ATCL KUNUNUA NDEGE NYINGINE MBILI

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), inatarajia kununua ndege nyingine mbili zenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 50 kila moja katika mwaka ujao wa fedha 2014/15 kwa ajili ya kuboresha huduma za usafiri wa anga ndani ya nchi.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, aliliambia Bunge juzi usiku kuwa ujio wa ndege hizo utaimarisha utendaji na kuongeza mapato ya ATCL.
Dk Mwakyembe akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2014/15, alisema ATCL katika mwaka huo wa fedha, imetengewa Sh bilioni mbili kuboresha utendaji wake.
Alisema katika mwaka huo wa fedha, ATCL itapanua wigo wake wa kutoa huduma za uwanjani kwa ndege za kampuni nyingine, kufufua ukumbi wake wa kupumzikia abiria ulioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA) na kuanzisha huduma za kusafirisha abiria kutoka uwanja wa ndege.
Alisema ATCL imeendelea kutoa huduma za kusafirisha abiria katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma na Hahaya – Comoro kwa kutumia ndege yake aina ya Dash 8 Q300.
“Aidha, kuwasili kwa ndege ya kukodi aina ya CRJ-200 yenye uwezo wa kubeba abiria 50 mwezi Machi, 2014 ni kwa lengo la kuendelea kutekeleza mkakati madhubuti wa kuimarisha na kuboresha huduma za ATCL, ikiwa ni moja na kuanzisha safari mpya za ndege,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
Alisema katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Machi, 2014, ATCL ilisafirisha abiria 35,001 walioingiza mapato ya Sh bilioni 7.7 kwa kutumia ndege yake moja ya Dash 8, ikilinganishwa na abiria 24,530 waliongiza Sh bilioni 2.9 katika kipindi hicho hicho mwaka 2012/13 kwa kutumia ndege aina ya Boeing-737.
Kuhusu Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), alisema katika mwaka 2014/15, Serikali imetenga Sh bilioni tisa kwa ajili ya kufanya matengenezo ya ndege nne za Serikali, kununua vipuri mbalimbali kwa ajili ya ndege hizo na kukarabati hanga la Wakala huo.

No comments: