AJIRA MPYA 700,000 KUPATIKANA MWAKA 2014/2015



Serikali inatarajia kuzalisha ajira 700,000 katika mwaka wa fedha ujao wa 2014/2015, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na tatizo la ajira.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ya Sh bilioni 23.
Alisema ajira hizo zitapatikana kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, itakayotekelezwa na taasisi za Umma, Programu ya kukuza ajira kwa vijana pamoja na hatua za uwekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC, Mamlaka ya Maeneo Huru ya Biashara (EPZA) na sekta binafsi.
Kabaka alisema ili kukuza ajira kwa mwaka huu, wizara imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa programu ya kukuza ajira kwa vijana, ambayo imelenga kuwajengea vijana uweo na stadi mbalimbali za kazi na ujasiriamali.
Alisema awamu ya kwanza ya miaka mitatu ya utekelezaji wa programu hiyo, itaanza mwaka huu ambapo Sh bilioni tatu zimetengwa kwa ajili hiyo.
Kabaka alisema kwa mwaka wa fedha uliopita hadi kufikia Aprili mwaka huu, ajira 630,616 zilizalishwa katika sekta za kilimo ajira 130,974, Elimu 36,073, Ujenzi na Miundombinu 32,132, Nishati na Madini 453 na  Afya 11,221.
Alisema TASAF 8686,sekta nyingine za Serikali 2,321 ,sekta binafsi 211,970,viwanda vidogo na vya kati 7,192,miradi ya uwekezaji kupitia maeneo huru ya uwekezaji (EPZ) 26,381 mawasiliano 13,619 na kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) 149,594.
Kabaka alisema mwaka huu Wizara itaanza utekelezaji wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, baada ya kukamilisha kanuni za tozo kwa waajiri wote wa sekta ya umma na binafsi watachangia katika kuendesha mfuko wa fidia kwa wafanyakazi .
Waziri Kabaka alisema katika kusimamia ajira kwa wageni na kulinda ajira kwa Watanzania kwa mwaka wa fedha uliopita ilipokea maombi 7,432 ya vibali vya ajira za wageni vya daraja B na kati ya maombi hayo 6,237 sawa na asilimia 83.9 yalipewa kibali,1175 yalikataliwa na maombi 20 yalisitishwa kwa uchunguzi.
Akiwasilisha maoni  ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wake, Said Mtanda alitaka Serikali kukamilisha mchakato wa uanzishwaji wa mfuko wa pensheni ya wazee ili wazee nao waboreshewe hali  zao za maisha.
Pia, Kamati ilishauri Serikali kuangalia mfumo wa elimu kwa kufanya utafiti wa kina wa mitaala iliyopo ili kuona mitaala gani itakayowezesha vijana kujiajiri wenyewe kwani takwimu zinaonesha  vijana wanaomaliza vyuo vikuu nchini kila mwaka ni 400,000 mpaka milioni moja.
Alisema lakini wanaopata ajira ni wastani kati ya 80,000 hadi 100,000 katika sekta za umma na binafsi, suala linaloonekana ajira kwa vijana bado ni tatizo kubwa.
Mtanda alisema kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, inakadiriwa vijana 850,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka nchini huku asilimia 40 ni waliofeli kidato cha nne.
Alisema benki hiyo inakadiria kuwa ifikapo mwakani, kutakuwa na ongezeko la vijana milioni 1.3 katika soko la ajira.

No comments: