BAJETI WIZARA YA MAMBO YA NJE



HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015


1.     UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba niungane na wenzangu walionitangulia kutoa pole kwa familia, kwako binafsi na kwa Bunge lako Tukufu kwa misiba iliyotokea katika mwaka huu wa fedha, ambapo tuliondokewa na wabunge wenzetu wawili;  Mheshimiwa William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Taifa limepoteza watu waliokuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika, kwa nafasi hii napenda nitoe shukrani kwa Viongozi na Watanzania wote walioisaidia Wizara yangu wakati ilipopata msiba wa ghalfa wa aliyekuwa Balozi wa Malawi hapa nchini Marehemu Flossie Gomile Chidyaonga uliotokea tarehe 9 Mei, 2014. Napenda kutoa shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa usafiri wa ndege wa kusafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani kwao Blantyre, Malawi.

Mheshimiwa Spika, wakati kumbukumbu ya kifo cha Mzee Nelson Rolihlahla Mandela bado ingalipo, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Watanzania wote na Waheshimiwa Wabunge kwa maombolezo hayo. Pia, kumshukuru tena Mheshimiwa Rais wetu kwa hotuba aliyoitoa kwenye mazishi yale kwa niaba ya Watanzania wote,  iliyogusa sana nyoyo za ndugu zetu wa Afrika Kusini, hadi kupelekea Serikali yao kututumia salamu rasmi za upendo na shukrani kwa yote ambayo Tanzania imeyafanya huko nyuma wakati wa vuguvugu la ukombozi  na wakati wa kipindi cha msiba huo.


Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii pia kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nne. Ni dhahiri kwamba chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha amani, usalama na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuimarisha ushawishi wa Tanzania katika nyanja za Kikanda na Kimataifa kupitia diplomasia thabiti na imara. Pamoja na utendaji wake kuonekana kwetu, mtazamo wa watu wa nje ya Tanzania pia unadhihirisha hivyo. Tarehe 9 Aprili 2014, Mheshimiwa Rais alitunukiwa tuzo ya kuwa kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo Barani Afrika kwa mwaka 2013, huko jijini Washington DC.  Tuzo hiyo ya heshima kubwa niliyoipokea kwa niaba yake, ilitolewa na jarida maarufu la kimataifa liitwalo African Leadership Magazine Group.

Mheshimiwa Spika, ninawaomba Watanzania wenzangu, tuendelee kushirikiana na wenzetu duniani kote katika kudumisha demokrasia, amani, usalama, umoja na mshikamano bila kujali rangi, kabila, dini au itikadi zetu za kisiasa. Napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba jumuiya ya kimataifa inatambua na kuthamini mchango wa Tanzania katika maeneo hayo ya utawala bora na hivyo kuichukulia kama mfano wa kuigwa.

Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kuwashukuru Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Stephen Masato Wassira (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao nzuri. Hotuba zao sio tu zimechambua kwa kina masuala ya kiuchumi, kijamii, kiusalama na kisiasa na kutoa dira ya Taifa letu katika mwaka ujao wa fedha, bali zimegusia pia mambo kadhaa ya msingi yanayohusu Wizara yangu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wameshawasilisha hotuba zao, ambazo kwa namna moja au nyingine ziligusa maeneo yanayohusu Wizara yangu. Kama mnavyofahamu, Wizara hii inashughulikia masuala mtambuka ambayo yanagusa na kuguswa na Wizara, Idara na Taasisi zote yanapokuja masuala ya nchi, kanda, kimataifa na mashirika mbalimbali duniani. Wajibu wetu mkubwa ni kuratibu masuala hayo na utekelezaji unabaki kwa Taasisi husika.

Mheshimiwa Spika,  naomba nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati na Makamu wake Mheshimiwa Azan Zungu (Mb.) kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuchambua na kushauri Wizara yangu kuhusu bajeti wakati wa vikao vya Kamati. Uchambuzi na ushauri walioutoa utakuwa nguzo muhimu katika utekelezaji wa bajeti hii na majukumu ya Wizara yangu na hivyo kusimamia utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa ukamilifu zaidi kwa manufaa ya nchi yetu.


Mheshimiwa Spika, pongezi zangu pia kwa Wabunge wapya watatu waliojiunga nasi mwaka huu, ambao ni Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwan Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Nawapongeza kwa kuchaguliwa kuwawakilisha wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mheshimiwa Spika, pia nawashukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Bwana John M. Haule, Katibu Mkuu; Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu; Wakurugenzi, Mabalozi na Wafanyakazi wote wa Wizara yangu waliopo Makao Makuu, Ofisi yetu ya Zanzibar na katika Balozi zetu mbalimbali duniani, kwa ushirikiano wanaonipa na kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika niwashukuru wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, hususan wa Jimbo la Mtama kwa kuniunga mkono katika shughuli za maendeleo jimboni na mkoani kwa ujumla. Shukurani za pekee ziwaendee mke wangu Mama Dorcas Membe na watoto wetu kwa kunivumilia pale ninapolazimika kuwa mbali na familia kwa muda mrefu na kunitia moyo katika kutimiza majukumu yangu ya kulitumikia Taifa.

2.     TATHMINI YA HALI YA DUNIA

Mheshimiwa Spika, hali ya dunia kwa sehemu kubwa ni shwari ingawaje bado kuna changamoto kubwa ya vitendo vya kigaidi. Mbali na changamoto hiyo, viongozi duniani pamoja na jumuiya za kimataifa wanaendelea kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri sana maisha ya walimwengu. Aidha, amani duniani ipo lakini usalama wake umeathirika kwa kiwango kikubwa na migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kwenye baadhi ya nchi. Kwa upande wa maendeleo na kuboresha maisha ya watu, nchi nyingi duniani zinajitahidi kufikia malengo ya milenia ambayo yanakoma mwakani lakini Umoja wa Mataifa utaendeleza baadhi ya malengo hayo baada ya 2015 ili dunia iwe na malengo endelevu ya maendeleo (SDGs). Napenda kutoa tathmini ya maeneo machache ya dunia ambayo kwa namna moja au nyingine yanatuhusu:-

2.1.         Mgogoro wa Syria
Mheshimiwa Spika, kama nilivyolieleza Bunge lako Tukufu kwenye hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2013/2014 kuhusu mgogoro wa Syria, hali imeendelea kuwa mbaya na hivyo kusababisha vifo vingi, wakimbizi wa ndani na nje na uharibifu mkubwa wa mali. Hali hii inazidi kuwa mbaya zaidi baada ya msuluhishi aliyechukua nafasi ya Kofi Annan, Mheshimiwa Lakhdar Brahimi naye kuomba kujiuzulu nafasi hiyo mwezi huu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masikitiko makubwa amekubali kujiuzulu kwake ifikapo tarehe 31 Mei 2014. Tanzania inaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea na jitihada za makusudi kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi, hususan kwa njia ya mazungumzo na hivyo kurejesha amani na utulivu kwa nchi na wananchi wa Syria.

2.2 Mgogoro wa Ukraine
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, pamekuwepo na mgogoro nchini Ukraine uliopelekea kujitenga kwa jimbo lake moja la Crimea na mengine kutaka kufanya hivyo. Mgogoro huo umetishia kuigawa dunia pande mbili, zile zinazounga mkono kujitenga zikiongozwa na Urusi na zile zinazopinga zikiongozwa na Mataifa ya Ulaya na Marekani. Msimamo wa Tanzania ni kutofungamana na upande wowote ili kuepuka kuingia kwenye mgogoro huo unaotishia amani na usalama wa dunia kwa kuirudisha tena kwenye vita baridi. Tanzania inaendelea kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kushughulikia mgogoro huu kwa kutumia hekima na busara ambayo itaiepusha dunia kuingia kwenye vita.

2.3 Hali ya Usalama Barani Afrika
Mheshimiwa Spika, hali ya amani na usalama Barani Afrika kwa kipindi cha mwaka 2013/2014 imezidi kuimarika. Baadhi ya migogoro kama vile wa Liberia, Cote d’Ivoire, Burundi, Guinea, na Madagascar imepatiwa ufumbuzi wa kudumu. Jitihada zinaendelea ili kutafuta suluhu kwenye migogoro ya kisiasa inayoendelea kwenye nchi kama Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri na Libya.
2.3.1 Somalia
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, hali ya usalama nchini Somalia imeendelea kuimarika ambapo mashambulizi ya kikundi cha Al Shaabab dhidi ya vikosi vya Serikali na Umoja wa Afrika yamepungua kwa kiasi kikubwa. Hali hiyo imefanya usalama wa raia kuimarika zaidi. Vilevile matukio ya uharamia katika Pwani ya Afrika Mashariki yamepungua sana. Tanzania inaipongeza Serikali ya Somalia kwa juhudi zake kubwa za kuimarisha hali ya usalama nchini humo. Aidha, tunapongeza Umoja wa Afrika na Jeshi la Afrika la kulinda amani nchini Somalia (AMISOM), na hasa majeshi ya Kenya ambayo yaliingia hadi Kismayu na kuiteka kabisa ngome ya Maharamia. Tanzania itaendelea kutumia ushiriki wake kwenye Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhakikisha kuwa amani na usalama nchini Somalia vinazidi kuimarika.

2.3.2 Sudan Kusini
Mheshimiwa Spika, dunia ilipatwa na mfadhaiko mkubwa mwezi Desemba 2013 baada ya taifa jipya na changa la Sudan Kusini kuingia kwenye mapigano makali ya wenyewe kwa wenyewe. Mapigano hayo yaliyoanza mwezi Julai 2013 yalisababishwa na kutoelewana kati ya Mheshimiwa Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini na aliyekuwa Makamu wake, Bwana Riek Machar. Hali hii ilitokea baada ya Rais Kiir kumfuta kazi Makamu wake huyo na baadhi ya viongozi wengine waandamizi.

Mheshimiwa Spika, mgogoro kati ya viongozi hao ulichukua sura mpya tarehe 14 Desemba, 2013 baada ya Serikali ya Sudan Kusini kutangaza kuwepo kwa jaribio la mapinduzi lililofanywa na wafuasi wa Bw. Machar. Baada ya tangazo hilo, Bw. Machar alikwenda mafichoni lakini wafuasi wake 11 walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini. Hatua ya kuwakamata wafuasi wa Bw. Machar ilizusha mapigano makali baina ya vikosi vya Serikali na wafuasi wa Bw. Machar, hususan kwenye majimbo ya Jonglei, Unity na Upper Nile. Kadri muda ulivyokwenda, mapigano yalichukua sura ya ukabila kati ya kabila la Ngok Dinka analotoka Rais Kiir na Nuer la Bwana Machar, ambapo idadi kubwa ya raia wasio na hatia waliuawa na wengine kulazimika kukimbia makazi yao.



Mheshimiwa Spika, kufuatia kuibuka kwa mapigano hayo, tarehe 24 Desemba, 2013, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuongeza askari kwenye kikosi chake kilichopo Sudan Kusini (United Nations Mission in South Sudan – UNMISS). Kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania kule Darfur, Lebanon na hasa DRC, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeiomba Tanzania kupeleka Kikosi cha Kulinda Amani Sudan ya Kusini na Serikali yetu tayari imeridhia ombi hilo. Aidha, tarehe 27 Desemba 2013, Wakuu wa Nchi wa IGAD (the Inter-Governmental Authority on Development) walifanya mkutano wa dharura mjini Nairobi, Kenya, kujadili mgogoro huo. Tarehe 30 Desemba, 2013 Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilifanya kikao mjini Banjul, Gambia, na kuunga mkono jitihada za IGAD kwa kuzitaka pande zinazohusika kuacha mapigano na kuanza mazungumzo.

Mheshimiwa Spika,  pande zinazohusika na mgogoro nchini Sudan Kusini zilianza mazungumzo mjini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 4 Januari, 2014. Kufuatia majadiliano hayo tarehe 23 Januari, 2014 pande hizo mbili zilitia saini Mkataba wa kusimamisha mapigano baada ya Serikali kukubali kuwaachia huru wafuasi 7 kati 11 wa Bwana Machar. Pande hizo mbili zilianza tena mazungumzo mwezi Februari 2014 ili kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro huo. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalikwama na kusitishwa baada ya upande wa Bw. Machar kushinikiza kuachiwa huru kwa wafuasi wanne waliobaki. 

Mheshimiwa Spika, tarehe 25 Aprili 2014, Serikali ya Sudan Kusini iliwaachia huru wafuasi wanne wa Bwana Machar waliokuwa bado wakishikiliwa na Serikali.  Kufuatia uamuzi huo wa Serikali, tarehe 9 Mei, 2014 Rais Kiir na Bwana Machar walifanya mazungumzo ya ana kwa ana, mjini Addis Ababa kwa mara ya kwanza tangu kuibuka kwa mgogoro huo na kuweka saini makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mheshimiwa Spika,   makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili zinazogombana katika kikao hicho cha Addis Ababa ni; kwanza pande zote mbili kuacha mapigano; pili, pande zote ziruhusu mashirika ya utoaji huduma za madawa, tiba na chakula kuwafikia waathirika ili kuwapa misaada hiyo; tatu, kuchuja askari ili wale watiifu wasajiliwe na kuingizwa kwenye jeshi la Taifa; nne kuunda Serikali ya Mseto na ya mpito na tano kutengeneza Katiba mpya.  Kutokana na makubaliano hayo, uchaguzi ambao ulitakiwa kufanyika mwakani 2015, sasa umeahirishwa.  Tanzania inaunga mkono makubaliano hayo.

2.3.3 Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mheshimiwa Spika, kama itakavyokumbukwa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliingia kwenye mgogoro baada ya waasi wa Kikundi cha SELEKA kufanya mapinduzi yaliyomwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bwana Francios Bozize mwezi Machi 2013. Kiongozi wa Kikundi cha SELEKA Bwana Michel Djotodia alichukua madaraka lakini uongozi wake ulishindwa kurejesha utulivu nchini humo. Hali ya usalama ilizidi kudorora zaidi mwezi Desemba 2013 baada ya kuanza kwa mapigano makali yaliyochukua sura ya udini, baina ya wanamgambo wa Kundi la SELEKA lenye wafuasi wengi wa Kiislamu na wanamgambo wa Kundi la ANTI-BALAKA lenye wafuasi wengi wa Kikristo. Mapigano hayo yalisababisha madhara makubwa nchini humo, ikiwemo idadi kubwa ya vifo vya raia na maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Mheshimiwa Spika, tangu kuibuka kwa mgogoro nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (Economic Community of the Central African States – ECCAS) na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya jitihada za kutatua mgogoro nchini humo. Umoja wa Afrika uliisimamishia uanachama nchi hiyo kwa kuwa Serikali yake iliingia madarakani kinyume cha sheria. Aidha, mwezi Julai 2013, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, ambalo Tanzania ni mjumbe, lilipitisha uamuzi wa kupelekwa Kikosi cha Afrika cha Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (Africa-led International Support Mission in the Central African Republic –MISCA) kuchukua nafasi ya vikosi vya nchi za ECCAS. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliridhia uamuzi wa kupelekwa kwa kikosi hicho chenye askari 6,000 tarehe 5 Desemba 2013, kuungana na askari wengine 1,200 wa Ufaransa waliokuwemo nchini humo. Kikosi hicho kwa sasa kinaundwa na askari kutoka Congo, Chad na Rwanda.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kulegalega kwa uongozi wa Bwana Djotodia, Wakuu wa Nchi wa ECCAS walifanya kikao nchini Chad tarehe 11 Januari, 2014. Wakati wa kikao hicho, Bwana Djotodia na Waziri wake Mkuu Bwana Nicolas Tiengaye walitangaza kujiuzulu. Tarehe 20 Januari, 2014 Bunge la Mpito la Jamhuri ya Afrika ya Kati lilimteua Bibi Catherine Samba-Panza, aliyekuwa Meya wa Mji wa Bangui, kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo hadi uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakapofanyika. Tangu kuingia madarakani kwa Serikali mpya na kuwasili kwa vikosi vya MISCA, hali ya usalama imeanza kuimarika.

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, tarehe 10 Aprili 2014, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la kuunda Kikosi cha Kulinda Amani nchini humo (UN Multilateral Integrated Stabilization Mission in Central African Republic – MINUSCA) kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi 30 Aprili, 2015 kuchukua nafasi ya MISCA. MINUSCA ambayo itakuwa na idadi ya walinda amani 12,000 inatarajiwa kuanza kazi rasmi mwezi Septemba 2014.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ikiwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha suluhu ya kudumu inapatikana nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

2.3.4 Misri
Mheshimiwa Spika, mgogoro nchini Misri umeendelea hasa baada ya Rais Mohamed Morsi kuondolewa madarakani mwezi Julai 2013 ambapo watu wengi wamepoteza maisha kutokana na mgogoro huo. Kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Afrika, Serikali yoyote inayoingia madarakani kwa nguvu na kinyume na Katiba, inapoteza uanachama wake AU na kuwekewa vikwazo.  Ni matumaini yetu kuwa baada ya uchaguzi kufanyika mwezi huu wa Mei, 2014 Misri itachukua tena nafasi yake kwenye Umoja wa Afrika, na kwamba hali ya usalama na kisiasa nchini Misri itakuwa na unafuu. Kama maoni ya magazeti na wanasiasa ni sahihi, basi Rais mpya wa Misri anategemewa kuwa Mheshimiwa Mohamed Fatah El Sisi. 

2.3.5 Libya
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama nchini Libya bado ni tete.  Baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi miaka mitatu iliyopita, na baada ya Balozi wa Marekani nchini Libya kuuawa, miaka miwili iliyopita mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya wageni na raia yanazidi kushika kasi siku hadi siku.  Hali imekuwa mbaya hadi kupelekea Waziri Mkuu kutekwa nyara na baadae kuachiliwa na Bunge kuvamiwa na kuchomwa moto. Mapigano na mauaji yanayoendelea, yanaifanya nchi ya Libya isitawalike na kusababisha ofisi nyingi za Ubalozi mjini Tripoli na Benghazi kufungwa. Tunashauri Watanzania wasiende Libya kwa sasa kutokana na hali iliyopo mpaka pale watakaposhauriwa vinginevyo.

2.3.6 Burundi
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na taarifa za hali ya kisiasa na kiusalama nchini Burundi kuwa kuna mvutano wa Viongozi wa vyama vya siasa. Hali hii inatokana na hofu kwamba Serikali iliyopo madarakani ya Rais Pierre Nkurunziza inataka kubadilisha katiba ili kumpatia Rais Nkurunziza nafasi nyingine ya kugombea Urais kwa mara ya tatu. Wanasiasa, hasa kutoka kambi ya upinzani na Viongozi wastaafu wanasema kuwa kubadili katiba kutavunja makubaliano ya Arusha ya Amani na Maelewano kwa Burundi (Arusha Peace and Reconcilliation Agreement for Burundi) na hivyo kuhatarisha Amani na usalama wa nchi hiyo.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Tanzania tunalo jukumu la kuhakikisha kuwa ndugu zetu wa Burundi hawatumbukii kwenye matatizo ya kisiasa na usalama. Tunaamini kwamba, Mheshimiwa Pierre Nkurunziza hana nia wala sababu ya kubadili katiba ili kumwezesha kuendelea kubaki madarakani. Hivi sasa, mawasiliano ya kumaliza tatizo hili yanaendelea kati ya Serikali yetu, Umoja wa Afrika na viongozi mbalimbali wa Burundi. Tunashawishika kuamini kuwa wale wote wanaoitakia mema Burundi wataisaidia katika kulimaliza tatizo hili hasa nchi za jirani zinazoizunguka.

2.3.7 Mapambano Dhidi ya Ugaidi

Mheshimiwa Spika, vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria na pia kikundi cha Al-Shabaab nchini Kenya ni vitendo vya kulaaniwa na kukomeshwa na wapenda amani wote duniani. Mauaji ya hivi karibuni ya watu wasiopungua 400 na utekaji wa wanafunzi wasichana zaidi ya 200 nchini Nigeria na vilevile mauaji ya jumla ya watu zaidi ya 100 kwa jirani zetu  Kenya ni ushaidi tosha wa kuitaka dunia kushirikiana kwa pamoja kupambana na vitendo vya kigaidi vya aina zote. Serikali yetu tayari imekwisha tuma salamu za pole tukilaani vitendo hivi na kutumia fursa hiyo kuwahakikishia wenzetu utayari wetu katika kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugaidi.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya amani na yenye utulivu mkubwa. Pamoja na tofauti zetu, tusikubali wala kushawishika kuzimaliza tofauti zetu kwa njia za kigaidi. Tuendelee na tabia ya kukosoana na kumaliza tofauti zetu kwa mazungumzo na njia zinazokubalika kisheria. Tuwe macho na watu wote wasioitakia mema nchi yetu.
 

3.     MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA MASUALA MUHIMU SADC NA UKANDA WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU

3.1.         Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kulinda amani, usalama na demokrasia kwenye nchi za Afrika. Kutokana na msimamo huo, Tanzania imechangia kikosi kimoja cha askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwenye Force Intervention Brigade (FIB) iliyoko chini ya kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini DRC (MONUSCO). FIB inaongozwa na kamanda Mtanzania, Brig Gen. James Alois Mwakibolwa, kwa ajili ya kupambana na waasi ndani ya DRC. Ninafurahi kutamka kwamba askari wetu kwa kushirikiana na majeshi ya DRC na MONUSCO walifanya kazi nzuri na kukisambaratisha kabisa kikundi cha waasi wa M23 ambao wamekuwa wakivuruga amani kwa muda mrefu mashariki mwa DRC na kupelekea kupatikana kwa amani ambayo ilikuwa imepotea kwa muda mrefu.


  
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika sanjari  na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 30 Januari, 2014, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilitoa taarifa kuhusu hali ya usalama inavyoendelea nchini humo baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Serikali na kikundi cha M23.

Mheshimiwa Spika, mwakilishi wa DRC alieleza kuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, hivi sasa Serikali yake imejielekeza katika kuvisambaratisha vikundi vya kijeshi vilivyosalia nchini humo ikianza na ADF-Nalu na baadaye FDLR. Mwakilishi huyo pia alieleza kuwa Bunge la nchi hiyo lilikuwa kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya msamaha (amnesty law) ambayo itafafanua ni waasi gani watanufaika nayo na wale ambao hawataweza kunufaika na sheria hiyo. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, sheria hiyo imekwishapitishwa tangu tarehe 5 Februari 2014. Kwa mujibu wa sheria hiyo, walioshiriki katika makosa ya kimbari, makosa ya kivita na jinai dhidi ya ubinadamu (genocide, war crimes and crimes against humanity) hawatanufaika nayo.

3.2.         Malawi
Mheshimiwa Spika, mazungumzo ya usuluhishi wa mgogoro wa mpaka kati yetu na Malawi bado yanaendelea.  Tarehe 20 na 21 Machi, 2014 tuliitwa Malawi kwenye jopo la usuluhishi lililopo chini ya uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.  Wengine ni Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na Rais Mstaafu wa Botswana Festus Mogae.  Pamoja nao kulikuwa na kikosi cha wanasheria sita waliobobea kwenye migogoro ya mipaka duniani.

Baada ya mjadala mkubwa uliotoa fursa kwa kila upande kuwasilisha hoja zake za kisheria mbele ya Jopo, Jopo lilishauri kuwa hoja za kisheria tuziweke pembeni kwa muda na badala yake kila upande uainishe hoja zisizo za kisheria.  Tulitakiwa tujadili hoja zinazogusa maisha ya kila siku ya kijamii.  Kwa mfano, Malawi wanatakiwa kueleza hasara watakazozipata endapo itaamriwa kuwa mpaka utapita katikati.  Na Tanzania tunatakiwa kueleza hasara tutakazozipata endapo itaamriwa kuwa mpaka utapita kwenye ufukwe wa Ziwa.

Mheshimiwa Spika, timu ya Tanzania ambayo inajumuisha Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara yangu sasa inaandaa majibu.  Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Anna Tibaijuka (Mb.) na Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika kujenga hoja nzito na zenye ushawishi wa kuuweka mpaka katikati ya Ziwa na siyo ufukweni. Na huo ndio msimamo wa Tanzania.  Aidha, kwa kuwa sasa Serikali mpya ya Malawi imechaguliwa na kuundwa, Jopo la usuluhishi litaitisha kikao cha pili ili kuendelea na shughuli za usuluhishi. Niwashukuru pia Mheshimiwa John Komba, Mbunge wa Mbinga na Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa ambapo waliambatana nasi na kutoa mchango wa hoja nzito kwa niaba ya wananchi wanaolizunguka Ziwa Nyasa.

3.3.         Zimbabwe
Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa nchini Zimbabwe kwa sasa ni shwari. Zimbabwe ilifanya Uchaguzi wake Mkuu wa Rais tarehe 31 Julai, 2013. Kabla ya uchaguzi huo, Zimbabwe ilifanya mchakato wa kutengeneza Katiba mpya kwa mafanikio makubwa. Tanzania ilishiriki katika uangalizi wa shughuli zote mbili kupitia timu ya uangalizi ya SADC ambayo niliiongoza mimi mwenyewe. Wananchi wa Zimbabwe walitumia nafasi yao ya kidemokrasia katika kuchagua viongozi wao na vyama walivyopenda kwa uhuru na haki. Katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Robert G. Mugabe aliibuka mshindi wa Urais kwa kipindi cha miaka mitano kwa kupata asilimia 61.09 ya kura zote. Aidha, timu ya uangalizi ya SADC iliridhika na maandalizi yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi katika mchakato mzima wa uchaguzi nchini Zimbabwe kwa mwaka 2013 na kwamba ulikuwa huru na wa amani.
3.4.         Madagascar
Mheshimiwa Spika, baada ya jitihada za SADC za kuandaa mazingira ya uchaguzi kufanyika Madagascar, na baada ya kufanikisha zoezi la kuwaomba viongozi wa zamani; Ravanomanana, Rajoelina, Rasiraka na Mama Ravaromanana kutogombea kwa sababu za kiusalama, wananchi wa Madagascar hatimaye walipiga kura tarehe 25 Oktoba, 2013 na kurudia Desemba 2013 ambapo Henry Martial Rakotoarimanana Rajaonarimampianina alichaguliwa kuwa Rais mpya wa Madagascar.  Hali ya kisiasa nchini Madagascar kwa ujumla ni shwari ingawa kuna kutoelewana kati ya Rais aliyeondoka Rajoelina na Rais wa sasa baada ya Rais mpya kukataa pendekezo la Rais Rajoelina la kutaka ateuliwe kuwa Waziri Mkuu.

 Mheshimiwa Spika, kufuatia ushindi huo, Wakuu wa Nchi wanachama wa SADC walikubaliana kwa kauli moja kuiondolea vikwazo nchi ya Madagascar na hivyo kuikaribisha rasmi kushiriki katika shughuli za SADC, ikiwemo kuhudhuria vikao vyote kama mwanachama halali. Kufuatia hatua hiyo Rais Rajaonarimampianina pia alikaribishwa rasmi kujumuika na kukalia kiti cha Madagascar katika mikutano ya Umoja wa Afrika (AU). Tuendelee kuwaombea amani ya kudumu wananchi wa Madagascar ili waweze kuijenga nchi yao.

4.     UTEKELEZAJI WA DIPLOMASIA YA UCHUMI

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara, Idara na Taasisi nyingine imeendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kuvutia wawekezaji wenye vigezo na sifa kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini. Mikakati inayotumika ni pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya ndani ya Kukuza Uchumi; Kuimarisha Ubia wa Kimataifa; Kuweka mbele Malengo ya Uchumi katika Ushirikiano Kati ya Nchi Mbili (Bilateral Cooperation); Kuimarisha Uhusiano wa Kimataifa (Multilateral Cooperation); kukuza ujirani mwema; na kukuza Ushirikiano wa Kikanda. Masuala haya yanatekelezwa kupitia ushiriki wetu kwenye Mikutano mbalimbali (Tume za Pamoja za Ushirikiano  na mikutano mingine ya nchi na nchi na ile ya Kikanda na Kimataifa); Ziara za Viongozi wa Kitaifa Nje ya Nchi; ziara za Viongozi wa Mataifa ya Nje hapa nchini; na ofisi za uwakilishi nje ya nchi.


Mheshimiwa Spika, kwa ufupi kabisa napenda kuelezea baadhi ya mafanikio tuliyoyapata kwenye sekta mbalimbali ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi:-

4.1.         Sekta ya Kilimo
Mheshimiwa Spika, mwaka jana nililiarifu Bunge lako tukufu  kuhusu mafanikio tuliyoyapata katika kutafuta masoko ya bidhaa zetu za kilimo kwenye soko kubwa la China. Mafanikio hayo ni pamoja na kuingia Mikataba, Makubaliano na Itifaki mbalimbali na Mamlaka pekee ya China inayoruhusu biashara za namna hiyo (Administration of Quality Supervision, Inspection and Quarantine – AQSIQ) ambayo imeruhusu Tanzania kuingiza zao la tumbaku nchini China. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hivi sasa Mamlaka hiyo imeruhusu pia mazao ya baharini kuingia nchini China. Makubaliano hayo yaliwekwa saini mbele ya Mawaziri Wakuu Mhe. Li Keqiang na Mhe. Mizengo Pinda wakati wa ziara ya Mhe. Waziri Mkuu nchini China mwezi Oktoba 2013.  Hii ni fursa adhimu kwa wavuvi wetu kupata soko la uhakika la bidhaa zao.

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuliwezesha zao la pamba kupata soko nchini China umefikia hatua nzuri, ambapo Mkoa wa Shinyanga na kampuni ya Dahong ya Jimbo la Jiangsu zimeingia Mkataba wa kuendeleza zao la pamba mkoani humo na kuuza katika viwanda vya Dahong, China. Mkataba huo unajulikana kwa jina la “Agreement On China-Tanzania Modern Agro-Industrial Zone” na ni mmoja kati ya mikataba mitano (5) iliyowekwa saini Oktoba 17, 2013 mbele ya Mawaziri Wakuu Mizengo Pinda na Li Keqiang mjini Beijing.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania Beijing, inafuatilia kwa karibu uingiaji wa Makubaliano na Serikali ya China yatakayoiwezesha Tanzania kuingiza China zao la muhogo kwa ajili ya matumizi ya viwandani ambako wanga wake unahitajika sana.  Mchakato huo upo katika hatua nzuri baada ya AQSIQ kutoa taarifa kwamba imeridhika na hoja za mapendekezo yetu na hivyo, Wizara inaendelea kufuatilia ujio wa timu ya wataalam wa AQSIQ nchini kujiridhisha kuhusu utoshelevu na ubora wa viwango vya zao hilo ili kukidhi mahitaji ya soko la China.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeziomba mamlaka za kilimo nchini kuanzisha michakato kama hiyo kwa mazao ya korosho, kahawa, ufuta, karanga, ngozi n.k, ili yaweze kuingia katika soko la China.  Uzoefu unaonesha kwamba bila kuwa na mikataba au makubaliano ya namna hiyo mazao yetu yatakumbana na vikwazo kuingia katika soko hilo. 

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano kati ya Nchi za Afrika na nchi za Kiarabu uliofanyika nchini Kuwait mwezi Novemba 2013, Serikali ya Kuwait iliahidi kutoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni moja kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano   kwa ajili ya mikopo nafuu kwa nchi za Afrika, hususan katika sekta ya kilimo.  Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Tume za Mipango za Tanzania Bara na Zanzibar imekwishawasilisha miradi kadhaa ya umwagiliaji na maendeleo ya jamii. 

Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huo, Serikali ya Saudi Arabia ilitenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni nne kwa lengo la kukuza uzalishaji na usalama wa chakula. Ili kuchangamkia fursa hiyo, Wizara yangu imekamilisha majadiliano ya kuingia Mkataba wa Ushirikiano na Saudi Arabia utakaowezesha nchi yetu kunufaika na fursa hiyo.  Ninatarajia kusaini Mkataba huo wakati wowote kabla ya mwisho wa Mwaka huu wa fedha. 

Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ametoa mchango mkubwa kwenye sekta ya kilimo. Msisitizo umekuwa katika masuala yanayohusu usalama wa chakula na majaribio ya kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo kwa lengo la kuwaongezea kipato wananchi na kukuza uchumi wa nchi. Kwa kutambua mchango wa Mheshimiwa Rais, mwezi Septemba 2013, Chuo Kikuu cha Guelph cha nchini Canada, kilimtunukia Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honorary Doctorate) ya Sheria. Mheshimiwa Rais amekuwa Mtanzania wa kwanza kutunukiwa shahada hiyo katika historia ya zaidi ya miaka 100 ya Chuo hicho maarufu kwa utafiti wa kilimo na magonjwa ya wanyama.  Mchango huo wa Mheshimiwa Rais ambao umetambuliwa na Chuo cha Guelph unatoa fursa kwa taasisi na vyuo vyetu vinavyojihusisha na kilimo kuwa na ushirikiano wa karibu na chuo hicho katika kufanya tafiti mbalimbali na kuendeleza sekta ya kilimo. 

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ukweli kwamba asilimia kubwa ya watanzania wanategemea kilimo na wanakabiliwa na changamoto ya umasikini wa kipato, serikali imefanya jitihada kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa ni moja ya nchi za majaribio ya mpango wa kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za kifedha (Inclusive Financing for Development) hususan wasioweza kumudu masharti ya kibenki.

Katika kufanikisha juhudi hizo, Wizara yangu iliratibu kwa mafanikio makubwa ziara ya Malkia Maxima wa Uholanzi aliyetembelea Tanzania kuanzia tarehe 11 hadi 13 Desemba 2013 akiwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Inclusive Financing for Development.  Malkia Maxima alifuatana na wakuu wa Mashirika Matatu ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia kilimo na chakula ambayo ni FAO, IFAD na WFP kuja kujionea maendeleo ya miradi iliyo chini ya mpango huo hapa nchini. Mpango huu umekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wadogo katika kupunguza umasikini na kuongeza usalama wa chakula.

4.2.         Sekta ya Nishati
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha uliopita Wizara yangu ikitambua umuhimu wa nishati katika maendeleo ya Taifa letu, ilifanya juhudi katika kutafuta uwekezaji katika sekta hiyo. Mwaka huu tumeendelea kupata fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpango mpya wa ushirikiano na Serikali ya Marekani kwenye uzalishaji umeme barani Afrika uitwao “Power Africa Initiative” uliozinduliwa hapa nchini tarehe 2 Julai 2013 na Rais Barack Obama wa Marekani pamoja na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania.  Tanzania ni miongoni mwa nchi sita barani Afrika zinazonufaika na Mpango huo. Nchi nyingine ni Kenya, Ethiopia, Msumbiji, Ghana na Nigeria. Katika mpango huo, Serikali ya Marekani imetenga kiasi cha Dola za Marekani bilioni saba wakati sekta binafsi nchini humo imeahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni tisa za kufanikisha utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuiandaa vyema nchi yetu kunufaika na nishati ya gesi iliyogundulika kwa wingi hivi karibuni, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini imeanza kutafuta fursa za kujifunza uzoefu wa wenzetu waliobahatika kuwa na nishati hiyo na kupata mafanikio makubwa ili nasi tuweze kuingia katika uchumi wa gesi na mafuta bila matatizo. 

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Balozi zake imeratibu ziara za mafunzo nchini India, Japan, Malaysia, Canada, Algeria, Oman, Australia na Qatar.  Aidha, tumeendelea kutafuta fursa mbalimbali za masomo kwa ajili ya wataalam katika sekta ya mafuta na gesi.  Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa matunda ya juhudi hizo yameshaanza kupatikana. Tayari nchi za Thailand, Australia, China na Canada zimetoa nafasi za masomo kwa wataalam wetu. Tunaendelea kutafuta fursa zaidi katika nchi zingine. 

Mheshimiwa Spika, juhudi zetu za kutafuta fursa za uwekezaji katika sekta ya Nishati zimewezesha nchi yetu kuingia makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na nchi ya Algeria ambapo miradi mbalimbali katika masuala ya gesi na umeme itatekelezwa. Kwa kuanzia tumekubaliana kuanzisha kwa pamoja migodi ya Phosphate kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea kwa matumizi ya ndani na kuuza nje.  Pia tumekubaliana kuanzisha Kampuni ya pamoja ya kusambaza umeme na kujenga kiwanda cha kusindika gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.  Kutekelezwa kwa miradi hiyo sio tu kutatoa ajira kwa wananchi wengi katika sekta ya huduma, lakini pia kutalipatia taifa fedha za kigeni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, aliyoifanya nchini Singapore mwezi Juni 2013, alikutana na viongozi wa Makampuni Makubwa ya Biashara. Kufuatia mkutano huo, Kampuni ya Pavillion Energy ya nchini Singapore imekubali kuwekeza katika sekta ya gesi nchini ambapo kwa kuanzia imenunua asilimia 20 ya hisa za Kampuni ya Ophir Gas kwa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.3.

4.3.         Sekta ya Biashara
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sekta ya biashara, Wizara yangu imeendelea kutafuta fursa mbalimbali za biashara kwa watanzania nje ya nchi na pia masoko kwa bidhaa zetu nje ya nchi.  Balozi zetu zote duniani zimeendelea kuwezesha upatikanaji wa taarifa juu ya maonesho ya biashara, masoko ya bidhaa na fursa za uwekezaji.  Mwaka huu Kampuni ya Dragon Mart ya Dubai imeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kushirikiana na TANTRADE.  Lengo la ushirikiano huo ni kujenga eneo la kisasa la maonesho ya kimataifa ya biashara nchini ambalo litakuwa linafanya maonesho ya biashara kwa kipindi cha mwaka mzima.  Kwa wale waliobahatika kufika katika jiji la Dubai na kutembelea Dragon City, hivyo ndivyo itakavyokuwa hapa, pale mpango huo wa kuanzisha eneo hilo hapa Tanzania utakapofanikiwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Shirika la Emirates, limekubali kuanzisha safari za ndege za Shirika lake lingine la FlyDubai kutoka Dubai kwenda Kilimanjaro, Dar es Salaam na Zanzibar. FlyDubai ni shirika lenye bei nafuu kwa wateja (budget airline), kwani mara nyingi nauli zake zinakuwa nusu ya nauli ya ndege nyingine ikiwamo Emirates. Huduma hii italeta unafuu mkubwa hasa kwa wafanyabiashara wetu wanaofanya shughuli zao kati ya Tanzania na Dubai au maeneo mengine kupitia Dubai.

4.4.         Sekta ya Utalii
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukuza utalii Serikali kupitia Ubalozi wetu wa Washington Marekani imefungua Ofisi tisa za Uwakilishi wa Heshima (Honorary Consulates) sehemu mbalimbali nchini Marekani. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka Taifa hilo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba soko kubwa la utalii duniani lipo China.  Wizara yangu kupitia Ubalozi wake nchini China imeanza mazungumzo na mamlaka za Utalii za China kuhusu utangazaji wa vivutio vya utalii vya Tanzania.  Aidha, wakati wa Ziara ya Waziri Mkuu nchini China mwezi Oktoba 2013, kampuni kubwa ya Usafirishaji wa Watalii ya Hong Kong Travels iliahidi kusafirisha watalii wapatao 10,000 kila mwaka kutembelea Tanzania. Kampuni hiyo imekubali ombi la Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja kuwekeza katika ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya Nyota Tano katika maeneo ya karibu na Mbuga za Wanyama kwa ajili ya kulaza watalii. 

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2013/2014, Wizara katika juhudi zake za kukuza utalii iliratibu kwa ushirikiano na TANAPA kongamano la vijana wa Tanzania na Saudi Arabia kuhusu Bio-Anuai lililofanyika mkoani Arusha mwezi Januari, 2014. Kongamano hilo lilisaidia sana kukuza diplomasia ya uchumi hasa kwenye kuwavutia watalii kutoka Saudi Arabia na wananchi wengine wa Nchi za Ghuba kuijua Tanzania.  Tayari misafara zaidi ya mitatu inayowahusisha wanafamilia za kifalme wa Nchi za Gulf Cooperation Council imefanya ziara nchini Tanzania ikifuata mfano wa vijana hao wa Saudi Arabia.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa katika ziara nchini China alifanya mazungumzo na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Ndege ya Hainan na South China Airlines ili kuwavutia waanzishe safari za moja kwa moja kutoka China kuja nchini ili kurahisisha usafiri wa watalii wanaotaka kuja nchini. Makampuni hayo yamekubali kutuma wataalam wake kuja nchini kufanya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika, mnamo tarehe 25 Machi, 2014, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mhe. Frank-Walter-Steinmeier, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani aliyewasili nchini na ujumbe wa watu 80 wakiwemo wafanyabiashara kutoka makampuni makubwa ya Ujerumani, Wabunge, watendaji wa Serikali na Waandishi wa Habari. Lengo la ziara yake lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Ujerumani hususan katika nyanja za utalii, biashara na uwekezaji. Kama sehemu ya mafanikio ya ziara hiyo, Mhe Steinmeier alimkabidhi Waziri wa Maliasili na Utalii, ndege ndogo kwa ajili ya kukabiliana na uwindaji haramu wa wanyamapori.

4.5.         Sekta ya Miundombinu na Uchukuzi
Mheshimiwa Spika, Ubalozi wetu Abu Dhabi kupitia Ubalozi Mdogo wa Dubai kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ulifanya vikao kadhaa na wamiliki wa mashirika makubwa ya ujenzi wa majengo ya biashara na ya makazi ambapo walifanikiwa kuwapata wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo. Mashirika yaliyokubali kuja kuwekeza Tanzania ni:- DAMAC, AL GHURAIR, SOBHA na NAKHIL. Mashirika hayo ndiyo yaliyojenga majengo makubwa na mashuhuri yanayoonekana katika Jiji la Dubai. Kampuni ya DAMAC ipo tayari kuwekeza kwenye eneo la ufukwe wa bahari, Kawe Dar es Salaam lisilopungua ukubwa wa ekari 1000, kwa kujenga Hoteli za Nyota 5, nyumba za kuishi (Villas) na uwanja wa kisasa wa Golf (golf course). Aidha, kwa kutambua fursa hiyo Ubalozi umeandaa mkutano wa wawekezaji wa Dubai na Tanzania tarehe 11 Juni, 2014, katika Hoteli ya Jumeirah Emirates Tower, Jijini Dubai. Shirika la NHC, ndio wanaoratibu ushiriki wa wawekezaji kutoka Tanzania. Tunawapongeza na kuwaahidi ushirikiano wetu.

4.6.         Sekta ya Ajira
Mheshimiwa Spika, baada ya mji wa Dubai kushinda kinyang’anyiro cha kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Biashara ya Dunia ya 2020 (World Expo 2020), ni wazi fursa nyingi zitapatikana kupitia maonesho hayo, hasa tukitilia maanani uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati yetu na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E).  Kati ya fursa hizo, ni pamoja na nafasi za ajira milioni mbili na laki nane ambazo serikali ya UAE itahitaji kuzijaza kwa ajili hiyo. Kwa kutambua fursa hiyo, Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wetu wa U.A.E tumejipanga kikamilifu ili kuchangamkia fursa hizo.
Mheshimiwa Spika, tayari Ubalozi umekutana na Shirika la Emirates (Emirates Group) ambalo ndio mmiliki wa Shirika la ndege la Emirates, Dnata, na FlyDubai, na kuweka mikakati ya kuongeza ajira kwa watanzania katika mashirika yote yaliyo chini ya Emirates. Shirika la Emirates limekubali kuajiri wafanyakazi kutoka Tanzania katika kada za wahudumu wa ndege (cabin crews), mafundi (technicians), maafisa mipango (planning assistants), watoa huduma kwa wateja na masuala ya tiketi (customer care and ticketing). Napenda kuwasihi watanzania wote wenye sifa zitakazotakiwa, waombe nafasi hizi kwa wingi mara zitakapotangazwa rasmi.

4.7.         Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPC)
Mheshimiwa Spika, katika kuratibu shughuli za Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPC), Wizara imeendelea kufanya vikao vya wadau wa ndani na nje ya nchi ili kutekeleza shughuli hizo.  Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara kwa kushirikiana na wadau kutoka Wizara nyingine, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi iliandaa awamu ya nane ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na India uliofanyika katika Hoteli ya Kilimanjaro, Hyatt tarehe 8 hadi 9 Julai, 2013. Maazimio ya Mkutano huo yalitiwa saini na mimi mwenyewe na Mhe. Prabeet Kaur, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa India. Maazimio ya Mkutano huo yanalenga katika kuweka maeneo ya ushirikiano wa Tanzania na India kwa kipindi cha miaka mitatu. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu shughuli na utekelezaji wa makubaliano ya JPCs mbalimbali ambazo nchi yetu imefikia makubaliano, hususan Algeria, Botswana, Kenya, Msumbiji, Rwanda na Zambia.

Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kutekeleza sehemu  ya majukumu yaliyotajwa hapo juu kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa, kikanda, kimataifa pamoja na sekta binafsi. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Australia, Brazil, Canada, China, Cuba, Finland, India, Italia, Ireland, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Malaysia, Marekani, Norway, Oman, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ureno, Urusi, Uswisi, Uturuki, Umoja wa Ulaya, FAO, IAEA, ILO, IMF, IOM, UNDP, UNEP, UN-HABITAT, UNWTO, UNHCR, UNICEF, UNFPA,  UNESCO, UNIDO, WHO World Bank na WWF kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi.


4.8.         Ziara za Viongozi wa Kitaifa Nje ya Nchi

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ndiyo msimamizi mkuu wa masuala ya Itifaki ya nchi. Katika kutekeleza jukumu hilo Wizara imeendelea kutoa huduma ya Itifaki kwenye sherehe zote na maadhimisho ya Kitaifa; kuratibu safari za Viongozi wa Kitaifa walipokwenda nje ya nchi; na kuratibu  mapokezi ya Viongozi wa Nje waliotembelea Tanzania. Wizara imeandaa na kuratibu ziara za kikazi za Viongozi wa Kitaifa katika nchi za:- Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika Kusini, Malawi, Namibia, Kenya, Uganda, Oman, Marekani, Canada, Ethiopia, Uingereza, Sri Lanka, Poland, Kuwait, Ufaransa, Falme za Kiarabu, India, Uholanzi na China.

Mheshimiwa Spika, ziara hizo zimefungua milango mipya ya ushirikiano kati ya nchi yetu na nchi hizo, kati ya wananchi wa nchi zetu na kati ya sekta binafsi kutoka pande zote. Aidha, ziara hizo pia zimechochea na kukuza biashara na kuimarisha mahusiano. Nitapata muda baadae mchana wa kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu jambo hili ambalo kila mara limekuwa linazua maswali.

4.9.         Ziara za Viongozi wa Nchi na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa Nchini
Mheshimiwa Spika,  kwa upande wa Viongozi wa Kimataifa kutoka nje ya nchi, Wizara iliandaa na kuratibu ziara za kikazi za Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi za; Marekani, Thailand, Burundi, Finland, Sweden, Uholanzi, Benin na Comoro.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara imehusika kikamilifu katika kuandaa na kuratibu ushiriki wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali na Mashirika ya Kikanda na Kimataifa kutoka nchi mbalimbali katika sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika, tarehe 09 Desemba, 2013, sherehe za maadhimisho miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar tarehe 12 Januari 2014 na maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sherehe ambazo zilizofanyika tarehe 26 Aprili, 2014.

5.     KUSIMAMIA MIKATABA NA MAKUBALIANO YA KIMATAIFA

5.1 Mikataba ya Kimataifa
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu la kusimamia Mikataba na Makubaliano baina ya Tanzania, nchi nyingine na Taasisi mbalimbali za Kimataifa, Wizara iliratibu na kusimamia uwekwaji saini wa Mikataba kati ya Tanzania na Nchi Nyingine (Bilateral Agreements) kama ifuatavyo:-
                                            i.            Mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Thailand  kuhusu kuanzisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi, 30 Julai 2013;
                                          ii.            Mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Thailand kuhusu Ushirikiano katika Utunzaji wa Wanyamapori, 31 Julai, 2013;
                                        iii.            Mkataba kati ya Tanzania na Thailand kuhusu kubadilishana wafungwa, 30 Julai, 2013;
                                        iv.            Mkataba kati ya Tanzania na Thailand kuhusu kulinda Uwekezaji, 30 Julai 2013;
                                          v.            Makubaliano (MoU) ya kuongeza muda wa matumizi ya Hati ya Makubaliano kati ya Wizara ya Nishati na Madini na Chuo cha Gem and Jewelery cha Thailand, 30 Julai 2013;
                                        vi.            Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ya Tanzania na Taasisi ya Clinton Foundation kuhusu ushirikiano katika masuala ya Kilimo, Agosti 2013;
                                      vii.            Mkataba wa Kimataifa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Nchi ya Kuwait kwa ajili ya Kukuza na Kulinda Uwekezaji, 17 Novemba, 2013;
                                    viii.            Mkataba kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Nchi ya Kuwait wa kushirikiana katika Sekta ya Utalii, 17 Novemba, 2013;
                                        ix.            Mkataba wa Wenyeji wa Mahakama ya Kimataifa iliyorithi shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa, 26 Novemba, 2013;
                                          x.            Hati za Makubaliano (Memoranda of understanding) baina ya Tanzania na Brazil, Iceland, Yemen, Seychelles, Swaziland, Zimbabwe, Qatar na Saudi Arabia katika Sekta ya Usafiri wa Anga, Desemba 2013;
                                        xi.            Mkataba wa Nyongeza kwenye Mkataba wa Uenyeji baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Kimataifa (MICT),  iliyorithi shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Februari, 2014;
                                      xii.            Mkataba kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kuhusu Mapambano dhidi ya Uharamia, Aprili 2014; na
                                    xiii.            Mkataba kati ya Tanzania na Kosovo kuhusu kuanzisha Mahusiano ya Kidiplomasia, Aprili 2014.
Mheshimiwa Spika, mikataba hii itasimamiwa na kutekelezwa na kila sekta husika. Wizara yangu itaendelea na jukumu la kuratibu uwekaji saini na kufuatilia utekelezaji wa mikataba na makubaliano mbalimbali baina ya nchi yetu na nchi nyingine pamoja na mashirika ya kimataifa.


6.     USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA JUMUIYA ZA KIMATAIFA, BARA LA AFRIKA NA KIKANDA

6.1.         USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu, japo kwa ufupi, mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushiriki wetu kwenye mikutano ya kimataifa na katika jumuiya mbalimbali ambazo nchi yetu ni mwanachama.

6.1.1.  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA);
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa nchi yetu kwenye Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), uliofanyika New York, Marekani kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba 2013. Katika Mkutano huo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na suala la ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ambapo Malengo ya Maendeleo ya Milenia tunayoyatekeleza sasa yatafikia ukomo. Katika kujadili ajenda hiyo, mjadala uligusa pia suala la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo kimkakati ndiyo yanaandaliwa kuchukua nafasi ya Malengo ya Milenia ifikapo 2015.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huo, Tanzania ilipata fursa ya kuelezea ulimwengu jitihada zake kwenye maeneo mbalimbali ya kukuza uchumi, kuendeleza kilimo, lishe na usalama wa chakula; utatuzi wa migogoro; na ushiriki wa nchi kwenye ulinzi wa amani kupitia Umoja wa Mataifa. Vilevile, Tanzania iliendeleza jitihada zake za kusimamia ukombozi duniani kuzitaka nchi zote zinazotawaliwa ikiwemo Palestina na Saharawi kupatiwa uhuru wake.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, Mheshimiwa Rais alishiriki kwenye Mikutano ya pembeni ya nchi na nchi na mingine ukiwemo Mkutano wa Kupambana na Ujangili kwenye mbuga za wanyama unaotishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama kama vile tembo na faru. Mheshimiwa Rais alitumia mkutano huo kuelezea ulimwengu jitihada zinazotumiwa na Serikali kupambana na ujangili, pia alitumia fursa hiyo kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuweka nguvu za pamoja katika kupambana na ujangili.  Matokeo ya mkutano huo ni kuanza kupatikana kwa misaada ya vifaa kwa ajili ya kupambana na ujangili kutoka Marekani, Ujerumani na Uingereza.

6.1.2    Kikundi Kazi cha kuandaa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mjumbe wa kikundi kazi cha nchi 30 kilichoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufanya majadiliano ya kuanzishwa kwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) yanayotarajiwa kurithi malengo ya maendeleo ya milenia baada ya muda wake kumalizika mwaka 2015. Kuanzia Machi 2013 hadi sasa imeshafanyika mikutano 11 ya majadiliano hayo na Wizara imekuwa ikishiriki kikamilifu ili kuona kwamba taifa haliachwi nje ya mchakato na maslahi ya nchi yanapata nafasi katika malengo ya maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wadau wote wanashirikishwa kikamilifu kwenye mchakato huo zikiwemo taasisi za serikali na zisizo za serikali, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango tayari imeshafanya makongamano manne; mawili Zanzibar na mawili Tanzania Bara. Makongamano haya yameshirikisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu Zanzibar na Tanzania Bara; Wakurugenzi wa Sera na Mipango, Zanzibar na Tanzania Bara; na taasisi mbalimbali zisizo za serikali kwa pande zote mbili. Lengo la makongamano hayo ni kuelezea kwa kina maendeleo ya mchakato huo na kupokea maoni na ushauri wa taasisi hizo kuhusu majadiliano hayo

6.1.3    Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 19)
Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 19) ulifanyika Warsaw, Poland tarehe 11 - 22 Novemba 2013. Pamoja na ujumbe wa Tanzania kushiriki kama nchi, Mheshimwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwawakilisha Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa  Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi  (CAHOSCC). Akiwa Warsaw, Mheshimiwa Rais alifanya kikao na Mawaziri wa Mazingira na “negotiators” wa Afrika na kuweka msimamo wa pamoja wa namna ya kuhakikisha maslahi ya Afrika yanalindwa kwenye mkutano huo na mingine ya mabadiliko ya Tabianchi. Mheshimiwa Rais alisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwenye masuala ya upatikanaji wa fedha, teknolojia na kuijengea Afrika uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la upatikanaji wa fedha, nchi tajiri na zenye viwanda duniani ziliahidi kuchangia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 100 kila mwaka hadi mwaka 2020. Kiasi hiki cha fedha kitasaidia nchi maskini kwenye masuala ya adaptation na mitigation.

6.1.4    Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara Haramu ya Wanyamapori
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa nchi kwenye Mkutano wa Kimataifa kuhusu Biashara Haramu ya Wanyamapori (London Conference on illegal Wildlife Trade) uliofanyika London, Uingereza, tarehe 12 na 13 Februari 2014. Mkutano huu uliikutanisha Jumuiya ya Kimataifa kwa lengo la kujadili na kutafuta mbinu za kupambana na hatimaye kutokomeza kabisa biashara haramu ya pembe za Ndovu na Faru. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika sana na biashara hii na Serikali imeendelea kupambana vikali na vitendo vya kijangili vinavyosabisha biashara hiyo haramu.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipata fursa ya kuifahamisha Jumuiya ya Kimataifa kuhusu juhudi na hatua ambazo Serikali ya Tanzania inachukua kutokomeza tatizo hili. Aidha, Mheshimiwa Rais alitumia jukwaa hilo kusisitiza umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa soko la bidhaa hizi linatokomezwa kabisa hasa kwenye nchi za Asia ambako ndiko kuna soko kubwa.

Mheshimiwa Spika, mkutano ulikubaliana pamoja na masuala mengine, kuongeza ushirikiano kati ya mataifa katika kudhibiti biashara hiyo; kupiga marufuku biashara hiyo bila kutoa ahueni kama ilivyokuwa inafanyika awali; kuhakikisha kuwa nchi zinapitisha sheria kali dhidi ya ujangili na kuhakikisha kuwa meno yaliyohifadhiwa sasa hivi yanakosa soko.

6.1.5    Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF)
Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa nchi kwenye Mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) uliofanyika Davos, Uswisi, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Februari 2014. Kupitia Jukwaa hili, Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji hasa katika sekta ya kilimo kupitia mpango wa “Grow African Partinership”. Aidha, katika mkutano huo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bodi ya Chai na Tanzania Smallholder Tea Development Agency ilisaini makubaliano na Kampuni ya Unilever. Makubaliano hayo ni baada ya Kampuni hiyo kuonesha nia ya kuwekeza kwenye kilimo cha Chai kupitia SAGCOT. Inatarajiwa kuwa uwekezaji huu utainua uzalishaji wa chai mara tatu zaidi ya kiwango kinachozalishwa sasa na kuingiza wastani wa Euro Milioni 110. Hatua hii itasaidia kuongeza mapato kutokana na bidhaa zitakazosafirishwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeingia makubaliano (MoU) na WEF katika maeneo ya uendelezaji wa miundombinu na usimamizi wa Maji. Makubaliano hayo yamefanyika baina ya Serikali kupitia Wizara ya Maji na “Water Resources Group Partnership” ya WEF. Makubaliano hayo yatasaidia kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya Maji na hivyo kuhakikisha usimamizi endelevu wa maji kwa maendeleo. Aidha, Makubaliano hayo yamejikita katika kuboresha huduma ya maji katika maeneo matatu ambayo ni upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi yote ya viwanda na majumbani; usimamizi wa maji taka; na umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo Serikali imenufaika kupitia Mkutano huo ni kwenye sekta ya miundombinu. Serikali iliingia mkataba na WEF chini ya mpango wa “Africa Strategic Infrastructure Initiative” wenye madhumuni ya kuvutia wawekezaji kwenye miundombinu na hivyo kuleta manufaa kwa uchumi (Infrastructure with larger multiplier effect). Mpango huu ambao pia unahusisha Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) umeichagua Bandari ya Dar es salaam kuwa sehemu ya miradi yake ya awali. Tayari AfDB ilituma timu yake nchini kufanya tathmini ya awali ya mradi wa upanuzi wa Bandari hiyo.
6.1.6.  Jumuiya ya Madola
Mheshimiwa Spika, Tanzania ilichaguliwa tena na Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola kuendelea kuwa mjumbe wa Kikundi Kazi cha Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG). Mawaziri wanaounda CMAG walinipendekeza na kunichagua kwa nafasi yangu kama Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa CMAG kwa mwaka 2013 - 2015. Kuchaguliwa kwangu ni mafanikio kwa Diplomasia ya nchi na kumedhihirisha jinsi nchi inavyoheshimika kwenye Jumuiya ya Kimataifa, ikizingatiwa kuwa CMAG ni chombo maalum na chenye hadhi ya kipekee kwenye muundo wa Jumuiya ya Madola kinachosimamia kanuni na taratibu za Jumuiya hiyo kwa nchi wanachama.
6.1.7    Diplomasia ya Michezo
Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Madola itakuwa na mashindano ya Olimpiki huko Glasgow, Uingereza mwezi Julai mwaka huu.  Katika mashindano hayo, vijana wanariadha wa Tanzania watashiriki katika maeneo ya mbio fupi na ndefu, pamoja na michezo ya mpira wa meza, ngumi, judo n.k vijana wasiopungua 50 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo.
Kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Wizara yangu, kwa kutumia diplomasia ya mahusiano katika michezo, tumeweza kupeleka vijana 50 pamoja na walimu wao kwenye makambi ya mafunzo Ethiopia, Uturuki, New Zealand na China.  Vijana wapo huko na taarifa tulizonazo ni kwamba mazoezi yanakwenda vizuri sana.  Ni matumaini yetu kuwa huko Glasgow, vijana wetu watafanya maajabu na kuijengea heshima nchi yetu.

6.2            USHIRIKIANO WA KIKANDA
6.2.1    Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika. Mwezi Agosti, 2013, Wizara iliratibu na kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Lilongwe, Malawi. Mkutano huo ulijadili na kufanya maamuzi mbalimbali yakiwemo yafuatayo:
a)     Kumteua Mheshimiwa Joyce Banda, Rais wa Malawi kuwa Mwenyekiti wa SADC hadi Agosti, 2014; Mhe. Banda alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Emilio Armando Guebuza, Rais wa Msumbiji;
b)    Kumteua Mheshimiwa Hifikepunye Pohamba, Rais wa Namibia kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC inayoshughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama. Mheshimiwa Pohamba alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
c)     Kumteua Dkt. Stergomena L. Tax kutoka Tanzania kuwa Katibu Mtendaji wa SADC kuchukua nafasi ya Dkt. Tomaz Agosto Salamao ambaye kipindi chake kilimalizika. Dkt. Tax amekuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuingoza Jumuiya hii katika miaka 33 ya uhai wake. Uteuzi huo ni uthibitisho mwingine wa kuzidi kushamiri kwa diplomasia ya Tanzania na umeendelea kuijengea heshima kubwa na kuitangaza nchi yetu  katika medani ya Kimataifa.; na 
d)    Kuendelea kutoa ushauri juu ya utatuzi wa migogoro mbalimbali ya kisiasa inayoendelea ukanda wa SADC.

6.2.2    Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR)

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (The International Conference on the Great Lakes Region -ICGLR). Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za ICGLR uliyofanyika tarehe 15 Januari 2014 Luanda, Angola na uliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu Mashariki mwa DRC; na pia kuziomba nchi zote za jirani na DRC zilizosaini Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano (The Peace, Security and Cooperation Framework for the DRC and the Region) kuendelea kutekeleza makubaliano yaliyoazimiwa katika Mpango huo ikiwemo kutohifadhi wala kusaidia makundi ya waasi.

Aidha, mkutano huu uliiagiza Sekretarieti ya ICGLR kwa kushirikiana na Ofisi ya Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi za Maziwa Makuu, Mhe. Mary Robinson kuandaa mkutano wa kwanza wa aina yake katika eneo letu utaokojadili suala la vijana na ukosefu wa ajira (ICGLR’s Special Summit on Youth and Unemployment). Mkutano huu unatarajiwa kufanyika mjini Nairobi, Kenya mwishoni mwa mwezi Juni 2014 na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wa ICGLR na pia wadau mbalimbali katika suala la ajira za vijana.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji vitega uchumi na biashara katika kuleta maendeleo ya haraka na endelevu, unaandaliwa mkutano mwingine maalum wa uwekezaji (the Private Sector Special Investment Forum) utakaofanyika baadaye mwaka huu. Lengo la mkutano huu ni kuchochea uwekezaji katika nchi za Maziwa Makuu hususan zile ambazo zimekumbwa na machafuko.

6.3            BARA LA AFRIKA
6.3.1    Umoja wa Afrika (AU)

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Balozi zetu imeendelea  kuratibu ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine Barani Afrika na kushiriki kwenye shughuli za Umoja wa Afrika (AU). Mwezi Julai 2013, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kuhusu UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria uliofanyika Abuja, Nigeria. Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo. Mkutano huu, pamoja na masuala mengine, ulipitisha Azimio linalozitaka nchi za Afrika kuchukua hatua za makusudi kutokomeza UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria Barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kuhusu Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Oktoba 2013, ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huo, ulijadili suala la kesi inayowakabili Viongozi Wakuu wawili wa Serikali ya Kenya kwenye ICC. Mkutano huo, ulipitisha Azimio ambalo pamoja na masuala mengine, lilisisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya haki na kukabiliana na ukiukwaji wa sheria, utawala bora, amani na usalama Barani Afrika pamoja na kuheshimu utu na mamlaka ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara vilevile iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, ambapo nilimuwakilisha Mheshimiwa Rais kuongoza ujumbe wa Tanzania. Mkutano huu ulijadili na kupitisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa letu, ikiwemo Msimamo wa pamoja wa Afrika kuhusu Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015 (Common African Position on Post – 2015 Development Agenda) na kuanzisha Chombo cha Mpito cha Kukabiliana na Migogoro Barani Afrika (African Capacity for Immediate Response to Crises – ACIRC).  Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa chombo hicho. Aidha, wakati wa Mkutano huo, Tanzania ilichaguliwa kwa muhula wa pili kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa kipindi cha miaka miwili hadi mwezi Aprili 2016.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwenye Baraza hilo, ambapo mwezi Desemba 2013, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi wa Baraza hilo uliofanyika mjini Banjul, Gambia, kwa ajili ya kujadili hali tete ya migogoro nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini. Mkutano huo ndiyo uliotoa pendekezo la kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

7                 WATANZANIA WAISHIO UGHAIBUNI NA SWALA LA URAIA PACHA (DUAL CITIZENSHIP)

Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza jukumu lake la kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) katika maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii ya nchi yetu.  Wizara, kwa kutumia kurugenzi yake ya Diaspora inaendelea na utafiti kwa kushirikiana na Balozi zetu duniani pamoja na uongozi wa Jumuiya za Diaspora ili kubaini idadi kamili ya Watanzania waishio nje, ikiwa ni pamoja na kubaini taaluma zao.
Changamoto na kilio kikubwa cha wana-Diaspora cha kutaka Serikali yetu ikubali na kuipitisha sheria ya kuruhusu uraia wa nchi mbili (dual citizenship) inashughulikiwa kikamilifu na Wizara yangu.  Wizara tayari imelifikisha suala la uraia pacha kwa Tume ya Jaji Warioba na tayari suala hili limewekwa kwenye Rasimu ya Katiba Mpya na tutajadili kwa nguvu za hoja na kwamba umefika wakati wa nchi yetu kuwa na sheria ya kuruhusu uraia pacha kwa maslahi na maendeleo ya Taifa letu. Ni matumaini yangu kuwa Bunge hili litaunga mkono pendekezo hilo.

8                 ULINZI NA UJENZI WA AMANI DUNIANI

Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni Jumuiya ya Kimataifa imeshuhudia Tanzania ikichukua majukumu kwa kushiriki moja kwa moja katika harakati za ukombozi na utatuzi wa migogoro Barani Afrika na duniani kote.  Mpaka sasa, Tanzania imeendelea kushiriki katika utatuzi wa migogoro na ulinzi wa amani ambapo imekuwa ikichangia Vikosi vya kulinda amani katika nchi mbalimbali zinazokabiliwa na migogoro.

Mheshimiwa Spika, hadi Machi 2014, Tanzania ilikuwa na jumla ya wanajeshi 2,259 kwenye maeneo manne (4) ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa. Maeneo hayo ni DRC (MONUSCO); Sudan (UNAMID); Lebanon (UNFIL); na Ivory Coast (UNOCI). Hii inaonesha jitihada za Tanzania za kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.

Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Tanzania kwenye misheni za kulinda amani unazidi kuifanya nchi yetu iaminike na kuheshimiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hii imedhihirishwa na uteuzi wa Watanzania kwenye nafasi za juu kwenye misheni hizo ikiwemo “Force Intervention Brigade – FIB” chini ya MONUSCO nchini DRC na UNAMID ya Darfur, Sudan.  Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa niaba ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ameiomba Serikali yetu ipeleke jeshi lake Sudani ya Kusini. Tumekubali.

Mheshimiwa Spika, ushiriki wetu kwenye maeneo hayo umewawezesha wanajeshi wetu kuendelea kupata uzoefu. Pia, wanajeshi hao wanaendelea kuongeza maarifa na mbinu za kijeshi na kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa vya kijeshi. Ushiriki wetu pia huwa ni nafasi nzuri ya kuanzisha au kuimarisha mahusiano ya kijeshi na nchi nyingine zinazoshiriki kwenye maeneo hayo.
Watanzania tunayo kila sababu ya kujivunia jeshi letu ambalo ni dogo lakini kali kweli kweli. Mmeona wenyewe nguvu ya jeshi letu kwenye Maadhimisho ya miaka hamsini ya Muungano kwenye Uwanja wa Taifa.

9                 MAADHIMISHO YA MIAKA HAMSINI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika, tarehe 26 Aprili, 1964 Jamhuri ya Tanganyika iliungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Watanzania tunajivuna kwamba tarehe 26 Aprili, 2014 Muungano umetimiza  miaka 50 tangu kuundwa kwake. Hatua tuliyoifikia ni ya kujivunia, kwani katika kipindi hicho zipo nchi nyingi zilizojaribu kuungana bila mafanikio.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka 50, Tanzania kupitia utekelezaji wa Sera yake madhubuti ya Mambo ya Nje tulikataa kufungamana na upande wowote; tukatetea haki za wanyonge; tukadai usawa; tukapambana dhidi ya ubaguzi wa rangi; tukapigania uhuru; na tukahimiza umoja na mshikamano wa Bara la Afrika. Msimamo wetu huu umetujengea heshima duniani na pengine tusingefanya hayo nje ya muungano.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Bunge lako Tukufu na na watanzania wote, tuendelee kuunganisha nguvu katika kutekeleza Sera yetu ya Mambo ya Nje ambayo inahimiza diplomasia ya uchumi. Tukumbuke kwamba nchi nyingi duniani sasa hivi zinaungana kwa malengo ya kukuza uchumi wao. Hivyo nasi tudumishe muungano wetu ili tuendelee kunufaika na kujenga uchumi wenye nguvu.

10            UTAWALA NA MAENDELEO YA WATUMISHI WIZARANI NA BALOZINI
Mheshimwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ina jumla ya Watumishi 401  ambao kati yao 152 wapo kwenye Balozi zetu, 234 wapo Makao Makuu na Watumishi 15 waliopo Idara ya Mambo ya Nje Zanzibar. Aidha, Watumishi wengine 12 wapo kwenye likizo bila malipo kwa kuwa wanafanya kazi katika mashirika mbalimbali ya Kimataifa.
Mheshimwa Spika, ili kuwezesha kuwajengea uwezo na kukidhi vigezo vya muundo kwa Watumishi, Wizara imeandaa mpango wa mafunzo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2015/2016.
Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wafadhili mbalimbali imeendelea kugharamia mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ambapo Watumishi 13 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi na watumishi 14 wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimwa Spika, katika kuendeleza uwakilishi wetu nje, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Mabalozi na Naibu Mabalozi kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali. Mabalozi walioteuliwa ni Mheshimiwa Naimi Switie Aziz (Addis Ababa), Mheshimiwa Anthony Ngereza Cheche (Kinshasa), Mheshimiwa Daniel Ole Njoolay (Abuja), Mheshimiwa Wilson Masilingi (The Hague), Mheshimiwa Chabaka Kilumanga (Moroni), Mheshimiwa Lt. Gen. Abdulrahaman Amiri Shimbo Rtd. (Beijing), Mheshimiwa Modest Mero (Geneva), Mheshimiwa Mbaruk Nasoro Mbaruk (Abu Dhabi), Mheshimiwa Liberata Rutageruka Mulamula (Washington D.C), Mheshimiwa Dkt. Azizi Ponaly Mlima (Kuala Lumpur), Mheshimiwa Dora Mmari Msechu (Stockholm), Mheshimiwa Lt. Gen. Wynjones Mathew Kisamba (Moscow) na Mheshimiwa Joseph Edward Sokoine (Idara ya Ulaya na Amerika). Aidha, Naibu Mabalozi ni; Bwana Mohamed Hija Mohamed (New Delhi), Bwana Juma Othman Juma (Muscat) na Bwana Omary Mjenga (Dubai).

Mheshimwa Spika, vilevile, Wizara imewateua Wakurugenzi Wasaidizi 16 kuziba nafasi zilizokuwa wazi katika Idara za; Diaspora (2), Itifaki (2), Ushirikiano wa Kimataifa (1), Ushirikiano wa Kikanda (2), Asia na Australasia (2), Ulaya na Amerika (1), Mashariki ya Kati (1), Afrika (1) Nje Zanzibar (1) na Sera na Mipango (3).
                                            
11            TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA
11.1       Chuo Cha Diplomasia
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Chuo cha Diplomasia kimeendelea kufanya maboresho ili kukidhi masharti ya Baraza la Ithibati ya Elimu ya Ufundi (National Council for Technical Education – NACTE). Chuo kimezidi kutambulika na kuimarika katika utoaji taaluma, ushauri na kufanya tafiti katika masuala ya utatuzi wa migogoro, itifaki, diplomasia ya uchumi, stratejia na menejimenti ya mahusiano ya kidiplomasia. Aidha, Chuo kimeendelea kuishauri Wizara yangu katika masuala ya kidiplomasia na kutoa mafunzo maalum kwa watumishi wa Wizara, Mabalozi na wenza wao. 

Mheshimiwa Spika, sambamba na kuongeza udahili kutoka wanafunzi 590 katika mwaka wa masomo wa 2012/2013 na kufikia wanafunzi 881 katika mwaka huu wa masomo 2013/2014. Chuo kipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kutoa shahada na kufundisha lugha za kichina kwa watanzania na kiswahili kwa wageni kuanzia mwaka ujao wa masomo.

Mheshimiwa Spika, katika kujiimarisha zaidi, Chuo kimejikita katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano 2012/2013 – 2016/2017 kwa kuboresha miundombinu kama ilivyoainishwa katika Master Plan ya Chuo, kuongeza ufanisi katika utoaji taaluma, kuajiri wataalam wenye sifa ili kufanya Chuo kiwe kituo bora cha kikanda kilichobobea katika taaluma, tafiti na utoaji ushauri wa kitaaluma katika fani za mahusiano ya kimataifa, diplomasia ya uchumi na stratejia. Mipango hii ina lengo la kukifanya Chuo kiwe na uwezo wa kujitegemea katika utekelezaji wa majukumu yake.


11.2       Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha  Arusha (AICC)
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kimeendelea kutuwakilisha vyema katika diplomasia ya mikutano na kuvutia utalii nchini kwa njia ya mikutano. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Kituo kimeweza kukaribisha wastani wa mikutano 61 kwa mwaka.  Kati ya mikutano hii, asilimia 30 ya mikutano ni ya kimataifa na asilimia 70 ni ya kitaifa.  Idadi hiyo ya mikutano imeweza kuleta Arusha wageni wanaokadiriwa kufikia 17,680 kila mwaka.  Kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2013, Kituo kiliweza kuwa wenyeji wa mikutano ya kimataifa 29 na ya kitaifa 33 iliyoingiza nchini wageni wanaokadiriwa kufikia 15,040.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni, 2013.  Katika kipindi hicho, kituo kilipata faida ghafi ya shilingi milioni mia moja tisini na moja, mia tatu thelathini na moja elfu na mia tatu themanini na tano (191,331,385.00) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na bila kuwa tegemezi kwa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2014/2015, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya shilingi bilioni kumi na tatu, mia nane themanini na tano milioni, mia saba na saba elfu, mia nane thelathini na mbili (13,885,707,832.00) kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato ikiwemo ya Kituo kipya cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ambacho kilikabidhiwa kwa AICC Agosti, 2013 na AICC inategemea kukopa shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na mali za kudumu zenye thamani ya shilingi bilioni tano, mia tisa sitini na tatu milioni, mia nne thelathini na sita elfu (5,963,436,000.00).

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itaendelea kuhakikisha Kituo kinatimiza moja ya jukumu lake la kupangisha asasi za kimataifa.  Taasisi mbili za Umoja wa Afrika (AU Advisory Board on Corruption na African Institute of International Law) zilizoanzishwa hivi karibuni, makao makuu yake ni katika kituo cha AICC.  Kwa kuzingatia upatikanaji wa nafasi baada ya Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (UN-ICTR) kupunguza shughuli zake na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kurudisha baadhi ya ofisi zake na kuhamia kwenye jengo lao jipya, Kituo kitaendelea kupokea taasisi zingine za kitaifa na kimataifa zitakazopenda kuweka makao yake jijini Arusha.

Mheshimiwa Spika,  ili kuhakikisha Mpango Mkakati wa Kituo unatekelezeka, Wizara yangu inaendelea kufuatilia ujenzi wa Kituo kipya cha mikutano mjini Arusha kitakachoitwa Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC). Mradi huo ni moja ya miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Watu wa China kupitia benki yao ya Exim. 

Mheshimiwa Spika,  vilevile, Wizara yangu baada ya kupata kibali cha Hazina iliidhinisha Kituo kukopa ili kiweze kujenga majengo matatu ya kisasa (condominium) katika viwanja vyake vilivyoko Arusha kwa ajili ya kupangisha. Aidha, kituo kina mpango wa kujenga maduka ya kisasa (shopping malls) kwa ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Serikali za Mitaa (LAPF) katika viwanja vyake vilivyoko Kaloleni, Arusha na kina mpango wa kupanua Hospitali yake iliyoko Arusha, kwa mkopo toka taasisi za fedha. 

11.3       Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM- Tanzania)
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mpangokazi wa APRM kwa mwaka wa fedha 2013/2014 baadhi ya shughuli zilizotekelezwa:

·        Kufanya uchambuzi wa masuala yaliyojitokeza katika Ripoti ya APRM na kuoanisha masuala hayo na Mipango ya Maendeleo ya Taifa ambayo ni pamoja na Mpango wa Maendeleo  wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16), MKUKUTA II, MKUZA II na mipango mingine;
·        Kutafsiri Ripoti ya Nchi ya Utawala Bora katika lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuifanya Ripoti hiyo ieleweke kwa watu wengi zaidi ukizingitia kuwa lugha ya Kiingereza ambayo Ripoti hii imeandikwa inafahamika na Watanzania wachache;
·         Kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa APRM Tanzania toka mwaka 2007 (ulipoanza) hadi Aprili 2014 kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kwa lengo la kuwafahamisha hatua zilizofikiwa. Pia kuwaomba Makatibu Wakuu waingize changamoto zilizobainishwa katika Ripoti ya Nchi ya Utawala Bora kwenye Mipango yao ya Wizara ya Muda Mfupi na wa Kati. Hatua hii ni mwanzo wa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kuondoa Changamoto za Utawala Bora zilizobainishwa na Ripoti ya APRM na kuzitolea Taarifa itakayowasilishwa kwenye vikao vya AU kila mwaka;
·        Kutayarisha mfumo wa tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kuondoa Mapungufu yaliyojitokeza ya Utawala Bora;
·        Kutayarisha makala zitakazotumika wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya Ripoti ya Nchi ya Tathmini ya Utawala Bora kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Makatibu Wakuu Tanzania Bara na Zanzibar, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, taasisi za kiraia na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, mipango ya baadae ya APRM ni kufanya uzinduzi wa Ripoti ya Nchi ya Utawala Bora ambao utafanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuendelea kuwafahamisha wananchi kuhusu matokeo ya Ripoti ya Nchi ya Utawala Bora (CRR); kufuatilia utekelezaji wa Mpango kazi wa Taifa wa kuondoa changamoto za utawala bora zilizobainishwa na kutayarisha Ripoti za utekelezaji za kila mwaka; na kuendelea kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia masuala mbalimbali ya Utawala Bora ambazo APRM Tanzania imeanzisha ushirikiano kama vile CHRAGG na PDB kwa lengo la kubadilishana uzoefu kwa manufaa ya nchi yetu.

12         MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
          Mheshimwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu iliidhinishiwa kutumia kiasi cha Shilingi bilioni mia moja na thelathini na nane, mia tatu hamsini na tisa milioni, mia tisa arobaini na nne elfu na mia mbili ishirini na moja (138,359,944,221.00). Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni mia moja na kumi, mia tatu hamsini na tisa milioni, mia tisa arobaini na nne elfu na mia mbili ishirini na moja (110,359,944,221.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni ishirini na nane (28,000,000,000.00) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Katika fedha zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida (Recurrent Budget), Shilingi bilioni mia moja na nne, mia tisa na sita milioni, mia mbili themanini na nne elfu na mia saba kumi na tisa (104,906,284,719.00) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) na  Shilingi bilioni tano, mia nne  hamsini na tatu milioni, mia sita hamsini na tisa elfu na mia tano na mbili (5,453,659,502.00) ni kwa ajili ya Mishahara.

Mheshimwa Spika, Wizara kupitia Balozi zake ilitarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni kumi na sita, milioni mia tisa sitini na sita, mia saba ishirini na tisa elfu na mia tatu (16,966,729,300.00) kama maduhuli ya Serikali. Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2014, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 12,909,470,376.00 ikiwa ni makusanyo ya maduhuli Balozini. Kiasi hicho cha makusanyo ya maduhuli ni sawa na asilimia 76 ya makisio ya makusanyo yote ya maduhuli kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Mheshimwa Spika, hadi kufikia tarehe 31 Machi 2014, Wizara ilikuwa imepokea kiasi cha Shilingi bilioni mia moja kumi na saba, milioni mia tatu ishirini na saba na mia tisa sitini na mbili (117,327,353,962.00). Kati ya kiasi hicho, Shilingi bilioni mia moja na sita, milioni mia nne tisini na mbili, mia nane arobaini na nane na arobaini na mbili (106,492,848,042.00) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, Shilingi bilioni nne, milioni mia tatu sitini na nane, mia saba na tano elfu na mia tisa ishirini (4,368,705,920.00) ni kwa ajili ya Mishahara na  Shilingi bilioni sita, mia nne sitini na tano milioni na mia nane elfu (6,465,800,000.00) ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

13              CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu imekabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutawala na kibajeti katika utekelezaji wa majukumu yake. Baadhi ya changamoto hizo ni upungufu wa Watumishi Makao Makuu ya Wizara na Balozini; upungufu wa vitendea kazi; uchakavu wa majengo ya ofisi na makazi Balozini; na uchakavu wa magari ya uwakilishi na huduma Balozini.

Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuomba kibali Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma cha kuajiri Watumishi wapya. Vilevile, Wizara imeendelea kununua vitendea kazi vya Watumishi kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Wizara itaendelea kutumia fedha za bajeti ya Maendeleo zinazopangwa katika bajeti kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele na kuishirikisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika kuingia ubia wa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopo Balozini. Halikadhalika, Wizara imepanga kutumia utaratibu wa higher purchase katika kufanikisha ununuzi wa magari Balozini. Utaratibu huu ni mzuri kwa kuwa utapunguza gharama za ununuzi wa magari hayo.

14         MALENGO YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015
         
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, pamoja na mambo mengine, Wizara yangu imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu yake kama ifuatavyo:-

                               i.            Kuitangaza nchi yetu kama moja ya nchi duniani yenye mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji;
                             ii.            Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi mbalimbali wahisani na mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo;
                          iii.            Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali kikanda na kimataifa kwa lengo la kuvutia wawekezaji na watalii; kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu; na kutafuta masoko;
                          iv.            Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
                             v.            Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC); Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA); kuanzishwa kwa Malengo Endelevu ya Maendeleo – Sustainable Development Goals – SDGs na agenda ya maendeleo baada ya kumalizika kwa kipindi cha Malengo ya Milenia 2015. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu masuala yote yanayogusa maslahi yetu;
                          vi.            Kuendelea kusimamia na kupigania maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizozitoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini;
                        vii.            Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Balozi ndogo na kuongeza umiliki wa nyumba za makazi na ofisi za Ubalozi katika Balozi zetu nje kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu;
                     viii.            Kutekeleza maelekezo ya Viongozi wa kitaifa pamoja na kuzingatia ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
                          ix.            Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati ya vyombo vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi muhimu ya Taifa letu;
                             x.            Kuendelea kusimamia na kuzihimiza Balozi zetu nje kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;
                          xi.            Kuendelea kuitambua Jumuiya ya Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya Taifa lao; na
                        xii.            Kuendeleza Ujirani Mwema.

15         MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu yaliyotajwa hapo juu, kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara yangu imepangiwa bajeti ya kiasi cha Shilingi bilioni mia moja tisini na moja, mia tisa kumi na tisa milioni na mia saba arobaini na nane elfu (191,919,748,000.00). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia moja sitini na moja, mia tisa kumi na tisa milioni na mia saba arobaini na nane elfu (161,919,748,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni thelathini (30,000,000,000.00) ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo. Aidha, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara, Shilingi bilioni mia moja hamsini na sita, mia moja hamsini na nane milioni na sabini na nane elfu (156,158,078,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi bilioni tano, mia saba sitini na moja milioni na mia sita sabini elfu (5,761,670,000.00) ni kwa ajili ya Mishahara.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi Mengineyo ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2014/2015, Shilingi bilioni moja, mia saba sitini na nne milioni (1,764,000,000.00) ni kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania (APRM), Shilingi bilioni moja, mia tano na nne milioni, mia tano sabini na nne elfu, mia nne sabini na nane (1,504,574,478.00) ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na Shilingi bilioni nne, tisini na nne milioni na mia tisa na mbili elfu (4,094,902,000.00) ni kwa ajili ya fedha za Mishahara na Matumizi Mengineyo ya Chuo cha Diplomasia.

Mheshimiwa Spika, katika fedha za bajeti ya maendeleo za kiasi cha Shillingi bilioni thelathini (30,000,000,000.00) zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2014/2015, kiasi cha Shilingi bilioni kumi na nne, mia moja sitini na saba milioni, mia tano na nne elfu (14,167,504,000.00) ni kwa ajili ya kukamilisha ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya balozi jijini Paris, kiasi cha Shilingi bilioni saba, mia nne ishirini na tano milioni (7,425,000,000.00) ni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi Mount Vernon-New York, kiasi cha Shilingi bilioni moja, mia tatu na tisa milioni, mia sita sitini na saba elfu na tisini na sita (1,309,667,096.00) ni kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo jijini Khartoum, Sudan, kiasi cha Shilingi bilioni nne, mia tisa hamsini milioni (4,950,000,000.00) ni kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi ya Ubalozi jijini New York, kiasi cha shilingi milioni mia moja arobaini na mbili, mia mbili ishirini na saba elfu (142,227,000.00) ni kwa ajili ya ukarabati wa  makazi ya Balozi jijini Geneva na kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni tano, mia sita na mbili elfu (2,005,602,000.00) ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la Makao Makuu ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Wizara yangu kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni kumi na nane, mia tano sitini na nane milioni, ishirini na mbili elfu, mia nne sabini na nane (18,568,022,478.00) kama maduhuli ya Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi hiki cha maduhuli tayari kimejumuishwa kama sehemu ya bajeti ya Matumizi Mengineyo ya Wizara.

16         HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu yaliyotajwa hapo juu, kwa mwaka wa fedha 2014/2015, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe  jumla ya Shilingi bilioni mia moja tisini na moja, mia tisa kumi na tisa milioni na mia saba arobaini na nane elfu (191,919,748,000.00). Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni mia moja sitini na moja, mia tisa kumi na tisa milioni na mia saba arobaini na nane elfu (161,919,748,000.00) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni thelathini (30,000,000,000.00) ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

1 comment:

Anonymous said...

I would like to thank you for the efforts you've put in writing this blog.

I'm hoping to view the same high-grade blog posts from
you later on as well. In truth, your creative writing abilities has
inspired me to get my very own website now ;)