WANAOTAKA KUWA WALIMU WA SAYANSI SASA KUSOMA BURE

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeongeza vigezo kwa wanafunzi watakaojiunga mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya Stashahada, ambapo kwa sasa itadahili wanafunzi wenye ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu pamoja na kuwagharimia watakaochukua masomo ya hisabati na sayansi.
Hatua hiyo imetokana na mikakati iliyowekwa na Wizara hiyo katika kuboresha elimu nchini na pia kutokana na upungufu wa walimu 26,000 wa masomo ya hisabati.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari Mkuu wa Wizara hiyo, Ntambi Bunyazu, wizara ilieleza kuanzia mwaka wa masomo 2014/2015 wanafunzi watakaojiunga na fani ya ualimu kwa masomo ya hisabati na sayansi watagharamiwa na serikali kupitia mfumo wa ruzuku na mikopo.
"Wanafunzi watakaokuwa na ufaulu wa Daraja la Kwanza watapatiwa ruzuku na wale wenye Daraja la pili na la tatu watapewa mkopo ili kuwasaidia katika masomo yao. Watakaofaulu mafunzo ya ualimu katika masomo ya Sayansi na Hisabati watapatiwa ajira moja kwa moja kulingana na taratibu za serikali," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, iliweka wazi vigezo vitakavyotumika kujiunga na mafunzo hayo.
Kabla ya kufanywa marekebisho hayo, wahitimu waliokuwa wakiomba nafasi za mafunzo walikuwa wanatakiwa kuwa na daraja la nne alama 27  katika mtihani uliofanyika katika kikao kimoja. Awe na ufaulu wa kiwango cha alama C katika masomo manne tofauti katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika katika vikao zaidi ya kimoja.
"Siku za nyuma ilikuwa mwenye daraja la nne alama ya 26 na 27 anaweza kuingia moja kwa moja kusomea ualimu ngazi ya stashahada lakini sasa watakaoingia moja kwa moja kusomea ualimu watakuwa ni daraja la kwanza hadi la tatu na wale wa daraja la nne waliopata alama 26 na 27 watasoma mwaka mmoja kwanza na baadaye watapatiwa mtihani wakifaulu ndipo wataingia kusomea ualimu ngazi ya stashahada,"alifafanua Bunyazu.
Wakati huo huo, waombaji wa mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya cheti wanatakiwa kuwa na ufaulu  wa daraja la tatu katika mitihani yao ya kidato cha nne kwa mwaka 2004 na 2012.
Waombaji wa nafasi zote hizo wanatakiwa kuingia katika tovuti ya wizara  kwa maelekezo zaidi.

No comments: