WATAALAMU WAZEMBE WA MIFUGO KUSHUGHULIKIWA

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani amesema Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria mtaalamu  wa mifugo, ambaye eneo lake litabainika kukabiliwa na ukiukwaji wa sheria ya ustawi wa wanyama.
Pia, amelaumu baadhi ya mamlaka za Serikali ikiwemo mahakama na taasisi za wanyamapori, zinazokamata mifugo na kuifungia kwenye maeneo yasiyostahili bila maji wala malisho mpaka kufa.
Aidha, amesema wakati mwingine hupiga mifugo risasi, kuwalazimisha wamiliki kulipa faini, jambo alilosema ni ukatili dhidi ya wanyama.
Dk Kamani ameagiza wasimamizi wa sheria na watoa huduma za wanyama, kusimamia ipasavyo kanuni za ustawi wa wanyama kazi, usafirishaji, uchinjaji na ufugaji wa mifugo kwa ujumla.
Alisema katika kuimarisha ustawi huo, wizara yake itaendelea kuhimiza elimu ya ustawi wa wanyama iingizwe kwenye mtaala wa shahada ya kwanza ya udaktari wa mifugo.
Alisema hayo Dar es Salaam  jana, alipokuwa akihutubia wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo katika sherehe za 14 za Siku ya Veterinari Duniani kwenye viwanja vya wizara hiyo.
“Aidha nawahimiza wataalamu wote wa afya ya mifugo wakishirikiana na wakaguzi wa ustawi wa wanyama kuhakikisha Sheria ya Ustawi wa Wanyama Sura ya 154, ya mwaka 2008 na kanuni zake  zinasimamiwa,” alisema.
Alisisitiza, “ikumbukwe kwamba wanyama hawana utashi kama binadamu, hivyo ni unyama uliokithiri kumtesa mnyama kwa kosa lililotendwa na binadamu.”
Akifafanua zaidi, alisema sheria haitasika kuchukua mkondo wake kwa mtu yeyote atakayepatikana akivunja sheria hiyo kwa makusudi na hata kumfutia usajili mtaalamu ikibainika eneo lake la kazi kuna ukiukwaji wa sheria na wanyama wanateswa.
Wakati huo huo, alikemea tabia ya watu kusafirisha kuku wakiwainamisha vichwa chini, kuwapiga mifugo.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Mifugo Tanzania, Profesa Dominick Kambarage alisema sekta ya mifugo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na wataendelea kusimamia utoaji bora wa huduma.

No comments: