza mradi huo (Implementation Agreement) na Februari, 2014 Kampuni ya China Merchants Holdings International Limited iliwasilisha andiko la mradi.  Hivi sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha uchambuzi wa andiko hilo ili kuendelea na hatua zinazofuata ikiwa ni pamoja na kukabidhi eneo la mradi kwa mwekezaji huyo. Kazi ya tathmini ya mali zilizo kwenye eneo husika itakamilika Juni, 2014 na malipo ya fidia yatafanyika katika mwaka wa fedha 2014/2015.

  iv.         Kuendelea na maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa Bandari za Mwambani (Tanga) na Mtwara, ambapo zabuni zilitangazwa tarehe 27 Machi, 2014 na zitafunguliwa tarehe 26 Juni, 2014. Kazi zinatarajiwa kuanza ifikapo Septemba 2014 na kukamilika Mwishoni mwa mwaka 2016.

    v.         Kuanza maandalizi ya ujenzi wa magati ya Pangani (Tanga) katika bahari ya Hindi, Ntama na Lushamba katika Ziwa Victoria na Kabwe katika Ziwa Tanganyika. Gati la Pangani Mkandarasi amepatikana ambaye ni M/S Alpha Logistics na ataanza kazi mwezi Juni, 2014 na muda wa utekelezaji ni miezi 12 na hivyo kazi zitakamilika mwezi Julai, 2015. Magati ya Ntama na Lushamba utekelezaji wake utaanza mwezi Juni, 2014. Kuhusu ujenzi wa gati la Kabwe utekelezaji wake utaanza mwezi Novemba, 2014;

  vi.         Kuimarisha usalama wa mizigo na bandari. Mamlaka imepanga kuanza utekelezaji wa mradi wa electronic cargo Tracking system ambapo zabuni za mradi zimeshaandaliwa na zinatarajiwa kutangazwa mwezi Julai, 2014.

vii.         Ununuzi wa Scanners kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo. Scanners tatu zimeagizwa na zinatarajiwa kuwasili Septemba, 2014: na

viii.         Ulipaji fidia kwa wakazi wa Kibirizi ili kupisha ujenzi wa gati. Umeanza na unatarajiwa kukamilika kabla ya Juni, 2014.



45.                 Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali za kusogeza huduma za kibandari karibu na wateja, tarehe 1 Mei, 2014, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ilifungua ofisi mjini Lubumbashi nchini DR Congo. Kupitia ofisi hii, wateja walioko DRC hawatalazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam wakiwa wamebeba fedha kwa ajili ya kulipia mizigo yao. Badala yake, wataweza kulipia huduma za bandari wakiwa nchini kwao DRC na kupokea mizigo yao kule kule. Aidha katika mwaka wa fedha 2014/15, Mamlaka imepanga kufungua ofisi nyingine katika nchi za Zambia, Burundi na Rwanda. Wizara inawasiliana na Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuona uwezekano wa kuwa na watumishi wa TRA katika ofisi hizo ili kuboresha ufanisi. Vile vile ili kuboresha huduma za forodha (Single Customs Territory – SCT) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mamlaka imetenga eneo la ofisi katika jengo la Ex-NASACO katika bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya wafanyakazi kutoka katika nchi za Jumuiya. Taratibu za kubadilishana taarifa kwa njia ya kielektroniki zimeshakamilika ili kuwezesha utekelezaji wa kituo kimoja cha forodha (SCT).



46.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu uendelezaji wa kituo cha mizigo cha Kisarawe (Kisarawe Freight Station) mtaalam mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kuendeleza eneo la Kisarawe amepatikana. Mtaalam huyo (Royal Haskoning wa Uholanzi) anatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai, 2014 na kukamilisha mwezi Januari, 2015.



47.                 Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya mwaka 2013/2014 niliahidi kuanza ujenzi wa gati Na. 13 na 14. Napenda kutoa taarifa kuwa mradi huu umechelewa kuanza kutokana na sababu kubwa tatu:

(i)            Gharama za ujenzi wa gati hizo mbili ya Dola za Marekani milioni 523 (karibu shilingi bilioni 837), bado ni juu mno na inayoendelea kuzua maswali mengi yasiyojibika pale gharama za miradi mingine ya aina hiyo hiyo zinapoangaliwa ambazo ni chini ya nusu ya gharama hiyo ya Dola za Marekani milioni 523;

(ii)          Gharama hiyo ya ujenzi ya Dola za Marekani milioni 523 ilifikiwa ili kujenga gati mbili za kisasa (na vifaa vyake) zinazoweza kuhudumia meli kubwa hata za aina ya Panamax zenye urefu wa mita 294.13, upana wa mita 32.31 na kina cha mita 12.04. Lakini mkandarasi CCCC/CHEC hakuwa mkweli kwani aliendelea na mchakato wa usanifu wa awali (hydrographical and topographical surveys) huku akijua kuwa gati namba 13 na 14 zisingeweza kuhudumia meli kubwa za aina hiyo ya Panamax kwani kipenyo cha kugeuza meli za ukubwa huo sehemu hiyo hakitoshi, mita 440 tu badala ya 600 ambazo kuzipata lazima tumege mita 160 za ardhi ya jeshi upande wa pili wa bandari. Aidha, gharama za kundoa mabomba ya mafuta chini ya bahari na kuyahamishia sehemu nyingine (pamoja na kituo chake cha KOJ) ili kuruhusu dredging ambayo ni lazima ifanyike kuweza kuhudumia meli kubwa zenye kina cha mita 12.04 haikuzingatiwa kwenye gharama za Dola za Marekani milioni 523. Vilevile kwa kuzingatia taratibu za kiusalama katika Bandari na kwa watumiaji bandarini, huduma kama hiyo ya KOJ kuwa katikati ya Magati ya Bandari haiashirii mazingira salama. Hivyo kwa kufumbia macho gharama hizo bayana, kampuni hizi mbili hazina nia njema ya kufanya biashara ya kiungwana.

(iii)        Mchakato wa ujenzi wa gati namba 13 na 14 ulisimama mwezi Septemba, 2013 baada ya kampuni hizo mbili za CCCC na CHEC, kuanza kuvutana kuhusu utekelezaji wa mradi huo. CCCC, kampuni mama ya CHEC ambayo ilikuwa imefungiwa (black-listed) na PPRA na hivyo kutakiwa kuwaachia CHEC mradi, haikutaka kuiachia CHEC mradi huo, hivyo ikateua afisa wake na kumpatia vitambulisho vya CHEC na CHEC ikamteua afisa mwingine. Mvutano huo ukapelekea tuwe na watu wawili bandarini wote wakiwa na nguvu za kisheria za kuiwakilisha CHEC. Kitendo hicho kikasababisha Deed of Novation iliyoandaliwa na TPA na kuridhiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutosainiwa kati ya Mamlaka na Mkandarasi mpaka sasa.

Kutokana na sababu hizo, Mamlaka ya Bandari inakusudia kuachana na Kampuni za CCCC na CHEC na hivyo kuanza taratibu za kushirikisha Kampuni zingine kutekeleza mradi huu kwa masharti yanayokubalika. Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameombwa ushauri kuhusu suala hili.  

Aidha, Benki ya Dunia kupitia International Bank for Reconstruction and Development (IBRD) kwa kushirikiana na DFID na TMEA zimekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu (soft loan) wa asilimia 65 na msaada (grant) wa asilimia 35 kwa ajili ya uendelezaji wa Gati namba 13 na 14, uboreshwaji wa Gati namba 1 – 7 na uongezaji wa kina cha lango la Bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na nia hiyo ya Benki na Washirika wake, TPA imeandaa Rasimu za Nyaraka za Zabuni (Draft Tender Documents) za utekelezaji wa miradi hii kwa njia ya Usanifu na Ujenzi (design and Build). Nyaraka zimewasilishwa Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata kibali. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2014/2015.



48.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu ukarabati wa bandari za Mwanza na Kigoma kazi ya kukarabati chelezo (slipway) katika bandari ya Kigoma inaendelea na inatarajiwa kukamilika Agosti, 2014. Aidha, mkandarasi wa kufanya ukarabati wa kreni ya kupakua na kupakia mizigo amepatikana na ataanza kazi Juni, 2014 na kukamilisha ukarabati mwezi Septemba, 2014. Kwa upande wa bandari ya Mwanza mshauri mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu wa kubainisha mahitaji ya kuendeleza bandari za Mwanza, Bukoba na Kemondo ataanza kazi Julai, 2014 na kukamilika mwezi Februari, 2015.



49.                 Mheshimiwa Spika kutokana na kazi nzuri na ya ufanisi ambayo Mamlaka ya Bandari imefanya ndani ya kipindi kifupi, Mamlaka imeamua kutumia faida iliyopata kuchochea nyenzo za uchukuzi pale zilipolala ili kuijengea Mamlaka mazingira ya kufanya kazi vizuri zaidi na hivyo kuchochea uchumi wa nchi:

(i) Ili kuondoa msongamano wa mizigo bandarini baada ya nchi kadhaa za jirani kuonesha nia ya kupitisha mizigo mingi zaidi katika Bandari ya Dar es Salaam, TPA imeamua kugharamia uundaji upya wa vichwa vitatu vya treni ambavyo vitatumika kuendeshea treni maalumu za mizigo (block trains) kwenda Kigoma kila wiki kuhudumia wafanyabiashara wa DRC, Burundi na wa Kigoma na kuendeshea treni maalumu zingine za mizigo kwenda Mwanza kila wiki kuhudumia wafanyabiashara wa Rwanda na Uganda kwa kushushia mizigo yao Isaka na Mwanza. TPA inatarajia wafanyabiashara wa Kigoma na Mwanza kuchangamkia fursa hii kwa hamasa.

(ii) TPA vilevile inaendelea na mazungumzo na uongozi wa TAZARA ili kutoa huduma za namna hiyohiyo kwa wafanyabiashara wa Zambia, Malawi na Mbeya ambapo vichwa viwili vya treni vinatarajiwa kuundwa upya. TPA inatarajia wafanyabiashara wa Mbeya watachangamkia fursa hii endapo mazungumzo kati yake na TAZARA yakifanikiwa.

(iii) Ili kuchochea uchukuzi wa majini ambapo bandari zake kwenye maziwa hazina shughuli za kutosha kutokana na uchache wa meli, TPA inaanza mkakati wa kununua meli za abiria na mizigo kwa awamu katika maziwa yote makubwa matatu kwa njia ya ubia. Kwa kuzingatia ratiba ya Serikali ya miradi ya utengenezaji wa meli mpya ambayo inaanzia Ziwa Viktoria na Tanganyika mwaka ujao wa fedha, TPA itaanza mradi wake wa kwanza mwaka wa fedha wa 2014/2015 katika Ziwa Nyasa ambako usafiri wa majini ni wa mashaka. Mamlaka itanunua meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo.



4.0       USAFIRI NA UCHUKUZI KWA NJIA YA ANGA




4.1       Udhibiti wa Usafiri wa Anga




50.                 Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga imeendelea kusajili ndege nchini kulingana na masharti ya usajili ambapo hadi Aprili, 2014, ndege 23 zilisajiliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini. Vilevile, viwanja vya ndege vya Mwanza, Musoma, Bukoba, Kigoma, Tabora, Arusha, Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa, Songea, Nachingwea na Kilwa Masoko vilikaguliwa na kupewa leseni za uendeshaji. Lengo la utoaji wa leseni ya uendeshaji ni kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria na kanuni za kitaifa na kimataifa za uendeshaji wa viwanja vya ndege zinazingatiwa.

  

51.                 Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ya kuanzisha Mfuko maalum kwa ajili ya kufadhili mafunzo ya urubani na uhandisi wa ndege imeendelea kutekelezwa. Katika mwaka 2013/2014, Mfuko ulianza kutumika kwa kufadhili Wanafunzi 5 katika mafunzo ya urubani. Katika mwaka 2014/2015 wanafunzi 10 watafadhiliwa kupitia Mfuko huu. Pamoja na kufadhili mafunzo hayo, Mfuko unakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti kuweza kupeleka wanafunzi wengi mafunzoni. Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili kutunisha fedha za Mfuko huu.

52.                 Mheshimiwa Spika, limejitokeza tatizo kubwa la uhaba wa ajira kwa marubani vijana ambao wamesomeshwa na wazazi wao au wadhamini wengine huku ongezeko la marubani vijana kutoka nje ya nchi likionekana. Serikali inaiagiza TCAA kuhakikisha kuwa utoaji wa leseni kwa marubani kutoka nje ya nchi unaambatana na vibali vya kazi (work permits) na Chama cha Marubani kishirikishwe katika mchakato wa kutoa vibali hivyo ili kuleta uwiano wa marubani wa ndani na nje wanaofanya kazi nchini. Aidha, TCAA isimamie kikamilifu utekelezaji wa Kanuni za uendeshaji ndege (Civil Aviation Operation of Aircraft Regulation) za mwaka 2012 ili idadi ya marubani katika ndege wakati wowote isiwe chini ya mwongozo wa aina ya ndege husika (aircraft flight manual) na cheti kinachoruhusu ndege kuruka (Certificate of Airworthiness) kinachotambuliwa na TCAA.

 

53.                 Mheshimiwa Spika, idadi ya abiria wanaosafiri kwenda na kutoka nje ya nchi iliongezeka kutoka abiria 2,010,240 mwaka 2012/2013 hadi kufikia abiria 2,251,469 mwezi Aprili, 2014. Hii ni sawa na ongezeko la abiria kwa asilimia 12. Aidha, abiria wanaosafiri ndani ya nchi waliongezeka kutoka abiria 2,420,922 katika mwaka 2012/2013 hadi kufikia abiria 2,808,270 mwezi Aprili, 2014,  sawa na ongezeko la asilimia 16. Sababu ya ongezeko la abiria wa safari za ndani ya nchi ni pamoja na kukua kwa uchumi,  kuongezeka kwa mashirika yanayotoa huduma ya usafiri wa anga, kufunguliwa kwa viwanja vipya kama Songwe - Mbeya, kukarabatiwa kwa viwanja vya Kigoma, Tabora na Arusha pamoja na kukua kwa utalii. Katika mwaka 2014/2015, idadi ya abiria wanaotumia usafiri huu inatarajiwa kufika 5,717,505. Vilevile, idadi ya abiria wa safari za nje inategemewa kuongezeka baada ya kupitia upya na kusaini mikataba ya usafiri wa anga kati ya Tanzania na nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya Fastjet, Mango na Proflight kuanza safari za kimataifa.



54.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka  2013/2014, safari za ndege (aircraft movements) ziliongezeka kwa asilimia 7.8 kutoka safari 242,745 mwaka 2012/2013 hadi safari  261,763 Aprili, 2014. Kati ya hizo, safari za kimataifa ziliongezeka kutoka safari 40,426 mwaka 2012/2013 hadi kufikia safari 41,235 mwezi Aprili, 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 2. Safari za ndani ya nchi pia ziliongezeka kutoka safari 202,319 mwaka 2012/2013 hadi kufikia 220,528 mwezi Aprili, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia 9. Kuongezeka kwa safari za ndege kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na mashirika kama Fast Jet na Tropical Air kuanza safari katika Kiwanja cha ndege cha Songwe na viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora kufunguliwa baada ya ukarabati.



55.                 Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya mwaka 2013/2014, niliahidi kuboresha mikataba ya usafiri wa anga (Bilateral Air Services Agreements - BASA) kati ya Tanzania na nchi mbalimbali na kuanzisha mikataba mipya ili kukidhi mahitaji ya soko na kurahisisha usafiri katika sekta hii muhimu. Hadi Aprili, 2014, Tanzania ilikuwa imeingia makubaliano ya BASA na nchi 52 ikilinganishwa na nchi 48 zilizokuwa zimesaini mkataba huo Aprili, 2013. Kati ya mikataba hiyo, mikataba 21 ndiyo ambayo kampuni au mashirika yake ya ndege yanatoa huduma kati ya Tanzania na nchi husika.  Aidha, hadi Aprili, 2014, mashirika ya ndege ya ndani na nje yanayotoa huduma nchini kwa utaratibu wa BASA yalifikia 25 ambapo safari za ndege kati ya nchi hizo na Tanzania zilikuwa 175. Katika mwaka 2014/2015, Tanzania inatarajia kuingia mikataba mipya ya usafiri wa anga au kupitia upya mikataba iliyopo na nchi za Australia, Italia, Sudan ya Kusini na Mauritius.



56.                 Mheshimiwa Spika, pamoja na majukumu ya kudhibiti na kusimamia shughuli na taratibu za usafiri wa anga nchini, Mamlaka ya Usafiri wa Anga pia hutoa huduma za uongozaji wa ndege katika anga lote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na mwingiliano wa majukumu ya kudhibiti na kutoa huduma, katika mwaka 2014/2015, Wizara itaangalia uwezekano wa kutenganisha majukumu ya udhibiti na utoaji huduma ya uongozaji wa ndege ili majukumu haya mawili yasikae chini ya Mamlaka moja. Aidha, ili kuimarisha usalama wa usafiri wa anga, Wizara imetenga shilingi bilioni 11.14 kwa ajili ya kununua rada mbili (2) za kuongozea ndege za kiraia.



4.2       Huduma za Viwanja vya Ndege


57.                 Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo la tatu la abiria (Terminal III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) umeanza rasmi Januari, 2014 baada ya kukamilika kwa kazi ya kufanya usanifu wa kina. Aidha, tarehe 24 Aprili, 2014 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya M. Kikwete aliweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la tatu la abiria. Mradi huu ambao ni mkubwa katika historia ya usafiri wa anga nchini unatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itahusu ujenzi wa jengo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5 kwa mwaka kwa gharama ya shilingi bilioni 293. Awamu hii inatarajiwa kukamilika Oktoba, 2015. Ujenzi wa awamu ya pili utaongeza uwezo wa jengo hadi kuhudumia abiria milioni 6 kwa mwaka na hivyo JNIA kuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 7.2 kwa mwaka. Mradi huu utakuwa na maegesho ya ndege za aina zote ikiwemo ndege kubwa kuliko zote aina ya Airbus 380.



58.                 Mheshimiwa Spika, kuhusu Kiwanja cha ndege cha Songwe, katika mwaka 2013/2014 Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imempata mkandarasi wa kutoa huduma za mafuta na sasa anaendelea na maandalizi ya kuanza kutoa huduma hiyo. Aidha, kazi za ujenzi wa maegesho ya ndege na jengo la abiria zinaendelea na zitakamalika Desemba, 2014.



59.                 Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya uboreshaji na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Kigoma na Tabora iliyowekewa jiwe la msingi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya M. Kikwete ilikamilika Juni, 2013.  Zabuni kwa ajili ya kuwapata makandarasi na wahandisi washauri kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya ukarabati wa viwanja hivi chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia zilifunguliwa Mei, 2014. Kazi za awamu ya pili zitahusisha ujenzi wa jengo la abiria, maegesho ya magari, barabara za kuingia viwanjani na upanuzi wa maegesho ya ndege. Kukamilika kwa awamu ya pili kutawezesha viwanja hivyo kuwa vya kisasa na kutumika kwa saa 24.



60.                 Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 niliahidi kukamilisha ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Mafia kwa kiwango cha lami. Napenda kutoa taarifa kuwa ukarabati wa kiwanja hiki uliogharamiwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCAT) ulikamilika na kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya M. Kikwete Oktoba, 2013. Aidha, katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 1.05 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo jipya la abiria, maegesho ya magari, ukarabati wa barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani pamoja na kituo cha umeme.



61.                 Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014 Bunge lako Tukufu liliidhinisha fedha kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Bukoba. Napenda kutoa taarifa kuwa kazi za ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki kwa kiwango cha lami zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika Septemba, 2014. Aidha, tarehe 24 Julai, 2013, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi wa kiwanja hiki. Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara za viungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami. 



62.                 Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya mwaka 2013/2014 niliahidi kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa viwanja kumi na moja (11) vya Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Moshi, Musoma, Lindi, Njombe, Songea, Singida, Bariadi (Mkoani Simiyu) na Tanga. Napenda kutoa taarifa kuwa, tayari Mhandisi Mshauri ameanza kazi hiyo Aprili, 2014 na inatarajiwa kukamilika Februari, 2015.



63.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Bunge lako Tukufu liliidhinisha fedha kwa ajili ya kuboresha kiwanja cha ndege cha Mwanza; kukarabati viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga pamoja na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mtwara. Napenda kutoa taarifa  kuwa:

     i.         Kazi zinazoendelea katika kiwanja cha ndege cha Mwanza ni pamoja na kuchimba eneo la kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege, ujenzi  wa nguzo za jengo la mizigo na jengo la kuongozea ndege, na ujenzi wa kalavati la kutolea maji ya mvua kutoka upande mmoja wa barabara ya kutua na kuruka ndege kwenda upande mwingine;

   ii.         Zabuni za kuwapata makandarasi wa kazi za ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga zinatarajiwa kutangazwa Juni, 2014. Aidha, taratibu za kumpata mhandisi mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa majengo ya abiria katika viwanja hivyo zinaendelea; na

 iii.         Kazi ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mtwara unaendelea na unatarajiwa kukamilika Julai, 2014. Aidha, kazi ya ukarabati wa muda katika barabara ya kuruka na kutua ndege ili kuwezesha kiwanja kitumike katika msimu mzima wa mwaka ilikamilika Novemba, 2013.



64.                 Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa kiwanja cha Ndege cha Arusha kinakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege za kubeba hadi abiria 70 ili kiendelee kuchangia katika uboreshaji na ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Katika mkakati wa kukifanya kiwanja cha ndege cha Arusha kuwa katika viwango vya kimataifa, Machi 2014, Mamlaka ilifungua zabuni ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya marejeo ya usanifu wa miundombinu ya kiwanja pamoja na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Aidha, zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa kazi ya kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kwa urefu wa mita 200 itatangazwa Juni, 2014.



65.                 Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha na kuboresha ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege nchini hasa baada ya kushamiri kwa matukio ya usafirishaji wa madawa ya kulevya kupitia viwanja vyetu vya ndege. Ili kufanikisha azma hiyo, katika mwaka 2013/2014, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilipata msaada wa vifaa vya kisasa vya utambuzi wa milipuko (Explosive Trace Detectors) kutoka Serikali ya Uingereza na Mamlaka imenunua mashine za kisasa za ukaguzi wa mizigo zenye uwezo wa kutambua madawa ya kulevya (Rapscan X-ray machines 600 series). Vifaa hivyo vilisimikwa katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere. Serikali inaendelea na taratibu za kufunga vifaa kama hivyo katika viwanja vya ndege vya Kilimanjaro, Mwanza, Songwe na Arusha.

66.                  Mheshimiwa Spika, kuhusu Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro Serikali za Tanzania na Uholanzi zilitiliana saini ya msaada wa Shilingi bilioni 34.5 (sawa na Euro milioni 15) kwa ajili ya ukarabati wa Kiwanja hiki. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ukarabati na upanuzi wa maegesho ya ndege, njia za viungio, jengo la abiria, njia ya kuruka na kutua ndege na ujenzi wa mfumo mpya wa maji taka. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kiasi cha Shilingi bilioni 47.15 (sawa na Euro milioni 20.5) kwa ajili ya kuendelea na awamu ya pili ya ukarabati wa KIA. Mradi huu utakapokamilika utaongeza uwezo wa KIA kuhudumia ndege nyingi, kwa ufanisi mkubwa na usalama zaidi.



67.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imepanga kutekeleza kazi zifuatazo:

     i.         Kuendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) pamoja na miundombinu yake katika kiwanja cha JNIA.  Shilingi bilioni 44 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi;

   ii.         Kukamilisha  ujenzi wa maegesho ya ndege na jengo kubwa la abiria, kuendelea na ujenzi wa uzio wa usalama na kusimika taa na mifumo  ya kuongozea ndege katika kiwanja cha  Ndege cha Songwe (Mbeya) ambapo Shilingi bilioni 9.05 zimetengwa;

 iii.         Kuendelea na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Mwanza. Serikali imetenga shilingi bilioni 12.05 kwa ajili ya kazi hiyo;

  iv.         Kukamilisha ukarabati wa Kiwanja cha ndege cha Bukoba na kulipa fidia kwa wakazi waliobaki. Shilingi bilioni 3.33 zimetengwa;

    v.         Kuendelea na  ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Kigoma katika kiwango cha lami ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni 4.05 ili kukamilisha kazi hii;

  vi.         Kuendelea na  ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Tabora ambapo Shilingi bilioni 12.87 zimetengwa kwa kazi hii;

vii.         Kuanza ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga kwa kiwango cha lami ambapo Shilingi bilioni 12.07 zimetengwa;

viii.         Kuanza ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kwa kiwango cha lami ambapo Shilingi bilioni 11.75 zimetengwa;

 ix.         Kufanya kazi ya usanifu wa kina wa ujenzi wa Kiwanja kipya cha Ndege cha Msalato katika kiwango cha lami ambapo Serikali imetenga shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kazi hiyo.

   x.         Kufanya matengenezo ya kiwanja cha ndege cha Mtwara. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege;

 xi.         Kuendelea na taratibu za maandalizi ya ulipaji fidia, upimaji na upatikanaji wa hati miliki ya ardhi kwa maeneo ya viwanja vipya vya ndege vya Bagamoyo (Pwani), Isaka (Shinyanga), Kisumba (Rukwa), Msalato (Dodoma), Ngungungu (Manyara), Omukajunguti (Kagera), Bariadi (Simiyu) na Nyansurura (Mara);

xii.         Kukamilisha ufungaji wa majenereta mapya, kuweka madaraja mapya ya kupandia na kushuka abiria (aerobridges) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; na

xiii.         Kuboresha mitambo na mifumo ya kufuatilia mienendo ya shughuli za usalama na uendeshaji wa kiwanja (CCTV) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Mwanza na Arusha.

xiv.          

4.3       Huduma za Usafiri wa Ndege




68.                 Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusaidia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili iweze kuboresha huduma zake na kujiendesha kibiashara. ATCL imeendelea kutoa huduma ya kusafirisha abiria katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Mtwara, Tabora, Kigoma na Hahaya-Comoro kwa kutumia ndege yake aina ya Dash 8 Q300. Aidha, kuwasili kwa ndege ya kukodi aina ya CRJ-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 50 mwezi Machi, 2014 kumeimarisha na kuboresha huduma za ATCL  na hivyo kuanzisha safari za ndege kwenda Bujumbura, Mwanza, Arusha, Songwe na Zanzibar. ATCL inatarajia kununua ndege nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 50 kila moja kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri wa anga ndani ya nchi. Ujio wa ndege hizi utaimarisha utendaji na kuongeza mapato ya ATCL. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga Shilingi bilioni 2 ili kuboresha utendaji wa ATCL.





5.0       HUDUMA ZA HALI YA HEWA




69.                 Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakiki na kuratibu utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na kutoa tahadhari dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa ili kuongeza mchango wa sekta hii katika kuendeleza sekta nyingine za kiuchumi na kijamii na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.



70.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara ilipanga kukamilisha malipo ya kuunda na kufunga Rada ya hali ya hewa mkoani Mwanza. Napenda kutoa taarifa kuwa kazi ya ufungaji wa Rada hii imeanza na inatarajiwa kukamilika Juni, 2014. Rada hii ni muhimu kwani itasaidia katika shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika Ziwa Victoria na kutoa tahadhari juu ya matukio ya hali mbaya ya hewa.



71.                 Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa ilifunga mitambo 11 ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe katika sehemu mbalimbali nchini. Aidha, ofisi ya utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi katika Bandari ya Zanzibar ilianzishwa na maandalizi ya kuanzisha ofisi za kutoa huduma za hali ya hewa katika Bandari za Mwanza, Kigoma na Itungi yanatarajiwa kukamilika Julai, 2014. Mamlaka pia iliboresha studio ya kuandaa taarifa za hali ya hewa iliyoko Dar es Salaam kwa kufunga vifaa vya kisasa. 



72.                 Mheshimiwa Spika, baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa katika mwaka 2013/2014 ni kama ifuatavyo:

     i.         Kukamilisha ukarabati wa vituo vya hali ya hewa vya Dodoma, Tabora, Mlingano pamoja na ofisi ya Hali ya Hewa iliyoko Kiwanja cha JNIA;

   ii.         Kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa Hali ya Hewa (central forecasting office) ilikamilika Machi, 2014. Aidha, kazi ya kufanya usanifu wa Michoro ya jengo hilo kwa ajili ya kuanza ujenzi inatarajiwa kukamilika Juni, 2014; na

 iii.         Kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kutoa mafunzo ya Shahada ya Hali ya Hewa (BSc. Met). Mwezi Oktoba 2013, jumla ya wanafunzi 15 walichaguliwa kujiunga na kozi hiyo. Kuanzishwa kwa kozi hii kutaboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa na kulipunguzia Taifa gharama za kusomesha wanafunzi nje ya nchi.



73.                 Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Mamlaka imetengewa jumla ya Shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa vya hali ya hewa, kujenga na kukarabati vituo vya hali ya hewa, kujenga uwezo wa watumishi, kuanza ujenzi wa Jengo la Utabiri wa Hali ya Hewa na kutekeleza programu ya Taifa ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Mikakati mingine ni kuanza kutumia rada ya pili ya hali ya hewa iliyoko Mwanza na mifumo ya kisasa ya utoaji wa utabiri. 







74.        Mheshimiwa Spika, kuhusu ushikiri wa kikanda, Wizara imeendelea kushiriki katika mikutano na shughuli mbalimbali za Jumuiya za Kikanda kama za Africa Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC), kwa lengo la kujenga uhusiano bora katika kuendeleza Sekta za Uchukuzi na Hali ya Hewa.





8.0       TAASISI ZA MAFUNZO




75.        Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuvihudumia vyuo vyetu vya mafunzo kwa lengo la kuviwezesha kutoa taaluma na wanataaluma wa kada mbalimbali katika sekta za uchukuzi na hali ya hewa. Vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Uchukuzi ni Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Chuo cha Hali ya Hewa - Kigoma, Chuo cha Usafiri wa Anga Dar es Salaam, Chuo cha Bandari Dar es Salaam na Chuo cha Reli Tabora. Katika mwaka 2014/2015 Wizara itaendelea kutoa kipaumbele katika kuhudumia vyuo hivyo ili viendelee kutoa wataalam wa Sekta ya Uchukuzi na Hali ya Hewa na kuboresha utendaji wa Sekta hiyo.



9.0       MASUALA MTAMBUKA


 


9.1       Kuzingatia masuala ya Jinsia




76.                 Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kulipa kipaumbele suala la ushirikishwaji wa wanawake katika sekta ya uchukuzi kwa kuzingatia Itifaki na Mikataba ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia. Katika kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake katika utekelezaji wa majukumu ya Sekta ya Uchukuzi, hivi sasa tuna wanawake madereva wa treni wanane. Kati ya hao, wawili wameajiriwa TRL na sita wameajiriwa na TAZARA; Marubani wanawake saba; kati ya hao, mmoja yuko ATCL, wanne wako Precision Air, mmoja yuko TCAA na mmoja yuko TGFA. Pia tuna waongoza ndege wanawake 16 ambao wako TCAA. Aidha, tuna wahandisi wanawake 39 wanaotumikia Taifa katika Taasisi mbalimbali za Wizara ya Uchukuzi. Kati ya hao wawili wanafanya kazi TRL, mmoja yuko ATCL, mmoja TGFA, watatu NIT, wawili TPA na mwingine yuko TMA. Wahandisi mitambo ya kuongozea ndege wanawake 15 wako TCAA na Wahandisi 14 wa fani umeme, mitambo, ujenzi na mawasiliano ambao wako TAA. Waendesha boti za kusukuma meli (tug) ni mmoja ambaye yupo TPA. Pamoja na ugumu wa kazi ya udereva wa magari ya masafa marefu, nafurahi kuwaarifu kuwa tuna madereva wanawake watatu wa mabasi na wawili wa malori.



9.2       Utunzaji wa Mazingira




77.                 Mheshimiwa Spika, uharibifu wa mazingira umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa Wizara yangu. Shughuli za kijamii zinazofanyika katika milima karibu na njia ya reli sehemu za Kilosa hadi Gulwe zimeendelea kuathiri huduma za uchukuzi wa Reli ya Kati kwa kiasi kikubwa. Naomba Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi wa Serikali za Mitaa waungane na Wizara katika kuelimisha Wananchi na kukemea vitendo vya kukata miti ovyo, kulima bila kufuata ushauri wa Wataalam na kulima kwenye kingo za mito na reli. Vitendo hivyo vinaharibu miundombinu hiyo hasa wakati wa mvua hivyo kuigharimu Serikali fedha nyingi za kufanya matengenezo.



10.0       SHUKRANI




78.                 Mheshimiwa Spika, ningependa sasa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote waliotoa ushirikiano katika kufanikisha malengo ya sekta. Hawa ni pamoja na Washirika wa Maendeleo ambao tunasaidiana nao katika kufanikisha utekelezaji wa program na mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta za uchukuzi na hali ya hewa. Shukrani za dhati ziende kwa nchi na mashirika ya kimataifa yaliyochangia katika maendeleo ya sekta yetu. Nchi na mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Bahari Duniani (IMO), Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), UNESCO, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi kwa Afrika (BADEA), Shirika la Maendeleo la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) Kuwait Fund, Malaysia, Jamhuri ya Korea, OPEC Fund, Umoja wa Nchi za Ulaya, Afrika Kusini, Uingereza, Marekani, Uholanzi, Japan, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), TMEA, DFID, India, China, Denmark, Norway, Ubelgiji, Ujerumani, Urusi, Sweden, Ufaransa, Finland, Singapore na wengine wengi. Napenda kuwaomba waendelee kushirikiana nasi katika kuimarisha sekta za uchukuzi na hali ya hewa.



79.                 Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kuwashukuru viongozi wenzangu wa Wizara ya Uchukuzi, nikianza na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Charles John Tizeba (Mb.), Katibu Mkuu Dkt. Shaaban Ramadhan Mwinjaka, Naibu Katibu Mkuu, Bi. Monica Lyanda Mwamunyange, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi za SUMATRA, TCAA, TGFA, KADCO, TAA, TPA, TRL, RAHCO, MSCL, TMA, SINOTASHIP, ATCL, DMI, NIT, TAZARA na TTFA, pamoja na watumishi wote wa Wizara na Taasisi. Ninafarijika kwa ushirikiano wanaonipa katika jitihada za kuendeleza sekta za uchukuzi na hali ya hewa. Nikiri kuwa bila mchango wao mkubwa, kazi yangu ya kuongoza sekta hii, ingekuwa ngumu.



11.0       MAOMBI YA FEDHA




80.                 Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka 2014/2015, Ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 527,933,790,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 93,306,391,000 zimetegwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 434,627,399,000 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Fedha za Matumizi ya Kawaida zinajumuisha Shilingi 33,027,291,000 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi na Shilingi 60,279,100,000 fedha za Matumizi Mengineyo (OC). Fedha za Miradi ya Maendeleo zinajumuisha Shilingi 273,140,000,000 fedha za ndani na Shilingi 161,487,399,000 fedha za nje.



81.                 Mheshimiwa Spika, naomba nimalize hotuba yangu kwa kukushukuru wewe binafsi, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza wakati nikiwasilisha hoja ya Wizara yangu. Hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya: www.mot.go.tz.  



82.                  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: