ANAYETUHUMIWA KUUA WAZAZI WAKE KWA SHOKA AKAMATWAMtuhumiwa wa mauaji ya kutisha aliyekuwa akisakwa na   Polisi pamoja na wananchi, kwa tuhuma za kuua wazazi wake wawili,  amekamatwa baada ya kujitokeza mwenyewe kuomba chakula, kutokana na njaa aliyokuwa nayo.
Mtuhumiwa huyo, Yusuph Njau (32), mkazi wa Kijiji cha Masama Roo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, alikamatwa jana saa 2:15 asubuhi na wananchi wenye hasira kali, akiwa katika moja ya nyumba ya ndugu yake, akisubiri kupewa chai.
Akizungumza na mwandishi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Roo, Khalfani Swai, alisema mtuhumiwa alitokea porini alikokuwa amejificha, baada ya kuua wazazi wake wawili, Shahidu Njau (60),  Minei Swai (57) na kuchoma moto nyumba ya familia hiyo.
Kwa mujibu wa Swai, wakati mtuhumiwa akiwa kwa ndugu yake aliyetambulika kwa jina la Halifa, jirani na Shule ya Sekondari ya Roo akisubiri kupatiwa chai, walijitokeza wananchi wenye hasira kali na kumkamata, baada ya ndugu yake huyo kupiga simu kwenye ofisi ya kijiji, kutoa taarifa za kuonekana kwa mtuhumiwa huyo.
"Tumefanikiwa kumkamata Yusuph aliyefanya mauaji ya kikatili, baada ya kutoka maporini  akiwa anahitaji msaada wa chakula…ambapo alifika kwa kaka yake kuomba chai, wakati akisubiri kupatiwa huduma hiyo ndugu yake akatupa taarifa ambapo tulifanikiwa kumtia mbaroni,” alisema Swai.
Aidha, Swai alisema mtuhumiwa huyo alinusurika kuuawa na wananchi wenye hasira kali,  ambao walidhamiria kumcharanga mapanga  kabla ya ndugu zake kufika haraka katika eneo la tukio, ambapo walimtorosha kwa gari na kumfikisha Kituo cha Polisi cha Boma Ng’ombe.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema Polisi kwa sasa wanaendelea na uchunguzi, ili kubaini sababu za mtuhumiwa kuchukua hatua ya kuua wazazi wake kikatili.
Kukamatwa kwa Yusuph,  kumekuja siku chache tangu alipoua wazazi wake wawili kwa kuwacharanga mapanga na shoka Mei 9 mwaka huu kisha  kuteketeza nyumba kwa moto, kwa lengo la kufuta ushahidi.

No comments: