BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI

HOTUBA YA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MHE. PROF. SOSPETER MWIJARUBI MUHONGO (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2014/15

A.        UTANGULIZI

1.   Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2013/14 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini yake kwa Mwaka 2014/15.

2.   Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kutekeleza  majukumu yangu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.   

3.   Mheshimiwa Spika, kipekee nawashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa uongozi na juhudi zao katika kuleta maendeleo ya Taifa letu na kwa ushirikiano wanaonipa katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini.
  
4.   Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza kwa dhati Rais wetu  Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kupewa Tuzo ya Utumishi Bora kwa kuwa Kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Bara la Afrika kwa Mwaka 2013. Hii ni heshima kubwa na Tunu kwa Watanzania wote kwa ujumla kwa kuthaminiwa na kutambuliwa kwa kiongozi wetu katika medani za kimataifa. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kumpa nguvu na hekima zaidi ya kutekeleza majukumu yake.

5.   Mheshimiwa Spika, napenda pia kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa hekima, busara, umahiri na bila kuyumba katika kusimamia Kanuni tulizojiwekea sisi wenyewe. Vilevile, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Victor Kilasile Mwambalaswa (Mb.), Makamu Mwenyekiti Mhe. Jerome Dismas Bwanausi (Mb.), na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuishauri na kuisimamia Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake, pamoja na kuchambua na kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka 2013/14 na Makadirio ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2014/15. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Nishati na Madini imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini katika kuandaa Bajeti inayowasilishwa kwenu.

6.   Mheshimiwa Spika, naomba  vilevile kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwapongeza Mhe. Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga na Mhe. Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Jimbo la Chalinze kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa wawakilishi wa wananchi katika Majimbo hayo. Aidha, napenda kuwapa pole familia, ndugu, jamaa na wananchi kwa kuondokewa na wapendwa wetu, Mhe. Dkt.William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga na Waziri wa Fedha; Mhe. Said Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze; na Mhe. John Gabriel Tupa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. Tunaomba Mwenyezi Mungu awarehemu na awapumzishe kwa amani.

7.   Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka 2013/14; na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2014/15.

B.  TAARIFA YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2013/14 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2014/15

8.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2013/14 katika Sekta za Nishati na Madini  ulilenga kufanya yafuatayo: kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika; kuongeza wateja wanaotumia umeme hususan vijijini; ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia; kuongeza kasi ya upelekaji umeme katika Makao Makuu ya Wilaya ambazo hazijapatiwa umeme; kusimamia na kudhibiti biashara ya mafuta; kuvutia uwekezaji katika Sekta za Nishati na Madini; kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali; na kujenga uwezo wa usimamizi na ufuatiliaji katika Sekta za Nishati na Madini ili kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.  
 
9.   Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zilizotekelezwa ni pamoja na: kuboresha utoaji na usimamizi wa leseni za madini; kuendeleza uchimbaji mdogo wa madini; kuimarisha usimamizi wa afya, usalama na utunzaji wa mazingira migodini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; na kuziwezesha Taasisi na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa manufaa ya Watanzania wote.

10.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, pamoja na masuala mengine, Wizara imelenga kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia inayojumuisha ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam na mitambo ya kusafisha gesi asilia; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kipaumbele chini ya mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN); kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini na Makao Makuu ya Wilaya; kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli katika Sekta za Nishati na Madini;  kuendeleza uchimbaji mdogo na wa kati wa madini; kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini; na kuvutia uwekezaji katika Sekta za Nishati na Madini, hususan nishati jadidifu (renewable energies) na makaa ya mawe.

   Taarifa ya Ukusanyaji wa Mapato kwa Mwaka 2013/14

11.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2013/14, Wizara ya Nishati na Madini ilipangiwa kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 220. Hadi kufikia tarehe 23 Mei, 2014 jumla ya Shilingi bilioni 147.14 zilikusanywa, sawa na asilimia 67 ya lengo. Juhudi zinaendelea ili kuhakikisha kuwa lengo la ukusanyaji linafikiwa kama ilivyopangwa na hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
    Matumizi ya Wizara kwa Mwaka 2013/14

12.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Wizara iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,289,329,129,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 110,216,384,000 zilikuwa ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi 1,179,112,745,000 zilikuwa ni fedha za maendeleo.

13.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 23 Mei, 2014 jumla ya Shilingi 83,202,288,459 sawa na asilimia 75 ya fedha za Matumizi ya Kawaida zilipokelewa. Aidha, jumla ya Shilingi 577,526,232,810 sawa na asilimia 49 ya  Bajeti yote ya Maendeleo zilipokelewa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 431,010,106,443 ni fedha za ndani, sawa na asilimia 58 ya fedha za ndani zilizotengwa na Shilingi 146,516,126,367 ni fedha za nje, sawa na asilimia 34 ya fedha za nje zilizotengwa. Hivyo, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 660,728,521,269 sawa na asilimia 51 ya Bajeti yote iliyoidhinishwa kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka 2013/14.

14.       Mheshimiwa Spika, kutokana na usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za Serikali, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Nishati na Madini ni miongoni mwa Wizara zilizopata Hati Safi ya Hesabu za Mwaka 2012/13 isiyokuwa na swali lolote. Wizara itaendelea kusimamia ipasavyo Sheria mbalimbali ili kuhakikisha fedha za walipa kodi zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu na kwa Watanzania wote bila upendeleo wa aina yoyote.

   Malengo ya Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali kwa Mwaka  2014/15

15.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15 Wizara ya Nishati na Madini inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 240.59. Kiasi hiki ni sawa na ongezeko la asilimia 9.36 ya lengo la Mwaka 2013/14 la Shilingi bilioni 220. Mipango na mbinu zitakazotumika katika ukusanyaji wa mapato ni pamoja na: kuboresha Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini; kuhakikisha kuwa wamiliki wote wa leseni za madini nchini wanatimiza masharti ya leseni zao; na kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali katika kuzuia utoroshaji wa madini.
       
16.       Mheshimiwa Spika, mipango mingine ni kuongeza udhibiti katika kukusanya mapato yatokanayo na madini ya ujenzi na viwandani; kuimarisha usimamizi wa wachimbaji wadogo kwa kuwatambua na kutoa huduma za ugani ili kuongeza tija katika uzalishaji madini; na kuwahamasisha Wananchi kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Sekta za Nishati na Madini kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na ada mbalimbali.

          SEKTA YA NISHATI

          UKUAJI WA SEKTA YA NISHATI

17.       Mheshimiwa Spika, Dira ya Maendeleo ya Taifa (Tanzania Development Vision, 2025) ilianza kutekelezwa Mwaka 2000. Kupitia Dira hiyo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imedhamiria kujenga uchumi wa kisasa utakaoiwezesha Tanzania kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja (GDP per capita)  kutoka wastani wa Dola za Marekani 640 hadi 3,000 ifikapo Mwaka 2025. Ili kufikia lengo hilo, nchi inahitaji kuwa na nishati ya kutosha, yenye uhakika na ya gharama nafuu. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendeleza jitihada za kuboresha upatikanaji wa nishati bora vijijini na mijini kwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya nishati ikiwemo ya umeme, gesi asilia na mafuta.

18.       Mheshimiwa Spika, sambamba na azma hiyo, Sekta ya Nishati imejumuishwa kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulioanzishwa na Serikali Mwaka 2013/14. Katika Sekta hiyo, miradi 29 iliainishwa ambayo inahusisha miradi 7 ya ufuaji, miradi 7 ya usafirishaji na miradi 14 ya usambazaji umeme pamoja na mradi mmoja wa miundombinu ya gesi asilia. Utekelezaji wa miradi ya BRN utachangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025.

19.       Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kudurusu na kuandaa Sera na Sheria mbalimbali katika Sekta ya Nishati ikiwemo Sera ya Taifa ya Nishati. Lengo ni kujenga mazingira yanayochochea uwekezaji kwa kushirikisha Sekta Binafsi, na hivyo kuongeza ufanisi na ushindani wa kibiashara katika Sekta ya Nishati.

      Mafanikio yaliyopatikana katika  Sekta ya Nishati

20.       Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2013/14 ni pamoja na: kuongezeka kwa idadi ya Watanzania waliounganishiwa umeme (connection level) kutoka asilimia 21 Mwaka 2012/13 hadi kufikia asilimia 24 Mwezi Machi, 2014. Ikumbukwe kwamba kiwango cha uunganishwaji wa umeme kilikuwa asilimia 10 mwaka 2005 wakati Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipoingia madarakani. Mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu waliofikiwa na huduma ya umeme (access level) kufikia asilimia 36 Mwezi Machi, 2014; kukamilika kwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme MW 60 huko Nyakato, Mwanza; kufunga vipozea umeme (transformers) vyenye uwezo wa MVA 15 katika vituo vya Bahari Beach, Gongolamboto, Kigamboni na Kunduchi; kufunga vipozea umeme viwili vyenye uwezo wa MVA 90 kila kimoja katika vituo vya Kipawa na Ubungo; kusainiwa kwa mikataba 35 ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini (Turnkey Phase II); kuwasili kwa mitambo miwili ya kufua umeme yenye uwezo wa MW 75, kati ya mitambo minne ya mradi wa MW150 wa Kinyerezi – I; na kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.

21.       Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni pamoja na: kupitishwa kwa Sera ya Gesi Asilia Mwezi Oktoba, 2013; kukamilika kwa ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam kwa asilimia 77.8; kukamilika kwa maandalizi ya kufunga mitambo ya kusafisha gesi asilia kwa asilimia 44.8; kugunduliwa kwa gesi asilia inayofikia futi za ujazo trilioni 4.8 kwenye visima vilivyopo kina kirefu cha Bahari na hivyo kufanya jumla ya kiasi cha gesi asilia kilichogundulika hapa nchini hadi sasa kufikia futi za ujazo trilioni 46.5; kuzinduliwa kwa duru ya nne ya utafutaji mafuta na gesi asilia katika kina kirefu baharini na Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika; na kuanzishwa kwa kitengo maalumu (Ministerial Delivery Unit - MDU) cha kufuatilia utekelezaji wa miradi ya BRN katika Sekta ya Nishati.

22.       Mheshimiwa Spika, mafanikio yote hayo ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 - 2015 inayosisitiza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya kujenga uchumi wa kisasa na imara unaozingatia maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Ukuaji wa uchumi imara ndio utakaotoa ajira mpya na matumaini mapya kwa vijana na maskini katika nchi yetu.

          SEKTA NDOGO YA UMEME

           Hali ya Uzalishaji Umeme

23.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa umeme nchini. Hadi mwishoni mwa mwezi Aprili, 2014 uwezo wa mitambo yote ya kufua umeme (total installed capacity) ulifikia MW 1,583 (maji - asilimia 35, gesi asilia - asilimia 34 na mafuta - asilimia 31). Uwezo huo wa mitambo yote ni sawa na ongezeko la asilimia 78 ikilinganishwa na MW 891 zilizokuwepo mwaka 2005 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani. Hili ni jambo la kujivunia kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

24.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013 kiasi cha umeme kilichoingizwa kwenye Gridi ya Taifa kiliongezeka na kufikia GWh 5,997.41 ikilinganishwa na GWh 5,760  za Mwaka 2012, sawa na ongezeko la asilimia 4. Aidha, mahitaji ya juu ya matumizi ya umeme kwa Mwaka 2013/14 yalifikia wastani wa MW 898.72 ikilinganishwa na MW 851.35 kwa mwaka 2012/13, sawa na ongezeko la asilimia 6.

          Miradi ya Kufua Umeme

          Mradi wa MW 60 Nyakato - Mwanza

25.       Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa mitambo ya MW 60 inayotumia mafuta mazito katika eneo la Nyakato, Jijini Mwanza. Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 8 Septemba, 2013. Kuzinduliwa kwa mradi huo kumeimarisha upatikanaji wa umeme katika Kanda ya Ziwa Victoria.

      Mradi wa Kinyerezi I - MW 150

26.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa MW 150 kwa kutumia gesi asilia katika eneo la Kinyerezi, Jijini Dar es Salaam unaendelea vizuri. Mradi huo utakapokamilika utapunguza utegemezi wa mitambo ya kukodi inayotumia mafuta kufua umeme ambayo ni ghali. Pia, mitambo miwili yenye uwezo wa kufua MW 75 kati ya mitambo minne (4) iliwasili nchini Mwezi Februari, 2014. Aidha, ujenzi wa misingi ya kuwekea mitambo na matenki mawili (2) ya kuhifadhi mafuta kwa matumizi ya dharura umekamilika. Kazi nyingine zinazoendelea ni ujenzi wa jengo la utawala, karakana pamoja na miundombinu ya barabara na maji. 

27.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa katika Mwaka 2014/15 ni pamoja na kukamilisha ufungaji wa mitambo ya kufua umeme; kujenga kituo cha kupozea umeme chenye uwezo wa kV 220/kV 400; kujenga njia ya kusafirishia umeme ya msongo wa kV 220 kutoka Kinyerezi hadi Kimara; na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 kutoka Kinyerezi hadi kituo cha kupozea umeme cha Gongolamboto. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 183 sawa na Shilingi bilioni 301. Katika Bajeti ya Mwaka  2014/15  Shilingi bilioni 90 sawa na Dola za Marekani milioni 55 ikiwa ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha mradi huu. Mradi unatarajiwa kukamilika katika Mwaka 2014/15 ikiwa ni sehemu ya  kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuondoa kero ya umeme nchini.

Mradi wa Kinyerezi II - MW 240

28.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali ilikamilisha majadiliano na Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Kusini (DBSA), ambapo mkopo wa asilimia 15 ya gharama ya mradi uliidhinishwa. Aidha, majadiliano kwa ajili ya mkopo wa asilimia 85 ya gharama za mradi, kati ya Serikali na Benki za Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) na Japan Bank of International Cooperation (JBIC) za Japan yamekamilika.

29.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Serikali itaanza kutekeleza mradi huo ikiwa ni pamoja na kuagiza mitambo na kuandaa eneo itakapofungwa mitambo hiyo. Mkandarasi wa mradi ni Kampuni ya Sumitomo Corporation kutoka Japan. Gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 344, sawa na Shilingi bilioni 564. Ili kuanza  utekelezaji wa mradi, fedha za nje Shilingi bilioni 1, sawa na Dola za Marekani 609,756 zimetengwa. Ujenzi wa mradi umepangwa kukamilika katika Mwaka 2015/16.

          Mradi wa Kinyerezi III - MW 300

30.       Mheshimiwa Spika, makubaliano ya ubia (Joint Venture Agreement)  kwa ajili ya kuendeleza mradi wa Kinyerezi III kati ya TANESCO na Kampuni ya China Power Investment (CPI) yamekamilika na kusainiwa Mwezi Oktoba, 2013. Taratibu za uundwaji wa Kampuni ya ubia zimekamilika, ambapo Serikali kupitia TANESCO itamiliki asilimia 40 ya hisa na CPI asilimia 60. Katika Mwaka 2014/15, TANESCO na CPI zitateua wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya kuanza kusimamia utekelezaji wa mradi huo. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa ni Dola za Marekani milioni 389 sawa na Shilingi bilioni 638.

          Mradi wa Kinyerezi IV - MW 300

31.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO iliingia Makubaliano ya Awali (MoU) na Kampuni ya Poly Technologies kutoka China Mwezi Septemba, 2013 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa Kinyerezi IV. Mradi utatekelezwa kwa njia ya ubia utakaozihusisha Kampuni za Golden Concord Development Limited (asilimia 40), China – Africa Development Limited (asilimia 30) za China na  TANESCO (asilimia 30).

32.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukamilisha upembuzi yakinifu wa mradi na Tathmini ya Athari za Mazingira na Kijamii (ESIA); kukamilisha mkataba wa ubia na uundwaji wa Kampuni ya ubia; pamoja na uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

33.       Mheshimiwa Spika, miradi niliyoieleza hapo juu inatekelezwa kupitia mfumo mpya wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya kimkakati ya Kitaifa  yaani BRN.

          Mradi wa Kuzalisha MW 600 Mkoani Mtwara

34.       Mheshimiwa Spika, Mwezi Novemba, 2013 Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO iliidhinisha utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa MW 600 Mkoani Mtwara. Mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Mtwara hadi Songea. Kampuni ya Symbion ya Marekani inayotekeleza mradi huo imeajiri Kampuni ya MPR Associates kutoka Marekani kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi. Kazi hiyo imeanza na inategemewa kukamilika Mwezi Juni, 2014. Baada ya kazi hiyo kukamilika Kampuni ya Symbion na TANESCO zitaanza majadiliano kuhusu masuala ya kiufundi na fedha. Utekelezaji wa mradi huo utaimarisha upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na kuingiza katika Gridi ya Taifa. Aidha, ujenzi wa mradi huo utawezesha kuuza umeme wa ziada nchi jirani zikiwemo Malawi na Msumbiji. 

          Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo – MW 80

35.       Mheshimiwa Spika, mradi wa Rusumo unatekelezwa kwa pamoja na nchi za Rwanda na Burundi. Mradi pia unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kutoka Rusumo hadi kwenye mifumo ya usafirishaji umeme kwa nchi husika. Kwa upande wa Tanzania njia ya kusafirisha umeme itaunganishwa katika Gridi ya Taifa katika kituo cha Nyakanazi. Kazi zilizokamilika katika Mwaka 2013/14 ni zifuatazo: upembuzi yakinifu; Tathmini ya Athari ya Mazingira na Kijamii (ESIA); kusainiwa kwa Mkataba wa Utekelezaji Mradi (Implementation Agreement); na Mkataba wa Wana Hisa (Share Holding Agreement). Aidha, majadiliano ya mkopo kati ya Serikali za Burundi, Rwanda na Tanzania, pamoja na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika yalikamilika. Mradi utaanza kutekelezwa Mwaka 2014/15, na utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 164, sawa na Dola za Marekani milioni 100. Fedha za nje zilizotengwa na Serikali ni Shilingi bilioni 2, sawa na Dola za Marekani milioni 1.22 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu.

         Miradi ya Kufua Umeme Kutokana na Makaa ya Mawe

36.       Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia uendelezaji wa miradi ya kufua umeme kutokana na makaa ya mawe ya Kiwira - MW 200, Mchuchuma - MW 600 na Ngaka - MW 400. Miradi ya Mchuchuma na Ngaka inatekelezwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC). Kwa upande wa mradi wa Kiwira unaosimamiwa na STAMICO, kazi zilizofanyika Mwaka 2013/14 ni kudurusu taarifa za kitaalamu za utafiti, upembuzi yakinifu na mazingira zilizofanyika miaka ya nyuma. Kazi zilizopangwa kufanyika katika Mwaka 2014/15 ni pamoja na: kufufua mgodi wenye uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za makaa ya mawe kwa mwaka; kukarabati mtambo wa kufua umeme uliopo mgodini wa MW 6; kukamilisha upatikanaji wa mbia kwa ajili ya mradi mkubwa wa kuzalisha MW 200; na kulipa fidia kwa watakaopisha mradi na njia ya umeme wa msongo wa kV 400 wa urefu wa kilomita 100 kutoka mgodini hadi eneo la Uyole, Mbeya ili kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 400, sawa na takriban Shilingi bilioni 656. Katika Mwaka 2014/15, Shilingi bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza baadhi ya kazi zilizotajwa hapo juu.

 Ukarabati wa Mitambo ya Kufua Umeme katika Kituo cha
 Hale

37.       Mheshimiwa Spika, mradi huu wa ukarabati wa mitambo ya kufua umeme katika kituo cha Hale unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden. Lengo ni kuwezesha kituo hicho kufua umeme kufikia uwezo wake wa juu kabisa wa MW 21 badala ya MW 10 zinazofuliwa sasa. Katika Mwaka 2014/15 Shilingi bilioni 3, sawa na Dola za Marekani milioni 1.83 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa mitambo hiyo.

        Kuimarisha Njia za Kusafirisha na Kusambaza Umeme

   (i)         Mradi wa Iringa - Shinyanga kV 400 (Backbone)

38.       Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu ujenzi wa kilomita 670 za usafirishaji umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma na Singida hadi Shinyanga. Aidha, vituo vya kupozea umeme wa msongo wa kV 400/220/33 pamoja na njia za usambazaji umeme za msongo wa kV 33 zitajengwa. Mwezi Novemba, 2013 TANESCO ilisaini mikataba ya ujenzi na Kampuni za KEC International Limited na Jyoti Structures Limited za India. TANESCO pia ilisaini mkataba na umoja (consortium) wa Kampuni za GS Engineering and Construction na Hyosung kutoka Korea Kusini kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Kazi nyingine iliyofanyika ni ulipaji wa fidia katika maeneo ya Igunga, Kishapu na Shinyanga. Pia, kazi za upimaji (detailed survey), utayarishaji usanifu na uidhinishaji wa michoro zinaendelea.

39.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika katika Mwaka 2014/15 ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya mradi; maandalizi ya usambazaji wa umeme wa Gridi katika vijiji zaidi ya 90 ambako mradi utatekelezwa; na kuanza ujenzi wa njia za usafirishaji umeme. Jumla ya Shilingi bilioni 2.50 sawa na Dola za Marekani milioni 1.52 zimetengwa kwa Mwaka 2014/15 ili kutekeleza mradi huu. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 500 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2 ni fedha za nje kutoka Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Korea (EDCF). Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 224 sawa na Shilingi bilioni 367.36 na unatarajiwa kukamilika Mwaka 2015/16.

      (ii)    Mradi wa Makambako - Songea kV 220

40.       Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ibara 63 (u) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 - 2015, Wizara inaendelea na taratibu za  kuanza utekelezaji wa mradi huo. Mradi utahusisha ujenzi wa kilomita 250 za njia za kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kutoka Makambako hadi Songea; kujenga vituo vikuu viwili  (Madaba na Songea) vya kupozea umeme wa msongo wa kV 220/33  na kuongeza uwezo wa kituo cha kupozea umeme cha Makambako; ujenzi wa kilomita 900 za njia za usambazaji umeme za msongo wa kV 33. Lengo la mradi huu ni kuunganisha Wilaya za Ludewa, Mbinga, Namtumbo, Njombe, Songea Mjini na Songea Vijijini katika Gridi ya Taifa. Mradi pia utahusisha kuwaunganishia wateja wa awali 30,000 ambao watatakiwa kulipia kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pekee.

41.       Mheshimiwa Spika, Mwezi Januari, 2014 TANESCO ilisaini mkataba na Kampuni ya Isolux kutoka Hispania kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme. Aidha, uchambuzi wa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme umekamilika na maombi ya “no objection” yamewasilishwa Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida). Vilevile, ulipaji fidia kwa watakaopisha mradi katika maeneo ya Mkoa wa Ruvuma umekamilika kwa asilimia 95 na uhakiki wa malipo kwa Mkoa wa Njombe unaendelea.

42.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, kazi zilizopangwa kutekelezwa ni kuanza ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme na vituo vya kupozea umeme pamoja na njia za kusambaza umeme. Jumla ya Shilingi bilioni 16.30 sawa na Dola za Marekani milioni 9.94 zimetengwa ili kutekeleza kazi zilizopangwa. Kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni Shilingi milioni 300 na fedha za nje ni Shilingi bilioni 16. Mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2015/16.

    (iii)    Mradi wa North - East Grid kV 400

43.       Mheshimiwa Spika, mradi huu ni wa ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme wa msongo wa kV 400 yenye urefu wa kilomita 664 kutoka Kinyerezi hadi Arusha kupitia Chalinze na Segera. Pia, mradi utahusisha ujenzi wa njia za kusafirishia umeme wa msongo wa kV 220 zenye jumla ya kilomita 104 kutoka Segera kwenda Tanga na kutoka Kibaha kwenda Bagamoyo. Aidha, vituo vikubwa vya kupozea umeme vya Bagamoyo, Chalinze, Segera na Tanga vitajengwa kwa ajili ya kuwezesha usambazaji umeme katika Wilaya na Miji Midogo ambayo njia za umeme zitapita. Kazi zilizokamilika Mwaka 2013/14 ni upembuzi yakinifu wa mradi; Tathmini ya Athari za Mazingira na Kijamii (ESIA); na upimaji wa awali wa ardhi. Aidha, kazi za usanifu wa michoro ya mradi na uchambuzi wa zabuni kwa ajili ya kumpata mshauri wa mradi zinaendelea.

44.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kwa Mwaka 2014/15 ni pamoja na kukamilisha upimaji wa ardhi na kuweka mipaka ya eneo la mradi; kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha eneo la mradi; na kumpata mshauri kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa mradi. Jumla ya Shilingi bilioni 1.50 sawa na Dola za Marekani 914,630 zimetengwa ili kutekeleza mradi huu. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 1.0 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 500 ni fedha za nje. Mradi unatarajiwa kukamilika Mwaka 2016/17.       

    (iv)    Mradi wa North - West Grid kV 400 

45.       Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400  kutoka Mbeya  kupitia Sumbawanga – Mpanda - Kigoma hadi Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 1,148. Awamu ya kwanza ya mradi itahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 340 kutoka Mbeya hadi Sumbawanga, na vituo vikubwa vipya vya kupozea umeme vya Uyole (Mbeya) na Sumbawanga.   
 
46.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizofanyika kwa Mwaka 2013/14 ni pamoja na kutathmini upya  Athari za Mazingira na Kijamii (ESIA); kudurusu upembuzi yakinifu baada ya kubadilisha njia ya kusafirisha umeme kutoka msongo wa kV 220 kwenda kV 400; upimaji wa mkuza itakakojengwa njia ya kusafirisha umeme; na kutathmini fidia kwa watakaopisha awamu ya kwanza ya mradi.

47.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kufanyika Mwaka 2014/15 ni pamoja na kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi ili kuwiana na mahitaji ya sasa ya msongo wa kV 400; upimaji wa mkuza itakakojengwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mbeya hadi Sumbawanga; na kulipa fidia kwa watakaopisha mradi. Fedha za ndani Shilingi bilioni 1.0, sawa na Dola za Marekani 609,756 zimetengwa. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Mwaka 2016/17. 


      (v)    Mradi wa Singida – Arusha - Namanga kV   400

48.        Mheshimiwa Spika, Ibara ya 63 (b) na (t) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 - 2015 inatoa msisitizo kuhusu kuunganisha Gridi yetu ya Taifa na nchi jirani ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Mradi wa Singida - Arusha - Namanga ni  sehemu ya mradi wa Zambia – Tanzania – Kenya (ZTK interconnector) yenye urefu wa kilomita 2,047. Kwa upande wa Tanzania, mradi utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Arusha na kutoka Iringa hadi Mbeya.

49.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, kazi zilizofanyika ni zifuatazo: kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa mradi na Tathmini ya Athari za Mazingira na Kijamii (ESIA); na upimaji wa mkuza kwa ajili ya njia ya kusafirisha umeme. Kazi zilizopangwa kufanyika Mwaka 2014/15 ni pamoja na kukamilisha tathmini ya mali na kulipa fidia; ujenzi wa kituo kipya cha kupozea umeme katika eneo la Kisongo, Mkoani Arusha na upanuzi wa kituo cha kupozea umeme Mkoani Singida. Kazi nyingine ni kuajiri mshauri wa mradi na kupata wakandarasi wa ujenzi wa vituo vya kupozea umeme na njia ya kusafirisha umeme; na kuandaa mpango wa kusambaza umeme kwenye vijiji vilivyo kando kando ya njia ya kusafirisha umeme. Fedha za nje zilizotengwa ni Shilingi milioni 500, sawa na Dola za Marekani 304,878 ambazo ni mkopo kutoka AfDB na JICA. Mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2016/17.    

50.       Mheshimiwa Spika, sambamba na jitihada hizo, Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa upanuzi wa njia ya usambazaji umeme ya Tunduma hadi Nakonde (Zambia) ya msongo wa kV 33 na urefu wa mita 100. Mradi pia utahusisha ufungaji wa kipozea umeme chenye uwezo wa kVA 200 na ukarabati wa njia ya kusambaza umeme kutoka Mbeya hadi Tunduma yenye urefu wa kilomita 40. Katika Mwaka 2013/14, upimaji na tathmini ya njia ya usambazaji umeme vilikamilika. Aidha, Kitengo cha kusimamia mradi kimeundwa na taarifa ya Tathmini ya Athari za Mazingira na za Kijamii imewasilishwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira la Taifa (NEMC) kwa ajili ya kupata idhini ya utekelezaji wa mradi. Katika Mwaka 2014/15, Serikali imetenga Shilingi bilioni 5, sawa na Dola za Marekani milioni 3.05 ili kuendelea na  utekelezaji wa mradi huu.

    (vi)    Mradi wa Bulyanhulu – Geita kV 220

51.       Mheshimiwa Spika, mradi unahusu ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 220 yenye urefu wa kilomita 55 kutoka Bulyanhulu hadi Geita. Mradi pia unahusisha ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha Geita chenye uwezo wa kV 220/33, usambazaji umeme katika vijiji vilivyopo ndani ya eneo la mradi na kubadilisha mita za umeme za kawaida (conventional meters) zipatazo 2,000 Mkoani Geita kwa kufunga mita za LUKU. Kazi zilizofanyika Mwaka 2013/14 ni pamoja na: kuundwa kwa Kitengo cha usimamizi wa mradi (Project Implementation Unit) na kuanza kwa taratibu za upimaji wa eneo la mradi. Aidha, tathmini ya zabuni ya kumpata mshauri wa mradi inaendelea.

52.       Mheshimiwa Spika, kazi zitakazofanyika Mwaka 2014/15 ni zifuatazo: kukamilisha upimaji wa eneo la mradi; kulipa fidia kwa watakaopisha mradi; kumpata mshauri na mkandarasi wa mradi; na kuanza utekelezaji wa mradi. Gharama za mradi ni Shilingi bilioni 41 sawa na Dola za Marekani milioni 25. Jumla ya Shilingi bilioni 2.50 sawa na Dola za Marekani milioni 1.52 zimetengwa ili kutekeleza mradi huu. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 2 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 500 ni fedha za nje kutoka Bank of Arab for Economic Development in Africa (BADEA). Mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2015/16.

          (vii)               Mradi wa Electricity V

53.       Mheshimiwa Spika, mradi unalenga  kuunganisha wateja wa awali 8,600 kwenye Wilaya za Bukombe, Busega, Kwimba, Magu, Mbogwe, Misungwi na Sengerema katika Mikoa ya Geita, Mwanza na Simiyu. Ujenzi wa njia za usambazaji wa umeme wa msongo wa kV 33 zenye urefu wa kilomita 480, kV 0.4 zenye urefu wa kilomita 231 na ufungaji wa vipozea umeme 109 utafanyika chini ya mradi huu. Shughuli nyingine ni ukarabati wa vituo vya kupozea umeme vya Ilala kV 132/33/11 na Sokoine kV 33/11, katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na upanuzi wa kituo cha kupozea umeme cha kV 220/132/33 Njiro, Mkoani Arusha.         

54.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 kazi zilizofanyika ni pamoja na: kuanza kwa ukarabati wa kituo cha kupozea umeme cha Sokoine Drive, Ilala (Dar es Salaam); kukamilisha ukaguzi wa maeneo na michoro ya kazi za usambazaji umeme; kukamilika kwa utafiti wa udongo kwenye vituo vya kupozea umeme vya Sokoine Drive, Ilala (Dar es Salaam)  na Arusha; kuanza kwa ulipaji fidia kwa watakaopisha mradi; kuwasili kwa vifaa vya usambazaji umeme ikiwa ni pamoja na nguzo 890 katika maeneo ya mradi; na kuendelea kwa kazi ya usanifu wa mradi.

55.       Mheshimiwa Spika, kazi zitakazotekelezwa katika Mwaka 2014/15 ni zifuatazo: kukamilisha ukarabati wa kituo cha Sokoine Drive, Ilala (Dar es Salaam) na Arusha. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 45 sawa na Shilingi bilioni 73.80. Jumla ya Shilingi bilioni 4, sawa na Dola za Marekani milioni 2.44 zimetengwa ili kutekeleza kazi zilizopangwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 3.50 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 500 ni fedha za nje kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2014/15. 

Mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Umeme Jijini Dar es   Salaam

56.       Mheshimiwa Spika, mradi huu unafadhiliwa na Serikali za Finland na Japan na unahusu ujenzi wa kituo kipya cha kupozea umeme mkabala na kituo cha City Centre cha msongo wa kV 132/33/11, ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme wa msongo wa kV 132 kutoka kituo cha Ilala na kuunganisha mfumo wa vituo vya kupozea umeme wa kV 33/11 vya City Centre, Kariakoo, Railway na Sokoine. Lengo la mradi huu ni kuboresha miundombinu ya umeme ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wenye ubora na uhakika zaidi katika Jiji la Dar es Salaam.

57.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa kwa Mwaka 2013/14 ni zifuatazo: kupatikana kwa eneo la ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha City Centre; kukamilisha upembuzi yakinifu wa mradi; ulipaji fidia kwa watakaopisha mradi; na kuanza kwa ujenzi wa kituo. Kazi zifuatazo zitatekelezwa kwa Mwaka 2014/15: kuendelea na ujenzi wa kituo cha City Centre na njia za usafirishaji na usambazaji umeme. Gharama za mradi ni Shilingi bilioni 123 sawa na Dola za Marekani milioni 75. Fedha za nje zilizotengwa ni Shilingi bilioni 1.0 na mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2014/15.

Mradi wa Ufuaji na Usambazaji Umeme – Biharamulo,  Mpanda na Ngara (ORIO)

58.       Mheshimiwa Spika, mradi unahusisha ufungaji wa jenereta zenye uwezo wa MW 2.5 kila moja katika Wilaya za Biharamulo, Mpanda na Ngara na hivyo kufanya jumla ya uwezo wa MW 7.5. Pia, ukarabati wa njia zilizopo na ujenzi wa njia mpya za usambazaji umeme zenye msongo wa kV 33 utafanyika. Lengo la mradi huu ni kuongeza uwezo wa ufuaji na usambazaji umeme katika Wilaya hizo.

59.       Mheshimiwa Spika, kazi zilizofanyika katika Mwaka 2013/14 ni pamoja na: kusainiwa kwa mkataba kwa ajili ya ufungaji jenereta hizo kati ya TANESCO na Kampuni ya M/s Zwart Techniek B.V. ya Uholanzi Mwezi Oktoba, 2013; kusainiwa kwa mikataba kati ya TANESCO na Kampuni ya Nakuroi Investment ya Tanzania kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mifumo ya usambazaji umeme Mpanda; na Kampuni ya NAMIS ya Tanzania kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mifumo ya usambazaji umeme katika Wilaya za Biharamulo na Ngara. Mikataba husika ilisainiwa Mwezi Desemba, 2013.

60.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15 kazi zitakazofanyika ni zifuatazo: kufunga jenerata katika Wilaya za Biharamulo, Mpanda na Ngara; kukarabati na kujenga njia mpya za usambazaji umeme katika Wilaya za Mpanda, Biharamulo na Ngara; na kutoa mafunzo kwa ajili ya usimamizi wa miradi kwa wajasiriamali na watumiaji wa umeme katika Wilaya hizo. Mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuwaunganishia umeme wateja wapya zaidi ya 100,000.

61.       Mheshimiwa Spika, gharama za mradi huo ni EURO milioni 33.15 sawa na Shilingi bilioni 81.55. Jumla ya Shilingi bilioni 22.50 sawa na Dola za Marekani milioni 13.72 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huu Mwaka 2014/15. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 22 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 500 ni fedha za nje kutoka Serikali ya Uholanzi. Mradi umepangwa kukamilika Mwaka 2015/16.

Usambazaji Umeme kupitia TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

62.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Ibara ya 63 (c) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 – 2015, inayohamasisha kuongeza idadi ya wananchi waliounganishiwa umeme mijini na vijijini.  Wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani kiwango cha uunganishwaji (connection level) nchini kilikuwa asilimia 10. Kufuatia jitihada mahsusi za Serikali ikiwemo punguzo la gharama za kuunganisha umeme pamoja na uwezeshaji chini ya Mfuko wa Nishati Vijijini (Rural Energy Fund - REF), kiwango cha uunganishwaji umeme kimeongezeka na kufikia asilimia 24 Mwezi Machi 2014. Lengo la Serikali ni kuwawezesha Watanzania asilimia 30 kuunganishiwa umeme (connection) ifikapo Mwaka 2015/16. Aidha, kiwango cha uunganishwaji umeme vijijini kimeongezeka kutoka asilimia 2 Mwaka 2005 hadi asilimia 7 mwishoni mwa Mwaka 2013.

63.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mwezi Machi, 2014 watu wanaopata huduma ya umeme (access level) walifikia asilimia 36 ya Watanzania waishio Bara. Hivyo, Watanzania wanashauriwa kutumia fursa ya huduma ya umeme ili ichangie katika shughuli za kiuchumi na kijamii na hivyo kuinua hali ya maisha yao mijini na vijijini na kuanza kupunguza na hatimaye kutokomeza umaskini.

64.       Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nyingine, mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini uliokuwa na miradi midogo 41 katika Mikoa 16 ya Tanzania Bara (Arusha, Dodoma, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga). Kuanzia Mwezi Julai 2013 hadi Aprili 2014, wateja wapya 15,817 walikuwa wameunganishiwa umeme kati ya wateja 22,000 waliotarajiwa. Aidha, kupitia lengo la BRN la kuunganisha wateja 150,000 kwa mwaka, jumla ya wateja wapya 138,931 waliunganishiwa umeme sawa na asilimia 92.62 ya lengo hilo. Ongezeko hili linatokana na uamuzi wa Serikali kupunguza gharama za kuunganishia umeme wa wateja wa njia moja (single phase) mijini na vijijini kwa wastani wa kati ya asilimia 30 hadi 77 ulioanza kutekelezwa Mwezi Januari, 2013.

65.       Mheshimiwa Spika, REA imesaini mikataba na wakandarasi 35 wa kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara. Utekelezaji wa mradi huo utaendelea katika Mwaka 2014/15, ambapo jumla ya Shilingi bilioni 290.20 sawa na Dola za Marekani 176.95 zimetengwa kutekeleza miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 269.20 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 21 ni fedha za nje kutoka Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD).

Mpango wa Kitaifa wa Kuhamasisha Uwekezaji kwenye Usambazaji Umeme

66.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Usambazaji Umeme Nchini kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia Mwaka 2013 hadi 2022 (The National Electrification Programme Prospectus). Katika kipindi hicho, Mpango huo utakuwa ndiyo mwongozo wa miradi ya Serikali ya kusambaza umeme vijijini. Maandalizi ya Mpango huo yamefadhiliwa na Serikali ya Norway.

Mradi wa Kusambaza Umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara

67.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia REA inaendelea na utekelezaji wa jumla ya miradi 52 ya kusambaza umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Hadi Mwezi Aprili, 2014 miradi 47, sawa na asilimia 97 ilikamilika, ambapo wateja 1,925 waliunganishiwa umeme. Kati ya hao wateja 1,135 ni kutoka Mkoa wa Lindi na wateja 790 ni kutoka Mkoa wa Mtwara. Gharama za miradi hiyo ni Shilingi bilioni 6.10, sawa na Dola za Marekani milioni 3.72. Katika Mwaka 2014/15, Serikali itakamilisha miradi mitano (5) iliyobaki. Gharama ya kuunganisha umeme kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni Shilingi 99,000 kwa umbali usiozidi mita 30. Gharama hizi zitatumika hadi kufikia Mwezi Juni, 2015. Natoa ushauri kwa wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia fursa hiyo kuunganishiwa umeme ili kuboresha maisha yao kupitia shughuli endelevu za kiuchumi na kijamii.

Tanzania Energy Development and Access Expansion Project (TEDAP)

68.       Mheshimiwa Spika, mradi huu ni wa uboreshaji wa mifumo ya Gridi (on-grid) na kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu kama vyanzo mbadala vya kufua umeme nje ya Gridi (off-grid). Kazi zilizotekelezwa Mwaka 2013/14 kwa upande wa Gridi ni zifuatazo: kukamilika kwa ufungaji wa vipozea umeme viwili vyenye uwezo wa MVA 20 katika kituo cha umeme cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Kukamilika kwa kazi hiyo kumeboresha upatikanaji umeme katika maeneo ya Mererani, Usa River na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Gharama za mradi huo kwa upande wa on-grid ni Dola za Marekani  milioni 114.50 sawa na Shilingi bilioni 187.78. Aidha, kwa upande wa mifumo ya nje ya Gridi, kazi zilizofanyika ni zifuatazo: kuwezesha ukamilishaji wa mradi wa maporomoko madogo ya maji wa Mapembasi (Njombe)  unaotekelezwa na Sekta Binafsi; kuwezesha wafuaji wa umeme wa uwezo mdogo (small power producers) kutumia mkopo kutoka Benki ya Dunia (IDA Credit Line); kugharamia ukamilishaji mradi wa pamoja na kufunga mifumo ya Umeme Jua katika Wilaya za Bunda, Geita na Tandahimba; na kukagua mifumo ya Umeme Jua katika Wilaya ya Sumbawanga chini ya Awamu ya Kwanza ya Sustainable Solar Market Packages (SSMP). Gharama za mradi kwa upande wa off-grid ni Dola za Marekani  milioni 47.50 sawa na Shilingi bilioni 77.90. Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya Dunia na Serikali ya Korea ya Kusini.

69.       Mheshimiwa Spika, kazi zitakazotekelezwa kwa Mwaka 2014/15 ni zifuatazo: kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro; kuendelea kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya nishati bora; na kufadhili ujenzi wa mitambo ya kufua umeme kwenye maporomoko madogo ya maji. Aidha, Awamu ya Pili ya SSMP itahusisha ufungaji wa mifumo ya Umeme Jua kwenye taasisi za kijamii, makazi ya watu na sehemu za biashara. Wilaya zitakazonufaika ni Biharamulo, Bukombe, Chato, Kasulu, Kibondo, Namtumbo, Sikonge na Tunduru. Jumla ya Shilingi bilioni 4.7, sawa na Dola za Marekani milioni 2.87 zimetengwa ili kutekeleza kazi zilizopangwa. Kati ya fedha hizo, fedha za ndani ni Shilingi milioni 700, sawa na asilimia 15; na fedha za nje ni Shilingi bilioni 4, sawa na asilimia 85 ya gharama zote za mradi.

70.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha uendelezaji wa miradi ya kufua umeme kwa kutumia maporomoko madogo ya maji. Katika Mwaka 2013/14, Serikali kupitia EWURA ilitoa leseni tatu kwa Kampuni za Mwenga Hydro Limited ya Mufindi (MW 4); Ngombeni Power Limited ya Kisiwani Mafia (MW 1.5); Mapembasi ya Njombe (MW 10); na Tangulf Express Limited ya Njombe (MW 10).

71.       Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya uwekezaji katika miradi midogo isiyozidi MW 10 ya kufua umeme kwa kutumia nishati jadidifu, katika Mwaka 2014/15, Serikali kupitia EWURA itakamilisha durusu ya Mwongozo wa mikataba ya kuuziana umeme (Standardised Power Purchase Agreement - SPPA) na Kanuni ya kukokotoa bei ya kuuziana umeme kwa miradi yenye uwezo wa  kufua umeme kati ya kW 100 mpaka MW 10. Kukamilika kwa Kanuni na Mwongozo huo kutaimarisha uwekezaji nchini kwani bei itazingatia gharama halisi za kufua umeme pamoja na aina ya teknolojia itakayotumika. Lengo ni kuongeza kasi ya kuwapatia wananchi huduma ya umeme, hususan vijijini.

Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme Kilombero na Ulanga

72.       Mheshimiwa Spika, mradi huu unatekelezwa chini ya Mpango wa Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) katika maeneo ya Kilombero na Ulanga. Katika Mwaka 2013/14 upembuzi yakinifu ulikamilishwa. Katika Mwaka 2014/15, kazi zitakazofanyika ni pamoja na zifuatazo: kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 220; ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha kV 220/33 chenye uwezo wa MVA 20; na ujenzi wa njia za kusambaza umeme. Ili kutekeleza mradi huu, jumla ya fedha za nje Shilingi bilioni 1.0, sawa na Dola za Marekani 609,756 zitatolewa na Umoja wa Nchi za Ulaya.

          Kuboresha Upatikanaji wa Umeme

73.       Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa huduma ya umeme katika shughuli za kiuchumi na kijamii, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuiwezesha TANESCO kutoa huduma bora. Miradi hiyo  ni ya kipindi cha mpito wakati Serikali inakamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme wa gesi asilia. Katika Mwaka 2014/15, jumla ya Shilingi bilioni 145, sawa na Dola za Marekani milioni 88 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 20, sawa na asilimia 14 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 125, sawa na asilimia 86 ni fedha za nje kutoka Benki ya Dunia.

74.       Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea na zoezi la kutathmini muundo wa TANESCO na kuandaa Mwelekeo Mpya wa Sekta Ndogo ya Umeme (Electricity Supply Industry Reform Roadmap). Vilevile, Serikali imempata mshauri Kampuni ya PriceWaterCoopers (PWC) kutoka Uingereza, ambaye ametoa ushauri kuhusu zoezi hilo. Serikali inategemea kutangaza Roadmap hiyo ifikapo Mwezi Juni, 2014.

75.       Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuupongeza uongozi wa TANESCO na watumishi wote kwa mabadiliko ambayo wameanza kuyatekeleza katika Shirika hilo na matokeo kuanza kuonekana. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuhamisha shughuli za ununuzi, utekelezaji wa Bajeti na Mipango kutoka Makao Makuu kwenda Ofisi za Kanda na Mikoa kwa nia ya kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi. Utaratibu huu utasaidia kuongeza kasi ya kupeleka umeme wilayani na vijijini pamoja na kuharakisha matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya umeme.


  Uboreshaji wa Huduma kwa Wateja

76.       Mheshimiwa Spika, pamoja na mahitaji ya juu ya umeme (Maximum Demand) kuongezeka kwa asilimia 8 kati ya Mwaka 2011 na 2013, TANESCO imehakikisha kuwa huduma ya umeme inaendelea kupatikana nchini. Sambamba na jitihada za TANESCO, inatarajiwa kuwa umeme wa uhakika utaendelea kupatikana kwa Mwaka 2014/15 kama ilivyokuwa kwa 2013/14. Pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali, naipongeza TANESCO kwa kuboresha utoaji huduma ya umeme nchini na hivyo kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii.

77.       Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kuhakikisha kuwa vifaa vyote muhimu vya kuunganishia umeme wateja vikiwemo nguzo, mita na nyaya vinapatikana kwa wakati. TANESCO pia imeendelea kuboresha huduma mbalimbali kwa wateja zikiwemo: kutumia mtandao (on-line) kupata fomu za maombi ya mwanzo ya kuunganishiwa umeme na kulipia ankara kwa wateja wanaolipa baada ya kutumia umeme; utoaji wa taarifa za katizo la umeme kwa ujumbe mfupi wa simu (sms);  kuanzisha vituo maalum (point of sales) vya kulipia umeme karibu na wanachi; kulipia umeme kupitia benki; mpango wa kuwaunganishia wateja majumbani na Ofisi za Serikali mita za LUKU utakaotekelezwa na kukamilishwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu pamoja kuongeza matumizi ya mita za kisasa zijulikanazo kama Automatic Meter Reading (AMR).


(i)     Uendelezaji wa Umeme wa Jua

78.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, wasambazaji wa mifumo ya Umeme wa Jua nchini  waliongezeka kufuatia kukua kwa mahitaji na matumizi ya aina hiyo ya nishati. Aidha, wawekezaji wengi walionesha nia ya kujenga mifumo ya Umeme wa Jua yenye uwezo wa kuanzia MW 50 hadi MW 500 kwa ajili ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Katika Mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya Umeme wa Jua.

79.       Mheshimiwa Spika, Mwezi Januari, 2014 Serikali ilisaini Mkataba na Kampuni ya Elektro-Merl kutoka Austria kwa ajili ya kuleta na kufunga jenereta 14 za Umeme wa Jua (Photovoltaic Generators) zitakazotumika kusambaza umeme vijijini. Mradi huo utatekelezwa katika Mikoa ya Dodoma, Katavi, Ruvuma na Tabora. Gharama za mradi huo ni Euro milioni 5.38 sawa na Shilingi bilioni 14.20.

(ii)   Uendelezaji wa Nishati ya Upepo

80.       Mheshimiwa Spika, taratibu za uendelezaji wa nishati ya upepo kupitia Sekta Binafsi zipo katika hatua mbalimbali. Majadiliano ya kuuziana umeme (Power Purchase Agreement - PPA) kati ya TANESCO na Kampuni ya Geo Wind Power (Singida) yanaendelea. Katika awamu ya kwanza (2015/16), Kampuni hiyo inatarajia kufua umeme wa MW 50 ambapo Dola za Marekani milioni 136, sawa na Shilingi bilioni 223 zitatumika. Aidha, Kampuni ya Wind East Africa Limited (Singida) iliendelea na maandalizi ya kufua umeme wa MW 100 na kulipa fidia kwa watakaopisha mradi. Vilevile, Kampuni ya Sino-Tan Renewable Energy Limited inatarajia kutekeleza mradi wa kufua umeme MW 100 katika eneo la Makambako, Mkoani Njombe. Kwa sasa Kampuni hizo zinatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi yao. Katika Mwaka 2014/15, Kampuni hizo zitakamilisha mikataba ya kuuziana umeme na TANESCO pamoja na taratibu za kupata mikopo.

(iii) Uendelezaji Tungamotaka (Biomass)

81.       Mheshimiwa Spika, Watanzania wengi bado wanategemea tungamotaka hasa kuni na mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia. Katika Mwaka 2013/14, Serikali ilikamilisha Mpango wa Kuendeleza Tungamotaka, ambao unalenga kuboresha matumizi ya nishati hiyo. Katika Mwaka 2014/15, kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukusanya taarifa kuhusu viwanda vinavyofua au vinavyoweza kufua umeme kutokana na mabaki yatokanayo na shughuli za viwanda vya sukari, mbao na karatasi.
(iv) Uendelezaji wa Bioenergies

82.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Rasimu ya Sera na Sheria ya Bioenergies, na kufanya tathmini ya kina kuhusu uzalishaji wa bio-diesel kwa kutumia mafuta ya mimea. Katika Mwaka 2014/15, utekelezaji utalenga kuhamasisha uendelezaji wa Bioenergies na kukamilisha Sheria ya Bioenergies. Jumla ya Shilingi milioni 800, sawa na Dola za Marekani 487,805 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo. Kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 300, sawa na asilimia 37.5 ni fedha za ndani; na Shilingi milioni 500, sawa na asilimia 62.5 ni fedha za nje kutoka Sida (Sweden) na NORAD    (Norway).

83.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali kwa  kushirikiana na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia (CARMATEC) ilitekeleza Mpango wa uendelezaji wa biogas katika ngazi ya kaya. Kupitia Mpango huo, jumla ya mitambo 9,000 ilijengwa katika Mikoa 22 nchini. Katika Mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya biogas majumbani, vituo vya afya, zahanati na katika shule mbalimbali.

(v)   Uendelezaji Jotoardhi (Geothermal)

84.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Kampuni inayoitwa Tanzania Geothermal Development Company Limited (TGDC). Kampuni hiyo itaratibu utafiti, uchorongaji visima, uendelezaji wa jotoardhi na kutoa ushauri wa kitalaamu. Serikali pia inatekeleza Mpango unaoitwa Scaling-Up Renewable Energy  (SREP) unaofadhiliwa na mfuko wa Climate Investment Funds (CIF) na kuratibiwa na AfDB. Serikali imepata Dola za Marekani 700,000 sawa na Shilingi bilioni 1.15 kwa ajili ya maandalizi ya mradi huu. Miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni uendelezaji wa nishati jadidifu vijijini (Renewable Energies for Rural Electrification) pamoja na matumizi ya jotoardhi kama chanzo kipya cha nishati nchini. Thamani ya mradi huu ni Dola za Marekani milioni 50, sawa na Shilingi bilioni 82.

85.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Serikali kupitia TGDC itachoronga visima vyenye kina kifupi katika Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupima mwongezeko wa joto chini ya ardhi. Aidha, Mpango wa kuendeleza Jotoardhi nchini utaandaliwa. Katika kuendeleza ushirikiano na nchi wanachama wa African Rift Geothermal (ARGeo) pamoja na kuhamasisha uendelezaji wa jotoardhi nchini, Serikali kwa kushirikiana na UNEP inaandaa kongamano la kikanda kuhusu Jotoardhi litakalofanyika Jijini Arusha Mwezi Oktoba, 2014. Katika Mwaka 2014/15, Shilingi bilioni 11.0, sawa na Dola za Marekani milioni 6.71 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 10.0, sawa na asilimia 90.9 ni fedha za ndani; na Shilingi bilioni 1.0, sawa na asilimia 9.1 ni fedha za nje.
 
(vi) Matumizi Bora ya Nishati

86.       Mheshimiwa Spika, matumizi bora ya nishati (Energy Conservation and Efficiency) ni mpango muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati na kupunguza uharibifu wa mazingira. Jitihada za kuendeleza matumizi bora ya nishati zimeelekezwa katika sekta za kiuchumi zikiwemo: afya, biashara, elimu, makazi, migodi, kilimo, usafirishaji na viwanda. Lengo la mradi huu ni kupunguza upotevu wa nishati hasa ya umeme. Katika Mwaka 2014/15, Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa kusimamia matumizi bora ya umeme (Demand Side Management) katika Taasisi za Serikali kwa kubadilisha jumla ya taa milioni 3.2 zitumiazo umeme mwingi (Incandescent bulbs) na kuweka taa zitumiazo umeme kidogo (Compact Fluorescent Light - CFL) na hivyo kuwezesha kuokoa takriban MW 37.9 baada ya mradi huu kukamilika. Kiasi hiki cha umeme kinaweza kutosheleza mahitaji ya Mkoa wa Mbeya. Mradi huu utatekelezwa katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Tanga ambapo matumizi ya umeme ni makubwa. Gharama ya kutekeleza mradi huu ni Shilingi bilioni 24, sawa na Dola za Marekani milioni 14.63.

87.       Mheshimiwa Spika, sambamba na mradi huo, TANESCO pia inafanya juhudi za kupunguza upotevu wa umeme katika njia za usafirishaji na usambazaji umeme (Supply Side Management), kwa kuboresha miundombinu yake. Katika Mwaka 2014/15, Serikali inakusudia kufanya yafuatayo: kujenga uwezo wa kitaasisi katika masuala ya matumizi bora ya nishati; kuratibu tafiti za kupunguza upotevu wa nishati; na ukaguzi wa matumizi ya nishati (Energy Audit) kwa kushirikiana na Kampuni ya KEMCO kutoka Korea Kusini ambayo imesaini Makubaliano ya Awali (MoU) na Wizara ya Nishati na Madini. Shilingi milioni 600, sawa na Dola za Marekani 365,854 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huu, ambapo Shilingi milioni 400, sawa na asilimia 66.67 ni fedha za ndani na Shilingi milioni 200, sawa na asilimia 33.33 ni fedha za nje kutoka Sida (Sweden).

          SEKTA NDOGO YA GESI ASILIA NA MAFUTA

  Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara  na Lindi hadi Dar es Salaam

88.       Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mwezi Aprili, 2014 mabomba yote 45,693 kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara (Madimba) na Lindi (Songo Songo) hadi Dar es Salaam yalikuwa yameletwa nchini. Ufukiaji wa mabomba hayo umekamilika kwa umbali wa kilomita 182 kati ya 542 sawa na asilimia 34. Kazi ya ujenzi wa Bomba la kutoka Songo Songo kupitia baharini hadi Somanga Fungu, lenye urefu wa kilometa 25.6 imekamilika kwa asilimia 100. Kwa ujumla ujenzi wa Bomba la gesi asilia umekamilika kwa asilimia 78. Kazi ya kuweka mkongo wa mawasiliano (Fibre Optic Cable) inafanyika sambamba na ufukiaji wa Bomba. Aidha, mtambo wa kuchimbia mabomba katika Mto Rufiji (horizontal drilling) uliletwa nchini Mwezi Aprili, 2014.

89.       Mheshimiwa Spika, shughuli za ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia katika eneo la Madimba, Mtwara na Songo Songo, Lindi zinaendelea. Hadi kufikia Mwezi Aprili, 2014 ujenzi wa nyumba za kuishi wafanyakazi kwa eneo la Madimba ulikuwa umekamilika kwa asilimia 90 na Songo Songo kwa asilimia 78. Aidha, ujenzi wa misingi (foundations) ambako mitambo ya kusafisha gesi asilia itafungwa umekamilika. Vilevile, utengenezaji (manufacturing) wa  mitambo yote ya kusafisha gesi asilia umekamilika kwa asilimia 60. Mitambo hiyo itaanza kuwasili nchini kuanzia Mwezi Julai, 2014 kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Kwa ujumla maandalizi ya kufunga mitambo ya kusafisha gesi asilia yamekamilika kwa asilimia 45.
90.       Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kwa dhati kukamilisha ujenzi wa Bomba ifikapo Mwezi Julai, 2014 na mitambo ya kusafisha gesi asilia ifikapo Mwezi Desemba, 2014. Mradi huu utagharimu Dola za Marekani bilioni 1.2, sawa na takriban Shilingi trilioni 2. Fedha za ndani zilizotengwa kwa Mwaka 2014/15 ni Shilingi bilioni 148, sawa na Dola za Marekani milioni 90.

         Usambazaji wa Gesi Asilia Lindi, Mtwara na Pwani

91.       Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umeweka matoleo (tie - out) kwa ajili ya kusambaza gesi asilia katika miji mikubwa yote ambapo Bomba hilo linapita ikiwemo miji ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Kisarawe. Serikali itawezesha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa ajili ya mitambo ya kufua umeme, matumizi viwandani, Taasisi mbalimbali, majumbani na kwenye magari katika Mikoa hiyo. Katika Mwaka 2013/14, zabuni ilitangazwa kwa ajili ya kumpata Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi na Tathmini ya Athari za Mazingira na Kijamii (ESIA) kwa ajili ya usambazaji wa gesi asilia katika miji ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Kisarawe. Mshauri amepatikana na anatarajiwa kuanza kazi Mwezi Juni, 2014 na kukamilisha kazi hiyo baada ya miezi mitatu (3). Kazi zitakazofanyika katika Mwaka 2014/15 ni pamoja na utafiti wa  mahitaji ya gesi asilia katika viwanda, Taasisi mbalimbali, magari na majumbani; na mfumo na miundombinu ya kufikisha gesi asilia katika maeneo yatakayoainishwa. Aidha, baadhi ya viwanda na kampuni mbalimbali zimeanza majadiliano ya mikataba na TPDC ili kupatiwa gesi asilia. Kampuni hizo ni pamoja na Dangote (Mtwara) na MEIS (Lindi) kwa ajili ya uzalishaji wa saruji; na Kilwa Energy (Kilwa) kwa ajili ya kufua umeme.

92.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kusimamia ukamilishaji wa upembuzi yakinifu wa mradi. Vilevile, Serikali itampata mshauri atakayefanya usanifu na michoro (Detailed Engineering Design and Drawings) ya miundombinu pamoja na vituo vya kujazia gesi asilia iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas) kwenye magari.  Mshauri huyo ataongoza zoezi la kumpata mkandarasi na atasimamia ujenzi wa mradi. Fedha za ndani zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo ni Shilingi bilioni 5.

           Shughuli za Utafutaji wa Mafuta

93.       Mheshimiwa Spika, utaratibu wa awali wa kupata Kampuni za kuja kufanya utafiti wa mafuta na gesi asilia nchini toka miaka ya 1952 ulikuwa kwa Kampuni husika kuomba eneo inalolitaka kufanya utafiti na kupewa bila ushindani. Kwa wakati huo, maeneo yaliyohusika yalikuwa ya nchi kavu na siyo kwenye kina kirefu cha Bahari. Kuanzia Mwaka 1973 hadi 1999, TPDC ilianza kujitangaza Kimataifa kwa nia ya kupata wawekezaji na kushawishi Kampuni za nje zenye uwezo, kuja nchini kwa ajili ya utafutaji mafuta. Kampuni zilizojitokeza ni:  Agip ya Italia; Aminex, BP, Heritage, Petrodel, Tullow za Uingereza; Ammoco na Exxon za Marekani; Artumas ya Canada; Beach Petroleum, Ndovu Resources na Swala za Australia; Bubin ya Ireland; KUFPEC na IEDC za Kuwait; Maurel and Prom ya Ufaransa; Motherland ya India; Shell ya Uholanzi; na Tanganyika Oil ya Misri yalikuja nchini kufanya utafiti katika nyakati tofauti. Tafiti hizo zilifanyika nchi kavu na Bahari ya kina kifupi.

94.       Mheshimiwa Spika, vitalu kwenye kina kirefu cha Bahari vilianza kutangazwa Mwaka 2000. Katika zabuni ya kwanza, Kampuni moja ilipatikana ambayo ni Petrobras ya Brazil. Katika Duru ya Pili iliyofanyika Mwaka 2001, Kampuni moja ilipatikana ambayo ni Shell ya Uholanzi. Katika Duru ya Tatu iliyofanyika Mwaka 2004, Kampuni tatu zilipatikana ambazo ni Ophir (Uingereza), Statoil (Norway) na Petrobras (Brazil). Duru zote hizo tatu zilifanyika nje ya nchi.

95.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali ilidurusu Mwongozo wa Mkataba wa Uzalishaji na Ugawanaji Mapato yatokanayo na Mafuta na Gesi Asilia (Model Production Sharing Agreement – MPSA, 2013). Kufuatia Mwongozo huo, uzinduzi wa Duru ya Nne ya Kuitisha Zabuni za Utafutaji Mafuta (Fourth Petroleum Licensing Round) kwenye vitalu saba (7) katika Bahari Kuu na kimoja (1) kwenye Ziwa Tanganyika Kaskazini ulifanyika hapa nchini Mwezi Oktoba, 2013. Shughuli hiyo ilizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Zoezi hilo lilifanyika kwa mara ya kwanza nchini baada ya kufanyika nje ya nchi mara tatu mfululizo. Kampuni za ndani na nje ya nchi zilizokidhi vigezo zilishiriki, ambapo hadi Aprili, 2014 kampuni 19 zilinunua taarifa za vitalu vilivyotangazwa. Zoezi hilo lilifungwa tarehe 15 Mei, 2014 ambapo kampuni 5 zilirudisha nyaraka za Zabuni (bidding documents), limesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa na kutoa fursa ya Watanzania kushiriki. Katika zabuni hiyo, Kampuni za kitanzania zilipewa upendeleo maalum wa kisheria wa alama za ziada. Hata hivyo, hakuna Kampuni ya Kitanzania iliyojitokeza kushiriki. Nitoe wito kwa Kampuni za Kitanzania kujitokeza kushiriki katika fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia. Hii  itaondoa dhana kwamba uwekezaji katika sekta hiyo ni kwa ajili ya kampuni za nje pekee. Nashauri Kampuni nyingine za kitanzania ziige mfano wa Kampuni za Swala Energy na Petrodel za nchini mwetu ambazo zinafanya shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Ugunduzi wa Gesi Asilia

96.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, jumla ya futi za ujazo trilioni 4.8 za gesi asilia ziligunduliwa katika visima vya Mkizi – 1, Ngisi – 1, Tangawizi – 1, na Mlonge – 1. Hadi kufikia Mwezi Aprili 2014, kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini ni futi za ujazo trilioni 46.5, sawa na mapipa ya mafuta bilioni 8.37. Kiasi hiki ni takriban mara tano ya gesi asilia iliyokuwepo Mwaka 2005 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani.  Kati ya kiasi hicho, asilimia 83 ni kutoka kina kirefu cha maji Baharini na asilimia 17 ni nchi kavu.

          Mradi wa Uzalishaji Mbolea kwa Kutumia Gesi Asilia

97.       Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza” Serikali itawezesha uanzishwaji wa kiwanda cha mbolea kitakachotumia malighafi ya gesi asilia inayopatikana hapa nchini. Jitihada hizi ni katika kuhakikisha upatikanaji mzuri na wa uhakika wa mbolea ili kuboresha kilimo chetu. Mwezi Agosti, 2013 Serikali kupitia TPDC ilitangaza zabuni ya kujenga kiwanda cha mbolea na  kampuni 19 zilionesha nia. Kati ya Kampuni hizo, 12 zilikidhi vigezo na hivyo kupelekewa Request for Proposal (RFP) ili ziwasilishe project write-up kwa ajili ya uchambuzi. Kampuni 6 zimeleta mapendekezo ya utekelezaji wa mradi na uchambuzi unaendelea wa kumpata mshindi. Taratibu za kumpata mwekezaji kwenye kiwanda cha mbolea zitakamilika kabla ya Julai, 2014 na maandalizi ya ujenzi yataanza Mwaka 2014/15.


98.       Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa ya Mafuta kwa kuandaa Rasimu ya Kanuni za Uratibu wa Mafuta ya Akiba (National Strategic Petroleum Reserve Regulations). Kampuni ya Oman Trading International (OTI) ilishinda zabuni ya kuiuzia mafuta TPDC. Kampuni ya OTI imekubali kuleta mafuta kwa mkopo, ambapo TPDC itailipa Kampuni hiyo fedha baada ya kuuza mafuta hayo. Lengo la utaratibu huu ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa na mafuta ya akiba wakati wote. Katika Mwaka 2014/15, Serikali itakamilisha maandalizi ya Kanuni za Uratibu wa Mafuta ya Akiba na kuanza utekelezaji wake.

Hisa za Serikali katika Kampuni ya Puma Energy Limited, TAZAMA na TIPER

99.       Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali iliendelea kusimamia na kushiriki katika shughuli za uendeshaji wa Kampuni za Puma Energy Tanzania Limited (asilimia 50), Tanzania Zambia Pipeline Limited (TAZAMA, asilimia 30) na Tanzania International Petroleum Reserve (TIPER, asilimia 50). Gawiwo litakalolipwa  Serikalini katika kipindi husika kutoka Kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited ni Shilingi bilioni 3.28.  Kampuni za TAZAMA na TIPER hazijawasilisha gawiwo Serikalini kwa kuwa bado hazijakamilisha hesabu zake za Mwaka 2013. Serikali itaimarisha usimamizi wa Kampuni hizo ili kuongeza gawiwo katika miaka ijayo.  Kufuatia kumalizika kwa vipindi vya Wajumbe wa Bodi hizi tatu (3), Serikali imeteua wajumbe wapya wa Bodi hizo Mwezi Machi, 2014.          Sera na Sheria katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia

100.   Mheshimiwa Spika, kama nilivyoahidi katika Hotuba yangu ya Mwaka 2013/14 mbele ya Bunge lako Tukufu, Serikali iliidhinisha Sera ya Gesi Asilia Mwezi Oktoba, 2013 ili kuimarisha usimamizi wa Sekta Ndogo ya Gesi Asilia. Aidha, Rasimu ya Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa (Local Content Policy) ziliandaliwa. Lengo la Sera hiyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki ipasavyo katika shughuli zote za rasilimali za mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. Rasimu ya Sera hiyo imesambazwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Wizara, Taasisi za Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kupata maoni yao. Wizara ingependa kupata maoni yenu kabla ya tarehe 30 Juni, 2014.

101.    Mheshimiwa Spika, Vilevile, Serikali imekamilisha Rasimu ya Kwanza ya Sera ya Petroli itakayotoa mwongozo kuhusu usimamizi wa  shughuli za utafutaji, uzalishaji na ugawanaji mapato yanayotokana na Mafuta na Gesi Asilia pamoja na usafishaji, uhifadhi, usafirishaji na usambazaji mafuta. katika Mwaka 2014/15 Rasimu hizo zitawasilishwa katika Mamlaka husika kwa ajili ya kuidhinishwa. Kukamilika kwa Sera husika kutaimarisha usimamizi wa Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na vijavyo.

102.   Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Rasimu ya Sheria ya Gesi Asilia imekamilika. Rasimu imepelekwa kwa wadau ili kupata maoni yao kabla ya kuikamilisha na kuiwasilisha katika kikao cha Bunge cha Mwezi Novemba, 2014.

Kudurusu Muundo wa TPDC

103.   Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za utafutaji mafuta na gesi asilia, uendelezaji wa matumizi ya gesi asilia na kusudio la kuongeza ufanisi katika utendaji wa TPDC, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPDC iliwasilisha Serikalini mapendekezo ya muundo mpya wa Shirika Mwezi Mei, 2013. Serikali ilitathmini mapendekezo hayo kwa kuangalia miundo na uzoefu kutoka nchi mbalimbali zilizonufaika na uwepo wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Baada ya tathmini hiyo Mwezi Aprili, 2014, Serikali kupitia Msajili wa Hazina iliidhinisha muundo mpya wa TPDC ili kuliwezesha Shirika hilo kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia (Upstream, Mid and Down-streams). Ili kutekeleza majukumu hayo, TPDC itaanzisha kampuni tanzu zikiwemo Kampuni ya Usafirishaji na Usambazaji wa Gesi Asilia (GASCO) na Kampuni ya Mafuta (COPEC). Ushiriki wa TPDC katika maeneo hayo utaimarisha mapato ya Serikali kwenye shughuli za mafuta na gesi asilia pamoja na kuboresha usimamizi wa Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia.

            Shughuli za Udhibiti wa Sekta ya Nishati

104. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, EWURA iliendelea kusimamia shughuli za udhibiti katika Sekta Ndogo za Umeme, Mafuta na Gesi Asilia. Serikali kupitia Kampuni ya Petroleum Importation Coordinator Limited (PICL) iliendelea kusimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS). Kati ya Mwezi Julai, 2013 na Aprili, 2014 mafuta yaliendelea kupatikana kulingana na mahitaji yetu. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2013 jumla ya lita bilioni 4.66 za aina mbalimbali za mafuta ziliingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Kati ya kiasi hicho, lita bilioni 2.76 sawa na asilimia 59 yalikuwa ni mafuta kwa matumizi ya ndani na kiasi cha lita bilioni 1.90, sawa na asilimia 41 yalikuwa kwa ajili ya nchi jirani. Aidha, kutokana na kuimarika kwa mfumo huo, wastani wa gharama (weighted average premium) za uagizaji mafuta ya petroli zimeshuka kutoka Dola za Marekani 59 kwa tani Mwezi Novemba, 2011 hadi Dola za Marekani 36 kwa tani Mwezi Aprili, 2014.

105.  Mheshimiwa Spika, katika Mwaka  2013/14 Serikali kupitia EWURA iliendelea kudhibiti ubora wa bidhaa za mafuta ya petroli nchini na kuchukua hatua stahiki za kisheria kwa wale waliothibitika kutozingatia viwango vilivyowekwa. Aidha, EWURA iliendelea kusimamia bei za mafuta katika soko la ndani ili kuhakikisha bei hizo zinaendana na mabadiliko ya bei katika Soko la Dunia na mwenendo wa thamani ya Shilingi ya Tanzania ikiwianishwa na Dola ya Marekani. Bei ya mafuta ya petroli nchini imeendelea kushuka kutokana na kuimarika kwa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na shughuli za udhibiti.

106. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya tathmini kuhusu manufaa ya uwekaji vinasaba katika mafuta, uanzishwaji wa matumizi ya Kanuni ya Kukokotoa Bei Kikomo pamoja na Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja. Matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa nchi imenufaika na shughuli za udhibiti wa Sekta Ndogo ya Mafuta kwa kupunguza uchakachuaji ambapo kati ya Mwaka 2010 na 2011, mapato ya Serikali yameongezeka kwa Shilingi bilioni 33.5. Aidha, kutokana na udhibiti wa uuzaji mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya nchi jirani (transit) mapato ya Serikali yameongezeka kwa Shilingi bilioni 468.5 kwa kipindi cha kati ya Mwaka 2010/11 na 2012/13.Vilevile, shughuli za udhibiti zimeongeza ufanisi katika uagizaji mafuta na matumizi ya miundombinu bandarini; pamoja na kuondoa upandaji holela wa bei za mafuta nchini.

107. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15 EWURA itaendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa ubora wa mafuta pamoja na Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja. Aidha, katika Mwaka 2014/15, Serikali itaboresha muundo wa PICL ili kuongeza ufanisi kwa kuzingatia uzoefu wa nchi jirani za Kenya na Msumbiji zinazotumia mfumo kama huo.


Changamoto katika Sekta ya Nishati na Mipango ya Kukabiliana Nazo

108. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya Nishati imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upatikanaji wa fedha za kutosha kutekeleza miradi; mahitaji makubwa ya umeme; kupunguza upotevu wa umeme; vivutio mwafaka kwa wawekezaji; gharama kubwa za umeme unaofuliwa kutokana na mafuta; uzingatiaji matumizi bora ya nishati; na mabadiliko ya tabia nchi.

109. Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Mwaka 2014/15 katika Sekta ya Nishati unalenga kukabiliana na changamoto hizo kwa kutekeleza mipango na miradi iliyotajwa katika Hotuba hii, pamoja na kudurusu, kutunga na kusimamia  Sera na Sheria zinazohusu Sekta ya Nishati kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.


SEKTA YA MADINI

 Mafanikio katika Sekta ya Madini kwa Mwaka 2013/14

110. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kutekeleza vipaumbele vyake katika Sekta ya Madini. Mafanikio yaliyopatikana katika Sekta hii ni pamoja na yafuatayo:  kukamilika kwa zoezi la high resolution airborne geophysical survey katika Mikoa ya Dodoma, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Singida, Tabora na Tanga Mwezi Oktoba, 2013; kukamilika kwa ground geophysical survey (kwenye Quarter Degree Sheet (QDS) - 7, geological mapping kwa QDS 18 na geochemical mapping kwa QDS 7) katika maeneo ya  Dodoma, Mbeya, Morogoro, Njombe, Pwani, Singida na Tanga; na kusainiwa kwa Makubaliano ya Awali (MoU) na Serikali ya Finland kwa ajili ya mkopo nafuu kuwezesha utafiti wa kijiosayansi na maeneo yenye madini katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani utakaoanza Mwezi Agosti, 2015.


111. Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kukamilika kwa Rasimu ya Sheria ya kusimamia shughuli za Mpango wa Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI); kusainiwa kwa makubaliano kwa STAMICO kumiliki mgodi wa dhahabu wa Tulawaka (Biharamulo) kutoka Kampuni ya African Barrick Gold; kutolewa kwa leseni nane (8) za uchenjuaji madini katika Wilaya za Bunda (2), Misungwi (1), na Mkoa wa Geita (5); Serikali kukusanya Shilingi bilioni 50.6 kama Kodi ya Mapato kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited na Shilingi bilioni 3.38 kutoka Kampuni ya Resolute Tanzania Limited; na malipo ya jumla ya Shilingi milioni 178.9 kwa Serikali kama Alternative Minimum Tax kutoka Kampuni ya Williamson Diamonds Limited.

112. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia upatikanaji wa malipo ya ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri za Geita, Kahama, Kishapu, Nzega na Tarime. Mapato yaliyolipwa tangu migodi hiyo ianze hadi Aprili, 2014 kwa Halmashauri hizo ni jumla ya Dola za Marekani milioni 10.58, sawa na Shilingi bilioni 17.35 kwa mchanganuo ufuatao: Mgodi wa Geita Dola za Marekani milioni 1.6, sawa na Shilingi bilioni 2.62 kwa Halmashauri ya Geita; Mgodi wa Bulyanhulu Dola za Marekani milioni 2.53, sawa na Shilingi bilioni 4.15 kwa Halmashauri ya Kahama; Mgodi wa Buzwagi Dola za Marekani  800,000, sawa na Shilingi bilioni 1.31 kwa Halmashauri ya Kahama; Mgodi wa North Mara Dola za Marekani milioni 2.4, sawa na Shilingi bilioni 3.94 kwa Halmashauri ya Tarime; Mgodi wa Resolute Dola za Marekani milioni 3.04, sawa na Shilingi bilioni 4.99 kwa Halmashauri ya Nzega; na Mgodi wa Almasi wa Mwadui Dola za Marekani 202,469 sawa na Shilingi milioni 332.05 kwa Halmashauri ya Kishapu.


113. Mheshimiwa Spika, Mafanikio mengine ni kukusanywa kwa mrabaha wa Shilingi bilioni 116.64 kutokana na madini yaliyozalishwa na kuuzwa; kukamilika kwa Mpango wa Uendelezaji wa Uchimbaji Mdogo wa Madini;  kuandaliwa kwa Mtaala wa utafiti wa madini na programu za uchimbaji mdogo wa madini; kufadhili mafunzo ya wanafunzi 148 katika  ngazi ya cheti na diploma katika fani za Madini, Petroli na Gesi Asilia; kuanza ujenzi wa madarasa mawili (2) katika Chuo cha Madini Dodoma kila moja likiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 140; na kuanzishwa kwa ofisi mbili za Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) katika Mikoa ya Arusha na Mbeya.

114. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2013/14, Serikali kwa upande wa Sekta ya Madini iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata Mpango Kazi uliowekwa na Wizara. Katika Mwaka 2014/15 maeneo mahsusi yatakayoleta matokeo makubwa katika Sekta hii ni pamoja na: kuimarisha makusanyo ya maduhuli yatokanayo na madini; kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo; kuboresha utoaji na usimamizi wa leseni za madini; kuimarisha usimamizi wa afya, usalama na utunzaji wa mazingira migodini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini; kuwezesha Mashirika na Taasisi za Serikali katika Sekta ya Madini; na kuendelea kuboresha mazingira ya kazi katika Ofisi za Madini za Kanda.

Mauzo na Thamani ya Madini yaliyouzwa nje ya Nchi

115. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 Wizara iliendelea kusimamia shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini kwa lengo la kuongeza mchango wa Sekta hii kwenye Pato la Taifa. Kutokana na mipango na miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Serikali, Sekta ya Madini imeendelea kuwa chachu katika ukuaji wa uchumi nchini. Hata hivyo, Sekta ya Madini ni mojawapo ya sekta zilizoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mtikisiko wa uchumi Duniani ambao uliambatana na kushuka kwa bei ya madini mbalimbali, hususan dhahabu na pia kushuka kwa upatikanaji wa mitaji ya nje (FDI).

116. Mheshimiwa Spika, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi yaliyouzwa na Migodi Mikubwa ya Dhahabu iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 640 Mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.79 Mwaka 2013. Uzalishaji wa madini ulipungua kutoka wakia 1,398,406 Mwaka 2005 hadi wakia 1,244,743 Mwaka 2013, sawa na punguzo la asilimia 10.9. Aidha, asilimia 69.27 ya mauzo ya madini yote ya migodi mikubwa nje ya nchi kwa Mwaka 2013 ilitokana na mauzo ya dhahabu.
       
117. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uzalishaji na mauzo ya madini katika migodi mikubwa nchini katika kipindi cha Mwaka 2013, jumla ya wakia milioni 1.24 za dhahabu, wakia 380,000 za fedha na ratili milioni 17.70 za shaba zilizalishwa na kusafirishwa nje ya nchi kutoka migodi mikubwa ya Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, Golden Pride, New Luika, North Mara na Tulawaka. Jumla ya thamani ya madini hayo ni Dola za Marekani bilioni 1.79 pungufu kwa asilimia 17.7 ukilinganisha na mauzo ya madini yaliyofanywa na migodi hiyo kwa Mwaka 2012 ya Dola za Marekani bilioni 2.17.  Vilevile, jumla ya karati 158,562 za almasi na gramu milioni 3.24 za Tanzanite zilizalishwa na migodi ya Mwadui na TanzaniteOne, sawia. Mauzo yote ya almasi na Tanzanite yaliyofanywa na migodi hiyo kwa Mwaka 2013 yalifikia Dola za Marekani milioni 50.53. Mrabaha uliolipwa Serikalini na wamiliki wote wa migodi mikubwa nchini katika kipindi hicho ni Dola za Marekani milioni 72.90, sawa na Shilingi bilioni 116.64. Mgodi wa Tulawaka uliopo Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera ulifungwa rasmi Mwezi Julai, 2013. Aidha, mgodi wa Golden Pride uliopo Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora ulifungwa rasmi Mwezi Februari, 2014. Ni wazi kuwa, kufungwa kwa migodi hiyo kutapunguza uzalishaji wa dhahabu na mapato ya Serikali.

          Kuimarisha Makusanyo ya Maduhuli Yatokanayo na Madini

118. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha makusanyo ya maduhuli ya Serikali yatokanayo na madini, Wizara ililenga kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 199.96 katika Mwaka 2013/14. Hadi kufikia tarehe 23 Mei, 2014 kiasi cha Shilingi bilioni 137.9 kimekusanywa, sawa na asilimia 69 ya lengo. Kushuka kwa makusanyo hayo kumetokana na kushuka kwa bei ya dhahabu katika Soko la Dunia.

119. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15 Serikali inategemea kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 209.96 kutoka katika Sekta ya Madini. Ili kufikia lengo hilo, Wizara itaimarisha ukaguzi na usimamizi wa Sekta ya Madini ili kuhakikisha kwamba wachimbaji wakubwa, wa kati, wadogo na wafanyabiashara wa madini wanalipa ada za leseni na mrabaha stahiki. Pia, Wizara itafungua ofisi mpya mbili (2) za Kanda ambazo ni Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki, ambayo Makao Makuu yake yatakuwa Musoma; na Kanda ya Ziwa Nyasa ambayo Makao Makuu yake yatakuwa Songea. Aidha, Ofisi nne (4) za Maafisa Madini Wakazi zitafunguliwa huko Bariadi, Moshi, Nachingwea na Njombe. Kufunguliwa kwa Ofisi hizo kumelenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

120. Mheshimiwa Spika, Wizara pia itaendelea kutekeleza mpango wake wa kuanzisha vituo vya ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani katika Kanda zote za Madini nchini. Mpango huo umewezesha jumla ya Shilingi bilioni 1.71 kukusanywa Mwaka 2012/13 kutoka Kanda za Mashariki, Ziwa Viktoria, Kati na Kusini ikilinganishwa na wastani wa Shilingi milioni 4 kwa mwaka zilizokuwa zinakusanywa hapo awali katika Kanda hizo kabla ya mpango huo kuanzishwa. Aidha, Wizara itaimarisha usimamizi wa uchimbaji na biashara ya Tanzanite ili kuhakikisha kuwa Taifa linapata manufaa stahiki ya uvunaji wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee.

Majadiliano na Kampuni za Madini

121. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya Mwaka 2013/14, niliahidi kuendelea kufanya majadiliano na baadhi ya wamiliki wa migodi mikubwa nchini wenye Mikataba ya Uendelezaji Migodi (Mineral Development Agreements – MDAs). Majadiliano hayo ni  kuhusu kubadilisha baadhi ya vipengele vya mikataba ili kuleta mapato zaidi ya fedha kwa Taifa.

122. Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kujadiliana na Kampuni ya African Barrick Gold (ABG) inayomiliki migodi mikubwa ya Bulyanhulu katika Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, Buzwagi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama na North Mara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kutokana na majadiliano hayo, Kampuni hiyo imekubali kuwa kuanzia Julai, 2014 italipa asilimia 0.3 ya mapato (turnover) kama ushuru wa huduma (service levy) kwa Halmashauri husika, badala ya malipo ya Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka iliyokuwa inalipwa hapo awali kulingana na MDA. Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Kampuni ya ABG kwa uamuzi huo na kuzishauri Kampuni nyingine kuiga mfano huo.

123. Mheshimiwa Spika, Kampuni ya ABG itaendelea kulipa moja kwa moja Dola za Marekani 200,000 kwa Halmashauri husika na ziada ya malipo yatakayotokana na asilimia 0.3 ya mapato itawekwa kwenye Mfuko Maalum utakaoanzishwa na kusimamiwa na Halmashauri husika. Mfuko huo utatumika kwa ajili ya kuendeleza miundombinu kwenye maeneo ya Halmashauri hizo katika nyanja za afya, barabara, elimu, maji na nishati. Ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa, Halmashauri husika italazimika kuwasilisha kwa Wizara ya Nishati na Madini Mpango wa utekelezaji kwa ajili ya idhini. Lengo ni kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa miradi ya maendeleo tu.  

Kuendeleza Shughuli za Uchimbaji Mdogo wa Madini

124. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, shughuli za uchimbaji mdogo zimeendelea kukua na kutoa mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, ambapo zaidi ya Watanzania milioni moja wamejiajiri katika shughuli hizo. Katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 – 2015, Ibara ya 56 (d) ambayo pamoja na mambo mengine, inasisitiza juu ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji, Wizara imeendelea kutoa mikopo ya masharti nafuu na ruzuku kwa wachimbaji wadogo kupitia Benki ya TIB. Mwezi Aprili, 2014 Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikabidhi hundi zenye jumla ya Dola za Marekani 537,000 sawa na Shilingi milioni 880.68 kwa miradi kumi na moja (11) ya wachimbaji wadogo ambayo ilikidhi vigezo vya kupata ruzuku. Vilevile, Wizara inatarajia kuipatia miradi mingine 18 ya wachimbaji wadogo mikopo yenye jumla ya Shilingi bilioni 2.3 ifikapo mwishoni mwa Mwezi Juni, 2014. Nawasihi wachimbaji wadogo kuandaa michanganuo yao ya miradi kwa ajili ya kuomba mikopo na ruzuku kupitia TIB ili watakaokidhi vigezo wapate ruzuku ama mikopo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji mdogo kwa tija. Wachimbaji wadogo wanashauriwa kupata ushauri wa bure wa kitaalamu kutoka Shirika la Taifa la Madini (STAMICO). Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wachimbaji wadogo waaminifu watakaotumia vizuri ruzuku wanazopewa, na watakaorejesha mikopo na kulipa kodi za Serikali.

125. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa mitaji na mikopo, Wizara imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 2.5 katika Bajeti yake ya Mwaka 2014/15 kwa ajili ya kukopesha wachimbaji hao. Pamoja na fedha hizo za mikopo, Serikali, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia imetenga jumla ya Dola za Marekani milioni 3.5, sawa na Shilingi bilioni 5.74 kama ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo, na kiasi cha Dola za Marekani milioni 1.1, sawa na Shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kununua mitambo miwili (2) ya uchorongaji miamba (drilling rigs). Mitambo hiyo itapelekwa katika Ofisi za Madini za Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Kusini Magharibi (Mbeya) ili kuwezesha utambuzi wa kiasi cha mashapo yaliyopo katika maeneo ya wachimbaji wa kati na wadogo yaliyogunduliwa kuwa na madini. Kiasi hicho kinafanya jumla ya fedha zilizotengwa kwa Mwaka 2014/15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo kufikia jumla ya Shilingi bilioni 10.04.

126. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo, kwa Mwaka 2013/14 Wizara iliendelea kutoa mafunzo kwa nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo ambapo jumla ya wachimbaji wadogo 420 walipatiwa mafunzo katika maeneo ya Handeni na Kilindi (250), Musoma (90) na Tunduru (80). Pia, katika kupanua wigo wa kutoa elimu kwa wadau wengi zaidi, vitabu 2,000 vya kuelimisha wachimbaji wadogo vilichapishwa na kusambazwa. Kwa Mwaka 2014/15, Wizara imepanga kutoa mafunzo kwa nadharia na vitendo kwa wachimbaji wapatao 1,000. Vilevile, Wizara itaendelea kutoa huduma za ugani ili kuboresha utendaji kazi wa wachimbaji wadogo nchini.

127. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 jumla ya maeneo 10 yenye ukubwa wa hekta 67,677.61 yametengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Maeneo hayo ni Nyamwironge (Kakonko), Ibaga (Mkalama), Makanya (Same), Mwajanga (Simanjiro), Itumbi B na Saza (Chunya), Ilujamate (Misungwi), Kalela/Kigogwe/Samwa (mpakani mwa Wilaya za Kasulu, Buhigwe na Kigoma Vijijini), Maguja (Nachingwea) na Nyangalata (Kahama/Nyang’hwale). Jumla ya maeneo yaliyotengwa hadi sasa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni 25 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,166.24. Aidha, jumla ya viwanja 8,800 vyenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 2,047.14 vimegawiwa kwa wachimbaji wadogo.

128. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri itakavyoonekana inafaa. Pamoja na kuongeza ajira kwa wachimbaji wadogo, utengaji wa maeneo unalenga kupunguza migogoro ya maeneo kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa na kati ya wachimbaji wadogo na wadogo (wenyewe kwa wenyewe). Vilevile, Wizara itafanyia tathmini maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo na yatakayobainika kuwa hayafanyiwi kazi yatatenguliwa na kugawiwa kwa waombaji wengine kwa mujibu wa Sheria.

Kuboresha Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini

129. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa utoaji wa leseni za madini, Wizara iliwezesha wamiliki wa leseni kupata taarifa za leseni kupitia tovuti maalum ya leseni (Mining Tenements Portal) na pia kuwawezesha wateja kupokea taarifa za maombi kupitia ujumbe mfupi wa simu (sms) na barua pepe. Hatua hizi zimelenga hatimaye kuwawezesha waombaji wa leseni kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao (on-line applications of mineral rights and payments). Pamoja na maboresho hayo, Wizara imeendelea kuhakiki taarifa za leseni kwenye mfumo wa utoaji wa leseni (data cleaning), kuondoa mlundikano wa maombi ya leseni na kuimarisha miundombinu ya mfumo wa leseni (MCIMS).

130. Mheshimiwa Spika, katika kipindi kati ya Julai, 2013 na Aprili, 2014 jumla ya maombi 7,640 ya utafutaji na uchimbaji madini yalipokelewa na kuingizwa kwenye Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini, ikilinganishwa na maombi 9,889 katika Mwaka 2012/13. Kati ya maombi yaliyopokelewa, 715 ni kwa ajili ya leseni za utafutaji wa madini; 6,909 yalikuwa ni ya uchimbaji mdogo; na 16 ni ya uchimbaji wa kati. Jumla ya maombi 3,994 ya leseni yalikataliwa kwa sababu ya kushindwa kutimiza masharti ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Aidha, jumla ya leseni 5,418 zilitolewa, kati ya hizo 482 kwa ajili ya utafutaji wa madini; 4,913 za uchimbaji mdogo; 22 za uchimbaji wa kati; na moja (1) ya uchimbaji mkubwa.

131. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mwezi Aprili, 2014 jumla ya leseni hai za madini nchini zilikuwa ni 39,958. Kati ya hizo, leseni za uchimbaji mkubwa ni 13; uchimbaji wa kati ni 381; uchimbaji mdogo ni 36,094; na leseni za utafutaji madini ni 3,470. Eneo la leseni hizo zote ni kilometa za mraba zipatazo 240,000 sawa na asilimia 27 ya eneo lote la nchi kavu ya Tanzania Bara.

132. Mheshimiwa Spika, wakati Sekta ya Madini ikiendelea kukua na kuongezeka kwa uwekezaji, imejengeka dhana kwamba wawekezaji wageni wanamiliki maeneo mengi kuliko Watanzania. Aidha, ipo fikra kwamba Serikali haijachukua hatua ya kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uwekezaji kwenye Sekta hii muhimu. Ukweli ni kwamba, Watanzania wanamiliki asilimia 70 ya leseni za madini, wageni asilimia 25 na asilimia 5 ya leseni hizo zinamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni.

133. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa leseni za madini, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kutoa Hati za Makosa (Default Notices) kwa wamiliki wa leseni za utafutaji na uchimbaji madini ambao hawatimizi masharti ya leseni. Aidha, Wizara imechukua hatua dhidi ya wamiliki waliohodhi maeneo makubwa ya leseni za madini nchini. Hadi kufikia Mwezi Aprili, 2014 Hati za  Makosa 336 zilitolewa zikihusisha leseni 253 za utafutaji madini na leseni 83 za uchimbaji madini. Aidha, jumla ya leseni 174 za utafutaji madini na leseni moja ya uchimbaji mkubwa wa madini zilifutwa. Vilevile, leseni 78 za utafutaji madini na leseni 34 za uchimbaji wa kati ziko katika utaratibu wa kisheria  wa kufutwa. Kati ya leseni zote zilizofutwa na zinazotarajiwa kufutwa, leseni 67 ni za wamiliki 10 waliobainika kuhodhi maeneo makubwa ya leseni za madini. Pamoja na hatua ya kufuta leseni, Wizara pia imechukua hatua ya kutomilikisha leseni mpya 214 kwa kampuni zenye leseni zinazozidi ukomo wa eneo la leseni la kilomita za mraba 2,000. Hatua hii imechukuliwa ikiwa ni sehemu ya usimamiaji wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

134. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuimarisha Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Data Recovery Center mjini Morogoro. Kituo hicho kitaimarisha usalama wa taarifa za leseni. Aidha, Wizara itaanza kupokea maombi ya leseni na malipo ya ada za leseni kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu utapunguza muda wa kushughulikia maombi ya leseni na kuongeza mapato ya Serikali. Vilevile, utapunguza ushawishi wa rushwa na upendeleo kwa waombaji wa leseni za madini. Wizara pia itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wanaokiuka masharti ya leseni zao na wale wanaohodhi maeneo makubwa ya leseni bila kuyaendeleza.

Kuimarisha Usimamizi wa Afya, Usalama na Utunzaji wa     Mazingira Migodini

135. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 Wizara iliendelea kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji madini zinaendeshwa kwa kuzingatia Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira. Hadi kufikia Mwezi Machi 2014, jumla ya migodi 351 ilikaguliwa, ikijumuisha migodi mikubwa mitano (5); migodi ya kati 56; na migodi midogo 290. Kaguzi hizo zimesaidia kuimarisha usalama na afya migodini. Wizara itaendelea kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake kwa kuimarisha ukaguzi katika migodi mikubwa, ya kati na midogo. Aidha, ukaguzi utafanywa katika maeneo ya uchenjuaji na leseni za utafutaji wa madini. Pia, leseni za biashara ya madini na maduka ya usonara yatakaguliwa kwa lengo la kuhakiki ulipaji wa maduhuli ya Serikali.

136. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utunzaji wa mazingira katika migodi mikubwa nchini, migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi, Golden Pride, North Mara, Tulawaka na WDL imekamilisha Mipango ya Ufungaji Migodi (Mine Closure Plans) kwa mujibu wa Kanuni za Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira na imeidhinishwa na Kamati ya Kisekta ya Ufungaji Migodi. Migodi ya Geita na TanzaniteOne imewasilisha Mipango ya Ufungaji Migodi ili kupitiwa na Kamati ya Kisekta kwa ajili ya uidhinishaji. Migodi ya El Hilal, New Luika na TANCOAL inatarajiwa kuwasilisha Mipango ya Ufungaji Migodi kabla ya mwisho wa Mwaka 2014.
       
137. Mheshimiwa Spika, kufuatia kufungwa kwa shughuli za uzalishaji katika migodi ya Tulawaka na Golden Pride, Wizara ilisimamia taratibu za makabidhiano ya mgodi wa Tulawaka kwa STAMICO kupitia Kampuni yake tanzu ya “STAMIGOLD Mining Company Ltd” ili kuendelea kuchimba mashapo ya dhahabu yaliyobaki baada ya Kampuni ya ABG kufunga shughuli za uchimbaji. Pia, taratibu za kufungwa na kukabidhi eneo la mgodi wa Golden Pride kwa Chuo cha Madini Dodoma zinaendelea.Ukarabati wa maeneo yote yaliyoathiriwa na shughuli za mgodi huo unaendelea na utakamilika ifikapo Mwezi Desemba, 2014. Aidha, maandalizi katika eneo la mgodi wa Golden Pride yataanza Mwezi Agosti, 2014 ili kuwezesha Wanafunzi 200 kuanza mafunzo katika eneo hilo. Baada ya majadiliano ya kina na Serikali, Kampuni ya Resolute imekubali kukipatia Chuo cha Madini Dodoma Dola za Marekani milioni 1.0, sawa na Shilingi bilioni 1.64 ili kuendeleza miundombinu ya kuanzisha Kampasi ya Chuo cha Madini kwenye eneo la mgodi wa Golden Pride na kuimarisha ulinzi. Kwa upande wake, Serikali imetenga Shilingi bilioni 1.0 katika Bajeti ya Mwaka 2014/15 kwa ajili hiyo.

138. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kukamilisha mikataba ya uwekaji wa Hati Fungani ya Ufungaji Migodi (Rehabilitation Bond for Mine Closure) kwa ajili ya migodi mikubwa nchini. Aidha, wachimbaji wadogo wataendelea kupewa elimu ya namna ya kuandaa mipango ya utunzaji wa mazingira (Environmental Protection Plans) ili kutimiza matakwa ya Sheria ya Madini ya Mwaka, 2010.

139. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini ya Urani nchini. Hata hivyo, kumekuwapo na mtazamo hasi kuhusu utafutaji na uchimbaji wa madini ya Urani nchini. Kutokana na hali hiyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilitekeleza mpango wa elimu kwa umma kuhusiana na madini ya Urani na shughuli za uchimbaji wa madini hayo. Elimu hiyo ilitolewa kwa njia ya makongamano katika maeneo ya Bahi na Namtumbo ambako shughuli za utafutaji zinaendelea. Kutolewa kwa elimu hiyo kumewezesha jamii husika kuwa na taarifa sahihi juu ya madini hayo na faida zake. Katika kipindi cha Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya semina na vyombo vya habari kuhusu uvunaji, uhifadhi, usafirishaji, matumizi ya madini ya Urani.

Usimamizi wa Shughuli za Baruti Nchini

140. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuimarisha usimamizi wa uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na matumizi ya baruti nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo, katika kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014, jumla ya tani 15,628.8 za baruti na fataki 2,177,062 ziliingizwa nchini kwa ajili ya utafutaji wa mafuta na gesi asilia na uchimbaji wa madini. Vibali 114 vilitolewa kwa ajili ya kuingiza baruti nchini; vibali 44 vilitolewa kwa ajili ya kusafirisha baruti nje ya nchi; vibali 85 vya kulipulia baruti; na vibali 12 vya maghala ya kuhifadhia baruti. Aidha, Wizara ilitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini wanaotumia baruti wapatao 420 katika Mikoa ya Mara (90), Ruvuma (80) na Tanga (250). Mafunzo hayo yalihusu utaratibu wa kisheria wa upatikanaji, usafirishaji, utunzaji na matumizi salama ya baruti. Lengo ni kuwaelekeza  na kuwaelimisha watumiaji wa baruti juu ya mambo muhimu ya usalama katika kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia baruti.

141. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2014/15 Wizara itaimarisha mipango na taratibu za usimamizi wa masuala ya baruti kwa kuzingatia Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963; kuendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wachimbaji wadogo wapatao 1,000 kuhusu matumizi bora na salama ya baruti; na kuendelea kufanya kaguzi mbalimbali kwenye maghala ya kuhifadhia baruti. Pia, Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 itaboreshwa ili iendane na wakati.

Kuhamasisha Shughuli za Uongezaji Thamani Madini

142. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini ambapo hadi kufikia Mwezi Machi, 2014 jumla ya leseni 32 za uchenjuaji wa madini ya dhahabu (Vat Leaching), leseni 1 ya uchenjuaji wa madini ya coltan na leseni 1 ya  uyeyushaji wa madini ya shaba  (copper smelter) zimetolewa. Pia, viwanda vitatu (3) vya  kuchenjua  madini ya shaba vyenye uwezo wa kuchenjua wastani wa tani 90,000 za shaba ghafi (Copper Oxide) kwa mwaka vimeanzishwa. Viwanda hivi vipo Dar es Salaam (Danformation), Mkuranga (Horus) na Mpanda (TPM Mining). Viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha shaba katika kiwango cha ubora wa kati ya asilimia 80 hadi 95. Maeneo yanayozalisha shaba ghafi kwa wingi kwa sasa ni Mbesa (Tunduru); Dreef, Kapanda, Kasakalawe na Sikitiko (Mpanda); Burega, Gagwe, Ilagala, Lusunu, Kabulanzwila na Mkanga (Kigoma); Ibaga na Ilangida (Mkalama); na Sufu (Chamwino). Makisio ya uzalishaji wa shaba ghafi kwa mwaka ni tani 1,200.

143. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kukarabati na kukiboresha kituo cha Jimolojia kilichopo Arusha (Tanzania Gemological Centre) ili kiwe cha kisasa zaidi ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya ukataji wa madini ya vito  (lapidary) na usanifu wa mawe (carving). Aidha, katika kukiimarisha kituo hicho, Wizara imenunua mashine 37 za aina mbalimbali zikiwemo faceting machine 20, triming machine 4, stone carving machine 4, bead making machine 6 na carbochon machine 3 kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ukataji na usanifu wa vito kwa vitendo. Pia, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo cha Jimolojia cha nchini Thailand (GIT) kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia Mwezi Julai 2013 hadi Juni 2015. Aidha, Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) kimesaini hati ya ushirikiano na Chama cha Wafanyabiashara wa Vito na Usonara cha Thailand (TGJTA) Mwezi Februari, 2014 ili kusaidia maendeleo ya tasnia ya vito nchini mwetu. 

144. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuendesha maonesho ya Vito na Usonara huko Arusha yakiwa na malengo ya kuvutia masoko ya uhakika hapa nchini; fursa ya kutangaza  rasilimali za madini ya vito yapatikanayo Tanzania; kukuza kazi za uongezaji thamani madini nchini kupitia programu mbalimbali kwa kutoa elimu ya uongezaji thamani madini kwa vikundi mbalimbali vya kinamama wanaojishughulisha na biashara ya madini ya vito; wazalishaji na wafanyabiashara wa  madini wa ndani kupata fursa ya kupata masoko ya kimataifa; kuifanya Arusha kuwa kituo cha biashara ya vito na usonara barani Afrika; na kukusanya mapato ya Serikali. Katika maonesho yaliyofanyika Arusha kuanzia tarehe 28 hadi 30 Oktoba 2013, nchi 29 zilishiriki ambapo jumla ya washiriki walikuwa ni 550 wakiwemo waoneshaji, wageni waalikwa na wanunuzi. Aidha, madini yenye thamani ya Shilingi bilioni 6.9 yaliuzwa na kuiwezesha Serikali kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 227.4 ikiwa ni mrabaha. Ili kuboresha zaidi maonesho yajayo, Wizara ilishiriki kwenye maonesho ya vito nje ya nchi yakiwemo Maonesho ya 53 ya Bangkok, Thailand; na  Maonesho ya Tucson, Marekani. Ushiriki huo umesaidia kujifunza namna bora ya kuandaa maonesho ya vito na kuwashawishi wafanyabiashara wakubwa kuja kushiriki kwenye maonesho yajayo ya vito ya Arusha ambayo yamepangwa kufanyika Mwezi Novemba, 2014.

145. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini hapa nchini yakiwemo madini ya shaba, vito, dhahabu na madini ya viwandani ili kuongeza ajira, kipato kwa wananchi na mapato kwa Serikali. Aidha, Wizara itakamilisha Sheria na Kanuni za Uongezaji Thamani Madini ili kusaidia kukuza na kusimamia shughuli za uongezaji thamani madini hapa nchini. Pamoja na juhudi hizo, baada ya kukamilisha ukarabati wa kituo cha Jimolojia kilichopo Arusha, Wizara itatekeleza mpango wa mafunzo ya uongezaji thamani kwa vitendo kwa Watanzania na hivyo kuifanya fani hiyo kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa Sekta ya Madini na upatikanaji wa ajira mpya kwenye tasnia hiyo.

Kuimarisha Usimamizi wa Biashara ya Madini

146. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini nchini, Serikali imeendelea kusimamia shughuli hizo kwa kukagua na kuhakiki madini yanayozalishwa, kuthaminisha, na kutoa vibali vya kuruhusu kusafirishwa kwenda nje. Katika kutekeleza lengo hilo, jumla ya leseni 621 za biashara ya madini (dealers - 361 na brokers - 260) zimetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Aidha, katika kupambana na wimbi la utapeli na udanganyifu katika biashara ya madini,  Wizara imeanzisha mpango wa kutangaza wamiliki wa leseni halali za biashara ya madini kupitia tovuti yake ili kusaidia wanunuzi wa madini kuwafahamu wafanyabiashara halali wa madini.
     
147. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15 Wizara itaimarisha ukaguzi wa biashara ya madini ili kupunguza udanganyifu unaoikosesha Serikali mapato. Pia, Serikali itakamilisha mazungumzo na nchi za India, Kenya na Marekani ili kuzishawishi kukubali kutambua Certificate of Origin ya Tanzanite. Hatua hii itapunguza utoroshaji wa madini. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za umma itaimarisha msako kwa ajili ya kuwabaini na kuwakamata wanaojihusisha na utapeli katika biashara ya madini.Kuendelea Kuvutia Uwekezaji katika Sekta ya Madini

148. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14, Serikali imeendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kushiriki kwenye warsha na maonesho ya ndani na nje ya nchi yanayokutanisha wawekezaji katika Sekta ya Madini, kwa mfano INDABA (Afrika Kusini), PDAC (Canada) na ADUC (Australia). Kupitia fursa hii, Serikali imetoa taarifa mbalimbali kuhusu mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na taarifa za kijiolojia ili kuvutia wawekezaji.

149. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini, kwa Mwaka 2014/15 Wizara itaendelea kushiriki katika warsha na maonesho mbalimbali ya ndani na nje ambayo huhudhuriwa na wawekezaji mbalimbali. Aidha, Wizara itaendelea kutoa taarifa za kijiolojia kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) zinazohitajika katika shughuli za utafutaji wa madini pamoja na kuboresha huduma za utoaji wa leseni ili zipatikane kwa wakati.

Kuimarisha Mazingira ya Kazi katika Ofisi za Madini za Kanda

150. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha Ofisi za Madini za Kanda ikiwa ni pamoja na kujenga ofisi za kudumu. Katika Mwaka 2013/14, taratibu za kujenga Ofisi za Dodoma, Mpanda na Mtwara zimeanza. Lengo la Wizara ni kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji majukumu likiwemo ukusanyaji wa maduhuli. Kwa Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuimarisha na kuboresha vitendea kazi kwenye Ofisi zote za Madini za Kanda na Maafisa Madini Wakazi na kukamilisha ujenzi wa ofisi za Dodoma, Mpanda na Mtwara.

Asasi ya Uwazi katika Tasnia ya Uziduaji (Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative – TEITI)

151. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 Kamati Tekelezi ya TEITI ilikamilisha rasimu ya Sheria itakayosimamia shughuli zake. Nchi wanachama wa EITI ambazo tayari zina Sheria hiyo zilishirikishwa katika maandalizi ya rasimu hiyo. Nchi hizo ni Ghana, Liberia na Nigeria. Lengo lilikuwa ni kupata maoni na uzoefu wa nchi hizo katika utekelezaji wa Sheria hiyo. Maoni yaliyopatikana Mwezi Oktoba, 2013 yametumika kuboresha rasimu hiyo, na taratibu za maandalizi ya muswada zinaendelea ili uwasilishwe katika kikao cha Bunge kabla ya Mwezi Novemba, 2014.

152. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali za kuweka wazi mapato yanayotokana na shughuli za kampuni zinazofanya utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia, TEITI iliendesha warsha kwa Waandishi wa Habari, Asasi za Kiraia na wananchi juu ya  matokeo ya Ripoti ya Tatu ya TEITI katika maeneo yenye uwekezaji. Jitihada hizi zinalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuhoji Serikali  katika  usimamizi wa rasilimali hizo. Warsha hizi zilifanyika tarehe 28 Juni, 2013 na 03 Julai, 2013 Jijini Dar es Salaam; tarehe 03 - 05 Julai, 2013 Jijini Arusha; tarehe 30 Septemba - 02 Oktoba, 2013 Jijini Mwanza; na tarehe 04 - 06 Novemba, 2013 Lindi na Mtwara. 

153. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa asasi ya EITI imefanya marekebisho ya masharti ya uanachama ili kuongeza kasi ya kuleta mabadiliko yanayokusudiwa katika kuongeza manufaa ya uvunaji wa rasilimali kwa wananchi kwenye nchi wanachama. Kuanzia Mwezi Julai, 2013 utekelezaji katika nchi wanachama ulianza kupimwa kwa kutumia viwango (EITI Standard) badala ya Kanuni za Mwaka 2011. Katika mabadiliko hayo, nchi wanachama zinatakiwa pamoja na hatua nyingine kuweka wazi rejista ya majina ya watu na kampuni zinazomiliki leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia.
       
154. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango wa EITI umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa  ni pamoja na utoaji wa takwimu zilizo nje ya kipindi husika na ucheleweshaji wa upatikanaji wa takwimu hizo kutoka kampuni za uchimbaji wa madini na gesi asilia; na kutoka katika Taasisi za Serikali zinazokusanya mapato, na hivyo kuathiri utoaji wa ripoti za TEITI kwa wakati. Ili kuondoa tatizo hili, natoa wito kwa kampuni na Taasisi za Serikali kuwasilisha takwimu sahihi na kwa wakati.

155. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, Kamati Tekelezi ya TEITI itaendelea kuandaa Sheria ya TEITI pamoja na kujenga uwezo juu ya uendeshaji wa EITI kwa wajumbe wa Kamati na Sekretarieti Tekelezi ya TEITI.  Katika kipindi hiki Kamati imepanga kuelimisha na kuhamasisha wananchi juu ya maeneo yafuatayo: utekelezaji wa EITI kwa kuchapisha na kusambaza taarifa za TEITI kwa  Mwaka 2011/12 na 2012/13; kukamilisha matayarisho ya Taarifa ya Tano ya TEITI inayohusisha malipo ya kodi na mapato ya Mwaka 2012/13; kusimamia tafiti mbalimbali za kupanua wigo wa utekelezaji wa EITI; kutekeleza mpango wa mawasiliano na kuendesha warsha na semina juu ya utekelezaji wa mpango wa TEITI; na kuiwezesha kifedha Sekreterieti na Kamati Tekelezi ya TEITI. Aidha, Kamati itazijengea uwezo Asasi za Kiraia, Idara za Serikali na kampuni za uziduaji juu ya utekelezaji wa mpango wa TEITI.

Uchambuzi na Uthamanishaji wa Madini ya Vito Kupitia TANSORT

156. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014, TANSORT ilithamini na kusimamia uuzwaji wa karati 128,000 za almasi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 33.3, sawa na Shilingi bilioni 54.61. Mauzo ya almasi hizo yaliingizia Serikali mapato ya Dola za Marekani milioni 1.7, sawa na Shilingi bilioni 2.79 ikiwa ni mrabaha. Aidha, Kitengo kilithamini tani 24,000 za madini ya mapambo; gramu milioni 10 za vito ghafi; na karati 166,000 za vito vilivyochongwa vikiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 25.2, sawa na Shilingi bilioni 41.33. Mauzo ya madini hayo yote ya vito yaliingizia Serikali mapato ya Dola za Marekani milioni 0.98, sawa na Shilingi bilioni 1.61.

157. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2014/15, TANSORT itaendelea kutekeleza majukumu yake yakiwemo: kuthamanisha almasi na madini ya vito ili kuwezesha Serikali kupata malipo stahiki ya mrabaha; kutayarisha miongozo ya bei ya almasi na madini ya vito; kutoa huduma za kijemolojia  kwa wachimbaji wadogo na wa kati; kusimamia mauzo ya almasi na madini ya vito ndani na nje ya nchi; kufanya tafiti za masoko na bei za vito; na kutoa ushauri kwa wachimbaji wadogo na wa kati kuhusu masoko, ukataji na ukadiriaji thamani ya vito.

Kuwezesha Mashirika na Taasisi za Serikali katika Sekta ya Madini

Chuo cha Madini cha Dodoma - MRI

158. Mheshimiwa Spika, uamuzi wa kukigeuza Chuo cha Madini Dodoma kuwa Polytechnic umeanza kutekelezwa katika Mwaka 2013/14. Jambo muhimu katika hatua hii ni kukipa Chuo mamlaka ya kujiendesha (autonomy), ambapo Wizara ya Nishati na Madini imewasilisha mapendekezo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa hatua zaidi. Aidha, maandalizi ya kukikabidhi Chuo cha Madini eneo la Mgodi wa Golden Pride (Nzega) uliofungwa yanaendelea ambapo makabidhiano rasmi yatafanyika Mwezi Desemba, 2014. Pamoja na juhudi hizo, Chuo cha Madini kimeandaa Makubaliano ya Awali (MoU) yatakayowezesha kushirikiana na Chuo cha Southern Alberta Institute of Technology  (SAIT Polytechnic) cha Canada. Lengo la hatua hii ni kuwezesha Chuo hiki kupata uzoefu wa kimataifa. 

159. Mheshimiwa Spika, Chuo cha Madini Dodoma kimeendelea kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 35 Mwaka 2005/06 hadi 547 kwa Mwaka 2013/14 katika ngazi ya Cheti na Stashahada. Chuo hiki kinatoa mafunzo katika fani za Jiolojia na Utafutaji Madini; Uhandisi Uchimbaji Madini; Uhandisi Uchenjuaji Madini; Sayansi za Mafuta na Gesi Asilia; na Uhandisi Usimamizi wa Mazingira Migodini. Aidha, katika Mwaka 2014/15, Chuo kitaanzisha kozi mpya ya Upimaji Migodi (Mine Surveying) na Jimolojia (Gemology) katika ngazi ya Cheti na Stashahada.
       
160. Mheshimiwa Spika, kuanzia Mwaka 2012/13 Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iliamua kwa makusudi kudhamini wanafunzi wa Tanzania kusomea fani za mafuta na gesi asilia ndani na nje ya nchi. Lengo ni kuhakikisha kwamba Wataalam wa Kitanzania wa kuhudumia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia wanapatikana. Hadi sasa, wanafunzi 109 wanapata udhamini katika Chuo cha Madini katika ngazi ya Stashahada. Aidha, katika kujenga uwezo wa Chuo hicho, jumla ya Wakufunzi 6 wanahudhuria mafunzo ya Shahada za Uzamili na Uzamivu katika nchi za Australia, Kenya, Sweden na hapa nchini. Aidha, Chuo kitaendeleza watumishi kitaaluma na kitaalamu ili waweze kutoa mafunzo yaliyokusudiwa ipasavyo kwenye Sekta za Nishati na Madini.

 Shirika la Madini la Taifa - STAMICO

161. Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya Mwaka 2013/14 niliahidi kuwa Serikali itafanya kila linalowezekana ili kuimarisha utendaji wa Shirika hilo. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Wizara ni kuwezesha STAMICO kuajiri watumishi wapya 78 ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, Shirika liliendeleza mradi wa Buckreef kwa ubia na Kampuni ya TANZAM 2000 kwa kukamilisha utafiti wa kimaabara wa njia bora za uchenjuaji miamba (metallurgical studies) katika maeneo ya Bingwa, Buckreef na Tembo Mines katika Mkoa wa Geita. Taratibu za uagizaji wa vifaa na mitambo kwa ajili ya uchimbaji na uzalishaji dhahabu zimeanza kwa lengo la kuanza uzalishaji Mwezi Novemba, 2014.

162. Mheshimiwa Spika, pamoja na kukamilisha utafiti wa Buckreef, Mwezi Aprili, 2014 Shirika lilianza maandalizi ya kuchenjua mabaki ya uchimbaji wa zamani (tailings) katika eneo la Buhemba. Aidha, mkataba rasmi wa ubia kati ya STAMICO na TanzaniteOne Mining Limited ulisainiwa  Mwezi Desemba, 2013. Chini ya ubia huo, mgawanyo wa faida ni asilimia 50 kwa 50 na watumishi wa STAMICO wamepelekwa mgodini kusimamia maslahi ya Taifa. Vilevile, STAMICO kupitia Kampuni yake tanzu ya STAMIGOLD imeshaanza uendelezaji wa maeneo ya “West Zone na Moja Moja” kwa kujenga barabara inayounganisha maeneo hayo na mitambo ya uchenjuaji ya mgodi wa Tulawaka uliopo Wilaya ya Biharamulo.

163. Mheshimiwa Spika,  katika Mwaka 2014/15 STAMICO imepanga kufanya yafuatayo: kuendeleza migodi ya Buckreef (Geita), Buhemba (Butiama), Tulawaka (Biharamulo) na TanzaniteOne (Simanjiro). Aidha, Shirika litaanzisha ununuzi na uchenjuaji wa madini ya bati (tin ore) katika Mkoa wa Kagera  na kufanya utafiti wa madini Rare Earth Metals katika leseni zake zilizopo Wilaya ya Nkasi.

Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania - TMAA

164. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2013/14, TMAA ilitekeleza majukumu yake na kuwezesha kupatikana mafanikio mbalimbali. Katika kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Aprili 2014, baadhi ya migodi mikubwa iliendelea kulipa kodi ya mapato kutokana na ukaguzi uliofanywa na TMAA kwa kushirikiana na TRA. Baadhi ya Kampuni hizo ni Resolute Tanzania Limited (Nzega, Tabora) iliyolipa Shilingi bilioni 3.38 na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (Geita) iliyolipa Shilingi bilioni 50.6 kama kodi ya mapato. Aidha, ukaguzi uliofanywa na Wakala umewezesha jumla ya Shilingi bilioni 4.86 kulipwa Serikalini na baadhi ya wamiliki wa migodi mikubwa na ya kati. Malipo hayo yanajumuisha mrabaha, ushuru wa huduma, ada ya mwaka ya leseni na kodi ya zuio.

165. Mheshimiwa Spika, ukaguzi uliofanywa na TMAA uliwezesha kukusanywa kwa mrabaha kutokana na madini ya ujenzi na viwandani katika Kanda za Mashariki, Kusini, Magharibi, Kati na Ziwa Victoria ambapo jumla ya Shilingi bilioni 1.72 zililipwa kama mrabaha katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014. Malipo hayo yametokana na uzalishaji wa jumla ya tani milioni 5 za madini ya ujenzi na viwandani yaliyokaguliwa na Wakala yenye thamani ya Shilingi bilioni 56.8.

166. Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kupata mrabaha na takwimu sahihi za madini yaliyozalishwa na migodi mikubwa kutokana na  ukaguzi na uhakiki wa madini yaliyozalishwa na kuuzwa na migodi mikubwa ya Bulyanhulu (Shinyanga), Buzwagi (Shinyanga), Geita (Geita), Golden Pride (Tabora), New Luika (Mbeya), North Mara (Mara), Mwadui (Shinyanga), TanzaniteOne (Manyara) na Tulawaka (Kagera). Ukaguzi huo ulisaidia kujua kiasi na thamani halisi ya madini yaliyozalishwa na kuuzwa katika kipindi husika. Ukaguzi huo umewezesha kukusanywa mrabaha wa jumla ya Dola za Marekani milioni 72.90, sawa na Shilingi bilioni 119.56 kwa Mwaka 2013.

167. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti utoroshaji wa madini na ukwepaji wa mrabaha, Wakala umeendelea kufanya ukaguzi kupitia madawati maalum kwenye Viwanja vya Ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza. Kwa Mwaka 2013, ukaguzi huo umewezesha kukamatwa kwa watoroshaji wa madini katika matukio 32 yaliyoripotiwa katika viwanja hivyo. Matukio hayo yanahusu utoroshaji wa madini nje ya nchi yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.1. Wahusika wamefikishwa mahakamani na baadhi yao wamehukumiwa na madini yao kutaifishwa na Serikali kwa mujibu wa Sheria za nchi.

168. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2014/15, Serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwa migodi mikubwa, ya kati na midogo kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ili kuhakikisha kuwa Taifa linanufaika ipasavyo na rasilimali yake ya madini. Aidha, Wizara kupitia TMAA itaendelea kuchukua hatua za makusudi kuelimisha umma kuhusu manufaa yanayopatikana kwenye Sekta ya Madini kama njia ya kukabiliana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu kwa lengo la kupotosha umma.

169. Mheshimiwa Spika, Wakala pia utaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kununua vitendea kazi vinavyohitajika na kuwaendeleza wafanyakazi kitaaluma na kujenga uwezo katika kubainisha maoteo ya mapato ya Serikali kutoka kwenye Sekta ya Madini kwa kutumia mfumo wa kisasa (revenue forecasting model) ili kuwa na takwimu za uhakika za mapato ya Serikali kutokana na Sekta ya Madini. Aidha, Wakala utakamilisha taratibu za usajili wa Maabara ya Wakala katika Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO 17025) ili iweze kutambulika kimataifa.

Wakala wa Jiolojia Tanzania - GST

170. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2013/14, Wakala umefanya utafiti wa kijiolojia na upatikanaji madini katika QDSs kumi na nane (18) kwenye Wilaya za Bagamoyo, Chamwino, Chunya, Dodoma, Handeni, Ikungi, Iramba, Kilindi, Ludewa, Makete, Mbinga, Mkalama, Mvomero, Singida na Songea Vijijini. Uchoraji wa ramani hizo unaendelea kukamilishwa. Aidha, Wakala umekamilisha utafiti wa jiokemia katika QDSs saba (7) kwa ajili ya utafutaji madini kwenye Wilaya za Dodoma, Ikungi, Iramba, Manyoni, Mkalama na Singida.

171. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini, Wakala pia ulifanya utafiti wa kina wa kijiofizikia (ground geophysical surveys) kwenye QDSs saba (7) katika Wilaya za Bagamoyo, Handeni, Iramba, Kilindi, Mkalama na Singida kwa ajili ya kufuatilia maeneo yaliyoonesha kuwa na viashiria vizuri vya kuwepo madini kutokana na utafiti wa kijiofizikia kwa kutumia ndege. Matokeo ya utafiti huo yanaendelea kutafsiriwa na taarifa zake zinaandaliwa na zitakamilishwa kabla ya Mwezi Januari, 2015.

172. Mheshimiwa Spika, ili kujiimarisha kiutendaji, Wakala umebadilisha mfumo wa kuhifadhi na kusambaza taarifa na takwimu za jiosayansi kwa kuziweka kwenye Computer Based Centralized Geo-Scientific Data and Information Management Systems. Mabadiliko hayo yanawezesha kuwa na takwimu za uhakika, zinazopatikana kwa urahisi na kwa wadau wengi zaidi.

173. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka 2014/15, Wakala umejipanga kuendeleza tafiti za kijiosayansi za upatikanaji madini, hususan technology metals, upatikanaji wa nishati ya jotoardhi, gesi za Helium (Mara) na Carbon Dioxide (Mbeya) na kuchora ramani 4 za kijiolojia katika Wilaya za Kilwa, Liwale, Nachingwea na Ruangwa pamoja na ramani mbili (2) za kijiokemia katika Wilaya za Liwale na Ruangwa.

  Changamoto katika Sekta ya Madini

174. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya Madini imekabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo: upatikanaji wa masoko ya uhakika ya baadhi ya madini yanayozalishwa na wachimbaji wadogo; kiwango kidogo cha uwekezaji wa mitaji katika uchimbaji mdogo wa madini; kiwango kidogo cha fungamanisho la Sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi; utoroshaji wa madini nje ya nchi; na upungufu wa watumishi wenye ujuzi katika kusimamia Sekta ya Madini.
        

Mipango ya Kukabiliana na Changamoto Zilizojitokeza

175. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, Wizara itaendelea kuboresha na kuimarisha Idara ya Madini kwa kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi na watumishi katika Ofisi zake. Aidha, Wizara itaimarisha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini ili kuendelea kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini nje ya nchi.

C. AJIRA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU

176. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2013/14 Wizara imeendelea kuajiri na kuendeleza watumishi wake ili waweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi zaidi ikilenga kuinua mchango wa Sekta za Nishati na Madini kwenye Pato la Taifa. Katika kipindi hicho, jumla ya watumishi walioajiriwa na Wizara na Taasisi zake katika kada mbalimbali ni 227. Kati ya hao, Wizara iliajiri watumishi 36, TMAA 11, STAMICO 78, REA 4 na TPDC  51. Vilevile, TPDC inaendelea na utaratibu wa kuajiri watumishi wapya 226. Aidha, katika kuendeleza watumishi, Wizara ilipeleka watumishi 80 katika mafunzo ya muda mfupi na watumishi 60 katika mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi. Katika Mwaka 2014/15, Wizara na Taasisi zake inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 508 katika kada mbalimbali. Kati ya hao, watakaoajiriwa na Wizara ni watumishi 207; TMAA 29; STAMICO 79; GST 52; MRI 74; TPDC 51; na REA 16.

177. Mheshimiwa Spika, Wizara pia kwa kutambua kwamba masuala ya mafuta na gesi asilia ni maeneo mapya nchini, itaendelea kutekeleza Mpango Kabambe wa Uendelezaji wa Rasilimali Watu (Marshall Plan on Capacity Building and Development in Oil and Gas Industry). Hii ni miongoni mwa mipango ya Serikali kuhahakikisha kuwa nchi inakuwa na wataalamu wa Kitanzania wa kutosha katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia. Mpango huu unashirikisha vyuo mbalimbali nchini vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na Chuo Kikuu cha Dodoma ambavyo pamoja na fani nyingine vimeanzisha pia mitaala kuhusu mafuta na gesi asilia (BSc in Petroleum Engineering,  Petroleum Chemistry na BSc Petroleum Geology).

178. Mheshimiwa Spika, baada ya mitaala hiyo kuanzishwa, Wizara kwa Mwaka 2013/14 ilitoa ufadhili kwa vijana wa Kitanzania 9 katika Chuo Kikuu cha Dodoma kusomea Shahada ya uhandisi wa Mafuta na Gesi Asilia; 109 Chuo cha Madini Dodoma kusomea Stashahada ya Sayansi ya Mafuta na Gesi Asilia; 59 VETA – Mtwara kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya Lindi na Mtwara kusomea ufundi stadi ambao utawawezesha kupata ajira sehemu za uzalishaji wa mafuta na gesi asilia; na wanafunzi 9 kusomea Shahada ya Uzamili katika masuala ya Mafuta na Gesi Asilia huko Uingereza. Aidha, Watanzania 8 walipata ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na mmoja nchini Ufaransa kusomea Shahada ya Uzamili ya Mafuta na Gesi Asilia. Vilevile, watumishi 38 kutoka Taasisi mbalimbali walihudhuria mafunzo ya muda mfupi yaliyofadhiliwa na Serikali ya Uholanzi ambayo yalifanyika nchini Tanzania na Uholanzi. Vilevile, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimewezesha jumla ya wanafunzi 19 kwenda nchini Norway kusomea Shahada ya Uzamili ya Mafuta na Gesi Asilia. Kati ya wanafunzi hao, 11 wanasoma Msc. in Petroleum Engineering na 8 wanasoma Msc. in Petroleum Geology.

179. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha utendaji wa watumishi wake, Wizara kwa Mwaka 2014/15 inatarajia kupeleka mafunzoni watumishi 246 katika mafunzo ya muda mfupi na watumishi 95 katika mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi. Aidha, pamoja na kuendelea kuwalipia wanafunzi  wa Kitanzania walioanza masomo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, Wizara kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inatarajia kuwapeleka Watanzania katika nchi mbalimbali kwenye mafunzo ya Shahada za Uzamili, ambapo 10 watasomeshwa na Serikali ya Brazili;  10 Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China; na wawili (2) Serikali ya Thailand katika masuala ya mafuta na gesi asilia. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na nchi na mashirika mbalimbali ili kuongeza idadi ya Watanzania watakaosomeshwa katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia kwa ajili ya kusimamia Sekta hiyo.

180. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki pia, Wizara itaanzisha mpango maalum wa kutoa mafunzo ya kusimamia Sekta ya Nishati kwa kushirikisha Washirika wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Sweden na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Fedha zitakazotumika kutekeleza mpango huo, ambazo zimetengwa katika Bajeti ya Mwaka 2014/15 ni Shilingi bilioni 7.80 sawa na Dola za Marekani milioni 4.76.

181. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza tija na motisha kwa watumishi, kwa Mwaka 2013/14 Wizara iliwapandisha vyeo  jumla ya watumishi 57 katika fani mbalimbali na kuwathibitisha kazini watumishi 36. Katika Mwaka 2014/15 Wizara inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 157 ambao wamepata sifa za kitaaluma na wenye utendaji mzuri wa kazi kulingana na Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 1999. Aidha, ili kuongeza ufanisi wa masuala ya Sheria katika Sekta za Nishati na Madini zinazokua kwa kasi, Serikali imeboresha muundo wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kukipandisha hadhi Kitengo cha Sheria na kuwa Idara kamili. 

182. Mheshimiwa Spika, katika kujali afya za watumishi, kwa Mwaka 2013/14, Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kutekeleza  Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa Mwaka 2006 kwa kuwahudumia watumishi wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) na wenye Ukimwi waliojitokeza kwa kuwapa lishe na madawa maalumu. Katika Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kutoa elimu mahali pa kazi ili kuzuia maambukizi mapya na kuwahudumia waathirika wa Ukimwi kadri watakavyojitokeza. Sambamba na jitihada hizo, Wizara pia itaendelea kuhamasiha watumishi kupima afya hususan kuhusiana na magonjwa ya shinikizo la damu (blood pressure), kisukari na saratani.

Elimu kwa Umma kuhusu Rasilimali za Nishati na Madini

183. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uelewa kuhusu masuala mbalimbali katika Sekta za Nishati na Madini, kuanzia  Mwaka 2013/14 Wizara imeweka Mpango wa kutoa elimu kwa wananchi. Ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,  Wizara inatumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari na Viongozi wa aina mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Dini. Mpango huo ulizinduliwa rasmi Jijini Dar es Salaam na Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Januari, 2014.

184.  Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango huo, kati ya Mwezi Januari na Machi 2014, Wizara imefanikisha kufanyika kwa makongamano matatu (3) katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia pamoja na Sekta ya Madini, yakilenga pamoja na mambo mengine, kuonesha faida zinazopatikana kwa Watanzania katika uwekezaji kwenye rasilimali hizo. Katika Makongamano hayo jumla ya washiriki 605 walihudhuria, kati ya hao 209 walikuwa katika Kongamano lililofanyika Dar es Salaam, 227 Lindi na Mtwara  na 169 Pwani. 

185. Mheshimiwa Spika, kimsingi makongamano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na washiriki kupata ufafanuzi ulio sahihi katika masuala yanayohusu Sekta za Nishati na Madini. Washiriki wengi wamekiri kuelimika na kuahidi kueneza elimu sahihi katika maeneo yao. Aidha, kupitia makongamano haya, washiriki hao kwa niaba ya Watanzania walishuhudia kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuendeleza Sekta hizo kwa manufaa ya Watanzania. Moja ya ushuhuda ni ule uliotokea wakati Washiriki wa kongamano la Mikoa ya Mtwara na Lindi walipotembelea eneo la Madimba panapojengwa mitambo ya kusafisha gesi asilia, ambapo mmoja wao alitamka wazi kuwa “kumbe Serikali inafanya mambo makubwa lakini wananchi kwa kutoyajua, wanaendelea kudanganywa kila siku kwa kupewa taarifa zisizo sahihi”.

186.  Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza mafanikio hayo, Wizara katika Bajeti yake ya Mwaka 2014/15 imeamua kwa dhati kuanzisha programu maalum ya kuelimisha umma (Public Awareness Program), ambayo itawezesha Wizara kutoa elimu juu ya utekelezaji wa shughuli zake kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo luninga, magazeti, redio, makongamano, tovuti na mihadhara. Lengo la Wizara ni kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania juu ya Sekta hizo ili kuwa na taarifa sahihi za shughuli zinazotekelezwa na Serikali yao na faida zinazopatikana.
D.USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

187. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa shughuli zake, Wizara ya Nishati na Madini inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali. Kwa niaba ya Serikali napenda kutoa shukrani kwa Serikali za Algeria, Brazil, Canada, China, Finland, Korea ya Kusini, Marekani, Norway, Sweden, Thailand, Trinidad na Tobago, Ujerumani na Urusi. Vilevile, natoa shukrani kwa Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Exim ya China, Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA), Benki ya HSBC, Benki ya BADEA, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), Umoja wa Ulaya (EU), pamoja na Taasisi na Mashirika ya AFD (Ufaransa), CIDA (Canada), DANIDA (Denmark), ECDF (Korea Kusini), FINIDA (Finland), JICA (Japan), MCC (Marekani), NORAD (Norway), OFID (Saudi Arabia), ORIO (Uholanzi), Sida (Sweden), IFC, UNDP, Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Climate Investment Fund (CIF), USAID (Marekani) na JBIC (Japan).

E. SHUKRANI

188. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. Stephen Julius Masele, Mbunge - Jimbo la Shinyanga Mjini, anayesimamia masuala ya Madini; na Mhe. Charles Muhangwa Kitwanga, Mbunge - Jimbo la Misungwi, anayesimamia masuala ya Nishati. Nikiri wazi kuwa Naibu Mawaziri hao wamekuwa msaada mkubwa kwangu katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, namshukuru kwa dhati aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. George Boniface Simbachawene, Mbunge - Jimbo la Kibakwe kwa mchango mkubwa alioutoa akiwa Wizara ya Nishati na Madini. Namtakia mafanikio katika majukumu yake mapya aliyoaminiwa na Mhe. Rais katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

189. Mheshimiwa Spika, nawashukuru Mwenyekiti, Makamu na wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwanza kwa ushauri na maelekezo yao wanayoyatoa katika kuongeza ufanisi wa Wizara yangu. Kamati hii imekuwa chachu muhimu katika kutoa miongozo ya kusaidia kutatua matatizo na changamoto zinazoikabili Wizara. Nawashukuru viongozi na wajumbe wote wa Kamati hii na ni matumaini yangu kuwa wataendelea kutoa ushirikiano ili kuendeleza Sekta za Nishati na Madini kwa faida ya Watanzania wote.

190. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nawashukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim C. Maswi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Ngosi X. Mwihava kwa ushirikiano wanaonipa na kwa utendaji wao mahiri ambao unaiwezesha Wizara hii kusonga mbele siku hadi siku. Nakiri kuwa viongozi hawa wamekuwa kiungo muhimu na wenye umakini mkubwa katika timu yangu ya ushindi ya Wizara. Aidha, nawashukuru Kamishna wa Nishati na wa Masuala ya Petroli; Kamishna wa Madini; Wakuu wa Idara, Sehemu na Vitengo.

191. Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi za EWURA, PICL, PUMA, REA, STAMICO, TANESCO, TIPER na TPDC; Wenyeviti wa Bodi za Ushauri za GST, TMAA na MRI pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Madini kwa ushirikiano wanaonipa katika kuongoza Wizara. Ili Bodi hizi zifanye kazi vizuri zinahitaji Menejimenti nzuri na yenye mwono wa mabadiliko. Nawapongeza sana Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara; na watumishi wote kwa ujumla kwa ushirikiano wao katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ndani ya Wizara, Taasisi na Kampuni zetu.

192. Mheshimiwa Spika, kwa unyenyekevu kabisa napenda kuwashukuru na kuwapongeza Viongozi wote wa Dini nchini kwa kukubali kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini katika kuelimisha jamii kwa kauli mbiu isemayoUendelezaji wa Rasilimali za Gesi Asilia, Mafuta na Madini kwa Amani na Maendeleo ya Nchi Yetu”. Kupitia viongozi hawa Wizara imeendelea kuelimisha jamii juu ya rasilimali zake katika makongamano mbalimbali nchini. Aidha, navishukuru vyombo vya habari na wadau wengine kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini katika kutoa habari na kuelimisha wananchi juu ya uendelezaji wa rasilimali zetu kwa manufaa ya Taifa letu. Nawaomba Viongozi wa Dini na wadau wengine tuendelee kushirikiana ili kuleta maendeleo endelevu kupitia rasilimali za nishati na madini. Napenda kuwahakikishia kuwa Wizara ya Nishati na Madini haitarudi nyuma katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo na changamoto mbalimbali zinazoikabili na itaendelea kushirikisha jamii na wananchi kwa ujumla katika hatua zake za utekelezaji.

193. Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa namshukuru sana mke wangu Bertha Muhongo pamoja na wanangu Godfrey Chirangi, Dkt. Musuto Chirangi, Dkt. Bwire Chirangi, Rukonge Muhongo, ndugu, marafiki na Wananchi kwa ujumla kwa msaada mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kusimamia Wizara ya Nishati na Madini kwa umakini na ubunifu wa hali ya juu.

F:   HITIMISHO

194. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Mwaka 2014/15 inakusudia kuimarisha na kuendeleza Sekta za Nishati na Madini ili kuongeza zaidi mchango wake katika kujenga uchumi imara wa Taifa utakaotoa ajira mpya kwa Watanzania na kupunguza umaskini nchini.
          
195. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi 1,082,555,622,000.00 kama ifuatavyo:

(i)   Bajeti ya Maendeleo ni Shilingi 957,177,170,000.00 sawa na asilimia 88.4  ya  Bajeti  yote  ya Wizara. Kati ya fedha hizo, Shilingi 652,805,000,000.00 ni fedha za ndani, sawa na  asilimia 68.2  ya  fedha za maendeleo na Shilingi 304,372,170,000.00 sawa na asilimia 31.8 ni fedha za nje; na
(ii) Matumizi ya Kawaida ni Shilingi 125,378,452,000.00 sawa na asilimia 11.6 ya Bajeti yote ya Wizara. Kati ya fedha hizo Shilingi 26,912,948,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara, Mashirika na Taasisi zake (sawa na asilimia 21.47 ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida au asilimia 2.49 ya Bajeti yote) na Shilingi 98,465,504,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (O.C), sawa na asilimia 78.53 ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida au asilimia 9.1 ya Bajeti yote.
196. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: