WATOTO 78 WAZALIWA KWENYE MKESHA WA PASAKA

Watoto 78 wamezaliwa usiku wa Pasaka katika hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam, wa kiume wakiwa 44 na wa kike 29.
Kwa upande wa Hospitali ya Mkoa ya Amana, Msimamizi wa Hospitali hiyo Getruda Masawe alisema katika hospitali hiyo, walizaliwa watoto 68 na kati yao  28 wa kike na 40 ni wa kiume.
Alisema miongoni mwa watoto hao, wapo mapacha wa kiume na wamezaliwa wakiwa na afya njema. Hakuna matatizo kwa wazazi hao na watoto.
Muuguzi Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Linnah Kinabo alisema watoto  watano wamezaliwa hospitalini hapo na kati yao  wanne ni wa kiume na mtoto mmoja ni wa kike.
Alisema watoto wote wana afya njema na  wamezaliwa kwa njia ya kawaida, isipokuwa mtoto mmoja ndio alizaliwa kwa njia ya upasuaji.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi ya wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walisema wana furaha ya kujifungua salama.
Fatuma Richard, Mkazi wa Gongo la Mboto ambaye ni mzazi pekee aliyejifungua mtoto wa kike katika hospitali hiyo kubwa kuliko zote nchini, alisema amefurahi kujifungua salama wakati huu wa Pasaka.

No comments: