AFA NA KUHARIBIKA NYUMA YA KITUO CHA POLISI



Mkazi wa Kijiji cha Lubungo wilayani Mvomero, Juma Mbega, amekutwa amekufa na mwili wake kuharibika nyuma ya Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Morogoro.
Akizungumza na mwandishi jana baada ya kugundulika kwa mwili wa Mbega, mjukuu wa marehemu Nuru Adam, alisema kwa muda mrefu babu yake huyo alitoweka nyumbani kwao. 
Kwa mujibu wa Adam, babu yake huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka, ambao ulisababisha augue ugonjwa wa  akili na muda mwingi alikuwa akiingia kwenye maofisi na migahawani kuomba fedha na chakula.
Alisema mara ya mwisho alionekana akifanyakazi ya kumenya viazi katika mabanda ya chipsi kwa ujira wa fedha kidogo na chipsi, na nyakati za usiku alikuwa akilala kwenye baraza za maduka maeneo ya mjini.
Nuru alisema yeye na ndugu zake walishindwa kumhudumia babu yao kwa kuwa yeye mwenyewe alikuwa akigoma kurudi nyumbani. 
Baadhi ya mashuhuda waliokuwepo jirani na eneo hilo, walidai walimuona babu huyo wiki iliyopita na jana walianza kusikia harufu ikitokea kwenye kichaka nyuma ya Kituo kikubwa cha Polisi.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, baadaye walipata taarifa kupitia
mtu aliyekuwa akiokota chupa za plastiki, kwamba ameona  mwili wa binadamu ukiwa umeharibika na habari zilipofika Polisi, askari walifika na kuchukua mwili wa babu huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema    uchunguzi wa kifo hicho unaendelea na mwili wa Mbega umeshakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

No comments: