WAZEE WA KIMILA WAKAMATA BUNDUKI ZA KIVITA NA RISASI 17

Wazee wa kimila kutoka  makabila ya Wasonjo na Wamasai wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, wamekamata silaha tatu za kivita, risasi 17 na magazini mbili.
Mafanikio hayo yamekuja siku nne tu tangu wazee hao, walipounda timu maalum kusuluhisha migogoro ya ardhi baina ya makabila hayo kwenye vijiji vya Mgongo na Olorien. 
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alisema wazee hao walikamata silaha hizo  juzi saa 10:30 asubuhi wilayani Ngorongoro baada ya timu hizo kuanza kazi yake,
Silaha hizo zilisalimishwa na wananchi  na zilikuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria.
Alizitaja  silaha hizo kuwa ni  SMG moja yenye namba NH-4200, ikiwa na magazini yenye risasi tano, SAR yenye namba 20034823 ikiwa na risasi saba, zilizopatikana katika kijiji cha Olorien na G3 yenye namba D60365 ikiwa na magazini yenye risasi tano, iliyopatikana Kijiji cha Mgongo.
Kusalimishwa kwa bunduki hizo, kumetokana na operesheni iliyofanywa na polisi na wananchi  kati ya Aprili 10 na 19 mwaka huu, kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa mtu mmoja, wa kijiji cha Olorien, Aprili 8, mwaka huu.
Tukio hilo lilifuatiwa na tukio lingine, linaloaminika kuwa ni ulipizaji wa kisasi la Aprili 10 mwaka huu, ambapo gari la abiria, aina ya Land Rover, kutoka vijiji vya Wasonjo kwenda Loliondo, lilishambuliwa kwa risasi na watu wawili waliuawa na wengine saba kujeruhiwa vibaya.
Kamanda alisisitiza kuwa timu hiyo ya usuluhishi, itakapomaliza  kazi yake katika vijiji hivyo viwili, itaendelea  katika vijiji vingine.

No comments: