WANAFUNZI, SHULE ZINAZOFANYA VEMA KUZAWADIWA

Katika kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu, Serikali itazawadia wanafunzi na shule zilizofanya vyema katika mitihani ya Elimu ya msingi na Sekondari.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam juzi  na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dk Shukuru Kawambwa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Wiki ya Elimu.
Kwa mujibu wa Dk Kawambwa, maadhimisho ya wiki hiyo ya Elimu itakayoanza Mei 3 hadi 9 mwaka huu ni ya kwanza nchini na yanalenga katika kutambua juhudi za kuendeleza ubora wa Elimu nchini.
“Pamoja na malengo mengine, wiki hii italenga katika kutoa motisha na zawadi kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri, ikiwa ni utekelezaji wa wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa,” alisema Waziri Kawambwa.
Miongoni mwa malengo ya BRN katika kukuza ubora wa elimu nchini ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wa shule zinazoonekana kuvuka viwango vya kukuza ubora.
Kwa mujibu wa Dk Kawambwa, maadhimisho hayo yatakayofanyika mjini Dodoma yatazinduliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pia yatafungwa na Rais Jakaya Kikwete.

No comments: