ATI YATANUA DHAMANA YA BIMA KATIKA MIRADITaasisi ya African Trade Insurance Agency (ATI), imeanisha mikakati yake ya mwaka huu, ambapo kwa Tanzania inatarajia kutoa dhamana ya bima katika miradi ya nishati, miundombinu, huduma za kifedha, mawasiliano, kilimo na uzalishaji wa viwandani.
Katika miaka mitano iliyopita taasisi hiyo, ilitoa dhamana kwa Tanzania katika miradi ya nishati, huduma za kifedha, mawasiliano na sekta ya usafiri yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5 ambayo ni sawa na asilimia 10 ya dhamana zilizotolewa kwa nchi wanachama 10 wa taasisi hiyo.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, George Otieno, wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa wanahisa wa ATI na kutoa ripoti ya mwaka ya taasisi hiyo, unaotarajiwa kufanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Alisema taasisi hiyo, pia ina mpango wa kufanyakazi na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuwezesha benki za kawaida nchini kuweza kupata mitaji kwa urahisi, kusaidia wafanyabiashara wa kawaida na wa chini ili nao waweze kukuza biashara zao za ndani na nje.
Naye Mwakilishi wa ATI Tanzania, Tusekile Kibonde, alisema kwa mujibu wa ripoti ya utekelezaji ya taasisi hiyo kwa mwaka 2013, taasisi hiyo ilisaidia kuvutia jumla ya Sh bilioni 132 katika biashara na uwekezaji nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ATI na Msimamizi wa Bima Tanzania, Israel Kamuzora, aliwataka Watanzania kuacha utamaduni wa kukwepa kuweka akiba, na kutumia fursa zilizopo kujiendeleza kwa faida ya baadaye.
ATI ambayo ni Shirika la Bima linalofanyakazi Afrika nzima, kwa sasa lina wanachama 10 ikiwemo Tanzania wa nchi za Jumuiya ya Soko la Pamoja la Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (Comesa) na ina mpango kuziingiza katika uanachama nchi za jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).
Katika ripoti yake ya mwaka ATI imetoa dhamana ya dola za Marekani bilioni 30 kwa nchi zote wanachama katika miradi mbalimbali, ambapo kwa mwaka jana imepata faida ya Sh bilioni 2.4 ikiwa ni sawa na asilimia 144.

No comments: