AFARIKI KWA CHAKULA KINACHODHANIWA KUWA NA SUMU



Mkazi wa Kitunda aliyetambuliwa kwa jina la Shabani Linus (35) amekufa baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Marietha Minangi, tukio hilo ni la juzi saa 9  alasiri katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam.
Alisema mtu huyo alikufa wakati akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo baada ya kufikishwa akiwa na maumivu makali ya tumbo, kichwa na kutapika baada ya kula chakula akiwa kazini kwake asubuhi.
Inadaiwa marehemu huyo alikula mihogo na chai kwa mama lishe na muda mfupi alianza kulalamika maumivu ya tumbo.
Alisema kutokana na tukio hilo watuhumiwa wawili ambao ni Tatu Hamisi (30) na Bibie Ally (20) wote ni mama lishe  wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano. Maiti imehifadhiwa hospitalini hapo.
Katika tukio jingine, watu watano wamenusurika na ajali kufuatia daladala waliyokuwa wamepanda kuwaka moto.
Ajali hiyo ni ya juzi saa 3 usiku katika Barabara ya Bagamoyo eneo la Mbezi Cotex, ambapo gari aina ya Toyota Coaster yenye namba T848 BDZ inayofanya safari zake kati ya Tegeta na Msata, likiendewa na Michael Msemwa (37) ghafla liliwaka moto kwenye dashibodi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema katika tukio hilo watu watano akiwemo dereva wa gari hilo walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Aliwataja watu hao kuwa ni Joekonia Msemwa (33) ambaye ni kondakta, Mashiala Ramadhani (39), Wilfred Felix (19) ambao walikimbizwa Hospitali ya IMTU kwa matibabu na baadaye walihamishiwa Hospitali ya Mwananyamala ambapo wamelazwa hospitalini hapo. Chanzo cha moto huo na thamani ya gari bado haijajulikana.

No comments: