WANAWAKE 100 SALAMA DHIDI YA SARATANI YA KIZAZI

Zaidi ya wanawake 100 waliojitokeza kupima maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi katika Jukwaa la Familia Kitchen Party Gala, lililofanyika Dar es Salaam juzi, wamethibitika kutokuwa na ugonjwa huo.
Jukwaa hilo hufanyika katika mikoa mbalimbali chini ya ufadhili wa Shirika linalojishughulisha na masuala ya afya la PSI Tanzania kwa ushirikiano na Asasi ya Women in Balance ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia upimaji huo uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee juzi jioni, Meneja wa Mradi wa Uzazi wa Mpango wa PSI, Catheline Paul alisema zaidi ya wanawake 100 waliopima wamekutwa hawana maambukizi ya ugonjwa huo ambao ni tishio kwa wanawake nchini.
“Imekuwa ni bahati nzuri kwamba tofauti na Dodoma na Mwanza ambako karibu wanawake tisa walikutwa wana ugonjwa huo, leo kwa Dar es Salaam wanawake waliopima wamethibitika kuwa hawana maambukizi na wamepewa elimu ya kujikinga,” alisema Paul.
Awali, Mratibu wa Familia Kitchen Party Gala, Vida Mndolwa alisema hamasa ya wanawake kujitokeza kupima afya kupitia jukwaa hilo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku hatua inayotoa matumaini ya kupungua kwa vifo vya akinamama kutokana na masuala ya uzazi.
Alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwa mikoa ya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam, ni azma ya waandaaji kuona kuwa wanawake katika maeneo mengine nchini wanafikiwa ili kupewa elimu kuhusu afya ya uzazi, Ukimwi, malaria, ndoa, malezi ya watoto na ujasiriamali.
“Kama inavyofahamika kuwa ni vigumu kuweza kuwakusanya wanawake wengi kiasi hiki ili kuwafanyia vipimo vya afya zao, lakini kupitia jukwaa hili mwamko wao umekuwa ni mkubwa kwani pamoja na kupima afya wamekuwa wanapata burudani na kuzungumza masuala yanayohusu kujitambua na kujithamini,” alisema Mndolwa.
Mratibu wa Mawasiliano wa PSI, Mohammed Mziray alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Asasi ya Women in Balance katika kuendesha jukwaa hilo katika maeneo mbalimbali nchini baada ya majaribio ya awali katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam kuonesha mafanikio makubwa.

No comments: