BAJETI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAKAZI


HOTUBA YA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, MHESHIMIWA PROF. ANNA  KAJUMULO TIBAIJUKA  (MB),  
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI  YA  WIZARA  YA ARDHI, NYUMBA NA  MAENDELEO  YA MAKAZI 
KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15

UTANGULIZI
1.              Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu likubali kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka wa fedha 2013/14 na malengo ya Wizara katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha  2014/15.

2.              Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, nampongeza Mhe. Dkt. Asha Rose Migiro kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge lako na Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, nawapongeza Mhe. Ridhiwani Kikwete na Mhe. Godfrey Mgimwa kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu na kuimarisha safu ya Wabunge vijana wa CCM.

3.              Mheshimiwa Spika, naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu kuwa azipokee na kuzilaza mahala pema peponi roho za marehemu Mhe. Dkt. William Augustino Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mbunge wa Jimbo la Kalenga na Mhe. Saidi Bwanamdogo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze. Vilevile, kwa namna ya pekee natoa pole kwa Watanzania wenzangu walioathirika na majanga mbalimbali likiwemo la mafuriko yaliyotokea sehemu mbalimbali nchini kati ya mwezi Machi na Aprili, 2014. Sina budi kuwalilia na kuwakumbuka wananchi kadhaa wa Wilaya ya Muleba Kata ya Mazinga, Nyakabango, Kimwani na Rulanda waliouawa na mamba na viboko kutoka Hifadhi ya Taifa ya Rubondo. Maisha yao hayakupotea bure nimetoa taarifa kuepusha mashambulizi mengine. Aidha kuna wananchi ambao wamepoteza maisha yao katika migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini. Nichukue nafasi hii kuwapa pole wafiwa, njia pekee ya kuwaenzi ndugu zetu hao ni kumaliza migogoro hii tukawa taifa na jamii inayomaliza tofauti kwa majidiliano (...dialogue and not confrontation). 

4.              Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na  Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mpanda Mashariki, kwa uongozi wao mahiri. Nawashukuru kwa ushauri, maelekezo na ushirikiano wanaonipa, ulioniwezesha kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa ya kuongoza sekta hii mtambuka na muhimu katika maendeleo ya Taifa letu. Nawapongeza kwa dhati Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; pia, Mhe. Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; na Mhe. Balozi Ali Idd Seif, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar. Sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na za miaka 50 ya Uhuru zilionesha jinsi gani taifa hili linasonga mbele kwa amani, mshikamano na upendo. Tanzania imekuwa kisiwa cha amani si kwa kubahatisha bali kwa uongozi imara chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

5.              Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe kwa kuongoza shughuli za Bunge kwa ufanisi. Mwenyezi Mungu aendelee kukuongoza na kukupa nguvu, afya na hekima za kumudu zaidi majukumu yako. Pia, nampongeza Mhe. Job Yustino Ndugai,  Mbunge wa Kongwa na Naibu Spika wa Bunge letu kwa utendaji mzuri katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.

6.              Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini kwa kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu yangu nikiwa Mbunge wao. Pamoja na kuwa na kazi nyingi za kitaifa, wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini wamekuwa wakinipa ushirikiano mzuri na kujitahidi kukutana nami ninapopata nafasi kufika jimboni kwa kuhudhuria vikao na mikutano katika tarafa zao au kupokea wageni na wataalaam waelekezi ninaowatuma kufika kusukuma maendeleo yetu. Kama Waziri, tena wa Ardhi, muda wa kuwa jimboni ni mdogo. Pamoja na hayo wananchi wa Muleba wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano ya Kata ninapofika ili tutathmini maendeleo, kujipanga vizuri na kula na kunywa pamoja. Muleba tunasema “Ebitaina mahyo tibyela”. Au “Kazi bila pongezi haiendi”. Ninawashukuru sana kwa moyo huo wa upendo ambao umewaumbua wanaodhani kuwa kukaa mbali ni kukosa mahusiano.

7.              Mheshimiwa Spika, aidha, ninawashukuru ndugu, jamaa na marafiki wanaonisaidia na kunipa ushirikiano wa karibu katika kutimiza majukumu ya Uwaziri na Ubunge.  Nawashukuru wananchi na kuwahakikishia popote pale mlipo, iwe Tarafa ya Nshamba, Kimwani au Muleba yenyewe, kwamba tutayalinda mafanikio tuliyoyafikia na kuongeza kasi zaidi ili kufikia malengo ya kulinda amani, utulivu na kufikia maisha bora. Namuomba Mwenyezi Mungu amwezeshe kila mwananchi kulitambua hili na kuchangia katika nafasi yake kwa kadri ya uwezo wake kufikia maisha bora. Mwisho, ninatuma salamu kwa mama yangu mzazi Ma Aulelia Kajumulo hapo Muleba. Sala zake za kila siku zimeendelea kuniimarisha katika kutekeleza majukumu yangu. Nasimama hapa nikiwa mzima wa afya kwa sababu hiyo.


8.              Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru kwa dhati viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao wamenisaidia katika kutekeleza majukumu yangu magumu hasa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi sehemu mbalimbali nchini. Hii imenipa nguvu mpya katika kutekeleza ilani ya CCM. Aidha, sina budi kutambua mchango wa viongozi wa dini na vyama vya hiari ambao nimeshirikiana nao katika kazi zangu za kutatua migororo na changamoto nyingi za sekta ya ardhi ambazo zinahitaji ushiriki wao, busara zao na kutambua na kutofautisha sheria na haki na uhusiano wake.

9.              Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee natoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. James Daudi Lembeli, Mbunge wa Kahama kwa ushirikiano mkubwa na ushauri wao ambao uliiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Natoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri, Mhe. George Bonifance Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe kwa ushirikiano na umoja tuliojenga katika kutekeleza majukumu yetu. Nawashukuru pia Katibu Mkuu Bw. Alphayo Japani Kidata; Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Selassie David Mayunga; watendaji katika Idara, Vitengo, Shirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara kwa ushauri na mshikamano wao katika kupanga na kutekeleza mipango ya Wizara. Zipo changamoto nyingi zinazoikabili sekta yetu lakini kwa mshikamano na umoja wao naamini tumeweza kuendelea kukabiliana nazo.


CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SEKTA YA ARDHI
10.            Mheshimiwa Spika, changamoto zinazoendelea kuikabili sekta yangu, kama nilivyoziorodhesha mwaka jana, zinagawanyika katika maeneo manne (4) makubwa kama ifuatavyo:
                i.                  Uelewa usiotosheleza wa wananchi kuhusu sekta yenyewe hasa sheria zake, taratibu na miongozo iliyopo; haki zao na wajibu wao;
               ii.                  Nafasi ya vyombo mbalimbali vya usimamizi  na utendaji wake;
              iii.                  Vitendea kazi vilivyopo na vinavyohitajika ili kukidhi mahitaji ya sekta nyeti ya ardhi ambayo ni kiungo muhimu katika maendeleo; na,
              iv.                  Mazingira ya utendaji yaliyopo  nje ya uwezo wa Wizara.
11.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kuwa itaeleza jinsi ilivyojipanga kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa majukumu yake.  Katika kutekeleza ahadi hiyo, Wizara imeongeza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu sheria za ardhi, kanuni na taratibu pamoja na kuandaa miongozo mbalimbali; kupunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa vitendea kazi katika sehemu za kazi kwa mfano, ununuzi wa mtambo mpya wa uchapaji wa ramani na nyaraka. Ili kuongeza    mahusiano na wadau wake na kuboresha mazingira ya utendaji yaliyoko nje ya uwezo wa Wizara, Wizara iliweza kuwashawishi wahisani wa maendeleo ambao tayari wameanza kuipatia Wizara rasilimali fedha za kutekeleza Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria za Ardhi. Pia, Wizara ipo katika hatua za kurekebisha muundo wake ili watumishi wa Sekta ya Ardhi walioko Halmashauri wawajibike moja kwa moja Wizarani.

12.             Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hayo, naomba sasa nieleze kwa kifupi utekelezaji wa Mpango wa Wizara kwa mwaka wa fedha 2013/14 na Shabaha za Mpango wa mwaka wa fedha 2014/15. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa takwimu nyingi za utekelezaji zinaishia mwezi Aprili, 2014 na zitakuwa tofauti ifikapo mwisho wa mwezi Juni, 2014.





MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2013/14 NA MALENGO YA
MWAKA WA FEDHA 2014/15

Ukusanyaji wa Mapato
13.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 100.05 kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato yanayotokana na Sekta ya Ardhi. Hadi Aprili, 2014 jumla ya Shilingi bilioni 37.03 zilikusanywa. Makusanyo haya ni zaidi ya maduhuli yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2012/13 kwa shilingi bilioni 14.27. Hata hivyo, mwenendo wa makusanyo kwa mwaka wa fedha 2013/14 ni hafifu yakilinganishwa na lengo la kukusanya shilingi bilioni 100. Sababu zilizochangia hali hiyo ni pamoja na kubainika kwamba makusanya ya nyuma yaliyopelekea malengo ya ukusanyaji mpya kuwekwa yalitokana na vyanzo visivyojirudia, yaani tozo kwa viwanja vipya wakati wa mradi wa viwanja elfu ishirini. Kwa hiyo pamoja na juhudi za kukusanya maduhuli kuongezeka na kupanda kwa viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali za ardhi bado malengo hayakufikiwa. Aidha utaratibu wa ulipaji wa kodi usio rafiki kwa wananchi, tabia ya kusubiri kulipa kodi dakika za mwisho wa mwaka wa fedha ambao bado unaendelea, na uelewa mdogo wa wananchi juu ya wajibu wao wa kulipa kodi pia umechangia kutokufikia malengo hadi sasa. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara inarekebisha viwango vya kodi, ada na tozo za ardhi pale ambapo zitadhihirika kuwa juu ya uwezo wa wananchi (affordability test); mazungumzo yamefanyika ili kuhakikisha utaratibu wa kufanya malipo unarahisishwa; na, kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu wajibu wa wamiliki wa viwanja na mashamba kulipa kodi. Aidha wanaoshindwa kulipa kodi ya ardhi watachukuliwa hatua na kubatilisha milki zao kwa kukiuka masharti ya miliki.
 
14.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15, baada ya kurekebisha uhalisia wa vyanzo vya walipa kodi tofauti na walipa tozo,  Wizara imeweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 61.32. Maduhuli haya yatakusanywa kwa kutumia mikakati ifuatavyo: kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi; kupanga, kupima na kumilikisha maeneo mapya; kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya pango la ardhi; kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia teknolojia za kisasa za malipo na kuhuisha viwango vya kodi ya ardhi. Aidha, Wizara yangu itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi kutimiza masharti ya umiliki wa ardhi ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ya pango la ardhi, ada na tozo nyingine kwa mujibu wa sheria.

Matumizi
15.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliidhinishiwa matumizi ya jumla ya Shilingi bilioni  108.3. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 10.20 zilitengwa kwa ajili ya mishahara; Shilingi bilioni 25.96 zilitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo; na Shilingi bilioni 72.17 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha za miradi ya maendeleo Shilingi bilioni 56.2 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 16 ni fedha za nje. Hadi Aprili, 2014 jumla ya fedha zilizopatikana ni Shilingi bilioni 47.94 sawa na asilimia  44.25 ya fedha zilizoidhinishwa. Jumla ya Shilingi bilioni 38.80 sawa na asilimia 81 ya kiasi kilichotolewa, zilitumika (Jedwali Na. 1). Ni matarajio yangu kwamba fedha zilizotolewa zitatumika hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2014.


UTAWALA WA ARDHI

16.             Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa ardhi nchini unahusisha mamlaka kuu tatu ambazo ni Halmashauri za Vijiji, Halmashauri za Wilaya na Miji na Wizara chini ya ofisi ya Kamishna wa Ardhi. Majukumu na mamlaka za usimamizi yameainishwa vema katika Sheria za Ardhi. Lengo la sheria ni kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikishwa ipasavyo katika suala zima la usimamizi wa rasilimali ardhi kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Taifa.

Ofisi za Ardhi za Kanda
17.             Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi, Wizara imeendelea kuanzisha na kuimarisha Ofisi za Ardhi za Kanda. Hadi sasa Wizara ina Ofisi za Ardhi za Kanda 7 ambazo ni Kanda ya Kusini (Mtwara), Ziwa (Mwanza), Mashariki (Dar es Salaam), Kaskazini (Moshi), Kati (Dodoma), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) na Magharibi (Tabora). Wizara imepanga kupeleka huduma za Mipango Miji na Vijiji, Upimaji na Ramani na Uthamini wa Mali katika ofisi hizo katika mwaka wa fedha 2014/15.

18.             Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14, Wizara yangu iliahidi kuanza kutoa huduma za ardhi katika ofisi ya ardhi ya Kanda ya Magharibi iliyopo mjini Tabora. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ofisi hiyo imeanza kazi rasmi na inahudumia mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Katavi, ambayo awali ilikuwa inahudumiwa na Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Nyanda za Juu Kusini (Mbeya). Ni matumaini yangu kwamba kwa kuanzishwa ofisi hiyo kutawawezesha wananchi kupata huduma za ardhi karibu na maeneo yao.

19.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara yangu itaigawanya Kanda ya Mashariki kuwa Kanda mbili; Kanda ya Dar  es Salaam na Kanda ya Mashariki. Kanda ya Dar es Salaam itahudumia Mkoa wa Dar es Salaam pekee kutoka makao makuu ya Wizara na Kanda ya Mashariki itahudumia Mikoa ya Pwani na Morogoro kutoka aidha mkoa wa Morogoro au Pwani kama itakavyoamuliwa na wadau. Kanda ya Mashariki itaanza kutoa huduma za ardhi kuanzia Julai, 2014. Hatua hii ni muendelezo wa kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi na kuongeza ufanisi.

Mkakati wa Kupima Kila Kipande cha Ardhi Nchini
20.            Mheshimiwa Spika, Sheria za ardhi zinatoa miongozo muhimu ya kusimamia ardhi na fursa ya kuhakikisha kuwa ardhi yote nchini inamilikiwa kisheria. Wizara imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi nchini kinapangwa, kinapimwa, kinamilikishwa na kinasajiliwa kisheria. Mkakati huu ambao umeanza kutekelezwa katika Wilaya ya Mvomero katika Mkoa wa Morogoro utasaidia kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi. Katika mwaka wa fedha 2014/15 utekelezaji utaendelea katika Wilaya za Kilosa na Kilombero, Mkoa wa Morogoro. Natoa rai  kwa wananchi na Halmashauri ambazo maeneo yao yatahusika katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati huu kutoa ushirikiano wa dhati mara zitakapofikiwa. Aidha, ninawaomba wananchi pia kutambua ardhi ikishapimwa na kumilikishwa itakuwa haramu kuivamia na kuitumia kwa matumizi ambayo hayakupangwa. Migogoro haiwezi kuisha kama kila mwananchi hatii matumizi yaliyopangwa.

Utekelezaji wa Sheria ya Ardhi
21.            Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inatoa fursa ya kuhakikisha kuwa ardhi yote nchini inamilikiwa kisheria. Hadi Aprili 2014, vijiji 20 vimewezeshwa kuandaa mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi ya kijiji, Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 972 vimetolewa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, Hati za Hakimiliki ya Kimila 24,945 zimetolewa na Hati Miliki 24,651 zimetolewa (Jedwali Na. 2). Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara yangu itaendelea na kazi ya uhakiki na upimaji wa vipande vya ardhi wilayani Mvomero na inatarajia kupima na kuandaa hatimiliki za kimila 70,000 na Hati Miliki 40,000. Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa zinapanga, zinapima, zinamilikisha viwanja na kuandaa Hati ili wananchi waweze kuwa na milki salama.

22.            Mheshimiwa Spika, Wizara ina jukumu la kushughulikia uteuzi wa wajumbe wa Kamati za Ugawaji Ardhi katika ngazi ya Taifa, Miji na Wilaya. Kamati hizi ni vyombo muhimu katika kushughulikia ugawaji wa ardhi nchini. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara imefanya uteuzi wa Wajumbe wa Kamati za Ugawaji Ardhi katika Halmashauri za Magu, Musoma, Kigoma/Ujiji, Bukoba, Kilosa, Morogoro, Masasi, Tandahimba, Bariadi, Lindi, Mpanda, Same, Kilolo, Sengerema, Manispaa ya Morogoro na Manispaa ya Moshi. Aidha, Kamati ya Taifa ya Ugawaji Ardhi pamoja na majukumu mengine inalo jukumu la kugawa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.  Katika mwaka wa fedha 2013/14 kamati hii ilipokea maombi 96 na kutoa ushauri wa kumilikisha viwanja 35 na mashamba 12 kwa ajili ya uwekezaji. Nazihimiza Halmashauri ambazo hazina Kamati za Ugawaji Ardhi za Wilaya na Miji kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wajumbe wa kamati hizo Wizarani ili uteuzi uweze kufanyika. 

23.            Mheshimiwa Spika, mojawapo ya majukumu ya Wizara yangu ni kusimamia uhamisho wa milki za ardhi. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kushughulikia maombi ya uhamisho wa milki 1,800. Hadi Aprili, 2014 Wizara imeshughulikia maombi ya uhamisho wa milki 3,079. Kwa mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itashughulikia maombi ya uhamisho wa milki 3,500. Vilevile, Wizara inaendelea na jukumu la kusimamia masharti ya umiliki wa ardhi na kuhakikisha kuwa miliki zinaendelezwa ipasavyo. Hadi Aprili, 2014 ilani za ubatilisho 3,581 zilitumwa kwa wamiliki waliokiuka masharti ya umiliki wakiwemo wamiliki wa mashamba yasiyoendelezwa nchini. Kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaendelea kushughulikia ubatilisho wa milki zote zinazokiuka masharti ya uendelezaji. Napenda kuwashauri wananchi wote wanaonunua milki za ardhi kuhakikisha wanafanya uhamisho wa milki na kuzisajili.

Usajili wa Hati na Nyaraka za Kisheria
24.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilikuwa na lengo la kusajili hati za kumiliki ardhi pamoja na nyaraka za kisheria zipatazo 80,000. Kati ya hizo hati za kumiliki ardhi  ni 35,000 na nyaraka za kisheria ni 45,000. Hadi Aprili, 2014 jumla ya hatimiliki na nyaraka za kisheria 50,592 zilisajiliwa.  Kati ya hizo hatimiliki ni 21,285 na nyaraka za kisheria ni 29,307, zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Ardhi Sura Na. 334 (Jedwali Na. 3A). Aidha, nyaraka 5,072 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Nyaraka, Sura117 (Jedwali Na. 3B). Pia, rehani ya mali zinazohamishika zipatazo 2,077 zilisajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Rehani ya Mali Zinazohamishika, Sura 210 (Jedwali Na. 3C). Aidha, katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inakusudia kusajili Hatimiliki 42,000,  Nyaraka za Kisheria 45,000 na Hati ya Sehemu ya Jengo/eneo 2,000.






Kuboresha Kumbukumbu za Ardhi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
25.             Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kutekeleza jukumu muhimu la utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na kuzisimamia ipasavyo kwa kuweka na kuimarisha mifumo ya kielektroniki. Mifumo hiyo ni pamoja na mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi wa Integrated Land Management Information System (ILMIS) na mfumo wa kutunza kumbukumbu za kodi ya ardhi (Land Rent Management System - LRMS).

26.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kuendelea na kazi ya kuweka mfumo unganishi wa kuhifadhi kumbukumbu za ardhi (Integrated Land Management Information System - ILMIS). Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imepata fedha za kujenga mfumo huo na ujenzi utaanza rasmi katika mwaka wa fedha 2014/15.

27.            Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea na kazi ya kusimika mfumo wa kielekitroniki wa kuhifadhi kumbukumbu na kukadiria kodi ya Ardhi. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga kusimika mfumo huo katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 20. Hadi Aprili, 2014 mfumo huu ulisimikwa katika Ofisi za Ardhi za Halmashauri 75 (Jedwali Na. 4). Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea na kazi ya kusimika mfumo wa kielekitroniki wa kuhifadhi kumbukumbu na kukadiria kodi ya ardhi katika ofisi za Ardhi za Halmashauri 30.

UTHAMINI WA MALI

28.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inalo jukumu la kuthamini na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali kwa madhumuni mbalimbali ya kuwezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kuna aina kuu mbili za uthamini ambazo ni Uthamini wa Kawaida na Uthamini wa Kisheria.

Uthamini wa Kawaida
29.            Mheshimiwa Spika, Uthamini wa Kawaida hufanyika kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma na hauna maelekezo maalum ya sheria. Uthamini huu hufanyika ili kuwezesha maamuzi mbalimbali kufanyika yakiwemo maamuzi ya mauzo au manunuzi ya mali, kuweka mali rehani, kuomba mikopo benki, dhamana ya mahakama, mizania na bima. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliweka lengo la kuthamini na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali 15,000. Hadi Aprili, 2014, Wizara iliidhinisha taarifa za uthamini wa kawaida wa mali 7,904 (Jedwali Na.5A). Kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itafanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa mali 10,000 kwa matumizi mbalimbali kadri maombi yatakavyowasilishwa.

Uthamini wa Kisheria
30.             Mheshimiwa Spika, Uthamini wa Kisheria hufanyika ili kuwezesha utozaji wa ada na ushuru wa Serikali kutokana na mauzo au uhamisho wa umiliki wa mali, utozaji malipo ya awali (premium) wakati wa kutoa milki, utozaji kodi ya pango la ardhi na ukadiriaji fidia za mali zinazoguswa na miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini. Katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ilipanga kufanya na kuidhinisha taarifa za uthamini wa fidia wa mali 40,000. Hadi Aprili, 2014 Wizara iliidhinisha taarifa za uthamini wa mali 29,898 kwa ajili ya kulipa fidia (Jedwali Na. 5B). Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itawezesha uthamini wa mali 30,000.

Viwango vya Thamani
31.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na zoezi la kuhakikisha uwepo wa viwango sahihi vya soko kwa ajili ya ukadiriaji thamani ya ardhi na mazao. Katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara ilipanga kuendelea kufanya uchambuzi wa takwimu za bei ya soko kwa lengo la kuhuisha viwango vya thamani sambamba na kuweka utaratibu endelevu wa kuhuisha viwango hivyo. Hadi Aprili 2014, Wizara imehuisha viwango vya thamani vya mazao mbalimbali katika Wilaya za mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Kigoma kwa kushirikiana na Halmashauri za Mikoa hiyo.  Aidha, Wizara imehuisha viwango vya thamani ya ardhi katika eneo la Makongo Juu Wilaya ya Kinondoni na Kata tatu (3) za Wilaya ya Temeke (maeneo ya Kimbiji, Pemba Mnazi na Kisarawe II).

Pia, Wathamini wa Halmashauri zote nchini wamepatiwa Mafunzo na Miongozo ya utaratibu wa kufanya uchambuzi wa takwimu za bei ya soko na kuweka viwango vya thamani ya ardhi na majengo. Lengo ni kuhakikisha mfumo endelevu wa uhuishaji viwango vya thamani kadri ya mabadiliko ya bei ya soko. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara imepanga kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya uwekaji na uhuishaji viwango vya thamani ya ardhi, majengo na mazao. Nawaagiza Wataalam wa uthamini nchini kushiriki kikamilifu kuhuisha viwango vya thamani ili viendane na mabadiliko katika soko la mali kwenye maeneo yao.

32.             Mheshimiwa Spika, Wizara ikiwa ni msimamizi wa taaluma ya uthamini imeandaa miongozo mbalimbali ya kuwajengea uwezo na weledi Wathamini wa kumudu majukumu yao kwa mujibu wa taratibu za kisheria na kitaaluma. Miongozo hiyo ni pamoja na; Mwongozo wa Utaratibu wa Uthamini wa Fidia; Mwongozo wa Uchambuzi na uwekaji viwango vya thamani ya soko la ardhi, majengo na mazao; na, miongozo ya ukadiriaji malipo ya premium wakati wa kumilikisha ardhi, kodi ya pango la ardhi na gharama za kuhamisha makaburi pale ardhi husika inapotwaliwa kwa manufaa ya umma. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itasambaza miongozo hiyo kwa wataalam na wadau wa uthamini nchini. Hivyo, nawaagiza wataalam na wadau wa uthamini kuzingatia yaliyomo kwenye miongozo hiyo ili iwawezeshe kutimiza wajibu wao na kuleta tija kwa umma kiuchumi na kijamii. Ninawataka wathamini kutambua kwamba baadhi yao wamekuwa chanzo cha migogoro kwa kujihusisha na vitendo visivyofaa kama kudai rushwa na hongo badala ya kuthamini mali za wananchi kwa ukweli na haki. Aidha, kumekuwa na migogoro mingi baada ya shughuli za uthamini ikiwa ni pamoja na uthamini hewa. Wizara tayari imeweka mikakati ya kuziba mianya hiyo kwa kutumia upimaji wa kielektroniki wa kila kipande cha ardhi na pia kutaka malipo ya uthamini yafanyike kupitia benki teule na hivyo kuwabana wale wanaotumia ujanja wa malipo kwa wathaminiwa hewa. Ninawaomba wananchi watupe ushirikiano katika utekelezaji wa malipo kupita benki kwa kufungua akaunti katika benki teule inapohitajika kufanya hivyo.


MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA YA WILAYA

33.             Mheshimiwa Spika, tangu Sheria ya Mahakama ya Ardhi Sura 216 ianze kutumika tarehe 1 Oktoba, 2003 jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 49 yameundwa.  Kati ya hayo Mabaraza 42 yanafanya kazi. Mabaraza haya yanasikiliza na kuamua migogoro ya ardhi na nyumba kwa lengo la kudumisha haki, usalama na amani katika jamii.

34.              Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga kununua samani na vitendea kazi pamoja na kukarabati majengo ya Mabaraza saba (7) ili yaanze kufanya kazi. Aidha, Wizara ilikusudia kuunda Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika Wilaya tano (5) za Kilindi, Mbulu, Kahama, Sengerema na Kasulu. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Wizara imekamilisha ukarabati wa majengo/ofisi za Mabaraza sita (6) pamoja na ununuzi wa samani na vitendea kazi zikiwemo seti za kompyuta. Hata hivyo, Mabaraza matano (5) hayajaundwa kutokana na hitaji kubwa la kuboresha mabaraza 49 yaliyoundwa.

35.            Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kushughulikia utatuzi wa migogoro ya ardhi na nyumba kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na iliahidi kuamua mashauri 11,000. Kuanzia Julai, 2013 yalikuwepo mashauri 18,328 na hadi kufikia Aprili, 2014 mashauri mengine 11,548 yalifunguliwa.  Katika kipindi hicho jumla ya mashauri 11,432 yaliamuliwa hivyo mashauri 18,444 yaliyobaki na yatakayofunguliwa yataendelea kushughulikiwa katika mwaka wa fedha 2014/15 (Jedwali Na. 6).

36.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 niliahidi kuendelea kufuatilia utendaji kazi wa wenyeviti ili kuhakikisha kuwa wanazingatia maadili ya kazi zao. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Wizara imeandaa Mwongozo wa maadili ya kazi ya Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya (Code of Conduct) utakaotumika kufuatilia utendaji wao wa kazi.

37.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuimarisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 49 kwa kuyapatia vitendea kazi ili kuyawezesha kutatua migogoro kwa haraka na kufikia uamuzi wa haki.  Aidha, Wizara itakarabati majengo/ofisi za Mabaraza ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.  Vilevile, Wizara itayapatia Mabaraza yaliyopo watumishi na kuendelea kuunda Mabaraza katika Wilaya zingine kwa lengo la kuharakisha utatuzi wa migogoro.


HUDUMA ZA UPIMAJI NA RAMANI

38.            Mheshimiwa spika, upimaji ardhi na utayarishaji ramani za msingi ni moja ya majukumu ya Wizara. Ramani hizo ni chanzo muhimu cha taarifa zinazohitajika katika kubuni na kutayarisha Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa sekta mbalimbali.


Utayarishaji Ramani
39.            Mheshimiwa spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga kukamilisha kujenga na kuimarisha kanzi ya taarifa za kijiografia (geodata base) katika Wilaya mpya 19 za Mikoa mipya minne (4) ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu; pamoja na kuendelea na utekelezaji wa kazi hiyo katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Mara. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa kazi ya kujenga na kuimarisha kanzi katika Wilaya zote 19 katika mikoa mipya minne (4) pamoja na mikoa ya Kagera na Mara imekamilika. Kazi hiyo inaendelea katika Mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itakamilisha kujenga na kuimarisha kanzi ya taarifa za kijiografia katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza na itaanza kazi hiyo katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Rukwa.

40.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kukamilisha kufunga mtambo mpya wa uchapaji ramani. Wizara imekamilisha ufungaji wa mtambo huo. Kuwepo kwa mtambo huo kunaiwezesha Serikali kuwa na uwezo wa kuchapa ramani zenye viwango stahiki kwa matumizi mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaandaa na kuchapa ramani za msingi za uwiano wa 1:2,500 kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam.  Aidha, Wizara itandaa ramani za kuelekeza (guide maps) katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya utalii kwenye mbuga za wanyama za Mikumi na Serengeti.



Mipaka ya Ndani ya Nchi
41.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushughulikia utatuzi wa migogoro ya mipaka ya kiutawala katika maeneo mbalimbali kwa mujibu wa Matangazo ya Serikali. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kujenga na kuimarisha taarifa za kijiografia kwa ajili ya kutafsiri Matangazo ya Serikali (GN) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Hadi Aprili, 2014 Wizara ilikamilisha kutafsiri Matangazo ya Serikali kwa Hifadhi za Taifa za Selous, Serengeti na Saadani. Aidha, alama za kudumu za mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo zimesimikwa na zinasubiri upimaji. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itafanya kazi ya upimaji wa mipaka kati ya hifadhi ya Serengeti na vijiji inavyopakana navyo pamoja na kutafsiri Matangazo ya Serikali. Aidha, Wizara itahakiki na kupima mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwa kushirikiana na TANAPA, wanavijiji na wadau wengine. Natoa rai kwa wapima wote nchini kutambua kwamba wanawajibu kuhalalisha upimaji wao kwa mujibu wa Sheria kwa kupata Baraka za Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kwa kazi zao. Migogoro imeibuka kwa upimaji holela bila kuzingatia matakwa hayo ya sheria.

Mipaka ya Kimataifa
42.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina jukumu la kuweka na kutunza alama za mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kuimarisha alama za mipaka saba ya kimataifa kati ya Tanzania na nchi za Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Uganda na Kenya. Hadi Aprili 2014, uwekaji wa alama za mpaka wa eneo la kilomita 51 za nchi kavu kati ya Tanzania na Msumbiji umekamilika. Mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika ziwa Nyasa mazungumzo yanaendelea. Vilevile, uwekaji wa alama 78 za mpaka kati ya Tanzania na Zambia umefanyika katika eneo la Tunduma/Nakonde lenye urefu wa kilomita 46. Uwekaji wa alama 70 za mpaka kati ya Tanzania na Kenya umefanyika katika eneo la Sirari lenye urefu wa kilomita 14.8. Uwekaji wa alama za mpaka kati ya Tanzania na Burundi umeanza katika Wilaya ya Ngara. Hadi Aprili 2014 alama 143 zimesimikwa na kupimwa. Mazungumzo ya upimaji wa mpaka kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamefanyika kwa nia ya kuanza upimaji.

43.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara yangu itaendelea na kazi ya upimaji wa mipaka kati ya Tanzania na nchi za Kenya, Burundi, Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja na kuandaa kanzi ya mipaka hiyo. Aidha, kuhusu mpaka kati ya Tanzania na Uganda, Wizara inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Uganda ili kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizoanza kufanyika katika mwaka wa fedha 2001/02.

Upimaji wa Mipaka ya Vijiji
44.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikiendelea na upimaji wa vijiji vinavyoendelea kuzaliwa katika Halmashauri mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kupima mipaka ya vijiji 100 katika wilaya za Songea, Tunduru, Nyasa, Namtumbo na Mbinga. Hadi Aprili 2014, Wizara imekamilisha upimaji wa vijiji 145 katika Wilaya za Nyasa (29), Mbinga (68), Wanging’ombe (22) na Bagamoyo (26).

Upimaji wa Viwanja na Mashamba
45.            Mheshimiwa Spika,  katika  mwaka  wa fedha 2013/14 Wizara  yangu  iliweka  lengo  la   kuidhinisha  ramani zenye  viwanja  60,000 na mashamba  1,000. Hadi  Aprili 2014, Wizara  imeratibu na  kuidhinisha ramani za upimaji  zenye  viwanja  67,237  na  mashamba  325  (Jedwali  Na. 7A). Katika mwaka wa fedha 2014/15  Wizara  imepanga   kuratibu  na kuidhinisha  ramani  za upimaji  zenye  viwanja  70,000  na mashamba  500.

46.            Mheshimiwa  Spika, ili kurahisisha   upimaji  wa ardhi na kupunguza  gharama  za upimaji  kwa wananchi,   Wizara katika mwaka  wa fedha 2013/14  iliahidi kusimika  na kupima  alama za msingi za upimaji  (control points) 300 katika   miji 50. Hadi Aprili, 2014 Wizara imeweza kusimika na kupima alama 104 katika miji saba (7) ya Sikonge (15), Kigoma Ujiji (20), Mbogwe (10), Karumwa (10) Katoro (5), Uvinza (20) na Bagamoyo (24). Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea kukamilisha usimikaji wa alama 240 zilizosalia katika miji hiyo (Jedwali Na. 7B).

47.            Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa huduma ya upimaji ardhi inasogezwa karibu zaidi na wananchi, Wizara yangu iliahidi kugatua Mamlaka ya kusimamia kazi za upimaji ardhi katika Kanda. Hadi Aprili, 2014 Wizara imefanya maandalizi ya kuhamishia huduma za upimaji na ramani katika ofisi za kanda sita zilizopo Tabora, Mwanza, Dodoma, Moshi, Mbeya na Mtwara. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaanza kutoa huduma za Upimaji Ardhi katika Kanda hizo.

48.            Mheshimiwa Spika, katika mkakati wa kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za Upimaji Ardhi, Wizara inaendelea na kazi ya kuzibadili kumbukumbu zilizopo kwenda katika mfumo wa kanzi ya kie-lektroniki (Digital Cadastral Database) ili ziweze kuunganishwa na mfumo unganishi wa kutunza kumbukumbu za ardhi (Integrated Land Management Information System – ILMIS). Ili kurahisisha  upatikanaji wa taarifa za upimaji ardhi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Wizara imebadilisha kumbukumbu za ramani 5,000 za Jiji la Dar Es Salaam na kuziweka katika ramani unganishi (Cadastral Index Map). Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaandaa kanzi ya viwanja katika miji mbalimbali nchini na kutayarisha vipengele (Modules) vitatu vya Mfumo wa Utunzaji Kumbukumbu za Upimaji Ardhi (Survey Registration System – SRS) ili kuboresha utoaji wa huduma za Upimaji Ardhi nchini.

Upimaji wa Ardhi Chini ya Maji
49.            Mheshimiwa Spika, jukumu mojawapo la Wizara ni upimaji wa ardhi chini ya maji na kutayarisha ramani zinazoonesha umbile la ardhi chini ya maji hususan milima, mabonde, miinuko na kina cha maji. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga kununua kifaa cha upimaji ardhi chini ya maji kijulikanacho kama echo sounder ili kuwezesha kazi ya upimaji vina vifupi iweze kufanyika. Kifaa hicho kimenunuliwa.

Mfuko wa Kupima Viwanja
50.             Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kusimamia   Mfuko wa Mzunguko wa Kupima Viwanja (Plot Development Revolving Fund – PDRF) ambao huzipatia mikopo Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kulipa fidia, kupima viwanja na kuvimilikisha kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kuongeza juhudi za ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo pamoja na Halmashauri sugu kukatwa madeni ya mikopo hiyo kutoka katika marejesho ya asilimia 30 ya fedha ambazo Halmashauri hurejeshewa baada ya makusanyo yake. Hadi Aprili, 2014 madeni kwa Halmashuri mbalimbali yamepungua kutoka Shilingi milioni 633.6 hadi kufikia Shilingi milioni 325.5 (Jedwali Na. 7C). Nahimiza Halmashauri zinazodaiwa kulipa madeni haya ili fedha hizi zikopeshwe katika Halmashauri zingine.

51.            Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhimiza Halmashauri kurejesha fedha zilizokopeshwa kutoka kwenye mradi wa viwanja 20,000. Hadi Aprili 2014, Halmashauri nne (4) zilizokopa fedha kutoka kwenye mradi huo zilirejesha sehemu ya mikopo yao na kufanya deni hilo kupungua kutoka shilingi bilioni 1.87 hadi kufikia Shilingi milioni 780.39 (Jedwali Na. 7D). Wizara itaendelea kufuatilia Halmashauri ambazo zinadaiwa ili ziweze kurejesha fedha hizo.


MIPANGOMIJI NA VIJIJI

52.            Mheshimiwa Spika, mojawapo ya majukumu ya msingi ya Wizara yangu ni usimamizi wa uendelezaji na udhibiti wa ukuaji wa miji na vijiji nchini. Jukumu ambalo hutekelezwa kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa kuhusiana na masuala ya uendelezaji miji na vijiji nchini.

53.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha muongo mmoja tumeshuhudia ongezeko la watu na kasi ya ukuaji wa miji na vijiji hapa nchini. Ongezeko hili linajidhihirisha katika takwimu za sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Wakazi wa mijini waliongezeka kutoka milioni 7.9 sawa na asilimia 23.1 mwaka 2002 hadi kufikia watu milioni 12.7 sawa na asilimia 29.1 mwaka 2012. Ongezeko hili limekuwa changamoto kubwa kwa Mamlaka za Upangaji miji kushindwa kutoa huduma za kiuchumi na kijamii kwa kiwango stahiki na kufanya miji yetu kukua kiholela. Suala la ukuaji wa miji endelevu ni kichocheo cha maendeleo hivyo tunahitaji kuwekeza katika ustawi wa miji kwa kizazi cha sasa na kijacho kwa kupanga na kusimamia uendelezaji wa miji hapa nchini.

Uandaaji na utekelezaji wa Mipango ya Jumla ya Uendelezaji Miji
54.            Mheshimiwa Spika, katika kupanga miji, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za miji nchini huandaa Mipango ya Jumla kwa ajili ya kusimamia uendelezaji na udhibiti wa ukuaji wa miji hiyo. Mipango hiyo iko ya aina mbili:  Mipango Kabambe ambayo hutoa mwongozo wa uendelezaji miji kwa muda mrefu wa miaka ishirini na Mipango ya Muda wa Kati ya Matumizi ya Ardhi ambayo hutoa mwongozo wa uendelezaji miji kwa muda wa miaka kumi. Kazi ya uaandaaji wa Mipango hiyo hufanyika kwa kutumia dhana shirikishi ambapo Mamlaka zote za Upangaji zinazohusika na mchakato huo hujengewa uwezo.

55.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ziliendelea kukamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa jiji la Dar es Salaam ambapo rasimu ya mwisho iliwasilishwa kwa wadau na Mtaalam Mwelekezi anaendelea kuiboresha kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji Mdogo wa Bagamoyo imekamilisha maandalizi ya Rasimu ya awali ya Mpango Kabambe wa mji huo. Pia, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ilikamilisha maandalizi ya Rasimu ya Mpango wa Muda wa Kati wa Matumizi ya Ardhi wa Mji wa Kilindoni. Rasimu za mipango hiyo ziliwasilishwa kwa wadau wa Halmashauri husika kwa ajili ya kuzitolea maoni. Wizara inaendelea kushirikiana na Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga na Mji wa Bariadi kuandaa Mipango Kabambe ya miji hiyo.

56.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Wilaya ya Mafia, Mji Mdogo wa Bagamoyo na Bariadi itakamilisha kuandaa Mipango ya Jumla ya miji hiyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha na Halmashauri za Arusha na Meru itaanza maandalizi ya Mipango Kabambe ya Jiji hilo na viunga vyake kwa kutumia Mtaalam Mwelekezi. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa za Lindi na Mtwara zitaanza maandalizi ya Mipango Kabambe ya Miji hiyo. Natoa wito kwa Halmashauri zote nchini ambazo hazina Mipango ya Jumla kutenga fedha za kuandaa mipango hiyo.

Uandaaji na Utekelezaji wa Mipango ya Kina ya Uendelezaji Miji
57.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea na utekelezaji wa hatua ya awali ya uandaaji wa Mpango wa Uendelezaji upya eneo la Manzese. Uhamasishaji wa wadau katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mtaa pamoja na ukusanyaji wa taarifa na takwimu za hali halisi ya eneo hilo umefanyika. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Njombe imekamilisha maandalizi ya Rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Upya Eneo la Kati la Mji huo. Pia, Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni imeanza zoezi la kuhuisha Mpango wa Kina wa Makongo kwa kutumia dhana ya kuendeleza eneo na kudai tozo ya maboresho (betterment fee). Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi hili itahusisha upimaji wa barabara kuu.

58.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni itaendelea na kazi ya kuchambua takwimu na kuandaa rasimu ya awali ya Mpango wa Uendelezaji Upya Eneo la Manzese. Wizara itaendelea na utekelezaji wa kuboresha Mpango wa Kina wa Makongo; zoezi ambalo litahusisha upimaji wa barabara za ndani (access roads) pamoja na kupima viwanja ndani ya eneo la Mpango. Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itawezesha uboreshaji wa eneo la Mbweni JKT kwa kuweka miundombinu stahiki. Aidha, Wizara itaendelea na utekelezaji wa jukumu lake la kukagua, kuidhinisha na kuhifadhi michoro ya Mipangomiji 500 ya maeneo yaliyopangwa. Vilevile, Wizara itaandaa miongozo ya namna ya kupanga matumizi ya ardhi katika miji midogo nchini.

Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni
59.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kuendeleza Mji wa Kigamboni; kuingia mkataba na makampuni mawili ya kujenga nyumba, kufanya uthamini wa mali na kulipa fidia kwa wananchi ili kupisha utekelezaji wa mradi na kujenga uwezo wa Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu haikuweza kutekeleza kazi hizo kama ilivyoahidi kutokana na ukosefu wa fedha. Hata hivyo, Wizara yangu imekamilisha uandaaji wa rasimu ya muundo wa Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni na kuanzisha ofisi yake katika eneo la mradi. Kulitokea ucheleweshwaji katika kumteua Mtaalamu wa Fedha (Transaction Adviser and Fund Raiser) kwa sababu ya kukidhi matakwa ya sheria ya manunuzi. Hatimaye mwezi Machi, 2014 mtaalam aliteuliwa na sasa ameanza kazi yake. Jambo hili linatarajiwa kuongeza kasi katika kupata fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi.

60.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara yangu itakamilisha Mpango wa Mji Mpya wa Kigamboni kwa kufanya mkutano wa wadau (public hearing) ili uweze kuidhinishwa; Kuandaa mipango ya kina ya maeneo yaliyopo ndani ya Mpango Kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni; Kuainisha, kulipa fidia na kupima maeneo ya miundombinu na umma katika eneo la mradi na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kabambe kupitia Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya Kigamboni kwa kushirikiana na wananchi.

61.            Mheshimiwa Spika, ninatoa rai tena kwa wananchi wa Kigamboni kuwa na imani na mradi huu. Ninawashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao na kutambua azma ya Serikali kujenga Mji Mpya wenye viwango. Jambo hili ni gumu na linachukua mda lakini hatua iliyofikiwa si haba kwa zoezi lenyewe. Niondoe wasiwasi kwa wale ambao wanadhani kwamba kazi hii imeshindikana kwa hiyo tuondokane nayo.  Mradi huu umetajwa kwa jina katika Ibara ya 60(b)(iv) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 ambayo inaahidi “Kuanzisha Mji Mpya wa Kisasa  wa Kigamboni (Kigamboni New City)”. Hii pekee ni ishara tosha kuonesha wajibu wa Serikali katika kutoa kipaumbele kutekeleza kazi hii.

62.            Mheshimiwa Spika, kazi ya kuanzisha mji ilianza kwa Serikali kuunda chombo cha Kigamboni Development Agency - (KDA) ambao ni Wakala wa Kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni. Tayari Makao Makuu ya Wakala huo yamefunguliwa huko Kigamboni ambayo ni hatua kubwa na muhimu katika utekelezaji wa mradi huu. Miaka 50 baada ya Uhuru, KDA ni Wakala wa pili kuundwa baada ya CDA ambayo inajenga Makao Makuu yetu hapa Dodoma. Nirudie tena kwamba ili kulinda maslahi ya wananchi, viwango vya fidia vilivyopangwa ni endelevu na wakati ukifika umahiri na umuhimu wake utaonekana. Ninahimiza wananchi wa Kigamboni kuendelea kuwa wavumilivu na kutokubali kurubuniwa kwa kuuza maeneo yao kwa wajanja ambao, baada ya viwango vya fidia kutajwa,  wamejitokeza wakitaka kununua ardhi za wananchi kwa bei poa ili wao baadaye wafidiwe na KDA. Itambuliwe kuwa viwango vya fidia katika Awamu ya Kwanza ya Mradi ni shilingi 35,000 kwa mita mraba sawa na shilingi 141,645,000 kwa ekari moja. Hiki ni kiwango kwa mujibu wa sheria kulingana na soko na thamani ya ardhi itakavyokuwa katika mji mpya.

63.            Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kigamboni watambue Mamlaka ya Upangaji Mji wao ni KDA na wasikubali na kuyumbishwa na wanaotaka kupima maeneo ya wananchi kabla ya fidia stahiki kulipwa. Pia nifafanue kwamba wananchi wa Kigamboni wataendelea kubaki Kigamboni katika makazi yatakayojengwa huko Uvumba- kata ya Kibada (Resettlement City). Wananchi watawezeshwa kutumia sehemu isiyopungua asilimia kumi ya fidia yao kununua hisa za KDA hivyo kuendelea kufaidi matunda ya mji mpya wa Kigamboni kwa sasa na vizazi vijavyo. Hii ndiyo njia ya kisasa kwa mwananchi kubaki kwenye ardhi yake katika soko huria wakati mji mpya wenye viwango unajengwa.

64.            Mheshimwa Spika, katika fani yoyote na kazi yoyote, hakuna viwango bila weledi na nidhamu kwa hiyo hali hii inataka pia uzalendo. Ninafurahi kuwatangazia kuwa Serikali imeomba msaada wa wataalam kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Jopo la wataalam wa Mipango Miji kutoka China litawasili Juni, 2014 ili kushirikiana na wataalam wetu katika Upangaji wa Mji Mpya wa Kigamboni, Miji ya Lindi na Mtwara. Wizara ina imani kuwa utaratibu wa kupata fedha za kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni ukikamilika mambo mengi ya mwanzo (teething problems) yatapungua na kasi utekelezaji wa mji huo itaongezeka.

Urasimishaji Makazi Holela
65.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilishirikiana na Halmashauri ya jiji la Mwanza kurasimisha makazi holela. Hadi Aprili 2014, jumla ya makazi 3,008 yalirasimishwa na jumla ya viwanja 2,308 vimepimwa na Hati miliki za muda mrefu 911 zimetolewa katika Jiji la Mwanza. Aidha, elimu ya urasimishaji na mikakati ya kuzuia makazi holela mijini imetolewa kwa wataalam wa Halmashauri 25 katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Iringa, Mbeya na Rukwa. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia Programme ya Taifa ya kurasimisha na Kuzuia Makazi Holela kwa kutoa elimu ya urasimishaji na mikakati ya kuzuia makazi holela mijini kwa wataalam wa Halmashauri katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Usimamizi na Udhibiti wa Uendelezaji wa Miji
66.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa elimu na kusambaza nakala za Sheria ya Mipangomiji Na.8 ya mwaka 2007 kwa wadau mbalimbali. Elimu ya Sheria hiyo imetolewa kwa wataalamu wa sekta ya ardhi katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma, Katavi, Singida na Dodoma. Lengo ni kuwajengea uwezo wataalamu wa Mipangomiji katika kutekeleza majukumu yao. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaendelea kutoa elimu ya Sheria hiyo na marekebisho yake kwa wataalam katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Usimamizi na Udhibiti wa Uendelezaji wa Vijiji
67.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilitoa elimu ya Mwongozo wa kupanga makazi ya vijiji kwa wataalam na wadau katika mikoa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Iringa, Njombe, Rukwa na Mbeya) ili kwenda sambamba na Programu ya Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT). Vilevile, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na Mvomero zilijengewa uwezo wa kuandaa Mipango ya Makazi ya Vijiji vinne (4) vya Fukayosi na Kidomole Wilayani Bagamoyo; Lukenge na Hembeti Wilayani Mvomero.

68.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Upangaji zikiwemo Halmashauri za Wilaya na Vijiji ili kuziwezesha kuandaa Mipango ya Kina ya Makazi ya Vijiji kwa ajili ya vitovu vya huduma vya vijiji 10 vinavyokua kwa kasi. Vilevile, Wizara itaandaa na kutunza Mfumo wa Kitaifa wa kumbukumbu za vijiji; itaendelea kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya uendelezaji makazi vijijini katika wilaya zenye Mipango hiyo zikiwemo wilaya za Urambo, Manyoni, Bariadi na Babati. Aidha, elimu ya mwongozo wa uandaaji wa mipango ya makazi ya vijiji itatolewa na miongozo hiyo kusambazwa katika mikoa iliyopo katika Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu. Natoa rai kwa Halmashauri za Wilaya zote nchini, hasa katika maeneo ambapo elimu hii imetolewa; wasimamie na kuwezesha upangaji wa makazi ya vijiji vyao, ili kuwezesha vijiji hivyo kuwa na makazi yaliyopangwa na kuwa na maeneo ya huduma za jamii.


MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI

Mpango wa Taifa wa Matumizi ya ardhi
69.             Mheshimiwa Spika,  umuhimu wa ardhi ni wa kipekee. Nikimnukuu R. S. Simpson kwenye kitabu chake cha Land Law and Registration, 1976 alisema:-
“ardhi ni chanzo cha utajiri wote. Kutokana na ardhi tunapata kila kitu tutumiacho chenye thamani iwe chakula, mavazi, nishati, makazi, vyuma au vito. Matumizi yote ya thamani yanatokana na ardhi yawe chakula, nguo, mafuta ya kuendeshea mitambo, hifadhi, chuma au mawe ya thamani (vito). Tunaishi juu ya ardhi na kutokana na ardhi na maiti au majivu yetu hurudi ardhini tunapokufa. Uwepo wa ardhi ni ufunguo wa uhai wa binadamu na mgawanyo na matumizi yake ni muhimu sana”.

70.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Serikali ilipitisha Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi. Madhumuni ya Mpango huo ni kuweka utaratibu wa kuongoza matumizi ya rasilimali za ardhi yenye usawa kwa ajili ya kuboresha maisha ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na kijamii na uendelevu wa rasilimali za kimazingira nchini; na hivyo, kuchangia katika jitihada za serikali katika utekelezaji wa MKUKUTA. Hivi sasa marekebisho ya mwisho pamoja na kuhuisha takwimu vipo katika hatua za mwisho ili uchapishwe na kusambazwa kwa wadau. Utekelezaji wa programu za kipaumbele (Kilimo, Mifugo, Maji, Makazi, Mipango ya Matumizi ya Ardhi) utaanza katika mwaka wa fedha 2014/15 kwa ushirikiano na wadau. 

71.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kutoa mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Wilaya kuhusu sheria za ardhi na mbinu shirikishi za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya za Newala, Tarime, Rorya na Maswa kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya. Hadi Aprili, 2014 Viongozi na watendaji wa Wilaya za Tarime, Rorya, Newala na Geita wamepewa mafunzo juu ya maudhui ya sheria za ardhi na sheria ya upangaji matumizi ya ardhi. Aidha, kazi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya hizo inaendelea. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itakamilisha kazi ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya za Tarime, Rorya, Newala na Geita pamoja na  kutoa mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Wilaya nne  kuhusu sheria za ardhi na mbinu shirikishi za uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya husika.

72.              Mheshimiwa Spika,  katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliahidi kukamilisha uandaaji na uchapaji wa Kanuni za Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 2007 na  kuchapisha na kusambaza toleo la pili la Mwongozo wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji. Wizara imekamilisha uandaaji wa Kanuni za Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007. Pia, Mwongozo wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi umechapishwa na kusambazwa kwa wadau. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itachapisha kanuni hizo na kuzisambaza kwa wadau na itatafsiri Mwongozo wa Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji katika lugha ya Kiswahili.

Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji
73.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliahidi kushirikiana na wadau kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 150 katika wilaya mbalimbali hususan za mipakani mwa nchi na zile zenye migogoro sugu  ya ardhi. Aidha, Wizara ilipanga kutekeleza mradi wa SAGCOT kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ili kutenga maeneo yanayotosheleza mahitaji ya matumizi ya ardhi ya wananchi, kutenga maeneo ya vyanzo vya maji na ardhi inayofaa kwa uwekezaji. Hadi Aprili, 2014 jumla ya vijiji 94 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya mbalimbali (Jedwali Na. 8). Pia, kazi ya kutekeleza mradi wa SAGCOT imeanza kwa Mkandarasi kupitia Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika ukanda wa Reli ya Uhuru. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itawezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 200 pamoja na kuendelea na uandaaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi ya vijiji na wilaya katika ukanda wa SAGCOT na kutenga maeneo ya uwekezaji.

MAENDELEO YA NYUMBA

74.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kusimamia Sekta ya Nyumba ili kuwezesha upatikanaji wa nyumba na kuona kuwa sekta hii inachangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara itaendelea kuweka sera na mikakati ya utekelezaji itakayowezesha wananchi kumiliki au kuwa na nyumba bora za gharama nafuu.

75.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara yangu iliahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha na Benki Kuu katika kuweka mifumo ya kifedha itakayowezesha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa mkataba wa mkopo wa Tanzania Housing Finance umerejewa upya ili kuipata kampuni ya Tanzania Mortgage Refinancing Company iliyowezeshwa kutoa mikopo ya nyumba au mtaji kwa benki za biashara ili nazo zitoe huduma ya mikopo ya nyumba kwa wananchi hata kama benki hizo hazijaanza kutoa mikopo kwa wananchi wanaonunua nyumba (Pre-financing). Hadi Aprili, 2014 jumla ya benki 19 zilikuwa zinatoa mikopo ya nyumba kwa miaka 15-20, tofauti na benki 10 zilizokuwa zinatoa mikopo ya nyumba kwa kipindi kisichozidi miaka 15.

76.            Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara yangu itatoa elimu kwa umma kuhusu utaratibu wa mikopo ya nyumba, ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wa mkopaji na mkopeshaji kwa mujibu wa sheria. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kuweka utaratibu utakaowezesha mikopo ya nyumba kutolewa kwa masharti nafuu kuliko mikopo ya kibiashara. Wizara itashirikiana na vyombo vya fedha kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya nyumba ikiwa ni pamoja na kuvutia waendelezaji milki binafsi ili wajenge nyumba za gharama nafuu za kuuza na kupangisha.

77.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara yangu iliendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania kukamilisha uundwaji wa Mfuko wa Mikopo Midogomidogo ya Nyumba. Mfuko huo umeanza kwa mtaji wa Dola za Marekani milioni 3 ambazo ni sehemu ya mkopo uliotolewa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa kuendeleza sekta ya nyumba hapa nchini (Tanzania Housing Finance Project). Aidha, Serikali iliendeleza mazungumzo na Benki ya Dunia kwa lengo la kupata fedha zaidi kwa ajili ya Mfuko huo. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itatoa elimu kwa umma kuhusu mfuko huo na kuwahamasisha kutumia huduma zake.

78.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara iliahidi kuandaa Sheria ya kusimamia Sekta ya Nyumba ikiwa ni pamoja na kuweka masharti ya uendelezaji nyumba, kuelekeza haki na wajibu wa waendelezaji nyumba, wanunuzi, wamiliki na wapangaji wa nyumba. Kazi hiyo itaendelea katika mwaka wa fedha 2014/15. 

79.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara iliahidi kuwa mpango wa nyumba kwa watumishi wa umma ungeanza kutekelezwa. Katika kuwezesha utekelezaji wa mpango huo Wizara ilizielekeza Halmashauri zote kutenga ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba kwa watumishi wa umma. Aidha, Watumishi Housing Company (WHC) iliyoundwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Shirika la Nyumba la Taifa itasimamia utekelezaji wa mpango huo. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara itaendelea kuwezesha utekelezaji wa mpango huo ikiwa ni pamoja na kuunda Mfuko wa Dhamana ya Mikopo ya Nyumba kwa Watumishi wa Umma.

Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba na Vifaa vya Ujenzi
80.               Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba  na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) una majukumu ya kutafiti, kukuza, kuhamasisha na kusambaza matokeo ya utafiti na utaalamu wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini.

81.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara kupitia Wakala imeendesha Semina na mafunzo kwa vitendo ambapo jumla ya washiriki 974 kutoka katika  Wilaya za Sikonge (100), Biharamulo (56), Halmashauri ya Arusha (160) na Muleba (550). Aidha, mafunzo kwa vitendo yalitolewa kwa wakufunzi na wahitimu wa VETA (47), Tarime (42), Korogwe (15) na Mafundi sanifu (4) kutoka Manispaa ya Tabora. Vilevile, jumla ya mashine 250 za kufyatulia tofali zilizalishwa. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wakala utaendelea kuhamasisha na kueneza teknolojia ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika Wilaya za Nkasi, Kishapu, Chunya na Tandahimba.

82.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara iliahidi kushirikiana na Halmashauri za Miji na Wilaya kuimarisha vikundi vya ujenzi wa nyumba vilivyoanzishwa na kutangaza huduma zinazotolewa kupitia vyombo vya habari. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Wakala umeendelea kujitangaza kupitia vyombo vya habari. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wakala utaendelea kujitangaza kupitia vyombo vya habari na kushiriki maonesho mbalimbali ya kitaifa ili kusambaza huduma kwa wananchi wengi zaidi.


SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA

Kuimarisha Utendaji Kazi wa Shirika
83.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara iliendelea kusimamia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika utekelezaji wa malengo ya Mpango Mkakati wake wa kipindi cha  mwaka 2010/11-2014/15 ikiwa ni pamoja na kuimarisha utendaji kazi. Shirika limeendelea kuboresha utendaji kazi wake kwa kuajiri wataalamu wa fani mbalimbali wapatao 31 kwa ajili ya kuongeza ufanisi na tija. Ajira hizi zimepandisha uwiano wa wafanyakazi wenye taaluma na wasiokuwa na taaluma kufikia asilimia 51 kwa 49 dhidi ya lengo la asilimia 70 kwa 30 ifikapo Juni, 2015.  Pia, watumishi wa ngazi zote walipatiwa mafunzo ya utambuzi na ulezi wa vipaji pamoja na ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi (public – private partnership).

84.            Mheshimiwa Spika, Wizara iko kwenye mchakato wa kurekebisha Sheria Na. 2 ya Shirika la Nyumba la Taifa ya mwaka 1990 iliyoliunda upya shirika hilo. Lengo la marekebisho haya ni kuliwezesha shirika kufanya yafuatayo:- kupanua wigo wa shughuli za Shirika ili liweze  kuwa mwendelezaji milki mkuu; kuliwezesha Shirika kuendesha shughuli zake katika mazingira shindani; na, kuoanisha sheria ya Shirika na sheria zingine.

Upatikanaji wa Ardhi kwa Ajili ya Ujenzi wa Nyumba
85.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Shirika liliweka lengo la kuendelea na mchakato wa ununuzi wa ardhi katika Wilaya mbalimbali nchini. Lengo la ununuzi huu ni kuliwezesha Shirika kuwa na hazina ya ardhi (land bank) ya kutosha itakayoliwezesha kutekeleza jukumu lake jipya la kuwa mwendelezaji mkuu wa miliki. Hadi Aprili, 2014, Shirika lilifanikiwa kununua ardhi yenye ukubwa wa ekari 3,686.9 na viwanja 464 (Jedwali Na 9A).  Pia, Shirika limeendelea na mchakato wa ununuzi wa ardhi yenye ukubwa wa ekari 2,627.5 iliyoko kwenye maeneo mbalimbali nchini. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litaendelea na ununuzi wa ardhi ambao kwa sasa umefikia hatua mbalimbali.

Ujenzi wa Nyumba za Makazi na Majengo ya Biashara
86.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Shirika liliweka lengo la kuendelea kukamilisha miradi iliyokuwa ikiendelea na kuanza miradi mingine mipya. Aidha, Shirika liliweka kipaumbele kwenye ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zisizopungua 20 kwa kila mkoa. Hadi Aprili, 2014, Shirika liliendea na utekelezaji wa miradi 26   ya ujenzi wa nyumba za makazi yenye jumla ya nyumba 1,947. Miradi hii, ililiwezesha Shirika kuifikia mikoa 14 kwa kujenga nyumba za gharama nafuu 921 na nyumba za gharama ya kati na juu 978 katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Dodoma. Kati ya nyumba hizo, nyumba 697 zilikamilika ambapo 193 ni za gharama nafuu na 504 ni za gharama ya kati na juu (Jedwali Na. 9B). Shirika pia linaendelea na maandalizi ya kuanza ujenzi wa miradi 31 yenye jumla ya nyumba za gharama nafuu 1,717 na miradi 18 yenye nyumba 3,493 za gharama ya juu na kati zitakazojengwa katika mikoa 17.  Katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litaendea kukamilisha miradi inayoendea; kuanza miradi mingine mipya ya nyumba za gharama ya juu, kati na nafuu na hivyo kuifikia mikoa yote ya Tanzania Bara kwa kujenga nyumba zisizopungua 50 kwa kila mkoa. 

87.            Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa kipindi cha 2010/11 – 2014/15, Shirika linauza asilimia 70 ya nyumba za makazi zinazojengwa na kupangisha asilimia 30. Hadi Aprili, 2014, Shirika limefanikiwa kuuza nyumba 456 katika miradi yake na kupata kiasi cha shilingi bilioni 43.95 kati ya Shilingi bilioni 67.05 zinazotarajiwa wakati miradi hii itakapokamilika.

88.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Shirika lilipanga kuendelea na utekelezaji wa miradi tisa (9) ya majengo makubwa ya biashara na majengo mengine 20 yanayojengwa kwa ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi.  Hadi Aprili, 2014 Shirika liliweza kukamilisha mradi wa jengo moja la ghorofa 10 lililojengwa kwenye Kiwanja Na. 1 Barabara za Ufukoni na Ali Hassan Mwinyi, Upanga - Dar es Salaam ambalo ni makao makuu mapya ya Shirika. Vilevile, Shirika lilianza ujenzi wa majengo manne (4) ya biashara ambayo ni jengo la ghorofa tano (5) lililoko Kiwanja Na. 2 Barabara ya Old Dar es Salaam mkoani Morogoro; jengo la ghorofa moja (1) katika Mtaa wa Kitope Manispaa ya Morogoro; jengo la ghrofa tano (5) lililoko Mtaa wa Lupa Way, Manispaa ya Mbeya; na, jengo la ghorofa tatu (3) lililoko Mitaa ya Mkendo na Kusaga mjini Musoma. Aidha, Shirika kwa kushirikiana na wabia wake liliweza kukamilisha miradi ya majengo 57 na miradi mingine 27 ya biashara   ilikuwa katika hatua mbalimbali za matayarisho ya kuanza ujenzi. Vilevile, Shirika lilikamilisha miradi 16 ya ubia iliyotekelezwa kwa kushirikiana na sekta binafsi na kuendelea na ujenzi wa miradi mingine minne (4).
 
89.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litaendelea na utekelezaji wa jumla ya miradi ya majengo ya biashara 30 ikiwemo inayoendea na ile ambayo kwa sasa iko katika hatua za maandalizi pamoja na kukamilisha miradi minne (4) ya ubia.
Undelezaji wa Vituo vya Miji Midogo (Satellite Cities)
90.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Shirika limeendelea na matayarisho ya kuanza jukumu lake jipya la kuendeleza vituo vya miji midogo kama mwendelezaji miliki mkuu (master developer). Wizara ilikabidhi rasmi Shirika eneo la Luguruni lenye ekari 156.53 na eneo la Kawe lenye ekari 267.71 kwa ajili ya kuyaendeleza. Aidha, Shirika kwa niaba ya Serikali liliingia Mkataba wa makubaliano (memorandum of understanding) na kampuni ya Surbana International Consultants ya Singapore kwa ajili ya kulipanga upya eneo la Luguruni. Pamoja na juhudi hizo, Shirika pia lilikamilisha matayarisho ya mipango ya kina (detailed plans) ya kuendeleza maeneo linaloyamiki ikiwa ni pamoja na eneo la Burka/Matevesi – Arusha lenye ekari 579.2 na eneo la Usa River - Arusha lenye ekari 296 na pia kuendelea na matayarisho ya mipango hiyo kwa maeneo ya Uvumba, Kigamboni (ekari 202) na Kawe.

91.            Mheshimiwa Spika, Shirika litaanza uendelezaji wa eneo la Burka/Matevesi kwa kujenga miundombinu pamoja na nyumba za gharama nafuu 200 kabla ya Juni, 2014. Uendelezaji wa miradi hii ambao utakuwa na nyumba za makazi zisizopungua 15,000 pamoja na majengo ya biashara, utaishirikisha sekta binafsi kulingana na sera ya sasa ya Serikali ya ushirika wa sekta ya umma na sekta ya binafsi (PPP). Katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litaendelea na ukamilishaji wa mpango wa kina wa eneo la Luguruni, Kawe na Uvumba na kuendelea na  uendelezaji wa maeneo ya Usa River na Burka/Matevesi.

Utafutaji wa Mitaji kwa Ajili ya Miradi na Mikopo ya Ununuzi wa Nyumba
92.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Shirika limeendelea kutafuta mitaji kwa ajili utekelezaji wa miradi ya ujenzi. Hadi Aprili, 2014 Shirika limefanikiwa kuingia mikataba ya mikopo ya kiasi cha Shilingi bilioni 210 na kuweza kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 124.  Aidha, Shirika limeendelea na juhudi za kuwahamasisha wanunuzi wa nyumba zake kutumia fursa za mikopo inayotolewa na benki za Azania Bank, Bank of Africa, CRDB - Bank, Exim Bank, KCB, NBC, Commercial Bank of Africa, NMB na Stanbic zilizoingia makubaliano ya kutoa mikopo ya ununuzi wa nyumba. Hadi Aprili, 2014, wanunuzi wapatao 89 waliweza kupata mikopo ya nyumba yenye jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni 12.2 na wengine wanaendelea na mchakato wa kupata mikopo hiyo. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Wizara kupitia Shirika itaendelea na juhudi za kupata mikopo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara pamoja na  kuwahamasisha wananchi kuchukua mikopo kwa ajili ya ununuzi wa nyumba zinazojengwa na Shirika au wanazoweza kujenga wenyewe.


Mapato ya Shirika
93.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Shirika lilitarajia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 68.2 kutokana na kodi za pango la nyumba zake na hivyo kuendelea kuchangia mapato ya Serikali kwa kulipa kodi mbalimbali. Hadi Aprili, 2014, mapato ya shirika yalifikia Shilingi bilioni 55.63 sawa na asilimia 98 ya lengo la kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014 (Jedwali Na. 9C). Mafanikio haya yalitokana na juhudi za ukusanyaji wa kodi za pango pamoja na malimbikizo ya madeni. Mapato hayo yaliliwezesha Shirika kuchangia mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shilingi bilioni 10.02 kupitia kodi mbalimbali kama vile kodi ya pango la ardhi, kodi ya ongezeko la thamani, kodi ya majengo, kodi ya mapato, ushuru wa huduma za Halmashauri za Miji na Manispaa, kodi za mapato ya wafanyakazi, ushuru wa maendeleo ya taaluma na mchango wa pato ghafi kwa Serikali Jedwali Na.9D.  Kwa mwaka 2014/15 Shirika linategemea kuingiza kiasi cha Shilingi bilioni 70.1 kutokana na kodi za pango la nyumba na hivyo kuendelea kuchangia mapato ya Serikali.

Matengenezo ya Nyumba na Majengo
94.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Shirika lilipanga kutumia jumla ya Shilingi bilioni 9.0 kwa ajili ya matengenezo makubwa ya nyumba na majengo yake. Hadi Aprili, 2014 Shirika lilitumia kiasi cha Shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya matengenezo ya nyumba zipatazo 3,500. Katika mwaka wa fedha 2014/15, Shirika litatenga kiasi cha Shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa nyumba na majengo ya yake.


HUDUMA ZA KISHERIA

95.            Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huduma mbalimbali za kisheria zimeendelea kutolewa na wizara. Huduma hizo zinajumuisha kutunga sheria mpya, kuhuisha sheria na kusimamia mashauri yanayohusu Wizara.

96.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara yangu iliahidi kuhuisha Sheria ya Ardhi, Sura 113; Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114; Sheria ya Mahakama za Ardhi, Sura 216 na Sheria ya Wapima Ardhi, Sura 324. Napenda kuliarifu bunge lako tukufu kuwa kazi ya  kukusanya maoni  ya wadau ili kuhuisha Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji na Sheria ya Mahakama za Ardhi imekamilika na mapendekezo yatawasilishwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua stahiki. Aidha, mchakato wa kuhuisha Sheria ya Wapima Ardhi utaendelea katika mwaka wa fedha 2014/15.

97.            Mheshimiwa Spika, katika  mwaka wa fedha 2013/14 Wizara ilipanga kuanza mchakato wa kutunga upya Sheria ya Utwaaji Ardhi. Kazi hii inaendelea na inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2014/15. Baada ya mchakato wa kutunga sheria hizo kukamilika,   miswaada husika itawasilishwa katika Bunge lako tukufu. Aidha, Wizara yangu itaendelea na utaratibu wa kuzihuisha sheria mbalimbali za utawala wa ardhi kila mara inapolazimu ili kuzifanya ziendane na wakati na kukidhi makusudio ya kutungwa kwake.


MAWASILIANO SERIKALINI

98.            Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatoa elimu kwa umma kuhusu sera, sheria, kanuni na taratibu zinazo simamia Sekta ya Ardhi nchini. Katika mwaka wa fedha 2013/14 niliahidi kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa umma kwa kuanzisha mtandao rasmi wa kijamii (official ardhi blog); kuhuisha mkakati wa mawasiliano; na kuimarisha kitengo cha Mawasiliano cha Wizara. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ilianzisha mtandao rasmi wa kijamii unaopatikana kupitia anuani: www.ardhi.go.tz/blog; pia, kitengo cha Mawasiliano kilipatiwa vitendeakazi pamoja na kuongezewa rasilimali watu. Vilevile, Wizara imekamilisha mchakato wa kumpata mtaalam mwelekezi atakayehuisha Mkakati wa Mawasiliano wa Wizara.
 
99.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/14, Wizara iliendelea kutoa elimu iliyolenga kuelimisha umma kuhusu sekta ya ardhi kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Wizara kwa kutambua umuhimu huo, iliendesha semina elekezi kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini. Pia, wizara ilishiriki kwenye vipindi vinne (4) vya moja kwa moja (live programmes) vilivyorushwa kupitia runinga na redio. Pia, Wizara inakamilisha uandaaji wa vitabu vya sheria za Ardhi vitakavyosomeka kwa maandishi nundu, hii ni  moja ya jitihada za kuhakikisha wadau wote muhimu wa sekta ya ardhi (wakiwemo wenye ulemavu wa macho) wanapata elimu kuhusu Sekta ya Ardhi.

100.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itakamilisha kuhuisha mkakati wa mawasiliano wa wizara;  kuratibu mawasiliano kati ya Wizara na wadau wake; kuandaa na kurusha vipindi vya televisheni na redio; na, kuboresha mawasiliano.


HUDUMA ZA UTAWALA NA RASILIMALI WATU

101.         Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kuboresha mifumo ya   usimamizi wa   rasilimali watu na uendeshaji wa ofisi ili kuleta tija na ufanisi wa kazi. Hatua hii inajidhihirisha kutokana na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa za kuboresha mifumo ya utendaji kazi na usimamizi wa rasilimali watu. Katika mwaka wa fedha 2013/14 Wizara imeendelea kutoa mafunzo, kuboresha mazingira ya ofisi, kutoa stahili kwa watumishi zinazoendana na masharti ya ajira zao, pamoja na kudumisha utawala bora. Msisitizo umelenga katika kutumia dhana shirikishi ya kupanga, kujenga uwezo, kutekeleza, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa majukumu ili kuboresha utendaji kazi na kusimamia nidhamu na watumishi.  Vile vile Wizara inaendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuhamasisha watumishi kujikinga na kupima afya zao.

102.         Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka jana, nililifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, wizara yangu ilikuwa inaendelea kujenga kituo cha kuhudumia wateja (customer service centre). Napenda kutoa taarifa kuwa Wizara imekamilisha ujenzi wa kituo hicho, na kwamba kituo hiki kitaanza kutoa huduma katika mwaka wa fedha 2014/15. Kituo hiki kitasaidia kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na Wizara na kuleta ufanisi zaidi katika utendaji kazi wa pamoja na kuepusha mianya ya rushwa. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuboresha utaoji wa huduma kwa kusimamia mifumo ya utendaji kazi, kuboresha mazingira ya ofisi, na kutoa stahili kwa watumishi zinazoendana na masharti ya ajira zao.

103.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ya rasilimali watu katika kufanikisha malengo yaliyopangwa, Wizara imeendelea kuwawezesha watumishi kuhudhuria mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwajengea uwezo zaidi. Katika mwaka wa fedha 2013/14 jumla ya Watumishi 166 walihudhuria mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na mfupi nje na ndani ya nchi. Kati ya hao 36 walipatiwa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi; 40 walipatiwa mafunzo yaliyohusu maadili katika utumishi wa umma; na, waajiriwa wapya 90 walipatiwa mafunzo ya awali (induction course). Katika kipindi hicho watumishi 88 wa taaluma mbalimbali waliajiriwa, watumishi 13 walibadilishwa kazi baada ya kupata sifa na   watumishi 8 walithibitishwa katika vyeo vyao.

104.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara inatarajia kuwapatia mafunzo ya aina mbalimbali watumishi 250 wa kada mbalimbali. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa afya za watumishi, Wizara katika mwaka wa fedha 2013/14 ilishiriki katika mashindano ya SHIMIWI na kufanikiwa kupata tuzo mbalimbali na pia iliandaa bonanza la michezo kwa watumishi wote. Vilevile viongozi wa michezo waliwezeshwa kuhudhuria mikutano na semina mbalimbali za michezo.

105.         Mheshimiwa Spika, ili kupambana na janga la UKIMWI katika sehemu ya kazi, Wizara imeendelea kuhamasisha watumishi kupima kwa hiari afya zao kwa kutumia utaratibu wa kuwaleta Wizarani wataalam wa huduma ya ushauri nasaha. Katika mwaka wa fedha 2013/14, watumishi 720 wa makao makuu walifanyiwa semina ya uhamasishaji, na watumishi 416 walipima na kufahamu hali za afya zao. Wizara imeendelea kuwapatia watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI msaada wa dawa na lishe. Katika mwaka wa fedha 2014/15 Wizara itaendelea kuhamasisha upimaji wa afya za watumishi kwa hiari na kutoa huduma stahiki.

Vyuo vya Ardhi
106.         Mheshimiwa Spika, Wizara ina vyuo viwili vya Ardhi vilivyopo Tabora na Morogoro. Vyuo hivi vinatoa mafunzo ya stashahada katika fani za Urasimu Ramani na Upimaji Ardhi; na, Cheti katika fani za Upimaji Ardhi, Umiliki Ardhi, Uthamini, Usajili na Uchapaji Ramani. Katika mwaka wa fedha 2013/14 idadi ya wahitimu ilikuwa 250 kati yao 178 walitoka Chuo cha Ardhi Morogoro na 72 walitoka Chuo cha Ardhi Tabora (Jedwali Na. 10).  Katika mwaka wa fedha 2014/15 Chuo cha Ardhi Tabora kitaanzisha mafunzo ya stashahada katika fani ya Umiliki, Uthamini na Usajili wa ardhi ambayo itawapa wanafunzi sifa ya kujiunga na vyuo vikuu. Fani hizi ni muhimu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la wataalam wa sekta ya ardhi. Aidha, Wizara itaendelea kuviimarisha vyuo hivi ili viweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Natoa wito kwa Halmashauri kuajiri wataalamu wanaohitimu katika vyuo hivi pamoja na kuwaendeleza watumishi wao kitaaluma kupitia vyuo hivi.


CHANGAMOTO MAALUM

Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi
107.         Mheshimiwa Spika, takriban katika kazi zote tunazotekeleza changamoto na kero kubwa imeendelea kuwa ni ongezeko la migogoro ya ardhi inayoibuka sehemu mbalimbali nchini. Ninachukua nafasi hii kuwaeleza kwamba kimsingi hakuna migogoro ya ardhi bali ni “migogoro ya watumiaji wa ardhi”. Ili kuondokana na migogoro hii ni muhimu kwa watumiaji wote wa ardhi kutambua ukweli huu na kujitathmini wenyewe pindi mgogoro unapoibuka.

Kuna aina  kuu sita za migogoro ya watumiaji wa ardhi vijijini ambazo ni:-
           i.     Migogoro Kati ya Wakulima na Wafugaji;
          ii.     Migogoro Kati ya Wafugaji na Hifadhi;
         iii.     Migogoro kati ya Wanavijiji na Wamiliki wa Migodi;
         iv.     Migogoro kati ya Wanavijiji na Wamiliki wa Mashamba Makubwa (Wawekezaji);
          v.     Migogoro ya Mipaka kati  ya Vijiji na Wilaya; na
         vi.     Migogoro ya Wanavijiji na Miji Inayopanuka.
Ufafanuzi wa kina wa migogoro hiyo na namna wizara inavyoishughulikia upo kwenye Kiambatisho Na. 1.


SHUKRANI

108.         Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inashughulikia majukumu mbalimbali ambayo ni mtambuka. Ni mategemeo yangu kwamba, Bunge litaendelea kuwa na mtazamo chanya na kuipa kipaumbele sekta ya ardhi kwa ujumla ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

109.         Mheshimiwa Spika, mafanikio ya Wizara yangu yametokana na kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo zikiwemo  taasisi za fedha za kimataifa, nchi wahisani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na mashirika ya kidini.  Wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), Shirika la Maendeleo la Ujerumani; na Serikali za Denmark, Sweden, Uholanzi na Uingereza kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara.

110.         Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa George Simbachawene (Mb), kwa kunisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. Pia napenda kumshukuru Katibu Mkuu Bw. Alphayo Japani Kidata, na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Selassie David Mayunga kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Nawashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo, Makamishna Wasaidizi na Wasajili Wasaidizi wa kanda, viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara, watumishi na wataalamu wote wa sekta ya ardhi kwa kunisaidia katika kutimiza majukumu yangu kwa ufanisi. Naomba kila mmoja wetu aendelee kutekeleza majukumu yake kwa kujielekeza katika kuiwezesha ardhi kuwaondolea wananchi umaskini. Natambua kuwa Wizara yangu haina nyenzo na rasilimali za kutosha kutimiza matarajio ya Watanzania,  lakini hata kwa kutumia rasilimali chache zilizopo kwa uangalifu  tutatoa mchango mkubwa kwa Taifa.

HITIMISHO

111.         Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2014/15 Wizara imeazimia kutekeleza Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sheria za Ardhi uliohuishwa mwaka 2013 (SPILL 2013); na Mpango Mkakati wa Wizara wa miaka mitano (2012/13 - 2016/17) ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na MKUKUTA II ambayo kwa pamoja yanalenga kufikia malengo makuu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.

112.         Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo Wizara imejipanga kutayarisha mipango ya kuendeleza miji na vijiji na kuisimamia,  kupanga matumizi ya ardhi, kupima ardhi, kuhakiki milki, kusajili na kutoa hati ili kuwezesha kuwepo kwa usalama wa milki. Natoa rai kwa mamlaka na asasi mbalimbali kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha kuwa ardhi inaziwezesha sekta zote ili kufikia malengo ya maisha bora kwa kila Mtanzania.


MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15
113.         Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza kazi zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2014/15, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liidhinishe makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kama ifuatavyo:-


Mapato ya Serikali
Shilingi
61,320,005,000




°
Matumizi ya Mishahara
Shilingi
11,536,899,480
°
Matumizi Mengineyo (OC)
Shilingi
42,933,854,000
Jumla Matumizi ya
Kawaida (A)
Shilingi
54,470,753,480




°
Fedha za Ndani
Shilingi
21,000,000,000
°
Fedha za Nje
Shilingi
13,379,977,000
Jumla Matumizi ya  Miradi ya Maendeleo (B)
Shilingi
34,379,977,000

Jumla ya Matumizi ya Kawaida na Matumizi ya Miradi ya Maendeleo (A+B) ni Shilingi 88,850,730,480.
114.         Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana  kwenye tovuti ya Wizara www.ardhi.go.tz.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. 

No comments: