WALIOPATA DIVISHENI 1 HADI 3 SASA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO

Serikali imesema sifa za mwanafunzi atakayeendelea na masomo ya kidato cha tano kwa mwaka huu ni  waliopata daraja la kwanza hadi la tatu pointi 31.
Aidha, katika kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi wa kujitegemea kwa kidato cha nne na sita na wale wa masomo ya maarifa yanakuwa bora, Serikali imekasimisha jukumu la kudhibiti vituo vinavyotoa masomo kwa Taasisi ya Elimu Tanzania.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema pamoja na mfumo wa alama kubadilika kutoka alama tano za miaka ya nyuma na kufikia alama saba, haijabadilisha kitu .
"Tumeongeza alama ili kuwatenganisha wanafunzi, lakini hii haijabadili kitu chochote, hivyo sifa za kuingia kidato cha tano zitakuwa ni daraja la kwanza hadi daraja la tatu," alisema.
Baada ya Serikali kuongeza alama za viwango, kutoka alama tano za awali (A,B,C,D na F) na kuongeza alama (A,B+, B, C, D, E na F) wazazi na wanafunzi wamekuwa na dukuduku la kutaka kufahamu sifa za wanafunzi kujiunga na kidato cha tano na vyuo .
Daraja kwa kwanza ni pointi 7 -17, daraja la pili pointi 18-24 na daraja la tatu ni pointi 25-31.
Aidha, akizungumzia kukwamua mwanafunzi wa kujitegemea ambao wameonekana ufaulu wao kutokuwa mzuri, Kawambwa alisema serikali imeamua kuipa jukumu TIE kudhibiti na kuhakikisha elimu inayotolewa kwenye vituo hivyo inakuwa bora na inayomwezesha mwanafunzi kufanya vizuri.
"Kuanzia mwaka huu, Taasisi ya Elimu Tanzania tumeipa jukumu la kukagua vituo na kuangalia elimu inayotolewa, na tutaendelea kuboresha mazingira kila wakati ili ufaulu wa wanafunzi hawa uwe mzuri," alisema.
Wakati huo huo, Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI inatarajia kuadhimisha Wiki ya Elimu ambayo pamoja na mambo mengine itatumika kutoa motisha na zawadi kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri kwa matokeo ya shule ya Msingi na Kidato cha Nne 2013.

No comments: