WATUHUMIWA WA MENO YA TEMBO WAENDELEA KUSOTA RUMANDE

Washitakiwa sita wa kesi ya kukutwa na kontena la meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 7.48  wanaendelea kusota rumande katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jana kesi hiyo ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika  au la.
Hata hivyo washtakiwa hao Mohammed Mussa , Mohammed Udole, Juma Makoma, Mohamed Hija,Omary Ally na Haider Ahmed, wote kutoka Zanzibar wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika.
Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba mosi na Novemba 13, mwaka jana, katika maeneo tofauti, Kinondoni, Dar es Salaam na Mjini Magharibi, Zanzibar walipanga njama za kutenda kosa.
Katika mashitaka mengine wanadaiwa kukutwa na nyara za Serikali, ambazo ni meno ya tembo, vipande 1,023, vyenye uzito wa kilogramu 2,915, yakiwa na thamani ya Sh 7,480,125,000.
Hata hivyo washitakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu mashitaka yao kwa kuwa  mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu. Kesi hiyo itatajwa tena Mei 8 mwaka huu.

No comments: