BAJETI YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI

HOTUBA FUPI YA WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI, MHE. DKT. TITUS MLENGEYA KAMANI (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MPANGO WA MAENDELEO NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015

1.0          UTANGULIZI


1.              Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, iliyochambua bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Wizara kwa mwaka 2013/2014 na mwelekeo wa kazi za Wizara kwa mwaka 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Mpango wa Maendeleo na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
2.            Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa Katavi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zao za kuongoza, kusimamia na kuendeleza amani, utulivu, mshikamano na uchumi wa nchi yetu. Pia, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, napenda kuwapongeza Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kushiriki katika mchakato wa kupata katiba. Tuna imani kuwa mchakato huo utatuwezesha kupata Katiba itakayofaa kwa kipindi kijacho. Aidha, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua mimi na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kaika Saning’o Ole Telele Mbunge wa Ngorongoro kuongoza Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na tunaahidi kutumia uwezo wetu katika kutekeleza majukumu tuliyopewa.

3.            Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kuteuliwa kwao na Mheshimiwa Rais katika nafasi zao mpya. Aidha, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wapya waliojiunga na Bunge lako tukufu kufuatia chaguzi ndogo zilizofanyika katika Jimbo la Chambani Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Jimbo la Kalenga Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa na Jimbo la Chalinze Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete.

4.            Mheshimiwa Spika, Wizara ilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Waheshimiwa Wabunge wenzetu; Hayati Mhe. Dkt. William Augustao Mgimwa aliyekuwa mbunge wa Kalenga na Hayati Said Ramadhani Bwanamdogo aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kutoa salaam za rambirambi kwa familia za marehemu, ndugu na wananchi wa majimbo waliokuwa wanayawakilisha. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina. Aidha, naomba nitumie fursa hii kuwakumbuka wananchi wenzetu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko, ajali na sababu mbalimbali.

5.            Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mhe. Profesa Peter Mahamudu Msolla, Mbunge wa Kilolo na Mhe.  Said Juma Nkumba, Mbunge wa Sikonge pamoja na wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa ushauri, maoni, maelekezo na ushirikiano waliotupatia katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara na maandalizi ya bajeti hii. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu itaendelea kuzingatia ushauri, mapendekezo na maoni ya Kamati na yale yatakayotolewa na Bunge lako Tukufu.

6.            Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa Katavi kwa hotuba yake nzuri yenye kutoa malengo ya Serikali na mwelekeo wa utendaji wa sekta mbalimbali pamoja na kazi za Serikali kwa mwaka 2014/2015. Aidha, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote waliotoa hotuba zao ambazo zimeainisha maeneo mbalimbali tunayoshirikiana katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi nchini. Vilevile, nawashukuru waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao kuhusu masuala ya maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi kupitia hotuba hizo.

2.0          HALI YA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI NA CHANGAMOTO ZILIZOPO


7.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013, sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2012 na kuchangia asilimia 4.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 4.6 mwaka 2012. Aidha, idadi ya mifugo nchini inakadiriwa kuwa ng’ombe milioni 22.8, mbuzi milioni 15.6 na kondoo milioni 7.0. Pia, wapo kuku wa asili milioni 35.5, kuku wa kisasa milioni 24.5 na nguruwe milioni 2.01. Viwango vya ulaji wa mazao ya mifugo kwa sasa ni wastani wa kilo 12 za nyama, lita 45 za maziwa na mayai 75 kwa mtu kwa mwaka.

8.            Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina ukanda wa pwani wa bahari wenye urefu wa kilometa 1,424 ambao umegawanyika katika eneo la Maji ya Kitaifa (Territorial Sea) lenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,000 na eneo la Bahari Kuu kilometa za mraba 223,000. Eneo la maji baridi linajumuisha maziwa makuu matatu ambayo ni; Ziwa Victoria (kilometa za mraba 35,088), Ziwa Tanganyika (kilometa za mraba 13,489) na Ziwa Nyasa (kilometa za mraba 5,700), maziwa ya kati na  madogo 29, mito na maeneo oevu.  Katika mwaka 2013, sekta ya uvuvi ilikua kwa asilimia 2.2 ikilinganishwa na asilimia 2.9 mwaka 2012. Kupungua kwa kasi ya ukuaji kumechangiwa na kupungua kwa mauzo ya samaki na mazao yake nje ya nchi. Aidha, mchango wa sekta hii kwa pato la Taifa umeendelea kuwa asilimia 1.4 kwa mwaka 2013. Vilevile, idadi ya wavuvi wadogo imeongezeka kutoka wavuvi 182,741 mwaka 2012/2013 hadi wavuvi  183,341 mwaka 2013/2014 na wananchi zaidi ya milioni 4.0 wameendelea kutegemea shughuli za uvuvi ikiwemo biashara ya samaki, uchakataji wa mazao ya uvuvi, utengenezaji wa zana na vyombo vya uvuvi na biashara nyingine.

9.            Mheshimiwa Spika, sekta za mifugo na uvuvi kwa kipindi cha mwaka 2013/2014 zimeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zilizoainishwa katika aya ya 10 ya hotuba yangu.

3.0          MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2013/2014 NA MWELEKEO WA BAJETI YA MWAKA 2014/2015

 

 UKUSANYAJI WA MAPATO

10.       Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa upande wa ukusanyaji wa maduhuli na matumizi ya fedha yamefafanuliwa kwa ufasaha kuanzia aya ya 12 hadi aya ya 14 ya hotuba yangu.

UBUNIFU NA UTEKELEZAJI WA SERA NA SHERIA ZA SEKTA  

11. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu, kupitia na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, mikakati na programu mbalimbali za kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi nchini. Katika mwaka 2013/2014,  sera na sheria za sekta za mifugo na uvuvi zimeendelea kupitiwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kibiashara kama ilivyoainishwa katika aya ya 16.

UENDELEZAJI WA SEKTA YA MIFUGO  


Uzalishaji na Biashara ya Mifugo na Mazao yake 

 

Zao la Maziwa

12. Mheshimiwa Spika uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa asilimia 3.5 kutoka lita bilioni 1.9 mwaka 2012/2013 hadi lita bilioni 2.0. Aidha, maziwa yanayosindikwa kwa siku yameongezeka kutoka lita 135,300 mwaka 2012/2013 hadi lita 139,800 mwaka 2013/2014. Pia, Wizara imeendelea kuboresha Mashamba ya Uzalishaji Mifugo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa mifugo ya asili ambapo katika mwaka 2013/2014  jumla ya mitamba 681 ilizalishwa katika mashamba ya Wizara na kusambazwa kwa wafugaji mbalimbali nchini.
13. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya uhimilishaji kama njia yenye tija ya kuzalisha mifugo bora. Katika mwaka 2013/2014, Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River pamoja na vituo vya Kanda vya Uhimilishaji vya Kibaha (Pwani), Dodoma, Lindi, ZVC Mwanza na Uyole (Mbeya) vimeimarishwa. Jumla ya dozi 58,210 za mbegu bora zimezalishwa na kusambazwa kwa wafugaji. Pia, ng’ombe 90,300 wamehimilishwa katika mikoa mbalimbali.

14. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha uhimilishaji nchini kwa kuzalisha dozi 190,000 za mbegu, kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha Sao Hill, kuimarisha Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa NAIC – Usa River na Vituo sita (6) vya Kanda vya Uhimilishaji. Aidha, Wizara itaendeleza teknolojia ya uhawilishaji kiinitete kwa kukamilisha ujenzi wa maabara ya TALIRI-Mpwapwa na kuitumia teknolojia hiyo.

Nyama - Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo, Nguruwe na Kuku

15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 553,455 mwaka 2012/2013 hadi tani  563,086 (nyama ya ng’ombe tani 309,353, mbuzi na kondoo tani 120,199 nguruwe tani 79,174 na kuku tani 54,360) mwaka 2012/2013. Aidha, wadau wameendelea kuhamasishwa kutumia mfumo wa unenepeshaji mifugo ambapo ng’ombe walionenepeshwa wameongezeka kwa asilimia 11 kutoka ng’ombe 155,206 mwaka 2012/2013 hadi ng’ombe 175,000 mwaka 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuhamasisha uzalishaji, usindikaji wa nyama, kuweka mazingira mazuri ili sekta binafsi iwekeze zaidi. Pia, Serikali itaendelea kuhamasisha unenepeshaji ili kufikia idadi ya ng’ombe 200,000 kwa mwaka.

16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2013/2014, Wizara imeimarisha minada ya Pugu (Dar es Salaam), Lumecha (Songea), Meserani (Arusha) na Nyamatala (Misungwi). Aidha, mnada wa upili wa Nyamatala umezinduliwa rasmi tarehe 8 Aprili, 2014. Minada ya Kirumi (Butiama) na Longido inaendelea kujengwa. Vilevile, wafanyabiashara 340 walipatiwa mafunzo kuhusu biashara, matumizi ya mizani na umuhimu wa kulipa mapato ya Serikali kwenye minada ya upili na ya mipakani. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea na ujenzi wa minada ya Longido na Kirumi na kukarabati minada ya Pugu, Weruweru, Sekenke, Kizota, Meserani na Igunga. Aidha, Serikali itaendelea kuratibu uuzaji wa mifugo katika minada na kuhamasisha matumizi ya mizani ya kupimia uzito wa mifugo.

17. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, jumla ya ng’ombe 1,215,541, mbuzi 960,199 na kondoo 209,292 wenye thamani ya shilingi bilioni 989.3 waliuzwa minadani. Katika mwaka 2014/2015, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kuhamasisha wadau kuwekeza katika ujenzi wa viwanda na  biashara ya mifugo na mazao yake ili kuongeza mauzo ya nyama ndani na nje ya nchi.

Uzalishaji wa Nyama katika Kampuni ya Ranchi za Taifa (National Ranching Company - NARCO)


18. Mheshimiwa Spika, NARCO imeendelea kuzalisha, kunenepesha, kuuza mifugo kwa ajili ya nyama na kuendesha machinjio ya Dodoma kwa ubia na Kampuni ya NICOL. Aidha, Kampuni imeendelea kutoa huduma za ushauri kwa wafugaji wanaozunguka ranchi 10 za mfano za Kagoma, Kalambo, Kikulula, Kongwa, Mabale, Missenyi, Mkata, Mzeri, Ruvu na West Kilimanjaro.  Katika mwaka 2014/2015, NARCO itaendelea na ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ruvu na kununua ng’ombe wazazi 1,200 ili kuongeza idadi ya ng’ombe katika ranchi zake. Aidha, jumla ya ndama 4,050 wanategemea kuzaliwa kutokana na ng’ombe wazazi 5,786. Pia, Kampuni itaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji kwa kutafuta mitaji mipya na kuvutia wawekezaji kwa ubia katika ranchi zake.

Kuku

19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, jumla ya vifaranga milioni 61 vya kuku wa nyama na mayai vilizalishwa nchini ikilinganishwa na vifaranga milioni 52 mwaka 2012/2013. Pia, mayai 348,000 ya kuku wazazi na mayai 6,240,000 ya kutotolesha vifaranga yaliingizwa nchini. Vilevile, uzalishaji wa mayai uliongezeka kutoka bilioni 3.7 mwaka 2012/2013 hadi mayai bilioni 3.9 mwaka 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuhamasisha wadau kuwekeza katika ufugaji wa kuku kibiashara na kushirikiana na wadau kuandaa maonesho yatakayowezesha wadau kuzalisha mazao bora.

Nguruwe

20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, uzalishaji wa nyama ya nguruwe umeongezeka kwa asilimia 35 kutoka tani 50,814 mwaka 2012/2013 hadi tani 79,174 mwaka 2013/2014. Ili kuimarisha ufugaji wa nguruwe nchini, Wizara imenunua nguruwe wa mbegu 24 mbari ya Large White na Duroc na kuwapeleka katika shamba la Ngerengere ili kuwazalisha na kusambaza mbegu bora kwa wafugaji. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha uzalishaji wa nguruwe nchini kwa kuongeza nguruwe wazazi katika shamba la Ngerengere. Aidha, Wizara itashirikiana na Halmashauri kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ufugaji wa nguruwe wa kisasa.

Ngozi

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,  ngozi zilizosindikwa na kuuzwa nje ya nchi ziliongezeka kutoka vipande vya ngozi za ng’ombe 969,060 vyenye thamani ya shilingi bilioni 32.3 na vipande vya ngozi za mbuzi na kondoo  2,582,525 vyenye thamani ya shilingi  bilioni 18.6 katika mwaka 2012/2013 hadi kufikia vipande vya ngozi za ng’ombe 1,060,777 vyenye thamani ya shilingi bilioni 39.4 na vipande vya ngozi za mbuzi na kondoo  2,715,436 vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.6 katika mwaka 2013/2014. Aidha, vipande vya ngozi za ng’ombe 250,000 vyenye thamani ya shilingi bilioni 12.5 vilisindikwa hadi hatua ya mwisho na kutumika kutengeneza bidhaa za ngozi hapa nchini ikilinganishwa na vipande vya ngozi za ng’ombe 212,000 vyenye thamani ya shilingi bilioni 15.0 katika mwaka 2012/2013.

22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara, Halmashauri 75 na Chama cha Wadau wa Ngozi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo imewajengea uwezo wataalam 40 wa Halmashauri. Aidha, imewezesha uimarishaji wa Chama cha Wazalishaji wa Ngozi cha Kitaifa na ukamilishaji wa taratibu za uanzishwaji wa Chama cha Wazalishaji wa Ngozi nchini, ambacho kitasimamia maslahi ya wazalishaji wa ngozi wakiwemo wafugaji, wachinjaji na wakusanyaji wa ngozi katika Halmashauri zote nchini. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kufufua na Kuendeleza Sekta na Viwanda vya Ngozi katika Halmashauri 75.

Matumizi ya Rasilimali za Ardhi, Maji na Malisho kwa Mifugo na Utatuzi wa Migogoro

23. Mheshimiwa Spika,  katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kuhimiza Halmashauri kuandaa Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi na kutenga maeneo ya ufugaji kwa ajili ya kuendeleza malisho ya mifugo katika Halmashauri zote nchini. Upatikanaji wa maeneo ya malisho utaepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Hadi sasa, vijiji 589 katika wilaya 80 ndani ya mikoa 22 vimepimwa na kutenga maeneo kwa ajili ya ufugaji na kufanya jumla ya eneo lililopimwa kufikia hekta milioni 1.51. Katika mwaka 2014/2015, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri itaainisha na kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya maendeleo endelevu ya rasilimali za mifugo katika Wilaya za Busega, Kiteto, Kilosa, Ngorogoro, Mvomero, Kilindi, Igunga, Iramba na Lindi.

24. Mheshimiwa Spika, Wizara inakemea tabia inayozidi kujengeka ya kutesa mifugo kwa kuinyima chakula na maji, kuipiga risasi au kuikata mapanga kwa kisingizio cha migogoro ya ardhi, kwani huko ni kuvunja Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya Mwaka 2008 - The Animal Welfare Act. No.19 of 2008.  Kosa haliwezi kurekebishwa kwa kutenda kosa.  Aidha, wafugaji wanasisitizwa kuheshimu shughuli za watumiaji wengine wa ardhi kwani jamii zote zinategemeana. Wizara itaendelea kuhamasisha jamii ya wafugaji kuanza kumiliki ardhi na kuiendeleza, kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji wa kuhamahama kwani siyo endelevu.  Katika mwaka 2014/15 Serikali itaangalia upya maeneo yaliyobinafsishwa na kushindwa kuendelezwa ikiwa ni pamoja na maeneo ya ranchi za Taifa na maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili yatumike kwa shughuli za ufugaji.
25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea  kuimarisha mashamba ya kuzalisha mbegu za malisho ya Vikuge (Kibaha), Sao Hill (Mufindi), Langwira (Mbeya), Mabuki (Misungwi) na Kizota (Dodoma).  Mashamba hayo yamezalisha mbegu za malisho tani 48.2 na marobota ya hei 497,620. Pia, sekta binafsi imezalisha marobota 425,000 ya hei. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora za malisho na kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa malisho na mbegu bora za malisho. Pia, Serikali itawezesha uchimbaji wa kisima kirefu cha maji ya mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same, kujenga malambo na majosho katika Wilaya za Chemba, Handeni, Kiteto, Kilwa, Chunya, Kilindi na Ngorongoro .

Utoaji wa Kifuta Machozi kwa Wafugaji

26. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa zoezi la kutoa kifuta machozi kwa wafugaji waliopoteza mifugo yao yote katika wilaya za Longido (kaya 2,852), Monduli (kaya 1,484) na Ngorongoro (kaya 1,791) kutokana na ukame uliotokea mwaka 2008/2009 umeendelea kutekelezwa. Hadi sasa  ng’ombe 17,214 (mitamba 17,202 na madume bora 12) na  mbuzi 6,190 wenye thamani ya shilingi bilioni 7.4 waligawiwa kwa wafugaji sawa na asilimia 70 ya malengo.

UDHIBITI WA MAGONJWA YA MIFUGO  

 

Maeneo Huru ya Magonjwa ya Mifugo

27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo cha Kanda ya Kusini Magharibi, mjini Sumbawanga kwa kukipatia vitendea kazi na wataalam. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha Eneo huru la Magonjwa ya Mifugo kwa kukarabati jengo la ofisi la Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo cha Kanda ya Kusini Magharibi, kuwajengea uwezo wataalam na kukipatia vitendea kazi.

Magonjwa ya Mlipuko

28. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara iliendelea kuratibu na kusimamia kampeni za chanjo ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo katika mikoa ya Arusha, Tanga, Morogoro na Kagera ambapo jumla ya mbuzi na kondoo 1,163,451 walichanjwa  dhidi ya ugonjwa huo. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itanunua dozi 1,000,000 za chanjo ya Sotoka ya Mbuzi na Kondoo na kuzisambaza katika mikoa ya Arusha, Tanga, Mara na Tabora iliyo katika hatari ya kuwa na mlipuko wa ugonjwa.

29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa Ugonjwa wa Mafua Makali ya Ndege hapa nchini na nje ya nchi. Ufuatiliaji huu umebaini kuwa ugonjwa huo haujaingia hapa nchini. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutoa tahadhari ili kuhakikisha kuwa virusi vya ugonjwa huo haviingii hapa nchini. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu. Aidha, Wizara itaendelea kushirikisha wadau wengine ikiwa ni pamoja na AU-IBAR kufuatilia mwenendo wa Ugonjwa ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kufuatilia  Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Ng’ombe nchini kwa kuchanja ng’ombe 290,000 katika mikoa ya Pwani, Kagera, Manyara na Tanga. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itanunua dozi 3,000,000 za chanjo kwa ajili ya kuendeleza uchanjaji katika mikoa yenye matukio ya ugonjwa ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga.

Magonjwa yanayoenezwa na Wadudu (Kupe na Mbung’o)

 

(i)            Udhibiti wa Kupe na Magonjwa yaenezwayo
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea  kushirikiana na wadau wengine kudhibiti kupe na magonjwa yanayoenezwa na kupe.  Aidha, Wizara imeendelea kutekeleza mpango wa  ruzuku ya asilimia 40 kwa dawa za kuogesha mifugo ambapo lita 10,736 zenye kiini cha pareto zilinunuliwa kwa thamani ya shilingi milioni 181.8 na kusambazwa katika mikoa 24. Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kuhamasisha matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa Ndigana kali ambapo jumla ya ng’ombe 113,955 walichanjwa dhidi ya ugonjwa huo katika mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora, Kagera na Pwani. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri na wadau wengine kuhamasisha matumizi ya chanjo hii, ujenzi na ukarabati wa majosho pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kuogesha mifugo.

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara ilishirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza Mkakati wa Kudhibiti Mbung’o na Nagana. Katika mwaka 2014/2015, Wizara kupitia Program ya Pan African Tsetse and Trypanosomiasis Eradication Campaign (PATTEC) itaendelea kudhibiti Mbung’o na Nagana kwa kutekeleza miradi ya kuangamiza mbung’o kwa ajili ya mikoa ya Mara - Ikolojia ya Serengeti, Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi.

Magonjwa ya Mifugo yanayoambukiza Binadamu


32. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kupitia Mradi wa Kutokomeza Kichaa cha Mbwa unaofadhiliwa na Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation kwa uratibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni imeendelea kudhibiti Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Morogoro, Mtwara na Pwani kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na wadau mbalimbali. Jumla ya dozi 200,000 zimesambazwa katika Halmashauri 24 zinazotekeleza mradi huu. Udhibiti wa magonjwa mengine ya mifugo yanayoambukiza binadamu ni pamoja na Homa ya Bonde la Ufa, Ugonjwa wa Kutupa mimba na Kifua Kikuu kama ilivyoainishwa katika Aya ya 43 na 44 ya Hotuba yangu.

Ukaguzi wa Mifugo na Mazao yake

33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, jumla ya ng’ombe 987,172, mbuzi 885,061, kondoo 275,197, nguruwe 440,000 na kuku 1,632,000 walikaguliwa na wataalam katika machinjio mbalimbali. Aidha, Wizara imeendesha mafunzo rejea kwa Wakaguzi  wa Nyama 12 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na wadau 34 kutoka machinjio ya Vingunguti. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kufuatilia usalama wa mazao yatokanayo na mifugo kwa kukagua mifugo na mazao yake ili kukuza biashara ya mifugo na kulinda afya za walaji.

Utambuzi, Usajili na Ufuati liaji wa Mifugo 

34. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji wa Mifugo kwa kutoa mafunzo kuhusu stadi za utambuzi wa mifugo na ukusanyaji takwimu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu utekelezaji wa mfumo wa kielektroniki wa Utambuzi na Ufuatiliaji wa mifugo kwa kutoa mafunzo kwa wataalam wa mifugo 75 kuhusu mfumo huo na kuhamasisha umma ili kuwezesha utambuzi wa mifugo 45,000 katika makundi ya wafugaji wa ng’ombe wa asili na kisasa.

 

UENDELEZAJI WA SEKTA YA UVUVI


Uvunaji wa Samaki na Uuzaji wa Mazao ya Uvuvi

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imetoa elimu ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi unaozingatia mfumo wa ikolojia na mazingira kwa wavuvi 641 kutoka Halmashauri za Bagamoyo, Kinondoni, Temeke na Mkuranga. Aidha,  Maafisa Uvuvi 16 wa Wilaya, Wavuvi 16 na Wawakilishi wa Vikundi vya Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi (Beach Management Units – BMUs) 16 kutoka Halmashauri 16 za Ukanda wa Pwani walipatiwa mafunzo kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali ya Jodari na samaki wanaopatikana katika tabaka la juu la maji.

36. Mheshimiwa Spika, nguvu ya uvuvi nchini imeongezeka kutoka wavuvi 182,741 na vyombo vya uvuvi 56,985 mwaka 2012/2013 hadi wavuvi 183,431 wanaotumia vyombo vya uvuvi 57,385 mwaka 2013/2014. Kutokana na nguvu hiyo ya uvuvi, jumla ya tani 375,158 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 1.4 zilivunwa ambapo kati ya hizo, tani 52,846 ni kutoka ukanda wa maji chumvi na tani 147,020 maji baridi ikilinganishwa na tani 365,023.38 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 1.3 zilizovunwa mwaka 2012/2013. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu, kusimamia uvunaji na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi na kufanya sensa za uvuvi katika bahari, Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa, Rukwa, Bwawa la Nyumba ya Mungu na Mto Rufiji kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji, uchambuzi na uhifadhi wa takwimu za uvuvi na kuhamasisha jamii za wavuvi kusimamia, kuendeleza na kulinda rasilimali za uvuvi kwa kuzingatia mfumo wa ikolojia na mazingira.

Uwezeshaji Wavuvi Wadogo 

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kupitia programu ya SmartFish na United Nations University Iceland imetoa mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi kwa ajili ya uandaaji, uchakataji na usambazaji wa mazao ya uvuvi kwa wavuvi 735 katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mara, Mwanza na Pwani na kuwezesha ujenzi wa vichanja vya kisasa 40 vya kukaushia samaki na majiko sanifu manne  katika Halmashauri ya Uvinza.

38. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na WWF, iliwawezesha wavuvi kutoka Halmashauri za Kilwa, Lindi, Mtwara, Pangani na Mafia kuhudhuria mafunzo ya  uchakataji wa samaki aina ya Jodari na utunzaji wa samaki wa mapambo; usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi kupitia BMUs na uendeshaji wa miradi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji na matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kutengeneza boti hasa za fibre na zana za uvuvi zinazokubalika kisheria. Vilevile, itaendelea kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kukamilisha ujenzi wa mialo minne katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, ujenzi wa karakana ya kutengeneza boti katika Ukanda wa Ziwa Nyasa (Mbamba Bay) na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi.

Ukuzaji wa Viumbe kwenye Maji


39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, jumla ya vifaranga 2,295,032 vimezalishwa na kusambazwa ambapo vifaranga 19,692 vimezalishwa katika vituo vya Serikali na  2,275,340 katika vituo vya sekta binafsi. Aidha, wananchi 2,604 wamehamasishwa kwa kupatiwa elimu ya ufugaji samaki na kutokana na uhamasishaji huo mabwawa ya kufugia samaki yameongezeka kutoka 20,134 mwaka 2012/2013 hadi 20,493 mwaka 2013/2014 yenye uwezo wa kuzalisha tani 3,546 za samaki. Pia, tani 320 za kambamiti zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.56 zimevunwa katika mabwawa ya kampuni ya Alphakrust katika Wilaya ya Mafia.

UTAFITI, MAFUNZO NA UGANI WA MIFUGO NA UVUVI 


Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kuimarisha vituo  vya utafiti vya TALIRI vya Kongwa, Mabuki, Mpwapwa, Naliendele, Tanga, Uyole na West Kilimanjaro kwa kuvipatia vitendea kazi na kukarabati miundombinu. Aidha, Taasisi imeendelea kutekeleza miradi ya utafiti wa mifugo ya kuboresha uzalishaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa; nguruwe;  kuku, malisho na masoko ya mazao ya mifugo.

41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, TALIRI imetathmini na kusambaza ng’ombe 143 aina ya Mpwapwa kwa wafugaji katika Manispaa za Dodoma na Tanga na Halmashauri za Chamwino, Kilindi, Kisarawe na Bagamoyo. Aidha, Taasisi imesambaza jumla ya madume 32 aina ya Friesian katika Wilaya za Bagamoyo, Muheza, Mufindi na Njombe na Mbuzi aina ya Malya 65 katika maeneo ya mikoa ya Dodoma  na Pwani.

42. Mheshimiwa Spika, kwa kutumia fedha za maendeleo chini ya COSTECH, TALIRI imekamilisha ujenzi wa jengo la maabara ya nyama, nyumba tatu za watumishi katika kituo cha Mabuki na ukarabati wa jengo la maabara ya viini tete Mpwapwa. Pia, inaendelea na ukarabati wa  jengo la maabara ya maziwa Uyole, ofisi ya Tanga na mabanda ya mbuzi West Kilimanjaro.

Utafiti wa malisho ya Mifugo
43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, jumla ya aina 39 za malisho ya asili zimekusanywa kwa ajili ya kufanyiwa tathimini vituoni. Vilevile, jumla ya marobota 44,347 ya malisho  yalivunwa katika vituo vya   Mpwapwa, Uyole na Kongwa. Katika mwaka 2014/2015, TALIRI itaimarisha miundombinu ya utafiti kwa kununua vifaa vya maabara, kemikali na samani katika maabara ya sayansi ya nyama ya Mabuki, Uhawilishaji Viinitete (Mpwapwa), maabara ya teknolojia ya maziwa (Uyole), maabara za lishe ya mifugo (Mpwapwa, Tanga, Naliendele na West Kilimanjaro).

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI)

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, TAFIRI imekarabati ofisi ya Utawala ya Kituo cha Kyela na kujenga uzio katika kituo cha Dar es Salaam; matangi 9 katika kituo cha Dar es Salaam kwa ajili ya utafiti wa majaribio ya vyakula vya samaki kutokana na malighafi asili. Pia, imechimba mabwawa ya vifaranga bora vya samaki katika kituo cha Mwanza na kuimarisha utafiti katika vituo vya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Kyela na kituo kidogo cha Sota (Rorya). Aidha, TAFIRI imebaini kuwa wingi wa samaki aina ya Sangara katika Ziwa Victoria umeshuka kutoka mavuno ya kilo 296 kwa saa mwaka 2008 hadi kufikia kilo 185 kwa saa mwaka 2013. Katika mwaka 2014/2015, Wizara  ikishirikiana na wadau wengine wa uvuvi itaendelea kuiwezesha TAFIRI kuendelea na tafiti za uvuvi na mazingira katika Bahari ya Hindi, maziwa, mito na mabwawa ili kubaini uwingi, mtawanyiko na ikolojia ya rasilimali kwa ajili ya kuweka menejimenti ya uvuvi endelevu.

Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Fisheries Education and Training Agency - FETA)

45.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, FETA imekarabati Kituo cha Kigoma na kupata usajili wa kudumu kutoka NACTE. Udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanachuo 943 mwaka 2012/2013 hadi wanachuo 1,073 mwaka 2013/2014. Aidha, Wakala umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam 54 kutoka nchi za SADC. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuiwezesha Wakala kutekeleza majukumu yake na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 1,073 hadi 1,500. Aidha, FETA itaendelea kujenga kituo cha Gabimori (Rorya) na kukarabati kituo cha Mikindani Mtwara.

Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (Livestock Training Agency - LITA)

46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, LITA imeongeza udahili wa wanafunzi kutoka 949 mwaka 2012/2013 hadi  2,215 wakiwemo 655 wa Stashahada na 1,560 wa Astashahada za Afya ya Mifugo na Uzalishaji. Vilevile, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na vyuo binafsi vya Visele (Mpwapwa) na Kaole (Bagamoyo) vimedahili jumla ya wanafunzi 492 wa Stashahada na Astashahada. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuiwezesha Wakala kutekeleza majukumu yake na kuongeza udahili wa wanafunzi   kutoka 2,215 hadi 2,500; kuhamasisha Sekta binafsi kuanzisha vyuo na kuongeza udahili kufikia lengo la wanafunzi 5,000 kwa mwaka ili kupunguza pengo la maafisa ugani na kuwezesha mafunzo ya ufugaji kibiashara kwa vijana (Emerging Young Commercial Farmers) ili waweze kujiajiri.

 

Huduma za Ugani

47. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau imeendelea kutoa elimu na kusambaza teknolojia za kisasa kuhusu uvuvi endelevu, ukuzaji bora wa  viumbe kwenye maji na ufugaji bora wa mifugo. Aidha, Wizara imeendelea kuboresha utoaji huduma za ugani katika sekta ya uvuvi kwa kutoa mafunzo elekezi ya ufugaji wa samaki kwa wataalam 11 na wadau  wa uvuvi 256 katika mikoa ya Tanga, Iringa na Morogoro.


Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (Tanzania Veterinary Laboratory Agency-TVLA)

48. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Wizara kupitia Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania ilitekeleza kazi za utambuzi, uchunguzi na utafiti wa magonjwa ya mifugo, uhakiki wa vyakula vya mifugo na madawa ya kuogeshea mifugo katika maabara zake za Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Tabora, Mpwapwa, Tanga, Kigoma, Iringa na Mtwara. Aidha, TVLA kwa kushirikiana na Idara ya Wanyama Pori imetengeneza vitambaa 300 na kuviweka  katika maeneo ya Pori la Akiba la Selous ili kudhibiti mbung’o. Katika mwaka 2014/2015, TVLA itaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuendelea kufanya utambuzi wa magonjwa mbalimbali ya mifugo, kuendeleza tafiti za magonjwa ya mifugo, kuzalisha  dozi 100,000,000 za chanjo ya Mdondo, dozi 500,000 za chanjo ya Chambavu, dozi 500,000 za chanjo ya Kimeta na dozi 250,000 za chanjo ya Ugonjwa wa Kutupa Mimba kwa Ng’ombe na Maabara Kuu ya Mifugo Temeke kukamilisha taratibu za kupata ithibati ya Kimataifa.

USIMAMIZI WA UBORA WA MAZAO NA HUDUMA ZA MIFUGO NA UVUVI


Bodi ya Nyama Tanzania

49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kuimarisha Bodi ya Nyama Tanzania kwa kuipatia wataalam na vitendea kazi. Aidha, Bodi imeandaa maelezo ya Sheria ya Nyama Sura 421 katika lugha ya Kiswahili na kutoa elimu kwa wadau kupitia vipindi vya redio 14 na kusambaza nakala 800 za vipeperushi. Vile vile, Bodi imehamasisha wadau wa tasnia ya nyama katika mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita, Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Pwani kusajili, ambapo wadau 116 wamesajiliwa na wadau wengine 50 wameunganishwa na soko la mifugo na nyama. Katika mwaka 2014/2015, Bodi ya Nyama Tanzania itaendelea kuimarisha Sekretarieti ya Bodi kwa kuajiri watumishi sita na kutambua na kusajili wadau 200 wa tasnia ya nyama na vyama vyao. Vilevile, Bodi itaendelea kuimarisha vyama vya wadau vya wafanyabiashara wa Mifugo na Nyama Tanzania (TALIMETA), Wasindikaji wa Nyama Tanzania (TAMEPA) na Wafugaji Tanzania (CCWT) kwa kushauri, kutoa mafunzo na kuratibu maendeleo ya vyama hivyo.

Bodi ya Maziwa Tanzania

50. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kuimarisha Bodi ya Maziwa Tanzania iliyoundwa kwa Sheria ya Maziwa Sura 262. Aidha, Bodi imeelimisha wadau 100 wa maziwa kuhusu Sheria ya Maziwa katika Mkoa wa Njombe. Katika mwaka 2014/2015, Bodi itaendelea kuelimisha  wadau wa maziwa kuhusu Sheria ya Maziwa Sura 262 na kuisimamia, kuwajengea uwezo wakaguzi 50 wa maziwa kutoka Halmashauri za mikoa ya Iringa, Njombe na Mara na kuhamasisha Halmashauri  kutekeleza Mpango wa Unywaji wa Maziwa Shuleni.

 

Baraza la Veterinari Tanzania 

51. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Baraza limeimarisha ukaguzi katika ngazi za kanda, mikoa na Halmashauri ambapo Wakaguzi wapya 20 wameteuliwa. Pia, imesajili madaktari wa mifugo 37, wataalam wasaidizi wa afya ya mifugo 221 na vituo 106 vya kutolea huduma ya afya ya mifugo. Katika mwaka wa 2014/2015,  Baraza litasajili madaktari wa mifugo 40, vituo vya huduma za mifugo 200, kuorodhesha na kuandikisha wataalamu wasaidizi 700, kutoa leseni kwa wataalam wasaidizi 110 na kufanya ukaguzi wa maadili kwa kushirikiana na Halmashauri 156 nchini.

 

Uthibiti wa Ubora na Usalama wa Mazao ya Uvuvi

52. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na Usalama wa Mazao ya Uvuvi na Maabara ya Taifa ya Udhibiti wa Ubora wa Mazao ya Uvuvi-Nyegezi imeendelea kuratibu na kusimamia ubora, viwango na usalama wa mazao ya uvuvi pamoja  na huduma  za kitaalam ikiwemo kufanya kaguzi mbalimbali za kuhakiki ubora wa mazao ya uvuvi katika viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi, mialo, masoko na kwenye magari na boti zinazosafirisha mazao ya uvuvi.

53. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha vituo vya Udhibiti Ubora wa mazao ya Uvuvi vya Bukoba, Dar es Salaam, Kigoma, Kilwa, Mafia, Musoma, Mwanza na Tanga, pamoja na Maabara ya Taifa ya Udhibiti wa Ubora wa Mazao ya Uvuvi - Nyegezi kwa kuvipatia watumishi na vitendea kazi. Katika mwaka 2013/2014, jumla ya sampuli 1,318 za samaki, maji, vyakula vya samaki na udongo zilifanyiwa uchunguzi. Kati ya hizo 966 zilichunguzwa kubaini uwepo wa vimelea vya magonjwa na 352 kubaini mabaki ya viuatilifu, madini tembo na kemikali. Matokeo ya uchunguzi wa sampuli hizi ulionyesha kukidhi viwango. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha vituo vya Ubora na Udhibiti wa Mazao ya Uvuvi na Maabara za Uvuvi – Nyegezi kwa kuvipatia vitendea kazi na mafunzo kwa watalaam.

 

USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UVUVI 

54. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Halmashauri imeendelea kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi kwa kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao ya uvuvi mipakani.

Udhibiti wa Uvuvi Haramu 

55. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeanzisha kituo cha doria cha Buhingu (Uvinza) na kufanya vituo vya doria kufikia 23. Pia, doria zenye siku kazi 6,201 zimefanyika na kuwezesha kukamatwa nyavu mbalimbali 33,861, vyandarua 123, mabomu 73, tambi za kulipulia mabomu 15,  mitungi ya gesi 48, viatu vya kuzamia jozi 35, miwani ya kuogelea jozi 11, mitumbwi 194, injini za boti 10, magari 12 na pikipiki 2. Aidha, samaki wachanga kilo 30,823 za sangara, 2,478 za sato, 1,112 za samaki aina nyingine na kilo 187 za samaki waliovuliwa kwa mabomu, kilo 682 za dagaa,  kilo 57 za Pweza, kilo 5 za majongoo bahari na kilo 210 za nyama ya Kasa zilikamatwa. Vilevile, watuhumiwa 319 walikamatwa kwa kujihusisha na uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi ambapo kesi 48 zilifunguliwa mahakamani. Katika mwaka 2014/2015, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuratibu na kusimamia uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi na kudhibiti biashara haramu ya mazao ya uvuvi kwa kufanya doria zenye siku kazi 6,000 katika maeneo ya maji baridi, Bahari ya Kitaifa (territorial waters) na maeneo ya mipakani. Aidha, itaendelea kuwezesha uanzishwaji wa Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) na kuimarisha vikundi vilivyopo.

Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi  Bahari Kuu
56. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi  Bahari Kuu (Deep Sea Fishing Authority) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inaendelea kufanya utafiti kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kuvutia samaki (Fish Aggregating Devises – FADs). Pia, Mamlaka imeendelea kuandaa mazingira rafiki ambayo yatawawezesha Watanzania kuingia ubia na wageni ili waweze kuwekeza kwenye uvuvi katika Bahari Kuu. Aidha, Mamlaka kwa kushirikiana na nchi wanachama wa Indian Ocean Tuna Commission (IOTC) za Comoro, Madagascar, Seychelles, Reuninon na Mauritius,  ilifanya doria za pamoja za siku 8, kukagua meli 8 zinazovua katika Bahari Kuu ya Tanzania. Pia, ukaguzi ulifanyika kwa meli 25 za uvuvi wa  purse seine na long liner  zenye Bendera ya Hispania, Taiwan na China katika Bandari za Dar es Salaam na Zanzibar, Mombasa, Mahe Victoria (Ushelisheli), Madagascar na Mauritius. Katika ukaguzi huo meli husika zilionekana kukidhi masharti ya leseni. Vilevile, leseni za uvuvi wa Bahari Kuu 68 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 1,472,153 sawa na shilingi bilioni 2.4 zilitolewa kwa meli kutoka mataifa ya Hispania, Ufaransa, Ushelisheli, Taiwan, Japan, Oman na China. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaiwezesha Mamlaka kukamilisha marekebisho ya Sheria na Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu, kuendesha doria na kufanya tathimini ya utendaji wa FADs. Pia, kuendelea kuhamasisha wavuvi wa Tanzania na wawekezaji wengine kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu na kusindika mazao ya uvuvi. Vilevile, kuendelea kutoa mafunzo ya uvuvi wa Bahari Kuu kwa wavuvi.

Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu

57. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia maendeleo ya rasilimali za uvuvi katika maeneo yaliyohifadhiwa kupitia kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu ambapo doria zenye siku kazi 800 zilifanyika iliyowezesha kukamatwa vifaa mbalimbali zikiwemo  mabomu 21 na tambi zake, chupa za mbolea ya Urea inayotumika kutengeneza mabomu na makokoro 5.  Katika mwaka 2014/2015, Kitengo kitafanya doria zenye siku kazi 416 katika eneo la kilomita za mraba 2,000 kwa lengo la kudhibiti uvuvi haramu kwenye Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu na pia kuvutia uwekezaji wa utalii.

3.3          MASUALA MTAMBUKA  


Uendelezaji wa Rasilimali Watu

58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeajiri watumishi 124 wakiwemo 71 wa kada za mifugo, 43 kada za uvuvi   na 10 kada mtambuka. Aidha, Maafisa Mifugo na Uvuvi 853 wameajiriwa na kupelekwa katika Sekretarieti za Mikoa 17 na Halmashauri 103 nchini kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. Vilevile, Watumishi 187 wamepandishwa vyeo, 8 wamebadilishwa  kazi baada ya kupata sifa za Miundo ya Utumishi na 57 wamethibitishwa kazini, 161 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi, 39 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu wakiwemo wa uzamivu sita (6), uzamili 22 na Shahada ya Kwanza 11 na 55 walipatiwa mafunzo elekezi.   Katika mwaka 2014/2015, Wizara inatarajia kuajiri watumishi 214 (wakiwemo mifugo 62, uvuvi 86 na mtambuka 66), kupandisha vyeo watumishi 223, kuthibitisha kazini watumishi 125 na watumishi 312 watahudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

 

Mawasiliano na Elimu kwa Umma 

59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, vipindi vitano kuhusu mafanikio ya sekta za mifugo na uvuvi na makala moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 vilitangazwa kupitia luninga na magazeti.  Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuimarisha Dawati la Malalamiko na Maktaba; na kutoa mafunzo kwa maafisa habari wawili. Aidha, itatoa mafunzo kwa maafisa kutoka vituo vya nje kuhusu mawasiliano kwa umma na kuchapisha na kusambaza kwa wadau nakala 1,000 za kalenda.

60. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kusimamia masuala mengine mtambuka ya Utawala Bora, Jinsia, UKIMWI, TEHAMA na Hifadhi ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kama yalivyoainishwa katika  Aya ya 110 hadi 115 ya Hotuba yangu.

4.0          SHUKRANI

61. Mheshimiwa Spika, Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wafugaji, Wavuvi, Wasindikaji, Wafanyabiashara na wadau wengine kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi nchini. Wizara inaomba waendeleze juhudi hizo na inaahidi kuendelea kushirikiana nao kuleta mapinduzi ya sekta za mifugo na uvuvi nchini. Aidha, napenda kuzitambua na kuzishukuru nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Nchi za Ulaya, Serikali za Australia, Austria, Brazil, Canada, Jamhuri ya Czech, Hispania, Iceland, Ireland, Japan, Jamhuri ya Watu wa China, Israel, Korea Kusini, Marekani, Misri, Norway, Poland, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uswisi pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya FAO, IAEA, UNICEF, UNDP, UNIDO na WHO na mifuko ya kimataifa ya GEF na IFAD kwa kuchangia katika maendeleo ya sekta za mifugo na uvuvi.

62. Mheshimiwa Spika, vilevile, nazishukuru taasisi za kimataifa ambazo ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika; Shirika la JICA, Shirika la KOICA, Shirika la Misaada la Ireland, USAID, Shirika la Misaada la Australia (AUSAID), DfID, Taasisi ya Rasilimali za Wanyama ya Umoja wa Afrika (AU-IBAR), Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), Shirika la Ushirikiano la Ujerumani (GTZ), United Nations University (UNU), Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na  Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) kwa michango yao katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi. Pia, nayashukuru Mashirika na Taasisi za hiari za Bill and Melinda Gates Foundation, ASARECA, NEPAD, International Livestock Research Institute, World Wide Fund for Nature, Indian Ocean Tuna Commission, South West Indian Ocean Fisheries Commission (SWIOFC), Heifer Project Tanzania, Overseas Fisheries Co-operation Foundation of Japan, Vetaid, Care International, OXFAM, Welcome Trust, World Vision, FARM Africa, Land O’ Lakes, Building Resources Across Communities, World Society for Protection of  Animals, Global Alliance for Livestock and Veterinary Medicine, Institute for Security Studies, International Land Coalition, British Gas International, Sea Sense, International Whaling Commission, SmartFish na Marine Stewardship Council.

63. Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kuwashukuru kwa dhati Mhe. Kaika Saning’o Ole Telele, Mbunge wa Ngorongoro na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa msaada wake wa karibu katika kusimamia kazi za Wizara. Aidha, napenda pia nitoe shukurani zangu kwa Katibu Mkuu Dkt. Charles Nyamrunda, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Yohana Budeba, Wakuu wa Idara na Vitengo, Taasisi na watumishi wote wa Wizara kwa ushirikiano wao katika kutekeleza majukumu tuliyopewa na Taifa na kufanikisha maandalizi ya bajeti hii. Vilevile, napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Busega kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa na kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu. Pia, naishukuru familia yangu kwa kuendelea kunitia moyo ninapotekeleza majukumu ya kitaifa.

5.0          BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015


64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Wizara inaomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ya jumla ya shilingi 66,142,627,000.00 kama ifuatavyo:-

(i)             Shilingi 40,952,022,00.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya hizo, shilingi 22,968,188,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE); na shilingi 17,984,834,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengine (OC);  na
(ii)           Shilingi 25,190,605,000.00 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya hizo, shilingi 23,000,000,000.00 ni fedha za ndani na shilingi 2,190,605,000.00 ni fedha za nje.

6.5 Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukurani zangu za dhati kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara kwa anuani: www.mifugouvuvi.go.tz.

66.       Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii nimeambatanisha Randama ya Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2014/2015.

67.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: