BABA WA 'MTOTO WA BOKSI' AGUSWA NA MATESO YA BINTIYEBaba mzazi wa mtoto wa miaka minne, aliyedhulumiwa haki yake ya utu na kuteswa kwa zaidi ya miaka mitatu kwa kufungiwa  ndani ya boksi tangu akiwa na umri miezi tisa, Rashid Mvungi hatimaye amepatikana na kusema kuwa mtoto huyo ni damu yake na kwamba yuko tayari kumlea  katika hali yoyote.
Mvungi alisema hayo jana, ambapo alisema tukio la mtoto wake kuishi ndani ya boksi, limemtia simanzi kubwa.
Alisema alikuwa na tabia ya kwenda kumuona mtoto wake kila mwezi na alikuwa akipeleka Sh 20,000 hadi 30,000 kwa ajili ya matumizi ya mtoto, tangu alipochukuliwa na mama yake mlezi.
Alisema, katika kipindi cha mwanzo alikuwa akipata fursa ya  kumuona mtoto na kwamba ana maendeleo mazuri.
Alisema katika kipindi cha karibuni, hakuwa  akipatiwa fursa hiyo, kutokana na kuambiwa mtoto amelala.
Aidha, alisema hakutaka kuonesha hofu yake juu ya majibu ya mama mlezi wa mtoto huyo, kwa kile alichodai ni kuogopa kufikiriwa tofauti na mama huyo.
Hata hivyo, alidai anamlaumu mama mlezi wa mtoto huyo kwa kumtesa mwanawe, ambapo alisema kama aliona amechoka kumlea, angemwambia ili ajue cha kufanya.
"Kama alikuwa amechoka kumlea angeniambia nami ningetengeneza mazingira ya kumchukua," alisisitiza na kuongeza kuwa, mama mzazi wa mtoto huyo aliugua kwa muda mrefu na kusababisha ashindwe kumnyonyesha, hali iliyochangia kudhoofika kwa afya ya mtoto kwa kuwa hakunyonya maziwa ya mama.
Aidha, alisema baada ya mama wa mtoto kufariki, mama yake mkubwa  alimuomba mtoto huyo ili akaishi naye, ambapo naye aliridhia, akiamini mama yake mkubwa angeishi naye vizuri.
Akizungumzia suala la ulemavu wa mtoto, alisema kuwa hakuwa mlemavu, isipokuwa afya yake ilikuwa dhaifu kutokana na kukosa maziwa ya mama, ambapo alisema  alikuwa anaweza kusukuma gari la watoto.
Akizungumzia suala la kushindwa kuishi na mwanawe, alisema kuwa alishindwa kutokana na kuwa hakuwahi kumwambia mkewe kuwa ana mtoto mwingine nje, kutokana na uzito wa suala lenyewe.
"Mwanaume yeyote wa kitanzania akizaa mtoto nje ya mkewe huwa anakuwa mzito kumpa taarifa mkewe kwa kuhofia kupoteza ndoa," alidai Mvungi.
Uchunguzi wa awali aliofanyiwa mtoto huyo, ulibaini alikuwa na nimonia na  ulegevu wa viungo, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viungo katika mwili wake kuvunjika.
Daktari Mshauri wa Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Hores Msaky alipozungumza na mwandishi juzi, alisema walimpokea mtoto huyo akiwa katika hali ya uchafu usio wa kawaida.
Msaky alisema waliamua kumfanyia vipimo vya awali pamoja na picha ya X-ray na kugundua mifupa yake si ya kawaida, inaonekana imevunjika ingawa hawajajua ni nini hasa kimesababisha kuvunjika kwake.
Akizungumza na mwandishi jana alipotembelea hospitalini hapo ili kujua  maendeleo ya mtoto huyo,  daktari  Msaky alisema bado wanaendelea kumpatia matibabu na kwamba  hali ya mtoto huyo kwa sasa inatia matumaini.
Alisema kuwa tayari jopo la madaktari, limekaa na kuamua kuwa wiki ijayo apelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Hatimaye juzi mateso ya mtoto huyo ambaye alikuwa  akiishi, kula na  kujisaidia akiwa ndani boksi kama mnyama, yalipungua baada ya  msamaria kutoa taarifa kuwa ndani ya nyumba, kuna kiumbe asiye na hatia na aliye katika mateso makali. Msamaria huyo alitoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Diana Zongo.
Zongo akiwa katika kazi zake za kawaida katika Mtaa wa Azimio anaoishi mtoto huyo, alipata taarifa kwa majirani kuwa kuna mtoto amefichwa ndani ya boksi na hamfanyii usafi wala kumtoa nje hali iliyomfanya amtafute Mwenyekiti wa Mtaa, Tatu Mgagala na kuongozana naye mpaka kwenye nyumba na kumkuta mtuhumiwa na kuanza kumhoji.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, wakati mtuhumiwa akijibu maswali alikuwa akibabaika na kwamba ghafla mtoto huyo alipiga chafya, hali iliyowapa wasiwasi na kuamua kuingia kwa nguvu chumbani kwa Mariam Said, hatua iliyomuokoa mtoto huyo kutoka katika mateso aliyokuwa nayo.
Mtoto huyo alikutwa akiwa ametapakaa uchafu, uliotokana na kinyesi na mkojo kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha kulala, meza yake ya chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema baba mzazi wa mtoto huyo, anashikiliwa kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
Akizungumzia sakata la kupotea kwa  kaka wa mtoto huyo, Kamanda Paul alisema baada ya kupata taarifa hizo, walijaribu kupeleleza na kubaini kuwa marehemu aliacha watoto wawili, ambao alizaa na wanaume wawili tofauti na kwamba  taarifa za awali walizonazo ni kwamba kaka yake mtoto huyo, alichukuliwa na baba yake mzazi.

No comments: