WANAHARAKATI WASIHI NAFASI ZAIDI KWA WANAWAKE

Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wanawake watatu pekee wanaotoka katika majimbo ya uchaguzi huku jumla ya wanawake wote ikiwa ni 26 kati ya wajumbe wote 82 hali ambayo wanaharakati wametaka kundi hilo lipewe nafasi zaidi kugombea nafasi za juu za uongozi. 
Kutokana na uwiano huo, vyama vya siasa nchini vimetakiwa kutoa kipaumbele na kushirikisha  wanawake katika kugombea nafasi mbali mbali za juu za uongozi katika vyombo vya uamuzi.
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Mzuri Issa alisema licha ya kuwepo nafasi za viti maalumu, uteuzi huo haujatosheleza kufikia malengo ya usawa wa kijinsia katika maendeleo.
“Kwa mfano alisema katika Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe 82, ni 26 tu wanawake katika nafasi za viti maalumu huku watatu wakitoka katika majimbo ya uchaguzi,” alisema.
Aliendelea kusema, “Vyama vya siasa vinatakiwa kutoa kipaumbele kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi katika majimbo ya uchaguzi.”
Alitoa mfano wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwa hakijatoa kipaumbele kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi kwani katika uchaguzi wa mwaka 2010 hakuna mwanamke aliyesimamishwa katika majimbo ya uchaguzi tofauti na CCM.
Mzuri alitaja nchi za Ulaya ikiwemo Denmark pamoja na Sweden ambazo zimetoa kipaumbele kwa wanawake kugombea nafasi za  uongozi kiasi kwamba, kwa sasa hakuna nafasi zilizotengwa maalumu kwa wanawake.
Alitaja pia nchi za Afrika, hususani Ghana, Msumbiji, Afrika Kusini pamoja na Rwanda kwamba zimefanikiwa kwa asilimia 64  kwa wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Tamwa inaendesha kampeni  kuhakikisha vyama vya siasa vinatoa kipaumbele na nafasi kwa wanawake kushiriki katika uongozi.

No comments: